Wednesday, September 29, 2010

Dk Slaa azungumzia mambo makuu matatu

Viti Maalumu

Kwanza amezungumzia suala la Viti Maalumu kupitia CHADEMA, akaweka wazi kilichoazimiwa na Kamati Kuu ya chama. Majina 105 kati ya 147 ya walioomba kuteuliwa viti maalumu, yamepitishwa; na sasa yatapelekwa Tume ya Uchaguzi kama sheria inavyodai. Walioteuliwa hawakutajwa majina kwa waandishi. Mfumo wa uteuzi ulizingatia vigezo sita (6) vilivyoainishwa na mtaalamu aliyeteuliwa na chama hicho ili kuifanya kazi hiyo, Dk. Kitila Mkumbo. Vigezo hivyo ni 1. Kiwango cha Elimu. 2. Uzoefu wa kazi ya kisiasa. 3. Uzoefu wa uongozi nje ya siasa. 4. Kugombea Jimbo. 5. Mchango wa mgombea katika chama na kampeni zinazoendelea. 6. Umri wa mtu katika chama. Kila kipengele kilikuwa na vigezo vidogo vidogo kama vinne, vyenye alama tofauti. Na kwa mujibu wa Dk Slaa na Kitila, viti hivyo vimetawanywa nchi nzima, kwa kuzingatia vigezo hivyo hivyo. Akahitimisha kwa kusema: "Ingawa kuna usemi kwamba siasa ni mchezo mbayan, kwa Chadema, siasa ni sayansi na unachezwa kisayansi." Alitumia pia fursa hiyo kusisitiza kuwa Chadema kimeweka wagombea 185 ambao ni ziaidi ya asilimia 75 ya wagombea ubunge nchi nzima; na kwamba idadi hiyo kinatarajia kuvuna wabunge wa kutosha, na kiko tayari kuunda serikali.

Usalama wa Taifa

Dk. Slaa alitumia fursa hiyo kutamka kwamba ana taarifa za kikachero kuwa Rais Kikwete ameagiza wana usalama wa taifa wasambae nchi nzima kuhujumu uchaguzi. Akasisitiza kwamba, "kwa sura ya sasa, Kikwete ameshashindwa...na amani ya nchi ikivurugika, Kikwete ndiye atabeba lawama na laana.." Alisisitiza pia kuhusu waraka uliosambazwa nchi nzima ukiwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchi nzima kufanya kila wawezalo kulazimisha ushindi wa CCM. Akasema hujuma hii inaweza kusababisha umwagaji damu, na kwamba asingependa itokee.

Utafiti na vitisho vya Synovate

"Tunasubiri kusikia Synovate wamefungua kesi. Kama hawajaenda, waende sasa. Wasipofanya hivyo tutawaharibia credibility yao hapa nchini na kimataifa. Chadema tunapofanya kitu chetu huwa haturudi nyuma. Hatuna woga. Gazeti lililoshitakiwa nalo lisiwe na woga." Baada ya hapo alionyesha vielelezo vya utafiti uliofanywa na Synovate, ambao katika kipengele GPO 6 liliulizwa swali: "Kama ucahguzi ungefanyika leo, nani ungempigia kura ya urais?" ambalo Synovate walikanusha kwamba halikuwamo katika utafiti wao, wakidai wanataka kuufanya baadaye kabla ya uchaguzi mkuu. Ukweli ni kuwa walifanya utafiti lakini CCM iliingiza 'mkono' wake baada ya kubaini kuwa matokeo hayo yalikuwa yanaonyesha Kikwete yuko nyuma ya Dk Slaa.

Tahadhari ya Mbowe

Freeman Mbowe alitoa tahadhari kwa Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, na Msajili wa Vyama vya Siasa, akisema wamepewa mamlaka ya umma, ambayo wakiyatumia vizuri wanaweza kulipeleka taifa kwenye amani, na wakifanya makosa wanalitumbukiza kwenye ghasia. Akasema kinatokea sasa, CCM wameshindwa siasa za majukwaani, na watatu hawa wako katika mikakati michafu ya kuvuruga uchaguzi. Akasema kama wanatakua kuugeuza uchaguzi wa uchakachuaji, hapatatosha! Aliwaomba Watanzania kuwa tayari kulinda maamuzi yao, kura zao. Akasisitiza: "Tunaomba Watanzania na jumuiya ya kimataifa mtuelewe..."

