Monday, October 30, 2006

Prof.Shivji na uandishi wetu

"...Hardly any one(including journalists themselves) takes journalism seriously, let alone with commitment." (Issa Shivji; Intellectuals at the hill, pg. 176). Soma nukuu kamili katika bolgu ya Maggid

Johnson Mbwambo je?

Anaandika kwa unyenyekevu mkubwa. Lakini hoja yake ni kali kweli kweli. Anajua kuna wanaotumiwa bila kujua. Anawajua. Anawaonea huruma; ama wao au vizazi vyao. Angependa wajitambue, wajirudi sasa. Warudi kazini kwao. Ni mpole, makini na muwazi. Msome. Huyu hapa.

Wednesday, October 25, 2006

Hata Wakubwa Wanaweza Kushitakiwa

Hivi kama kila Rais Mstaafu angechunguzwa na kushughulikiwa kama huyu hapa, Afrika ingeweza kupiga hatua gani katika mapambano dhidi ya rushwa? Hatua hiyo ingekomesha wizi na kuboresha maisha ya wananchi? Je, sisi Tanzania hatuna viongozi wanaotuibia wakiwa madarakani? Tuwafanyeje wanapostaafu?

Tuesday, October 24, 2006

CCM ukwasi mtupu, watumishi njaa kali


Posho za wakubwa ni mara 300 ya mishahara ya watumishi. Kama wakubwa wameshiba na wadogo wanalia njaa, kuna lolote litakalofanyika? SOMA hapa uone adha za watumishi waaminifu wa CCM, na majibu ya wakubwa wao kuhusu hatima yao. Madereva wa chama nao waja juu. Nadhani wanajiuliza. Bosi wao Yusuf Makamba, anapata manono katika mshahara wa Ubunge, Ukatibu Mkuu wa CCM na masurufu ya safari anayojilipa. PATA uhondo.

Bilioni za kichumi au kisiasa?

Unasemaje kuhusu bilioni moja za Kikwete kila mkoa? Kumbuka huyu ni mchumi na mwanasiasa. Katika uamuzi huu anafanya uchumi au siasa? Toa maoni. Wenzako wameshaanza.

Monday, October 23, 2006

Walimu mavumbini, wanafunzi wanaozwa


Haya jamani. Ona shule zetu zilivyo, miaka 45 baada ua uhuru. Yameenea nchi nzima. Wakubwa wanajisifu, na wanayataja na haya kama mafanikio ya MMEM. Haya yanatokea pia kwingine katika hali tofauti. Hata Dar es Salaam yapo, mita chache kutoka nyumbani na ofisini kwa Rais, Ikulu. Na hili la wanafunzi kujisaidia vichakani katika karne ya 21 tunaizungumziaje? Eti na ukosefu wa VYOO unasababisha shule kufungwa; huku baadhi ya walimu wakiiba fedha za MMEM. Huko Musoma, wanafunzi 600 wanasota. Ndiyo maana hata wazazi hawaamini kwamba watoto wao wasiojua hata kuandika majina yao wameshinda mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kwenda sekondari. Tuko makini kweli? Si hivyo tu. Wazee hawa maskini, wamefungwa jela kwa sababu serikali imeshindwa kujenga shule, na inawalazimishwa wachangie hata kama hawana pesa!

Uhamisho dhidi ya mabadiliko ya mawaziri

Tuulizane: Ni mabadiliko ya Baraza la Mawaziri au uhamisho. Wadau wanasemaje? Imalizie kwa kusoma hapa.

Natamani waandishi wote wangekuwa hivi

Kama waandishi wote wangekuwa hivi, ni hoja gani imebaki bila kujengwa? Ni nani angethubutu kuchezea taaluma yao? Ni nani angejaribu kuwaweka kwenye kiganja chake na kuwadhalilisha? Ni nani angewakuta wakimshambulia anayewatetea? Lakini upande mwingine unasema, kama waandishi wote wangekuwa hivi, tungewezaje kutofautisha pumba na mchele. Hakika, huwezi kuthubutu kumweka Deus Jovin katika kundi la pumba. Labda kama hujasoma hoja yake hii.

Sunday, October 08, 2006

Tunafaidi joto la kukumbatiwa; Tanzania inafaidi nini?

