Thursday, August 19, 2010

Wagombea urais warejesha fomu


Dk. Slaa

CHDM

Chadema

CCM

CCM

CCM

CUF

CUF

CUF

TLP

APPT-Maendeleo

Dini ya Obama yaleta kizaazaa


Wamarekani sasa wamekumbwa na mjadala mpya juu ya dini ya Obama. Kwa vipi? Kwa nini? SOMA hapa.

Tuesday, August 17, 2010

Serikali yatisha Maswali Magumu

JANA niliitwa Ofisi ya Idara ya Habari (MAELEZO) na kuhojiwa, nikiwa na Mhariri Mtendaji, Absalom Kibanda, juu ya ukali wa makala za Maswali Magumu ya Agosti 8, 2010 na ya Agosti 15, 2010, ambayo kwa taarifa nilizonazo yaliikera Ikulu, nayo ikaisakama MAELEZO. Kikao hicho kilishirikisha Mkurugenzi wa Maelezo, Clementi Mshana; Mkurugenzi Msaidizi, Raphael Hokororo na ofisa wa maelezo aitwaye Jovina, aliyekuwa anaandika muhtasari wa mazungumzo yetu. Tulizungumza mengi, lakini katika yote, nakumbuka nukuu ya mmoja wa vigogo hao wa MAELEZO akisema: "Mashujaa wote hawako hai...".

Wednesday, August 11, 2010

Pweza afanya vitu vyake


Wabunifu wameshaanza kufanya vitu vyao kuelekea Uchaguzi Mkuu. Eti na pweza ameshatabiri!

Tuesday, August 10, 2010

Dk. Slaa alazwa


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amelazwa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili. Blogu hii ilizungumza na Dk Slaa hospitalini hapo, akasema alilazwa jana Jumatatu kwa ajili ya matibabu ya mkono wake uliovunjika mfupa wa juu ya kiwiko wiki moja iliyopita. Kwa maelezo yake, alishauriwa na daktari aliyemfunga 'mhogo' (POP) katika hospitali ya Bugando, Mwanza, kwamba alipaswa kurejea hospitali kwa uchunguzi mwanzoni mwa wiki hii. Alikwenda Muhimbili mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jana Jumanne.

Habari za kulazwa kwa Dk. Slaa zilipowafikia mashushushu wa CCM na marafiki wa mafisadi, zilipokelewa kwa hisia za kishabiki, hata baadhi yao wakadiriki kueneza uvumi kwamba Dk. Slaa yu mahututi. Mwenyewe alipozungumza na blogu hii kwa simu alisema: "Siko mahututi. Ni jambo la kawaida, nililazimika kurudi hospitali kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya ziada, ikiwa ni pamoja na kufungua POP."

Akiwa Muhimbili, Dk Slaa anaweza ama kufungwa POP jingine au kufanyiwa pia upasuaji mdogo ili kuwezesha mkono kupona haraka. Alisisitiza kwamba kulazwa kwake hakuathiri mchakato wa maandalizi ya kampeni zake; na kwamba alikuwa akifanya kazi kwenye kompyuta yake kama anavyoonekana kwenye picha hii, iliyopigwa na Joseph Senga leo Jumanne jioni katika wodi binafsi, F, hospitalini Muhimbili.

Friday, August 06, 2010

Lipumba achukua fomu za urais


Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) jana alichukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alisema anagombea urais ili kukuza mapambano dhidi ya mafisadi.

Michelle Obama kanogewa Ikulu?


Michelle Obama ameanza kunogewa manono ya Ikulu? Soma HAPA uone jinsi vyombo vya habari vinavyoanza kummulika na kumjadili.

Kikwete aogopa mdahalo tena

KAMA alivyofanya mwaka 2005, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameogopa mdahalo na wagombea urais wenzake kutoka vyama vya upinzani. Taarifa ya Kikwete kuogopa mdahalo huo ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba na Naibu Mkuu wa Kitengo cha propaganda wa CCM, Tambwe Hiza, jana Agosti 05/08/2010, Dar es Salaam. Kikwete anakimbia mdahalo huo wakati maandalizi yakiendelea, huku mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Lipumba na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibrod Slaa wakisisitiza kuwa wanataka mdahalo huo ili wananchi wawapime kwa hoja. Hata hivyo, kukimbia kwa Kikwete hakutazuia mdahalo kuendelea. Wenzake watapewa fursa hiyo adhimu, na iwapo watamjadili in absentia atakuwa amepoteza fursa muhimu sana ya kujenga hoja na kujitetea kwa hoja zinazoelekezwa kwake na chama chake. Mwaka jana, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown wa Uingereza alianza kwa kukataa kushiriki mdahalo (ambao ulifanyika mwaka huu), lakini baadaye alikubali na kushiriki, na alifanya vizuri, ingawa hatimaye hakushinda uchaguzi. Lakini kwa jinsi washindi (Conservative) walivyokosa kura za kutosha kuunda serikali peke yao kama walivyotarajiwa, ni ishara kwamba mdahalo na utendaji wake waktia masuala mengine, hasa uchumi, vilimwinua Brown, akaungwa mkono na sehmu kubwa ya umma uliokuwa unambeza awali. Je, Kikwete ataendelea kuogopa na kupoteza fursa hii?

