Sunday, July 22, 2007

Tanzania isiyo na UKIMWI inawezekana?

Soma hapa.

Serikali Kupinduliwa

HABARI hii ilileta kizaazaa kati ya serikali na gazeti la MwanaHALISI Jumatano 18.07.2007. Serikali inagombana na maoni ya wakili na mwanasiasa maarufu, mmoja wa waasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini, Mabere Nyaucho Marando.

Marando anasema serikali inaweza kupinduliwa, iwapo wananchi watajua haki zao.

“Wewe unatumia lugha ya kupindua. Kwa lugha ya kawaida, kupindua ni kutumia nguvu za kijeshi. Lakini yapo mapinduzi mengine yanayowezekana. Ni yale yanayotokana na mwamko wa wananchi,” amesema.

Katika mahojianao maalum na MwanaHALISI juu ya miaka 15 ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, Marando amesema, “Wananchi wana uwezo wa kuipindua serikali kupitia njia halali ya sanduku la kura.”

Akihusisha hasa na madai ya wabunge wa CCM, Job Ndungai na Janet Masaburi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwamba elimu inayotolewa na HakiElimu inaweza kusababisha serikali kupinduliwa, Marando alisema:

“Hili linawezekana kabisa. Kinachohitajika ni mwamko zaidi kwa umma. Wananchi wakipata mwamko, wanaweza kuipundua serikali kwa njia ya kura.
Marando amesema serikali ya sasa imeshindwa kuwajibika na hivyo inaweza kung’olewa kwa nguvu za umma.

Amesema HakiElimu inafanya kazi nzuri na inaifanya vizuri na kwamba vyama vya upinzani havina budi kujifunza kutoka HakiElimu, hasa katika suala la utafiti wa hoja muhimu za haki za binadamu na maslahi ya jamii.

“Unajua, CCM inaumwa ugonjwa wa kusinyaa. Ugonjwa huu huvipata vyama vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu. Chama kikikaa madarakani kwa muda mrefu, kinasinyaa. Kinakuwa na mchoko,” anasema.

Katika mahojiano ambayo yamechapishwa katika toleo hili, Marando anasema, sababu za kuchukia CCM bado zipo, “Hiki bado ni chama cha kidkteta. Matumaini ya wananchi bado yapo, kwamba kuna siku watajikomboa kutoka udikteta huu.”

Kuhusu mafanikio ya upinzanai katika kipindi hiki, Marando anasema, “uwanja wa demokrasia umepanuka. Serikali inachukua hatua, japo kwa kiwango kidogo na bila upinzani serikali ingefanya itakavyo. Siridhiki, lakini angalau tumepata mahali pa kuanzia.”

Alipoulizwa CCM inaweza kujivunia nini katika miaka hiyo, Marando alisema, “Wanaweza kujivunia bahati yao nzuri ya kushikilia madaraka bila kuwa na sababu za msingi za kutawala na kuendelea kubaki madarakani wakati hawastahili kuwapo.”

Marando amesema CCM haina zaidi cha kujivunia, “Labda ujinga wanaowalisha kwa Watanzania kwamba CCM ndiyo baba na ndiyo mama, wakati si kweli. Wanaweza kujivunia pia rushwa ambayo wameifanya kuwa sera ndani ya CCM na serikali yake. Basi!”

Kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kifedha, Marando anasema, ni kweli vyama havina fedha wala wafadhili, “Lakini lazima wafanye kazi hiyo. Waende kwa Watanzania wenzao… kuomba msaada. Hilo ni jukumu lao na hawawezi kulikwepa hata kidogo.”


Soma Mahojiano na Marando

MwanaHALISI, Serikali wakaribia kuzichapa

Serikali ya awamu ya nne bado inaendelea kukosa uvumilivu. Huku rais Jakaya Kikwete akidai haogopi kukosolewa, matendo ya serikali yake yanaonyesha tofauti. Baada ya kulikosakosa Tanzania Daima mara kadhaa, sasa imeamua (kwa mara nyingine) kulivalia njuga gazeti la kila Jumatano la MwanaHALISI. Soma hapa. Kutokana na sakata hilo, Mchambuzi na Mwandishi mkongwe, Ndimara Tegambwage, anaipatia serikali TUISHENI ya bure.

Sunday, July 15, 2007

Marais wastaafu wafe au washitakiwe?

Rais mstaafu anapokufa taifa haliyumbi. Lakini wapo wanaosema kwamba akishitakiwa kwa makosa aliyofanya akiwa madarakani taifa litayumba. Hii ni kweli au kuna linalofichwa nyuma ya hoja hii? Soma mjadala.