Na Ansbert Ngurumo, Hull University, UK

NAANDIKA kumpa pole Rais Jakaya Kikwete kwa yaliyompata kutoka gazeti la Kenya wiki inayomalizika leo.


Nimesoma kwenye mtandao kwamba gazeti moja la Kenya limechapisha katuni inayoonyesha waandishi wa habari wa Tanzania wakimlamba miguu Rais Kikwete. Nimeiona katuni hiyo.


Nimesoma pia habari juu ya taarifa ya Ikulu kwamba Rais wetu na wasaidizi wake wamesononeshwa na katuni hiyo. Nimesoma pia kwamba Rais hatajibu lolote kuhusu katuni hiyo.


Nakubaliana na rais wangu kwa mambo mawili. Walioandika na kuchora katuni hiyo si Watanzania. Ni Wakenya. Na si Wakenya wote, wala si magazeti yote ya Kenya.


Hivyo Rais amefanya jambo jema kutojiingiza katika malumbano nao. Si wananchi wake.


Maana hata sisi tumekuwa tukiona magazeti yetu yanawachora viongozi wengine wa Afrika na sehemu mbalimbali za dunia. Yanawachora kadiri mitazamo yetu juu yao inavyokuwa wakati huo.


Na michoro hiyo haina masilahi yoyote ya kisiasa. Ina malengo mbalimbali ya kitaaluma. Inalenga kuburudisha wasomaji. Wakati mwingine inaleta ujumbe mpya - inaelimisha. Wakati mwingine inafikirisha.


Na katika kufanya hivyo, inafurahisha au inaudhi. Kwa mfano, kuna watu wamefurahia katuni hiyo kwa kuwa wanaamini kwamba waandishi wa Tanzania wanalamba miguu ya wakubwa. Wapo.


Wapo walioifurahia kwa sababu tu ya kufurahia ubunifu wa mchoraji. Wapo. Wengine wameifurahia kwa sababu wanapenda utani. Na wameona mtu aliyejitokeza kumtania rais wa nchi!


Wengine wameichukia. Si kwa sababu nyingine yoyote, bali kwa kuwa imemgusa na kumsema rais. Basi! Hawataki aguswe.


Wengine wameichukia kwa sababu wamesikia mwenyewe aliyechorwa ameichukia. Wanachukia pamoja naye.


Wapo walioichukia kwa kuamini kwamba imesema uongo. Wanasema imemdhalilisha Rais. Wanaongeza kuwa imewadhalilisha waandishi wa habari. Wapo.


Bila shaka sitakosea nikisema katika kundi hili wamo waandishi wenyewe. Maana tunajua kwamba wengi wetu, ingawa tunaandika na kuchambua mambo ya wengine kila siku, hatufurahii uchambuzi wa wengine juu yetu kama hautusifii.


Ni hulka ya kibinadamu. Kila mtu anataka asemwe vizuri. Hulka hii ndiyo inayowapa haki waliochukia pamoja na rais wetu.


Lakini wengine hawakuchukia wala kufurahi. Wameguswa tu na hoja ya mchoraji. Wanaweza kukuza mjadala mpya, na kumwambia Rais Kikwete na wasaidizi wake kwamba baada ya kuchukia watafute tafsiri halisi ya katuni hiyo.


Naamini, kama ilivyowahi kuandikwa na mwandishi mmoja ambaye simkumbuki jina, kwamba haiwezekani watu wote wakawa na tafsiri moja inayofanana juu ya katuni hiyo.


Haiwezekani. Hivyo, inabidi tuvumiliane katika kuelewa ujumbe unaoletwa kwetu kupitia katuni hiyo. Watu wenye akili hawatakosa la kuwaza. Wanaweza kuitumia kuboresha uhusiano kati ya rais au serikali na vyombo vya habari. Uhusiano unalisaidia taifa.


Maana kama wengi wanavyosema, nami naamini katika ukweli huu, uhusiano uliopo sasa kati ya rais na vyombo vyetu vya habari unalenga kuisaidia serikali, si nchi.


Ni uhusiano usiotambua kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola. Na hili halikuanzwa na Kikwete. Amelirithi. Lakini litamgusa zaidi yeye kwa kuwa amejitangaza kuwa rafiki wa vyombo vya habari.