Dk. Slaa afunika Moshi


Sehemu ya umati wa wakazi wa mji wa Moshi, wakisikiliza hotuba ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa (hayupo pichani), wakati wa mkutano wa kuomba udhamini, kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010. (Picha zote na Joseph Senga)


Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, akihutubia katika mkutano wake wa hadhara wa kuomba kudhaminiwa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010.


Mwenyekiti wa CHADEMA), Freeman Mbowe, akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi, katika mkutano wa hadhara wa kuomba udhamini wa mgombea urais wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010.


Msafara wa mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, ukipita katikati ya mji wa Moshi, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa ndege mjini humo, ambako alihutubia mkutano wa hadhara wa kuomba kudhaminiwa, kwenye Uwanja wa Manyema jana, huku ukisindikizwa na helikopta (juu) 05/08/2010.


Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Said Arfi, akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi na vitongoji vyake, katika mkutano wa hadhara wa kuomba udhamini kwa mgombea urais kupitia chama hicho, kwenye Uwanja wa Manyema 05/08/2010.

Wednesday, August 04, 2010

Dk Slaa mjini Mtwara na Songea

Dk. Willibrod Slaa katika msafara uliompokea mjini Songea (04/08/2010)

Dk. Slaa akihutubia wananchi mjini Songea (04/08/2010)

Dk. Slaa, akihutubia wananchi na kuomba udhamini mjini Mtwara (04/08/2010)

Tuesday, August 03, 2010

Dk. Slaa aiteka Mbeya




Picha hizi mbili zinaonyesha sehemu tu ya umati wa wakazi wa Mbeya mjini uliompokea Dk.Willibrod Slaa kumdhamini ili agombee urais 2010 kupitia Chadema (03/08/2010)

Monday, August 02, 2010

Dk. Slaa mgombea urais Chadema 2010



Huyu ndiye Dk. Willibrod Slaa, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Friday, July 09, 2010

Dk. Shein apeta

CCM Zanzibar wamepata mgombea urais. Matokeo ya kura za NEC Dodoma yanasema hivi: Shein 117: Bilal 54: Nahodha 33.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya vikao vya CCM zinasema Dk. Bilali alipata kura 119 kutoka wa wajumbe. Akafuatiwa na Dk. Shein (63) na Nahodha (22). Hayo ndiyo maajabu ya CCM, ma ndiyo maana Wazanzibari hawakosi kulalamikia kitendo cha rais wao kuchaguliwa Dodoma badala ya Zanzibar. Na hivi ndivyo Dk. Bilali alivyozibwa mdomo kwa kupewa nafasi asiyoitaka ya kuwa mgombea mwenza wa JK.

Wednesday, July 07, 2010

URAIS Z'BAR: Dk. Shein akamiwa


BAADHI ya wanaCCM Zanzibar waliopo Dodoma wametishia kumburuza mahakamani Dk. Mohammed Gharib Shein na kuzuia uchaguzi iwapo chama kitampitisha kugombea urais. Wengine walio Zanzibar wanaendelea kusambaza vipeperushi vinavyokihamasisha Chama cha Wananchi (CUF) kijiandae kuingia madarakani ikiwa Dk. Shein atapitishwa kugombea urais. Wanadai Shein si chaguo la Wazanzibari, bali la vigogo wa Bara na Rais Amani Karume. Na baadhi yao wananukuu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kuthibitisha kwamba Dk. Shein "amepoteza sifa" ya kugombea urais kwa kuwa amejiandikisha kupiga kura Bara. Ama kweli wamemkamia.

Sunday, July 04, 2010

Mdahalo wa wagombea urais Zanzibar

Taasisi huru ya habari nchini, Vox Media Centre Ltd, kwa kushirikiana na kituo cha Televisheni cha Star Tv, jana Jumapili, Julai 4, 2010ilifanya mdahalo kwa wagombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Hoteli ya Ocean View Hotel, saa 3.30 asubuhi hadi 7.00 mchana. Mdahalo huo, ambao ni wa kwanza katika historia ya siasa za Zanzibar, utarushwa na kituo cha Star Tv baadaye katika wakati utakaotangazwa baadaye mwanzoni mwa wiki hii. Wanahabari wengi za Zanzibar walishiriki, na kituo cha redio cha HITS FM kilirusha moja kwa moja matangazo ya mdahalo huo. Huu ni wa kwanza katika mlolongo wa midahalo ya kisiasa inayotarajiwa kufanyika mwaka huu kuelekea Oktoba 2010. Star Tv watarusha mdahalo huo Jumatano saa 4.30 - 5.30 usiku.

Tuesday, June 29, 2010

Raila Odinga apasuliwa kichwa

SOMA habari zake hapa.

Urafiki huu ni wa kweli?




Ama kweli, swala huyu ana bahati isiyo ya kawaida ya "kupendwa" na chui!

Friday, June 25, 2010

Ya Italia na Ufaransa


Mtu mmoja ameandika katika tovuti ya BBC, akizungumzia timu za Italia na Ufaransa, na kulinganisha nguvu ya timu hizo katika fainali mbili. Anasema:"Inashangaza kidogo kwamba katika fainali za 2006, Italia na Ufaransa walikutana uwanjani katika mechi ya mwisho ya fainali; katika fainali za mwaka 2010, timu hizo hizo zimekutana uwanja wa ndege" (wakiwa safarini kurejea makwao baada ya wote wawili kutolewa katika hatua ya awali).