Thursday, September 23, 2010

DK. Slaa akiwa Kilimanjaro



Dk. Slaa nyumbani kwa Mbowe

Akiwa katika Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, Dk Willibrod Slaa alifanya mikutano 12 kwa siku moja. Kesho yake akafanya mikutano katika majimbo ya Rombo na Vunjo. Akahitimisha kampeni za awali mkoani humo kwa kufanya kampeni katika majimbo ya Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Same Mashariki na Same Magharibi.

Alichokifanya mkoani Kilimanjaro kimeelezwa vema na wale waliosema “ameiteka Moshi” kwa maandamano ya watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, pikipiki na magari; huku yakisindikizwa na helikopta katika maeneo ya Moshi Mjini. Umati wa wakazi wa Moshi, uliandamana na kusimamisha shughuli zote za kijamii na kibiashara kwa zaidi ya saa nne – kuanzia saa 8 alasiri hadi saa 12 jioni.

Ujumbe kutoka kwa Dk Slaa:

Watanzania wameshakubali kufanya mabadiliko makubwa. Rais Jakaya Kikwete ajiandae kuaga Ikulu, astaafu baada ya mika mitano ambayo haikuleta matumaini yaliyotarajiwa. Serikali isitumie mabavu kuumiza wananchi wanaotaka mabadiliko. Isimwage damu kwa ajili ya maslahi binafsi ya wanaotafuta madaraka au wanaong’ang’ania madaraka.
Rais Kikwete asiviingize vyombo vya ulinzi katika dhuluma inayoweza kusababisha damu ya Watanzania kumwagika kwa ajili ya madaraka ya wachache.

Ujumbe kutoka kwa Freeman Mbowe:

Hatuwezi kuwa na serikali inayoongozwa kwa nguvu za giza badala ya nguvu za Mungu; rais anayelindwa na majini badala ya vyombo ya ulinzi na usalama. Rais Kikwete ajitokeze, akanushe kuhusika na majini ya Sheikh Yahya Hussein, ambayo aliahidiwa kutumiwa yamlinde ili asianguke tena hadharani.

Katika picha hii, Mbowe anawaongoza wananchi wa Moshi Mjini kuzomea CCM kwa kilio huku wamejishika vichwa katika uwanja wa Mashujaa.

Saturday, September 18, 2010

Kampeni ya Dk. Slaa: Mpya Mpya Katika Picha



Mchumba wa Dk. Slaa, Josephine, akisalimia wananchi wa Karatu mkutanoni, juzi Alhamisi.



Dk. Slaa hatumii shangingi. Hiki ndicho kipanya anachotumia katika ziara zake za kampeni. Katika picha hii, wananchi wa Arusha Mjini wanasukuma kipanya hicho kuondoka viwanja vya mkutano kuelekea hotelini jana Jumamosi jioni.




Jina la shabiki huyu wa Dk. Slaa halikupatikana mara moja. Ni mkazi wa Arusha Mjini.




Dk. Willibrod Slaa, akimnadi mgombea wa ubunge katika jimbo la Karatu kupitia chama hicho, ambaye anatarajiwa kuwa mrithi wake wa ubunge jimboni humo, Mchungaji Israel Natse, wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Bwawani mjini Karatu jana Ijumaa



Dk. Willibrod Slaa, akizungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Daudi Siasi, mara baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni zake kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Bariadi juzi Alhamisi.



Bendera za mashabiki Musoma Mjini: Dk. Slaa ni chaguo la vyama vyote



Wananchi Musoma: Dk Slaa ni Taa Mpya

Red Brigade wa Chadema Musoma Mjini



Red Brigade Musoma Mjini

Sunday, September 12, 2010

Hii ndiyo Bunda ya Dk. Slaa



Leo tuko Bunda. Acha picha hizi ziseme zenyewe. Maelezo mengine baadaye. Itoshe tu kusema kwamba miongoni mwa maelfu ya wana Bunda waliofurika kumsikiliza Dk. Slaa katika viwanja vya Sabasaba ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Isack. Alikaa jukwaa moja na Dk. Slaa, naye alimsifu kwa ukomavu wa kisiasa, lakini akamuonya kwamba kama alikuwa amekwenda pale kwa nia tofauti, atazame umma, apime nguvu yake na apeleke taarifa za kile anachosikia na kuona. Alimsimamisha DC huyo akawasalimia wananchi kwa kunyosha mikono juu.