Kwa kauli yake mwenyewe, mara kadhaa, amesema kwamba ana nia ya kushamirisha demokrasia katika Tanzania. Nionavyo mimi, Kikwete hawezi kushamirisha demokrasia bila kuviondoa vyombo vya habari katika utumwa.


Hawezi kushamirisha demokrasia iwapo vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira ya woga. Na anayeogopwa katika hili si mwingine, bali serikali. Hawezi kushamirisha demokrasia bila kuondoa sheria dhalimu ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa miaka zaidi ya 14 sasa; ambazo zinavinyima vyombo vya habari fursa ya kuwa huru na kufanya kazi bila kuogopa matumizi mabaya ya utashi wa wakubwa.


Yawezekana mchoraji wa katuni anajua hali halisi ya uandishi wetu na mazingira yanayotukabili. Anajaribu kuchora uhusiano uliopo kati ya waandishi na rais, anasema wanamlamba miguu.


Nasema hivi, hatumlambi miguu. Lakini simshambulii mchoraji. Ningekuwa naichora mimi ningemweka rais akiwa amewakumbatia waandishi, badala ya kuwaonyesha wakilamba miguu.


Kulamba ni alama tu kama ilivyo kukumbatiwa. Hata kama wapo ambao wangedhani kukumbatiwa ni kuzuri zaidi, sioni tofauti kimantiki.


Ninachoona katika kumbatio ni watu wanaofurahia joto la rais. Ikumbukwe kuwa watu hawa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya kubezwa na rais aliyeondoka. Alikuwa mwandishi, lakini hakutangaza kuwa rafiki yao.


Sana sana, alikuwa akilumbana nao kila alipopata fursa ya kufanya hivyo hadharani. Aliwaita waandishi uchwara. Aliwadharau wazi wazi. Bila shaka nao walimchukia.


Sasa huyu kaja. Amenyoosha mikono yote miwili. Katika mshangao wa ajabu, nao wamenyoosha mikono. Wamekumbatiana. Mh! Joto la rais!


Lakini bahati mbaya, huyu aliyewakumbatia haachii. Hawawezi kutoka. Wanabaki wanacheka. Wanapiga stori. Wanatabasamu. Habari zinapita. Haziandikwi.


Zitaandikwaje wakati mikono imekumbatiwa? Zitaandikwaje wakati zinamhusu aliyekumbatia na kukumbatiwa? Zitaandikwaje wakati kila mmoja anaogopa kutofautiana na mkubwa na kuleta malumbano yanayoweza kupoteza joto hili?


Zitaandikwaje wakati wengi waliokumbatiwa wanadhani jukumu lao ni kumsaidia aliyewakumbatia? Zitaandikwaje wakati baadhi ya ahadi zake hazijatimizwa? Hapo ndipo tulipo.


Lakini swali tusilojiuliza haraka haraka ni hili. Iwapo kila mmoja atataka ‘kumsaidia’ rais kutoka ofisini mwake; nani atamsaidia kutoka nje ya ofisi? Lakini zaidi ni wajibu wetu kumsaidia au kuisaidia nchi? Je, nchi yote inaishia kwa rais na wasaidizi wake?


Lipo swali la ziada. Iwapo kila mtu anataka kuwa mwandishi asiye rasmi wa rais, walioajiriwa kumsaidia rais watafanya kazi gani? Na kazi zetu zitafanywa na nani?


Uongo mbaya, waandishi wetu wengi wanampenda rais wetu. Sidhani kama wapo wanaomchukia.


Lakini lazima tuweke tofauti kati ya kupenda, kushabikia na kushangilia. Na tutofautishe mambo ya kushabikia na ya kushangilia. Tuweke tofauti kati ya kufagilia na kufikirisha.


Hata yeye anahitaji kuelimishwa. Hatuwezi kusema ana akili na uwezo wa kusifiwa kwa kila hatua anayoichukua. Anastahili kukosolewa. Na sisi ndio tungepaswa kuongoza Watanzania wenzetu kwa kumfanya rais wetu awe ‘smart’.