Monday, June 21, 2010

Siasa za JK na mwanaye

RAIS Jakaya Kikwete amemkabidhi mtoto wake Ridhiwani, fomu za kumuombea wadhamini 250 kwa mikoa 10 nchini ili kutimiza vigezo vya kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM. Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika nyumbani kwake mjini hapa ambapo zaidi ya vijana 40 watakaoongozwa na Ridhiwani walihudhuria. Mtoto huyo wa rais Kikwete, amechaguliwa kuwa kiongozi wa vijana katika kuhakikisha mgombea huyo anapata wadhamini wa kutosha kwa mujibu wa sheria na kanuni za CCM.

Kwa habari zaidi soma magazeti. Mzee wa Maswali Magumu amelijadili hili kwa kifupi.

The best thing: Brazil is winning


Nimefurahishwa na jinsi jamaa huyu alivyoripoti stori ya mechi kati ya Brazil na Ivory Coast.

Saturday, June 12, 2010

Saa mbili za Maradona


SOMA hapa ujue kwa nini Kocha wa Timu ya Taifa (Soka) ya Argentina, Diego Maradona, anapenda kuvaa saa mbili - moja kila mkono.

Wednesday, June 09, 2010

'Kichwa cha Zidane' chatukuzwa


Tazama wenzio wanavyokitumia kutangaza biashara zao na kuvuna mapesa. PICHA YA KWANZA PICHA YA PILI. PICHA YA TATU.

Thursday, June 03, 2010

Ziro ya Sumaye na Ombwe la Kikwete, kipi bora?

SOMA mjadala mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010. Usikose pia kusoma ONYO hili kwa Watanzania. Linakuhusu. Katika kuendeleza mjadala, Mtanzania mwingine amemtaka Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, aokoe jahazi. Kwa vipi? Soma HAPA.

Wednesday, May 12, 2010

Waingereza wapata serikali mpya

Mseto huu waweza kuwa bora kuliko miseto ya Kenya na Zimbabwe? Fuatilia muundo wa serikali mpya inayoongozwa na David Cameron.

Friday, April 23, 2010

Uchaguzi Mkuu: Mdahalo wa wanasiasa Uingereza

Watazame, wasikilize na watathmini wanasiasa hawa wanaogombea ukubwa wakijieleza katika mdahalo wao wa pili. Ni David Cameron (Conservative), Gordon Brown (Labour) na Nick Clegg (Lib Dem).

Tuesday, April 20, 2010

Mourinho haishiwi hoja kwa waandishi

Wakati Inter Milan na Barcelona zikijiandaa kuchuana katika ngwe ya kwanza ya nusu fainali, Kocha wa Inter, Jose Mourinho, amezungumza na waandishi kwa kujiamini. Msome hapa.. Na baada ya kuifunga Barcelona, aliwasifu vijana wake na kuwaponda washindani, lakini akaonya kuwa safari ya kuelekea Madrid bado ndefu. Naye Rais wa Klabu, Massimo Moratti, aliwasifu Inter, akammwagia sifa kocha, akisema: "wanatisha."

Thursday, April 08, 2010

Mgeni mwingine


Wageni bado wapo. Huyu ninayezungumza naye ni Maria Drantenberg, raia wa Norway, ambaye alinitembelea ofisini kwangu (06.Aprili.2010) kujadili hali na maendeleo ya vyombo vya habari na demokrasia Tanzania.

Wednesday, March 31, 2010

Kigogo wa kwanza CCM ajiunga CCJ


Ni Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe, ambaye amevijua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwa mantiki hiyo, kujivua ubunge. Ameandika historia. Na habari zinasema kuwa vigogo wengine wanajiandaa kumfuata. Tusubiri tuone.

Thursday, March 18, 2010

Tunajadili utendaji wa vyombo vya habari


Katika picha hii, nafafanua jambo kwa mgeni wangu Anni Lyngskaer, raia wa Denmark aliyenitembelea ofisini kwangu, kujadili utendaji wa vyombo vya habari nchini. (Picha kwa hisani ya Francis Dande Machi 17, 2010)

Monday, March 15, 2010

Wakaukosa mpira, wakatwangana wenyewe

Watatu wanamkaba mmoja kwa kuwa alikuwa anatisha! Mshambuliaji mahiri wa Salehe Mohammed wa Free Media FC (mwenye njano) akikabiliana na mabeki wa Mwananchi FC. 13.03.2010, Uwanja wa Sigara, Dsm.

Huu ndiyo mwisho wa Beckham kucheza soka?

Fuatilia uchambuzi huu.

Hata kabumbu twasakata


Mnamzungumzia Drogba? Wapo wengine, hata kama hawavumi! Siku zinasogea, lakini stamina haijapotea kabisa. Anza na hiyo. Nyingine zitafuata za Machi 13, 2010 (Free Media vs Mwananchi). Tulifungana idadi hii ya magoli. Wengine tuliacha vipande vya miguu uwanjani.

Tuesday, March 02, 2010

Thursday, February 18, 2010

Wabunge wetu vibogoyo

Nani amewang'oa meno wabunge wetu? Na tukilinganisha wabunge bubu na vibogoyo, nani zaidi?

Sunday, February 07, 2010

Wamerekani wanataka nini Tanzania?

SIFA hizi wanazotumwagia ni za nini? Nadhani wana lao jambo.

Mbaya kwa wanaotaka kusomea Uingereza

Waingereza wanaendelea kutufungia mipaka kwa kuweka masharti magumu zaidi dhidi ya wanaotaka kusomea Uingereza. Ipate hapa.