Dk. Slaa acharuka Mwanza



Dk Willibrod Slaa amecharuka mkoani Mwanza. Akiwa katika majimbo ya Geita, Buchosa na Nyamagana, mgombea huyo ametoa changamoto kali kwa CCM, hasa mgombea urais Jakaya Kikwete ambaye Dk. Slaa alisema ni "saizi yangu." Halafu akatumia fusa hiyo kumshughulikia, akisema rais huyo wa awamu ya nne hana mpango mkakati wala visheni ya kuwakomboa Watanzania. Badala yake, Kikwete amekuwa akitekeleza maagizo yake (Dk Slaa) katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hasa kwa kudai anapigana na ufisadi (ulioibuliwa na Dk. Slaa). Hata katika tukio la juzi la Kikwete kumchukulia hatua Meneja wa kiwanda cha Turiani, Morogoro, Dk. Slaa alisema hatua ya Kikwete ilitokana na msisimko wa siasa za uchaguzi, hasa baada ya Dk Slaa kutembelea Turiani, wiki mbili zilizopita, na kutoa kauli kwamba atashughulikia matatizo yao katika siku 100 za kwanza za utawala wake.

Vile vile, alisema Rais Kikwete amevunja rekodi ya kudanganywa kuliko marais wote duniani katika miaka mitano iliyopita. Alisema mwaka mwaka 2007, JK alifungua mradi hewa wa maji huko Pwaga, Dodoma; mwaka 2009 Rais Kikwete aliletewa Ikulu mkurugenzi wa halmashauri isiyohusika na kukabidhiwa gari la wagonjwa; na alizindua hoteli moja ya kitalii mkoani Arusha, kesho yake ikavunjwa uzio na TANROADS, na mwaka huu alisaini kwa mbwembwe sheria iliyochomekwa vipengele ambavyo havikujadiliwa Bungeni; na kwamba hata baada ya matukio yote hayo, hakuna mtu aliyewajibishwa.

Mwaka huu, siku alipozindua kampeni za CCM mkoani Mwanza, JK aliwaeleza wananchi kwa mbwembwe, kuwa Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha, alikuwa amepita bila kupingwa; jambo ambalo Dk. Slaa alisema si kweli kwani mgombea wa Chadema alikuwa ameweka pingamizi, ambalo hatimaye limemrejesha ulingoni. “Ama JK alidanganywa na Masha au alijidanganya mwenyewe au hakuwa makini…Kikwete si makini. Awaombe radhi wananchi wa Nyamagana kwa kuwadanganya.”

Alisema Kikwete amekuwa rais wa majaribio, na kwamba miaka mitano inatosha. "Imetosha, Kikwete aende akapumzike, muda wake umekwisha, miaka mitano inamtosha. “Hatuwezi kwa miaka mitano kuendelea kuwa na rais mtalii, asiyejua matatizo ya wananchi wake, anayetetea maslahi ya wawekezaji badala ya wananchi, asiye na visheni,” alisema.Dk Slaa alidai hata mipango mkakati kama MKURABITA, MKUKUTA na hata MINI-Tiger, hata na barabara anazojivunia JK kujenga ni za awamu ya tatu ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, si zalo la awamu ya nne.

Akiwa jijini Mwanza, alisisitiza juu ya umuhimu wa viwanda katika kujenga uchumi, ajira na ujira bora; akasema CCM iliua viwanda na makampuni ya umma zaidi ya 450 yaliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na hivyo kuua ajira na uchumi wa taifa. Alisema Chadema kinadhamiria kuanzisha viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo na mifugo, ili kuimarisha uchumi wa watu maskini, kwani raslimali zipo. Kilichokosekana, hadi sasa, ni ubunifu kwa upande wa watawala. Alisisitiza pia sera za elimu, afya, na makazi bora wa mujibu wa ilani ya Chadema.

Baada ya mkutano alisindikizwakwa maandamano na umati wa watu wazima na vijana, wakisukuma gari alilopanda kutoka uwanja wa Mirongo hadi Hoteli ya Nyumbani - umbali kwa kilometa zipatazo 5. Polisi walijitahidi kuwadhibiti wananchi hao, ikawa kazi bure. Hakukuwa na fujo yoyote. Walikuwa wakiimba, "rais, rais, Slaa; tumechoka mafisadi..." huku baadhi yao wakiwa na mabango yenye maandishi kuwa, "hatukubebwa na magari, tumekuja ejnyewe."

