Sunday, March 22, 2009

Buriani Jade Goody

MSANII maarufu wa runinga nchini Uingereza, Jade Goody, aliyekuwa anasumbuliwa na Kansa, ambaye aliolewa (shukrani zake hapa) na kubatizwa pamoja na watoto wake wawili, ameaga dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili 22, 03, 2009. Mwanamuziki Darren Hayes amemsindikiza Jade kwa kibao cha I miss you . Humjui Jade Goody? Maelezo haya yanaweza kukusaidia kumfahamu. Alijiandalia mazishi yake mwenywe, na alitaka yawe ya kifahari, iwe hafla ya kusherehekea maisha yake mafupi ya miaka 27, hata kama yatapambwa na machozi ya baadhi ya baadhi ya waombolezaji. Apumzike kwa amani!

Tusaidiane kuepusha ugaidi huu

UGAIDI gani huo? Soma hapa. Na hii je uliipata?

Saturday, March 21, 2009

Rajoelina: Mimi ni rais

Madagascar ina kiongozi mpya Andry Rajoelina (34) ambaye ameapishwa Machi 21, 2009 baada ya kuiangusha serikali ya Marc Ravalomanana. Naona wamepuuza vitisho na kemeo la SADC na AU; na ingawa hata mabalozi wamesusa hafla ya kuapishwa kwake, habari ndiyo hiyo. Rajoelina anasema, 'nimeshakuwa rais.'

Papa Benedicto XVI na Kondomu

KAULI ya hivi majuzi ya Papa Benedicto XVI kupinga matumizi ya kondomu katika vita ya UKIMWI imezua mjadala mpya, huku wengine wakimlaani kwamba anakwamisha mafanikio ya jitihada za kupambana na maambukizi ya UKIMWI na kwamba hakupaswa kutoa kauli hiyo. Wengine wamemkosoa kwamba si kweli kwamba matumizi ya kondomu yanaongeza kasi ya maambukizi ya UKIMWI kwa sababu taarifa za kitafiti zinaonyesha umuhimu wa kondomu katika kuzuia maambukizi. Hata hivyo, taarifa hizo hizo zinadai kwamba kinga ya kutumia kondomu si ya asilimia 100.

Lakini Papa ni kiongozi wa dini, na ujumbe wake unazingatia maadili yanayosimamiwa na madhehebu ya imani yake. Kama huo ndiyo msimamo wa kanisa lake, tulitarajia aseme nini? Ahubiri nini? Asiposema hayo aliyosema atakuwa Papa tena? Na kama kondomu haizuii kwa asilimia 100 Papa amekosea nini?

Thursday, March 19, 2009

Tuesday, March 17, 2009

Wananchi wachukua Ikulu Madagascar

Ndo hivyo! Rais Marc Ravalomanana wa Madagascar ameondolewa madarakani. Alipewa muda aondke mwenyewe kwa hiari, akashindwa kusoma alama za nyakati. Sasa yametimia! Jeshi limeingilia kati, na aliyekuwa kiongozi wa upinzani, Andry Rajoelina (34) kaingia Ikulu. Ona hapa eti wanaondoa mapepo ya Ravalomanana Ikulu!

Lucy Kibaki kashika hatamu au mpini?

Ukisikia mke kushika hatamu, Mke wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya amedhihirisha hilo. Hakika huyu ameshika zaidi ya hatamu - ameshika mpini; mumewe ameshika makali. Lakini si wapimane ubavu kimya kimya, katika faragha? Kwa nini wanamwaga mtama mbele ya kuku wengi? Ndiyo maana nasema wote wawili wamenichefua. Bofya hapa ucheke kwa furaha au hasira.

Saturday, March 14, 2009

Uongozi unaoahirisha majukumu utafanikiwa?

Waislamu wameibuka tena wanataka serikali itekeleze ahadi yake juu ya Mahakama ya Kadhi. Nilishawashauri, na nilisisitiza hivyo katika makala yangu mojawapo ya Novemba mwaka jana. Nasisitiza kuwa wasipowabana wakubwa ahadi hii nayo itayeyuka kama lilivyo suala la Mwafaka wa Zanzibar. Vyovyote itakavyokuwa, litawatesa wakubwa ifikapo 2010.

Friday, March 13, 2009

Wapime watawala wetu kwa swali hili dogo

UKITAKA kujua uwezo au udhaifu wa viongozi wetu waulize maswali. Wala yasiwe magumu. Maswali mepesi tu yanatosha kuonyesha uwezo na upeo wao. Bonyeza hapa utazame na kusikiliza swali dogo lilivyogaragaza wakubwa katika mjadala wa masuala ya kiuchumi.

Monday, March 09, 2009

Watawala wetu mitumba ya kisiasa?

Ni vema TANESCO imejitoa katika biashara chafu ya ununuzi wa genereta mitumba za Dowans. Lakini king'ang'anizi cha serikali kufanya biashara ya mitumba hii, na kauli ya kukata tamaa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Dk. Idris Rashid baada ya wabunge kumjia juu, vinaweza kupata tafsiri nyingi tata kama wanavyosema wananchi. Mi najiuliza: Wenzetu hawa wanang'ang'ania mitumba kwa sababu wamezoea siasa za mitumba, nao ni wanasiasa mitumba?

Kabumbu: Kumbukumbu Muhimu

Wapenzi wa soka mtakaoweza kutazama mechi hizi, nawaletea kumbukumbu za mechi chache muhimu za Kombe la Dunia. Mnaweza kuanza na hii iliyochenzwa na akina PELE mwaka 1970 muone Brazil ilivyoichapa Italia; usipitwe na bao la 'Mkono wa Mungu' lililofungwa na Maradona katika fainali za mwaka 1986; itazame mechi bora kati ya Brazil na Ufaransa mwaka 1986; fuatilieni tathmini fupi ya Kombe la Dunia mwaka 1998 na kifafa cha Ronaldo de Lima.

Linki hizo hapo zinafunguka vema kwa walio Uingereza. Walio nje ya Uingereza nao wanaweza kutumia lakini inabidi wajipatie proxy server ya bure ya UK na wawe na kaufundi kiasi ka kuifiksi. Wale walio Marekani, kama wanatumia Intaneti yenye kasi kubwa wanaweza kufaidi uhondo huu kupitia ESPN360. Vinginevyo, nenda Yahoo World Cup Coverage.

Monday, March 02, 2009

CNN wailetea Afrika programu mpya

MWEZI huu wa Machi 2009, kituo maarufu cha Televisheni cha CNN International kinaanzisha programu mpya kwa Afrika itakayojishughulisha na kutangza masuala ya kitamaduni, michezo na biashara ya bara letu katika mtazamo mpya. Habari kamili hii hapa.

Sunday, March 01, 2009

Michelle Obama rasmi


Hii ndiyo picha rasmi ya Michelle Obama iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Februari 27, 2009. (AP Photo/The White House, Joynce N. Boghosian).

Kifuta machozi cha Richmond

MJADALA na mvutano unaoendelea kuhusu nia ya serikali, kupitia TANESCO, kununua mitambo ya Dowans kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura, unaleta hisia mchanganyiko. Wapo wanaodhani ni mradi makini na halali kwa maslahi ya taifa. Wengine wanashtuka kwa kuwa Dowans ni dada yake Richmond, na wanadhani hii ni janja ya serikali kuwabeba akina Richmond kupitia mlango wa nyuma; kuwapa kifuta machozi kwa yaliyowatokea huko nyuma.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'