Wednesday, February 03, 2010

Misri katika 10 bora za Fifa

Soma hapa upate pia zilizopanda na zilizoshuka Afrika.

Saturday, January 30, 2010

Ngoma ya Dodoma ichezewe Unguja?

Dare s Salaam

WANAOTILIA shaka hoja yetu ya muda mrefu kuwa Tanzania inakabiliwa na ombwe la uongozi, watazame kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.

Chama tawala kinaendelea kumeguka. Mwenyekiti hajui aunge mkono kundi gani katika mmeguko huo.

Anaitisha vikao vikuu vya chama, wasaidizi wake wanamgomea, naye anaviahirisha. Wabunge wa chama tawala wanamgomea Waziri Mkuu (mwenyekiti wao) wakipinga muswada wa gharama za uchaguzi. Chama tawala kinaweweseka na kutishwa na “chama hewa” cha CCJ, ambacho kimekwua gumzo nchi nzima kwa wiki nzima, ingawa hakijasajiliwa.

Hiki ni chama ambacho kimekufa kabla ya kuzaliwa, maana wenye chama chao wamekosa ujasiri wa kujitambulisha na chama chao. Wamekikana.

Lakini CCM imekiogopa mno kiasi cha kusambaza waraka nchi nzima kuwaonya wanachama wake dhidi ya CCJ; huku ikijua ifika kuwa wanachama wa CCJ ndio hao hao wa CCM!

Chama imara, chenye uongozi imara, kisingepata kizunguzungu kwa hisia za kuundwa kwa chama kingine. Lakini CCM kimetudhihirishia kwamba nguvu pekee inayokipa uhai ni dola.

CCM bila dola – bila majeshi, bila tume za uchaguzi, bila serikali na taasisi nyingine zinazokitegemeza – hakipo.

Yanayokitikisa CCM ni mengi, hata nguvu ya chama chenyewe upande wa Zanzibar, ambayo sasa imeakisi nguvu halisi ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Rais Karume ametunisha msuli, CCM (Bara) imenywea; Serikali ya Muungano imenyong’onyea. Na kwa hali ya kisiasa ya sasa nchini, tunaweza kusema kwamba walau sasa Karume ameonyesha maana ya kuwa rais wa nchi.

Rais wa nchi ni yule anayesimama kidete kutetea kwa nguvu zote masilahi ya watu wake, hata ikibidi atofautiane na wenzake.

Rais Karume ameona bora kutofautiana na viongozi wenzake wa Muungano, iwapo kwa kufanya hivyo, ataweza kutetea maslahi ya kile kinachomfanya aitwe rais.

Katika miezi miwili iliyopita, Karume amekuwa na utambuzi wa ajabu wa nguvu na umuhimu wake katika siasa za Tanzania. Amekohoa, wenzake wa Bara wamepata mafua!

Ameamua kuwa muasi. Sasa wao wanamuita msaliti. Lakini hakuanza leo. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa usaliti wa Karume ulianzia Butiama, mwanzoni mwa mwaka 2008, alipoathiri mwelekeo wa hoja ya serikali ya mseto Zanzibar; akapendekeza isitekelezwe bila kura ya maoni.

CCM, ambayo ilikuwa imeshaafikiana na Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kamati ya mwafaka, kwamba iwepo serikali ya mseto Zanzibar, ilinywea na kuimba wimbo wa Karume.

Kwa hiyo hata sasa hivi, (wapinzani wa Karume) wanapojitapa kwamba wanafuata maazimio ya Butiama, ukweli ni kwamba wanafuata mapendekezo ya Karume. Na yeye anayasisitiza maazimio hayo kwa sababu ni zao la maoni yake. Hajapoteza!

Bahati mbaya Karume alichelewa kutambua nguvu yake. Siku zote alijiona yeye ni makamu mwenyekiti wa CCM, Visiwani. Alisahau kwamba yeye ni rais, kiongozi wa nchi.

Wengine tunadhani kwamba kilichomfanya awe mnyonge ni mchakato wa kisiasa uliomfikisha Ikulu. Haukuwa mchakato sahihi, wala haukuwa huru na wa haki. Alijua kuna walioshinda na waliotawala. Yeye alikuwa kwenye kundi la watawala, lakini hakuwa katika kundi la washindi.

Imemchukua miaka tisa (9) kujiamini na kutumia urais wake kutetea Wazanzibari. Katika miaka tisa iliyopita, ngoma ilikuwa inapigwa Dodoma, Karume anaichezea Zanzibar.

Sasa ameshtuka. Ameamua ngoma ya Wazanzibari ipigwe na kuchezewa Unguja! Ametuma ujumbe mzito kwa CCM na serikali. Wenye akili wameshaupokea; kwamba si haki na si sahihi kwa CCM kumchukulia Karume kama wanavyomchukulia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Pius Msekwa, au Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

CCM (Muungano) ilipoandaa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu Wazanzibari wakagoma ikaahirisha, na baadaye ikaandaa kikao cha dharura Karume na wenzake wakagoma kuhudhuria, ikaahirisha tena; imedhihirisha kwamba haiwezi kwenda bila nguvu ya Karume.

Sisi siri kwamba kama Karume angehudhuria vikao hivyo, wenzake wa Bara wangevitumia (kwa wingi wao na ubabe wa kihistoria) kumbana na kumwadabisha.