Friday, September 10, 2010

Dk. Slaa akemea majini ya Sheikh Yahya Hussein


Dk. Willibrod Slaa amemkemea mnajimu Sheikh Yahya Hussein (pichani) aliyeahidi kumpa Rais Jakaya Kikwete 'ulinzi wa majini,' ili kukabiliana na nguvu za giza zinazomwandama na kumwangusha majukwaani. Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Katoro, jimbo la Busanda, Mwanza, Dk. Slaa alisema "nchi haiwezi kuongozwa na uchawi. Haiongozwi na imani za watu, kila mtu ana imani yake, lakini tusifike mahali tukaongoza nchi kwa uchawi."

Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumkemea Sheikh Yahya kwa kauli hiyo iliyotolewa juzi Dar es Salaam, la sivyo wananchi wataamini mnajimu huyo anatumiwa na CCM kuleta hofu katika jamii. Aliwakumbusha wananchi kuwa mwanzoni mwa mwaka huu, Sheikh Yahya alisema mtu yeyote atakayegombea urais na Kikwete, atakufa. Dk. Slaa alisema: "Sisi wengine ni majabali, hatuogopi."

Thursday, September 09, 2010

Nukuu ya Leo kutoka kwa Dk. Slaa



"Simamia, Dhibiti, Wajibisha."
Hii ni kauli nzito iliyotolewa na mgombea urais kupitia Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akisisitiza umuhimu wa uongozi unaowajibika na kuwajibisha, ili kuokoa raslimali za taifa na kuzielekeza katika huduma za jamii. Akasema anahitajika kiongozi anayeweza kufanya mambo hayo matatu, ili kuwezesha serikali kuokoa pesa na kuziingiza katika kulipia elimu na afya. Alitoa kauli hii mjini Ngudu, Mwanza, katika mkutano wake wa tano leo, mara baada ya kuwaeleza wananchi kuhusu sera za afya na elimu, kwamba zitalipiwa na serikali, na kwamba vyanzo vya mapato ya kulipia huduma hizo vipo, na kwamba serikali ya JK inashindwa kuyatekeleza hayo kwa sababu inaishi katika anasa. Meneo mengine aliyotembelea leo ni Itinge, Mwandoya, Hungumalwa na Mwamashimba.

Alizungumzia umuhimu wa serikali kufumua mikataba yote mibaya, hasa ya madini, inayopoteza mabilioni ya shilingi kila siku, ili kumpunguzia Mtanzania mateso yanayosababisha na uongozi usiojali wananchi. Amekuwa akisema kila mahali kuwa serikali ya sasa inakumbatia wawekezaji, inatelekeza wananchi.

Dk Slaa pia alizungumzia pia suala la mishahara ya wafanyakazi, akisema iwapo ataingia madarakani, ataiboresha kwa kufanya kima cha hini kiwe Sh 315,000; huku akiwaongezea marupurupu ma maslahi ya nyongeza katika huduma za ujenzi wa makazi bora na bima za afya. Huku akiwakumbusha hongo iliyotolewa na JK mwezi uliopita kwa kuwaingizia wafanyakazi nyongeza katika mishahara, kinyume cha bajeti iliyopitishwa na Bunge, Dk. Slaa alisema hawataiona nyongeza hiyo baada ya uchaguzi kwa kuwa si rasmi. Alisema kwamba katika majibu ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa Chadema kuhusu pingamizi walilomwekea JK wakidai ameongeza mishahara kinyemela, hakuna mshahara wowote ulioongezwa rasmi, hivyo msajili akakosa kigezo cha kisheria cha kumtia JK hatiani. Lakini nyongeza hiyo ilikuwapo. Aliwakumbusha kuwa JK alikataa kura za wafanyakazi; akasema yeye (Slaa) anazitaka. Kuhusu pesa hizo zilizoongezwa kinyemera, alimalizia kwa nukuu nyingine muhimu, akiilekeza kwa wafanyakazi:
"Zimeingizwa sasa, baada ya uchaguzi hamzioni. Mlizoingiziwa...mmeliwa."