Sunday, July 01, 2007

Amina aliiogopa CCM kuliko wauza mihadarati

Alisema: "nawajua ni watu wa namna gani...wanaweza kunidhuru...”

Buriani Amina Chifupa; umekwenda kishujaa
Na Ansbert Ngurumo, Hull
1.
Amina Mpakanjia;
Nani asiyekujua?
Nani hajakusikia?
Nani hakukutambua?

2.
Eti umetukimbia?
Sikubali nakataa;
Nani kakuondoa?
Lipi umemfanyia?

3.
Amina, mi siamini;
Kwamba tena sikuoni;
Haraka hiyo ya nini?
Wakimbia ‘fanya nini?

4.
Najua hukuwa radhi;
Kwenda chini ya aridhi;
Yatoka wapi maradhi;
Bila idhini ya Kadhi?

5.
Bado ulikuwa dogo;
Miongoni mwa vigogo;
Yako marefu malengo;
Sasa wayapa kisogo.

6.
Umekwenda kwa lazima;
Siku zote tutasema;
Umeondoka mapema;
Nani amekusukuma?

7
Mungu ndiye anajua;
Kwanini watangulia;
Ameshindwa kuzuia;
Majonzi ya Tanzania.


8
Kama angetuuliza;
Nani kumtanguliza;
We tusingekupoteza;
Kura tungezipunguza.


9
Si wewe mwenye hatia;
Ulopaswa tangulia;
Wapo walokuvizia;
Sasa umewakimbia!

10.
Wapo waliokubeza;
Mwenyewe ukanyamaza;
Pole pole ukaanza;
Hadi wao kushangaza.

11.
Kisomo chako kidogo;
Si kama chao vigogo;
Kiliyabeba magogo;
Kuwaachia usongo.

12.
Woga ‘liweka pembeni;
Na nchi yako usoni;
Lionekana makini;
Kama vile wa zamani.

13.
Vijana uliwawaza;
Hata wale wasocheza;
Sumbawanga hadi Mwanza;
Ulisema: ‘hawa kwanza.’

14.
Soka ulishangilia;
Timu yetu saidia;
Nguvu kuiongezea;
Us’okuja shuhudia.

15.
Watoto ulitetea;
Kama mama asilia;
Ulijua Tanzania;
Hao yawategemea.

16.
Yatima ‘lisaidia;
Tumaini ‘liwatia;
Wagonjwa ‘lisalimia;
Wote uliwawazia.


17.
Tabasamu lilijaa;
Huruma lilichochea;
Urembo ulitumia;
Wengi kuwahudumia.

18.
‘Liitwa Mama shughuli;
Kwa kazizo mbalimbali;
Hata kuwapamba wali;
Mambo yako kali kali.

19.
Kikwete anauliza;
Sitta huyo kanyamaza;
Chifupa amepoteza;
Nani ‘tambembeleza?

20.
Wapo ul’oshambulia;
Kwa haki nakutetea;
Mihadarati bugia;
Hukutaka kusikia

21.
Nyota yako iliwaka;
Hata kwa wasoitaka;
Haya sasa umetoka;
Lije walilolitaka?

22.
Sadaka uliyotoa;
Sote tunaitambua;
Hata walokusumbua;
Hili watalijutia.

23.
Hatuwezi simangana;
Sasa twafarijiana;
Ila twaweza ‘onyana;
Hata kushauriana.

24.
Amina umetoroka;
Waacha moto wawaka;
Umejitoa sadaka;
Tutakayoikumbuka.

25.
Twajua ‘metangulia;
Sote tutaelekea;
Ila moja twatambua;
Umekwenda kishujaa!

26.
Umekimbia kwa kasi;
Kuliko hata ya fisi;
Vijana watakumisi;
Wabunge hata na sisi.

27.
Kina mama wanalia;
Mwenzao wakumbukia;
Wasanii nao pia;
Nyimbo wanakuimbia.

29.
Maisha yako twakiri;
Ni mafupi na ya heri:
Marefu yaliyo shari;
Umeachia wapori.

30.
Tulia na Malaika;
Pale atapokuweka;
Tabasamu cheka cheka;
Yametimu, yamefika.

31.
Ukiukuta mpira;
Cheza na Hawa na Sara;
Shambulia mduara;
Hata mbinguni, ahera.

32.
Mpakanjia na mwana;
Baba na Mama Amina;
Kubali ya Maulana;
Itikieni: Amina.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'