Kwa hatua yake ya sasa, ya kuwagomea na kuitisha kikao maalumu huko Zanzibar, amethibitisha kwamba ana uwezo wa kuzichonga siasa za Zanzibar zikawa tofauti na jinsi ambavyo wenzake wasio Wazanzibari wanataka ziwe.

Amewafungua macho wana CCM wenzake wa Zanzibar kwamba wakiamua, wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika taifa lao. Sasa wametambua, na wamedhihirisha kwamba wao si mkoa ndani ya Tanzania, bali ni taifa ndani ya taifa.

Wana serikali yao; katiba yao; bendera yao; Bunge (Baraza la Wawakilishi) lao; tume yao ya uchaguzi; wimbo wao wa taifa.

Utaifa huu wa Zanzibar ndiyo uliowafanya Karume na hasimu wake mkuu kisiasa, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kukutana na kujadili mustakabali wa taifa lao.

Kwa Karume na Maalim Seif, Uzanzibari wao ni muhimu kuliko Utanzania wao. Imesemwa mara nyingi, na sasa wao wamethibitisha, kwamba linapofika suala la maslahi ya Zanzibar, CUF na CCM ni kitu kimoja.

Kwao, maendeleo ya Zanzibar, kwa muda mrefu, yameathiriwa na kile wanachokiita “ukoloni wa Bara.” Hawa ni watu wanaopigana kujinasua kwenye “ukoloni” wa Serikali ya Muungano.

Ndiyo maana Karume na Maalim Seif wameungana sasa. Kwao, Zanzibar kwanza; Tanzania baadaye.

Si hilo tu, lakini pia wanazingatia ukweli kuwa Wazanzibari wasipoamua kushughulikia matatizo yao wenyewe, wakiamua kuwaachia wabara wayamalize kwa niaba yao, hayatakoma.

Wamechoka kuendesha siasa za Zanzibar kutoka Dodoma; maana wanaweza kufanya hivyo wakiwa Unguja.

Rais Karume aliingia madarakani kwa nguvu, jeuri na aibu. Sasa anajiandaa kuondoka madarakani kwa heshima na utukufu uliowashinda watangulizi wake.

Watafiti na wachambuzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar wanajua na wamesema mara kadhaa kwamba Rais Karume aliupata urais wake bila ushindi utokanao na wingi wa kura halali.

Sasa amepata ushindi dhidi ya nguvu kongwe za CCM zitokazo katika Serikali ya Muungano (Bara), na ameanza kushinda hila za wasaidizi wake na washindani wake wa Zanzibar wanaohaha kumrithi baadaye mwaka huu.

Karume huyu hawezi kuendeshwa kwa maazimio yanayotokana na ushawishi au nguvu ya hoja za akina Msekwa au Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba. Kwake, hawa nao ni sehemu ya “wakoloni” hao wa Muungano.

Ndiyo maana wanaojua siasa za Zanzibar wanakiri kwamba kama Karume asingekuwa nyuma ya ajenda ya CUF kutaka katiba irekebishwe, kuanzishwe serikali ya mseto na mchakato huo usimamiwe na Karume mwenyewe, wana CCM katika Baraza la Wawakilishi wasingeunga mkono hoja ya chama hicho cha upinzani.

Na kama kuna ujumbe CCM inapaswa kuupata kutoka kwenye uamuzi wa baraza kuridhia hoja ya CUF ni mmoja – kwamba umma wa Wazanzibari sasa unaandaliwa kwa kura ya maoni itakayokuwa kama watakavyo watawala.

Ndiyo maana baadhi yetu tunaiona serikali ya mseto Zanzibar inakuja. Ndiyo tafsiri ya kauli ya Karume kwamba rais kutoka Pemba si dhambi. Ndiyo maana naye sasa ana ujasiri wa kuimba wimbo ule ule wa wapinzani, wa muda mrefu, kuwa mafuta ya Zanzibar (kama yapo) yasiwe suala la Muungano.

Wala hatulalamiki, maana huu ni uamuzi uliochelewa. Zanzibar yenye amani haiwezi kuongozwa kwa siasa za ubabe, jeuri, vinyongo na visasi. Wala haiwezi kuwa chini ya chama kimoja tu, maana hata wanaotangazwa kuwa wameshindwa wanakuwa na karibu nusu ya kura zote zilizopigwa.

Lakini kuna jambo ambalo CUF wanalisisitiza; kwamba baada ya miaka 10 madarakani, Rais Karume hana tena uchu wa madaraka. Amekua, ameongoka na yuko tayari kutambua na kutimiza matakwa ya Wazanzibari.

Yupo tayari kuwaunganisha Wazanzibari na kustaafu kwa mbwembwe. Anatafuta ushujaa ambao rais yeyoye mpya atakayeingia madarakani angependa kuutafuta baada ya miaka 10 Ikulu.

Kwa hiyo, ni vema Karume anayemaliza na mwenye nia, apewe fursa (ya walau miezi 6 hadi miaka miwili) asimamie utekelezaji wa makubaliano yake na Maalim Seif.

Katiba irekebishwe, sheria za uchaguzi zirekebishwe, tume ya uchaguzi irekebishwe, wapiga kura wandikishwe upya (vema) na kadhalika. Baada ya hapo, uitishwe uchaguzi huru na wa haki; atakayeshinda amkaribishe aliyeshindwa (maana itakuwa kwa asilimia ndogo tu) waunde serikali ya mseto.