Wednesday, September 08, 2010

Slaa akata anga Usukumani

Leo Dk Willibrod Slaa ameingia mkoani Shinyanga kusaka kura za urais. Na Chopper yake imeanza kazi upya baada ya kufanyiwa matengenezo madogo kwa siku nne zilizopita. Habari nyingine baadaye.

Hii ndiyo Kauli ya First Lady wa Slaa

Kwa waliokuwa wanasubiri kauli ya First Lady wa Dk. Slaa, hasemi tena. Soma hiki hapa:

Josephine Mushumbusi, amezungumza kupitia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia ni wakili wa Dk Willibrod Slaa, Tundu Lissu, akaviambia vyombo vya habari kuhusu tuhuma zinazowakabili yeye na Dk. Slaa kuwa kwa mara nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimerejesha mfumo wa uchaguzi unaobadilishwa kuwa mfumo ya kijinga (a silly season). Akasema kwamba CCM wamekuwa wakikishambulia Chadema kuwa ni chama Wachagga; kwamba baadhi ya viongozi wake ndio walimuua Chacha Wangwe; na kwamba Dk Slaa ametumwa na kanisa Katoliki kugombea urais; lakini baada ya kuona hadithi hizo zimepuuzwa, sasa wameibuka na suala jipya na “ndoa za Dk. Slaa” wakidhani zitawasaidia kugeuza macho ya umma kutoka kwenye masuala muhimu ya wakati huu.

Akasema CCM hawataki Dk. Slaa na Chadema wajadili wizi, ubadhirifu wa fedha na mali za umma; hawataki wajadili wizi wa Sh. bilioni 772 zilizoibwa katika mwaka 2008/9 tu, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali; hawataki Chadema itaje majina ya wezi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT); hataki Chadema wajadili jinsi JK na rafiki zake, akina Edward Lowasaa, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na Rostam Azizi walivyofilisi taifa hili; hawataki Chadema ijadili madai halali ya wafanyakazi wa Tanzania na ahadi za ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’ CCM hawataki Chadema kijadili sera mbadala ambazo zinalenga kuwakomboa Watanzania kutoka lindi la umaskini.

Wanataka kulielekeza taifa zima katika kujadili masuala ya ‘chumbani’ kwa Dk. Slaa; analala na nani, ana wake wangapi, kawapata wapi na kadhalika; ili kwa kufanya hivyo mgombea wao awarubuni wananchi kwa ziara mikoani na ahadi kemkem zisizotekelezeka.

Tundu Lissu amesisitiza kuwa kila wanapoona wamebanwa, CCM huwa wanabuni njama za kukomoa washindani wao, kama walivyofanya huko nyuma. Alitoa mifano ya kilichotokea miaka ya 1995 na 2005.

Mwaka 1995: Kwa kumwogopa Mrema aliyekuwa tishio kwa CCM, walimtumia mwanamke mmoja, aitwaye Angelina, wakidai ni kimada aliyezaa na Mrema; akawa analala getini kwa Mrema, Masaki, Dar es Salaam. Wakamdhalilisha. Baada ya uchaguzi, Mrema akashindwa, na suala la Angelina halikujadiliwa tena.

Mwaka 2005 tishio la CCM ilikuwa Chama cha Wananchi (CUF), hasa Zanzibar. CCM wakamtumia Inspekta Jenerali wa Polisi, Omar Mahita, siku chache kabla ya uchaguzi, kudai kuwa amekamata lori lenye mapanga, majambia, visu na silaha nyingine zenye nembo ya CUF. Wakakipaka chama matope. Baada ya uchaguzi, hatukuelezwa lolote kuhusu visu hivyo.

Mwaka huo huo, katika uchaguzi wa ndani ya chama, baada ya kundi la JK kuona limezidiwa mno, likaamua kumzushia Dk. Salim Ahmed Salim likidai ni Mwarabu, na muuaji wa Rais Abeid Amani Karume. Wakamhujumu, Na baada ya uchaguzi hawakuzungumzia tena uarabu wa Dk. Salim.

Mwaka 2010: Tishio la CCM ni Chadema na Dk. Slaa. Baada ya kuona upepo unawaendea vibaya, CCM wameamua kufanya siasa za mtaro wa maji taka; hizi wanazotumia watu kumwandama Dk Slaa.