Afike mahali hata anapotaka kuzungumza nasi, ajiandae vizuri. Lakini ameshatujaribu mara kadhaa. Ameshinda.


Ipo mifano mingi, lakini nitatoa michache. Wizara ya Nishati na Madini ilipotangaza uamuzi uliotokana na mjadala kati ya Rais Kikwete na Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, kwamba itailipa serikali sh bilioni tisa ambazo ni dola za Marekani milioni saba, hakuna aliyejitokeza kuhoji kwa nini tulipwe kiasi kidogo mno kutoka kwenye migodi mitatu!


Ama tulisahau au hatukujua kwamba kampuni hiyo iliwahi kufanya mazungumzo na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kukubaliana iwe inalipa dola milioni tano kwa mgodi mmoja wa Bulyanhulu, mwaka 1999.


Maana yake, kama alivyosema mwanaharakati wa mazingira, Tundu Lissu, serikali ya sasa itaambulia dola milioni 2.3 kutoka kila mgodi.


Kama ingebanwa kwa mazungumzo ya awali na Mkapa, kampuni hiyo ingelipa dola milioni 15.


Tumeibiwa mchana. Lakini tulimsifu Rais Kikwete kwa hatua aliyochukua. Ndiyo, tumemsifu rais. Tumefaidi joto la kukumbatiwa. Tanzania imefaidi nini?


Rais alipotoa hotuba mbovu jijini Mwanza mwishoni mwa mwezi Julai kuhusu mapanki na silaha, vyombo vya habari vichache - kumbukumbu zangu zinaonyesha havizidi viwili - vilimkosoa baadaye, na wasaidizi wake walikiri kwamba alikosea.


Lakini lugha iliyotumiwa ilikuwa ya kidiplomasia kwamba alishauriwa vibaya; alikoseshwa. Vilivyobaki vyote vilikuwa vikishangilia jinsi alivyomzodoa mtengeneza filamu. Havikutaka kuzama katika mantiki ya filamu hiyo. Havikutazama maisha halisi ya wakazi wa maeneo husika. Kisa? Viliogopa kupoteza joto la rais. Lakini havikumsaidia.


Karibu kila mwandishi anajua kwamba tatizo tulilo nalo katika Bwawa la Mtera, ambalo linadaiwa kusababisha kukosekana kwa umeme wa kutosha nchini, si ukosefu wa maji. Tunajua bwawa limejaa matope.


Tunajua pia kwamba ubabe wa serikali ndio ulioifanya ikatae ushauri wa kitaalamu kwamba bwawa hilo si mradi wa kuaminika wa kuzalisha umeme.


Tunajisifia kwamba viongozi wetu wanatusikiliza tukiwashauri kupitia vyombo vya habari. Mbona tunaendelea kuimba wimbo wao (wa uongo) kwamba tatizo la Mtera ni ukosefu wa maji?


Ipo dhana, ambayo baadhi yetu hatukubaliani nayo kivitendo, kwamba baadhi ya habari haziandikiki. Ipo dhana pia kwamba baadhi ya wakubwa hawaandikiki.


Na wanaosema hivi wanakiri kwamba: “Mkapa licha ya ubabe wake, alikuwa anaandikika, halafu anajibu mapigo… Sumaye pia alikuwa anaandikika, wala hafuatilii kuwasumbua waandishi.”


Ni ujumbe mzito kwa serikali inayowapenda wanahabari, inayowazungumzia vizuri jukwaani, lakini haiboreshi mazingira ya kisera na kisheria kwa ajili yao kufanya kazi kitaaluma. Inaogopa nini?


Nasi wenyewe tunaipa jeuri, kiburi na ubabe tunapokaa na kunyoosha mikono bila kufanya lolote kuikumbusha, kuikemea, kuihoji na kuisumbua.


Tuseme ukweli. Kama ‘Katuni ya Kikwete’ ingetumika katika gazeti lolote nchini, lingekuwa limefungiwa; maana wenzetu hawajajifunza kuvumilia wanapokosolewa. Inawezekana hawajikosoi pia?

Uchambuzi huu unapatikana pia katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Oktoba 8, 2006 na katika tovuti www.freemedia.co.tz Wasiliana na mwandishi kwa simu +447904159823 au barua pepe ansbertn@yahoo.com
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'