Mwisho wa yote, Karume atastaafu kama shujaa; na Wazanzibari watakuwa wameanza siasa mpya za ushindani usio na uhasama. Nani asiyeitaka Zanzibar ya namna hii?

Ni wazi, wapo baadhi wanaonufaika na siasa za Zanzibar kwa jinsi zilivyo leo. Wapo pia wanaojiandaa kugombea urais baada ya Karume, na wasingependa kuendeleza urithi wa Karume na Maalim Seif.

Kete yao ni moja. Iwapo Karume ataondoka bila kuyaingiza kwenye mfumo mazungumzo yake na Maalim Seif, yatafutika siku ya kwanza ya utawala mpya, naye ataishi maisha ya kula pensheni ya aibu.

Hadi sasa, Karume, kwa hiki kidogo alichofanya, amekuwa shujaa mbele ya Watanzania wengi. Amefuta aibu ya muda mrefu, na amevaa ujasiri wa ajabu unaojitokeza kwa sura ya uasi na usaliti.

Akitaka kuupoteza ushujaa wake huu, alegeze kamba, apoteze nia, awasikilize wanaomsonga kutoka Bara na visiwani. Aatapoteza ushujaa na heshima yake binafsi, na ataitokomeza amani ya Zanzibar ambayo sasa iameanza kuchanua.

Wakristo wanaamini kwamba kama Yuda asingemsaliti Yesu, kile wanachokiita ukombozi wao kisingepatikana. Yawezekana Karume pia amegundua kwamba asipomsaliti Rais Jakaya Kikwete na CCM yake, ukombozi wa Wazanzibari hautapatikana.

Kwa nini asiasi kama amegundua kuwa wakubwa hawana nia njema na Zanzibar? Na kama tunataka ukombozi wa Zanzibar, kwa nini tusimsaidie Karume kuwadhibiti “wahuni” wa Bara wanaohaha kumzuai asiasi zaidi?

ansbertn@yahoo.com +255 653 172 665

Saturday, December 19, 2009

Sindiketi za watawala

Maswali Magumu wiki hii: Baada ya miaka takribani 15 ya mtandao, baada ya kuonja madhara yake, sasa watawala wameunda sindiketi. Tuwasaidieje?

Thursday, December 17, 2009

Wakubwa waumbuliwa na vitu vidogo vidogo

Rais George W. Bush aliumbuliwa na mlango. Baadaye aliumbuliwa na kiatu. Gordon Brown na Al Gore waliumbuliwa na mlango.

Monday, December 14, 2009

Waitaliano wambonda Waziri Mkuu wao

Nilipoandika kujadili tukio la msafara wa Rais Jakaya Kikwete kurushiwa mawe mkoani Mbeya, mwandishi mmoja aliandika kunijibu akisema, 'Ansbert, rais hapigwi mawe.' Hata hivyo, tayari rais alikuwa ameshapigwa mawe! Lakini wakati ule sikujua pia kwamba wapo wenzetu ambao wameshavuka enzi za mawe, sasa wanarusha hata makonde kwa 'marais' wao. Tazama Waitaliano walimvyomtwanga na kumtoa damu Waziri Mkuu wao, Silvio Berlusconi. Nadhani dunia ya kisiasa inabadilika kwa kasi ya ajabu!

Monday, December 07, 2009

Kwanini tuchague jiwe?

Imerudiwa kutoka Desemba 23, 2007.

Sunday, November 29, 2009

Sunday, November 22, 2009

Chafya ya Rais Mkapa

Ole wao Mkapa akipiga chafya!

Sunday, November 01, 2009

Pinda kaishitaki Ikulu; wabunge wataishinda?


WIKI hii Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameichongea Ikulu kwa Watanzania - bila kujua. Kauli yake kwamba Ikulu ndiyo imeiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) iwahoji wabunge kwa kile kinachoitwa 'posho mbili,' inazua maswali ya msingi juu ya nia ya Ikulu kubuni hila za kuua mjadala wa kitaifa juu ya serikali na Richmond.

Ni kielelezo cha uwezo mdogo wa serikali kimkakati kutumia TAKUKURU kuwaandama wabunge wale wale wanaoituhumu TAKUKURU hiyo hiyo. Taifa liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu na ufisadi wa watawala; maazimio ya Bunge kuhusu Richmond hayajatekelezwa; taifa linasubiri taarifa ya serikali kuhusu suala hili, kumbe wao wanaleta utoto wa 'posho mbili' zao?

Nani amewaruhusu Ikulu na TAKUKURU kupachika ajenda dhaifu katika nafasi ya ajenda kuu? Nani amewaruhusu kuandama wabunge wale wale ambao katika mjadala wa kashfa ya Richmond ndio waliopendekeza kigogo wa TAKUKURU achukuliwe hatua?

Hivi mtu akikutuhumu na wewe ukamtuhumu unakuwa mtu safi kuliko yeye, na unapata nguvu ya kumchukulia hatua? Ikulu na TAKUKURU wanadhani njia sahihi ya kujisafisha ni kuwaandama wanaoituhumu TAKUKURU na Richmond yao?