Tundu Lissu alisema kuwa Chadema hawako tayari kufanya siasa za majitaka; na kwamba Watanzania hawako katika kujadili mambo hayo, kama hali ya afya za wagombea, ambao baadhi wanadaiwa kuwa na virusi vya ukimwi kiasi cha kubadili damu kila baada ya miezi, na kwamba kwa sababu ya unyonge huo, baadhi yao waanguka mara kadhaa jukwaani.

Akasema wao hawatazungumzia baadhi ya wagombea urais wana wake wangapi, mahawara wangapi, na wamewaweka katika ofisi gani za umma, wapi wamepewa mikataba minono ya fedha kwa upendeleo, na kadhalika. Akasisitiza kwamba Chadema haitajibu uchafu unaosambazwa na vyombo vya habari, lakini akasema, “sauti yetu itasikika iwapo wataenda mahakamani.”

Akasema Chadema itazungumzia umaskini wa Watanzania na namna ya kuupunguza au kuuondoa; jinsi Tanzania ilivyo nchi ya tatu katika Afrika lakini wanakijiji wanalazimishwa kujenga shule za kata huku serikali ikifuja mabilioni ya pesa (kama hizo bilioni 772/- zilizotafunwa ndani ya mwaka mmoja.

Akasema Chadema itajadili malipo ya anasa kwa mawaziri, maisha duni ya polisi, walimu, wauguzi na makundi mengine yanayonyonywa katika jamii. Akasema Chadema itajadili jinsi ya kuboresha afya za wananchi.


Akasema, “hatutaki siasa za chumbani, bali za hadharani.”

Kwanini wamshambulie Dk Slaa? Kwa sababu ni Dk. Slaa.

- Ana rekodi ya kuwashinda CCM mara tatu, kwa miaka 15 mfululizo
- Amekuwa sauti kuu ya wananchi Bungeni, inayotetea masilahi ya umma
- Kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kuwapo Tanzania ndani ya miaka 50, ni Dk Slaa pekee aliyetaja hadharani mafisadi 11 bla woga wowote. Walioathirika kwa ujasiri wake ndio hao wanaomsakama sasa kwa mambo ya chumbani badala ya mambo ya hadharani.

Monday, September 06, 2010

JK hawezi kushinda bila njama chafu?

SIJUI kwa nini JK na wapambe wake hawajifunzi. Mwaka 2005 walilazimika kumwita Dk Salim Ahmed Salim "mwarabu na muuaji wa Rais Karume." Naamini laana ya Dk. Salim imekuwa inamwandama JK kwa miaka yote minne. Na sasa baada ya kuona upepo mkali dhidi ya JK, na kama vile hawana uwezo wa kujifunza, wameanza kumshambulia binafsi, Dk Slaa. Lakini kwa bahati mbaya, aina hii ya mashambulizi itakapogeuzwa na kuelekezwa kwa JK, watakuwa wamemmaliza mtu wao. Najiuliza: Hivi JK amechoka kiasi hicho?

Sunday, September 05, 2010

Slaa ataka Watanzania wapate 'Slaa' mwingine Bungeni


Mgombea urais kupitia Chadema Dk. Willibrod Slaa amewataka wananchi wa Singida Mashariki kumchagua Tundu Lissu kuwa mbunge wao, ili kuziba pengo lake (Slaa) ambaye baadhi ya wananchi wamekuwa wakimlilia kwamba angebaki Bungeni kuwatetea. Dk Slaa alisema Tundu ni kiongozi jasiri, ambaye iwapo atakuwa katika Bunge na Halmashauri atatetea maslahi ya wananchi wote, kama alivyofanya Dk. Slaa kwa miaka 15 mfululizo. Dk. Slaa alisema hayo wakati akimnadi Lissu katika mikutano ya hadhara jimboni mwake, kwenye maeneo ya Makiungu, Dung'unyi, Ntuntu na Mang'onyi mkoani Singida.

Saturday, September 04, 2010

Tendwa aalikwa Ikulu kuteta na JK


MSAJILI wa Vyama Vya Siasa, John Tendwa, ameonekana Ikulu. Alikwenda kukutana na Rais Jakaya Kikwete Alhamisi majira ya saa 9.00 alasiri. Wachunguzi wa mambo wanasema wito wa Tendwa Ikulu una uhusiano na pingamizi la Chadema dhidi ya JK, ambalo limeikalia vibaya CCM, na linatarajiwa kutolewa jibu na Tendwa Jumatatu keshokutwa. Kama haki itatendeka au la, ni jambo jingine; na matokeo yake yatajulikana hapo baadaye. Je, yawezekana Tendwa anajipalia mkaa? Kama hakutarajia, sasa hana ujanja. Tumeshajua!