TAKUKURU ambayo haikuona ufisadi wa Richmond kulipwa milioni 152 kwa siku, tena bila kuzalisha umeme; TAKUKURU ambayo haikujua suala la EPA hadi lilipoibuliwa Bungeni; TAKUKURU ambayo haikujua wizi wa Deep Green Finance: TAKUKURU iliyoshindwa kushughulikia ufisadi katika ununuzi wa rada na ndege ya rais; TAKUKURU iliyoshindwa kuona ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa Kiwira; TAKUKURU inayoshindwa kuchunguza upotevu wa mabilioni ya pesa za Watanzania katika miradi michafu ya vigogo (orodha ni ndefu), ndiyo hii inayoona uchungu wa shilingi 50,000 za posho ya wabunge?

Hata kama posho hizo zina utata, watu wenye akili na uchungu na taifa wanaweza kuruhusu suala hili lifunike mjadala wa ufisadi wa Richmond? Huu ndiyo uwezo na upeo wa Ikulu na TAKUKURU kulinda watu wasiozidi wanne na Richmond yao kwa kunyamazisha na kutisha wanaohoji ufisadi huo?

Watu hawa wanajua kuwa ipo siku wataondoka Ikulu au TAKUKURU? Wanajua kuwa kuna maisha baada ya hila zao hizi za kisiasa au wanadhani watafia katika ofisi hizo ili tusiwahoji? Baada ya Ikulu kulinda na kusaidia watuhumiwa wengine wa Richmond kustaafu kwa heshima, inaona hii ndiyo njia mwafaka ya kuiondoa TAKUKURU katika matope ya Richmond? Hivi wanadhani kwamba hata kama wabunge wakiogopa wakanyamaza, wakaacha kuihoji serikali juu ya Richmond, vigogo hawa wanakuwa watumishi safi mbele ya umma na dhamiri zao wenyewe?

Mkakati huu wa Ikulu na TAKUKURU si uhuni mwingine uliovuka mipaka kwa serikali inayoongozwa na wale wale waliotuambia majuzi kuwa hawana nia ya kuwaziba midomo wabunge? Tusikilize kauli zao au tutazame matendo yao?

Hivi serikali inadhani watu pekee wenye akili wako Ikulu na TAKUKURU, kiasi cha kutupangia ajenda dhaifu ndani ya ajenda kuu, na kutarajia sisi tufuate upepo wao wa kisiasa na kucheza ngoma yao 'isiyokesha?'

Kama huu ndiyo mtiririko wetu wa kufikiri, viko wapi vipaumbele vya kitaifa? Ni haki tupotoshwe na propaganda za Ikulu na TAKUKURU, tuanze kuwajadili na kuwazomea wabunge ambao wamegundua janja hii ya Ikulu na TAKUKURU, wakawa jasiri kugoma na kutoa kauli thabiti?

Ni lini taifa hili litaacha kulea na kuenzi ukondoo, likatukuza ushujaa hata kama ni wa wachache wanaoweza kuwaambia watawala "hapana?"

Katika wakati ambapo taifa zima liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu ya watawala hao hao, tuache kujadili athari za Richmond tujadili posho mbili za wabunge? Kama walikuwa na nia njema na suala hili si wangelitafutia nafasi yake baada ya kuturidhisha na utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu Richmond?

Mbona tunajua kuwa hata rais mwenyewe na mawaziri wake wanaposafiri mikoani na kwingine wanapewa takrima hizo hizo na wenyeji wao? Ni Ikulu na TAKUKURU ipi itamchunguza rais?

Ni haki Watanzania wanyimwe fursa ya kujua hatima ya Richmond kwa ajili ya kuridhisha matakwa ya Ikulu na TAKUKURU kabla wakosaji wa TAKUKURU hawajawajibishwa?

Tumefika mahali ambapo serikali inatukuza na kulinda vigogo na Richmond yao kuliko maisha ya Watanzania milioni 40?

Wala Pinda hakuhitaji kusisitiza maagizo ya Ikulu kwa TAKUKURU, kabla hajatueleza nani aliiagiza TAKUKURU kuisafisha Richmond. Tunachojua ni kwamba TAKUKURU ipo chini ya ofisi ya rais. Hivyo, Ikulu na TAKUKURU ni kitu kimoja. Pinda anaweza kutusaidia kujibu Ikulu, TAKUKURU na Richmond ni vitu vingapi?

Hivi Pinda anadhani tumesahau kauli yake kwamba suala la hatua za serikali dhidi ya mkurugenzi wa TAKUKURU liko mbele ya rais linafanyiwa kazi? Kumbe ndiyo kazi yenyewe hii? Na Pinda anadhani ameipa Ikulu sifa?

Je, vitisho hivi vya Ikulu na TAKUKURU kwa wabunge ndiyo tafsiri ya kauli ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwamba yeye na Rais Jakaya Kikwete wametoka mbali hawawezi kutenganishwa?

Au ndiyo tafsiri ya kauli ya Lowassa, muda mfupi kabla ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka jana, alipowaonya wabunge akisema 'sote hapa ni wanasiasa, tukiamua kushughulikiana nani atabaki?'

Au ndiyo utekelezaji wa kauli ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hosea, alipobanwa na wabunge katika moja ya semina alizowaandalia katika hoteli ya Whitesands, Dar es Salaam, wakamhoji kwa nini hajawajibika kutokana na uzembe wa ofisi yake katika sakata la Richmond, naye akakasirika na kusema atawashughlikia wao kwanza?

Pinda alidhani akisema TAKUKURU imetumwa na Ikulu wabunge wote wangeogopa na kutakatifuza makosa ya watawala? Je, hii si dalili kwamba serikali inaficha udhaifu na uchafu wa Ikulu kwa kutumia TAKUKURU kuwatisha wanaohoji kilichopo nyuma ya pazia?

Na hapa ndipo tunapowageuzia kibao wabunge wenyewe. Tuliwaambia, tukawashauri mapema wakati serikali ilipoleta muswada wa kubadili Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kuwa TAKUKURU; tukasema taasisi hii haiwezi kufanya kazi ya kudhibiti wala kuzuia rushwa kama itaendelea kuwa chini ya ofisi ya rais.

Tulijua kwamba ofisi ya rais nayo inahitaji kuchunguzwa na kudhibitiwa, na kuwa serikali haitaki kuiondoa ofisi hiyo chini ya rais ili kuwalinda ama rais mwenyewe, au wasaidizi wake au rafiki zake au jamaa zake iwapo watakumbwa na masuala yanayohitaji mkono wa TAKUKURU.

Tulipendekeza iundwe chini ya chombo kinachojitegemea ili kiweze kusaidia kumulika kote kote bila woga wala upendeleo. Lakini dhamira ya serikali ilipitishwa na wabunge wale wale waliojifanya wanakipenda sana chama chao (CCM) kuliko taifa.

Katika hili la sasa, wabunge hawa wanaopambana na TAKUKURU wanapaswa kujua kwamba wanapambana na nguvu nyingine nyuma yake. Wataweza kuishinda? Je, wananchi watabariki hila za Ikulu na TAKUKURU?

Je, wabunge wetu sasa wameanza kuelewa hekima yetu ya kuiondoa TAKUKURU ofisini kwa rais? Maana hekima ya kawaida inatujulisha kuwa si marais wote watakuwa waadilifu. Wabunge wanajua mchezo unaochezwa na watawala, maana baadhi yao walikuwamo katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kilichomchachafya na kumtisha Sitta na wenzake.

Viongozi wale wale wa vikao vya NEC ndio hao hao wanaoituma TAKUKURU iwarudie kina Sitta kwa hila mpya. Si wamalize sula la Richmond kwanza tuone jeuri yao? Je, wabunge wataweza kuinyamazisha Ikulu na TAKUKURU?

Watawala wanadhani wabunge na wananchi hawajui walengwa wanaotafutwa na wanaolindwa katika sakata hili? Hivi Ikulu haiwezi kuwa imara bila kuwakumbatia mafisadi?

MAKALA hii inapatikana pia katika tovuti ya TanzaniaDaima

Friday, October 30, 2009

Wednesday, October 28, 2009

Sasa tumejua, tatizo ni rais

Baada ya Rais Jakaya Kikwete kukiri kwamba wasaidizi wake walimshauri apumzike akakataa, ndiyo sababu akazidiwa hadharani pale Mwanza, sasa kumeibuka hoja mpya. Je, kama rais anadiriki kuwapuuza wasaidizi wake katika suala nyeti la afya yake, nao wananywea; atawezaje kuwasikiliza wasaidizi na washauri wake katika masuala ya uchumi, siasa, usitawi wa jamii na mengine? Si inawezekana rais ana washauri wazuri wa mambo mengi tu lakini hawasikilizi? Hii si sehemu ya ushahidi kwamba rais ndiye tatizo?

Wednesday, October 14, 2009

Tunayojivunia ndiyo haya?

Kwa mazingira haya ya elimu tunajivunia sera zilizopo na utekelezaji wake?

Sunday, October 11, 2009

JK akianguka tena daktari wake atasemaje?

SI vema kudhani kwamba viongozi wetu hawawezi kuumwa. Lakini ndivyo madaktari wa Rais Jakaya Kikwete wanavyotaka tuamini. Kwani wanadhani wakisema rais anaumwa tutamnyanyapaa? Kwani yeye si binadamu tu? Taarifa yao kwa umma, ambayo inakanusha tetesi za rais kuumwa, wakati yeye anazidiwa hadharani, si dalili kwamba wenyewe wanamnyanyapaa? Hili ndilo swali gumu la wiki hii. SOMA HAPA.

Thursday, October 01, 2009

Hotuba ya Mke wa Gordon Brown

Msikilize na mtazame Sarah Brown akimpigia debe mumewe, ingawa maji ya kisiasa yako shingoni mwa mumewe. Hotuba yake inaweza kuwavutia wanachama wa Labour. Je,itawashawishi wapigakura waliokwishachukia na kuamua kuleta mabadiliko?

Sunday, September 20, 2009

Salaam za Eid El Fitr 2009


Asalaam Aleykum Waislamu wote, popote pale mlipo. Hongera kwa kuhitimisha mfungo wa Ramadhani. Nakutakieni amani na heri ya Eid El Fitr.

Sunday, September 13, 2009

Rais Kikwete amefanikiwa kujidanganya


BAADA ya kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete akijaribu kujibu maswali ya wananchi katika televisheni, huku nikijua kuwa hizo ni propaganda za kisiasa kuelekea 2010, nimeridhika kwamba hajamndanganya mtu yeyote bali yeye mwenyewe. Kwanini? Soma hapa.

Friday, September 04, 2009

Zitto Kabwe ataweza?

Zitto Kabwe ameamua kuwania uongozi wa juu kabisa wa chama chake, na tayari amekiri kwamba si mwa msukumo wake binafsi. Je, ataweza? Soma hapa Ukishamaliza hiyo unaweza kujikumbusha na hili pia.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'