Friday, September 03, 2010

Dk. Slaa aiteka Manyara



Dk. Slaa ameiteka Manyara. Na wananchi wa Manyara wamemteka pia. Ilikuwaje? Kwanza, walijaa katika mikutano yake katika majimbo ya Hanang na Mbulu. Pili, walizuia misafara yake kokote alikopita wakitaka awahutubie, walau kwa dakika moja tu! Tatu, walimwahidi kufanya mabadiliko makubwa mwaka huu kwa kuchagua wabunge na madiwani wa Chadema, ili kukifanya CCM kuwa chama cha upinzani. Kipya ni kwamba alitumia usafiri wa Kipanya (Hiace) badala ya helikopta kutoka Babati hadi Mbulu, kwa sababu helikopta ilipata hitilafu kidogo jana Jumatano mara baada ya kutua mjini Babati ikitokea eneo la Bashnet. Katika picha ya kwanza, ni umati ulijitokeza kumlaki Dk. Slaa katika eneo la Haydom, jimboni Mbulu; na katika picha ya pili Dk Slaa anamtambulisha mgombea ubunge wa Hanang, Rose Kamili, katika eneo la Endosak, jirani na nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Thursday, September 02, 2010

Slaa amrudi Makamba


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema kuwa vigogo wa CCM hawana ubavu wa kumnyooshea kidole kuhusu maisha yake binafsi. Akihutubia wananchi katika mji wa Babati, mkoani Manyara, Dk. Slaa alisema iwapo wataendelea kuacha masuala ya kitaifa na kujihusisha na maisha yake binafsi, naye atawavaa na kuwavua nguo mmoja baada ya mwingine, kwani anawajua. Na kwa kuanzia, alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, awaeleze Watanzania kwa nini alifukuzwa ualimu wa shule ya msingi. Dk. Slaa alisema yeye hakufukuzwa upadri, kama Makamba anavyodai; bali aliamua kuacha kwa kufuata sheria za kanisa, na akapewa kibali kutoka Vatican kinachomruhusu kuwa mlei na kuoa. Alisema iwapo Makamba atadanganya wananchi kuhusu kilichosababisha afukuzwe ualimu, Dk. Slaa atamuumbua. Habari za uhakika zinasema Makamba alifukuzwa ualimu (mkuu) wa shule kwa kosa la kumbaka na kumpa mimba mtoto wa shule.

Naye Mkuu wa msafara wa Dk. Slaa, Suzan Kiwanga, alimtolea uvivu mke wa rais, Salma Kikwete, akisema anatumia pesa za umma kuzunguka nchi nzima anafanya kampeni huku akijua kuwa hatambuliki katika ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kauli ya Kiwanga iliongezewa uzito na Dk. Slaa aliyesema: "Nchi hii ina rais mmoja, ni Kikwete. Mke wa rais si rais. Anatembea kwa msafara wa magari 21 huku akilindwa na kupewa heshima zote na viongozi wa serikali; kama nani? Na raisi mwenyewe atatumia magari mangapi? Lakini hii yote ni matumizi mabaya ya kodi za wananchi, na huu ni ufisadi," alisema huku akishangiliwa na umati uliokusanyika katika uwanja wa Kwaraha mjini babati.

Ilisemekana kwamba, asubuhi ya leo, kabla ya mkutano wa Dk. Slaa, Salma alitaka kuuteka uwanja huo na kuutumia kwa mikutano yake ya hadhara, lakini wananchi wa Babati wafuasi wa Chadema walimtolea macho na kumfukuza uwanjani hapo. Hali hii ndiyo ilisababisha kauli ya Kiwanga, ambaye alisema: "Laiti ningemkuta hapa, sementi hii (sakafu) ingegeuka vumbi." Akasisitiza kwamba kama Salma angekuwa anataka kufanya siasa, angechukua fomu agombee urais kama mumewe ili apate fursa ya kuzurura na kufanya mikutano. Lakini si vema kutumia pesa za Ikulu au za asasi yake ya WAMA kufanya siasa.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'