Sunday, January 28, 2007

Karume ndiye mwenye ufunguo Zanzibar


Na Ndimara Tegambwage

ZANZIBAR yaweza kuwa chimbuko jingine la “kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa,” ambako kulimfukuzisha urais, Aboud Jumbe.
Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa anataka kumaliza kile anachokiita “mpasuko” wa kisiasa katika visiwa ya Unguja na Pemba na kwamba hataki mwanachama yeyote wa chama chake, CCM awe kikwazo.
Hili ni kama apizo. Kwanza Rais Kikwete amesema na kurudia kwamba amedhamiria kumaliza “tatizo la Zanzibar.” Lakini katika apizo anasema hataki mtu yeyote kumchafulia.
Amesema atakayejiingiza na kujaribu kuzuia juhudi za kuleta ufumbuzi, atafukuzwa uanachama wa CCM. Si kawaida kwa rais kutumia vitisho vya aina hiyo katika suala linalohusu utatuzi wa mgogoro.
Kikwete alisema kama rais, lakini amevaa kofia ya mwenyekiti pia wa CCM. Je, inawezekana ni uenyekiti wake unaofanya atishie kumvua mtu uanachama au kuna jambo la nyongeza? Je, wenye nafasi ya kutibua ufumbuzi ni wale wa CCM peke yao?
Je, inawezekana rais au mwenyekiti wa CCM amegundua kuwa mpasuko wa Zanzibar umeletwa na kulelewa na viongozi wa CCM au wanachama wake, na si wananchi kwa ujumla au wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi – CUF? Kwa nini rais atishie kumvua uanachama, mtu au tuseme kiongozi yeyote wa CCM?
Kwa kuzingatia hali ya Zanzibar, ufunguo wa mgogoro ulioghubika nchi hiyo, ni Rais Aman Karume. Kulainika kwake kunaweza kufanya mgogoro uyeyuke na kukamia kwake kunaweza kufanya hata juhudi za Rais Kikwete kukwama.
Mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya CCM na CUF, yakiongozwa na makatibu wake wakuu, Yusufu Makamba na Maalim Seif, ni hatua ya kukamilisha kile ambacho Rais Kikwete ameishaandaa.
Bila shaka Kikwete atakuwa ameandaa kwa ushirikiano na Rais Karume. Vinginevyo ameandaa na wahasimu wa Karume ndani ya CCM na huko huko visiwani. Hili linajitokeza katika sura mbili.
Kwanza, ni ukaidi wa CUF kwamba hata sasa hawatambui ushindi wa Karume na hawako tayari kuingia katika muwafaka wa tatu. Hili linaonyesha CUF wanaweza kuwa wameona mzani unaelemea upande upi na wanataka kutumia karata yao kufanikisha majadiliano ya sasa.
Kwani Karume, kama Rais Mstaafu, Salmin Amour, hajatimiza matakwa yote ya muwafaka wa pili kati ya CCM na CUF na huenda akatoka madarakani bila kuutekeleza wote.
Pili, ni jinsi Yusufu Makamba alivyokwenda Zanzibar. Katika mazingira ambayo inasemekana Naibu Katibu Mkuu wake, Salehe Ramadhani Feruzi “alimkimbia,” bila shaka kuna mambo ambayo hayaendi sawa katika mpangilio wa kumaliza mpasuko.
Feruzi, pamoja na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, ni miongoni mwa marafiki wakubwa wa Rais Karume. Kutokuwepo kumlaki Makamba, uwanja wa ndege na ofisini, kunaashiria upinzani, aghalabu wa chinichini, wa kile ambacho Makamba na Kikwete wanajaribu kunadi.
Habari zisizothibitishwa zinasema pamoja na ujumbe wa Makamba kwa viongozi wa CCM Zanzibar na CUF, alibeba pia vitisho vingi kwa Rais Karume, zikiwemo shutuma hapa na pale, ili kumlainisha na kuzuia upinzani kwa hoja za Kikwete.
Hata hivyo, hiyo ni hali iliyotegemewa. Karume hawezi kukubali haraka kufanya kazi na mahasimu wake; lakini hawezi kuasi uamuzi wa chama chake. Yote mawili ni shubiri kooni.
Rais Kikwete anajua yote haya mawili. Anajua hali inayomkabili Karume ikiwa ni pamoja na upinzani mkubwa ndani ya CCM kutoka kwa waliokuwa wakimuunga mkono au walioshindana naye kuwania uteuzi wa kugombea urais mwaka 2005.
Katika hali hii, nani, kama si Rais Karume, ambaye Kikwete alimlenga, pale alipotishia kwamba atakayekuwa kizingiti katika kuleta ufumbuzi atafukuzwa uanachama CCM?
Kwani uanachama wa CCM unawauma sana viongozi na “wakubwa” wengine, ambao huweza kupoteza nafasi zao za uongozi, hata urais wa Karume, kuliko wanachama wa kawaida.
Wachunguzi wa siasa za CCM wanasema kilichompata Jumbe kinaweza kumpata Karume iwapo atakaidi mapendekezo ya Kikwete. Kwanza kwa kutangaza hali ya kuchafuka kwa siasa, ambazo hakika zilichafuka tangu zamani, na pili kutafuta njia ya kumweka kando kupitia Dodoma.
Rais Aman Karume alipigiwa kampeni kubwa Dodoma na Kikwete na wenzake, mwaka 2000 kwa tiketi ya vijana. Vikao vyote vya juu ya CCM vilizizima kwa kampeni za “kijana Zanzibar” na kwamba chaguo pekee alikuwa Aman Karume.
Leo hii, wakati Rais Kikwete anataka kuondoa kile alichoita mpasuko Zanzibar, si tu anahitaji, bali pia analazimika kupata, ushirikiano wa “ndugu yake katika siasa za ujana za 2000.
Lakini iwapo ushirikiano hautapatikana, na iwapo Kikwete na Karume hawatakuwa na msimamo mmoja, uwezekano wa Kikwete kumtosa Karume, tena pale Dodoma, kupitia vikao vya CCM, uko wazi kabisa.
Wachambuzi wa siasa wanauliza iwapo Kikwete anaweza kumtosa Karume ili kumaliza mgogoro, ambao kumalizika kwake kunaweza kuondoa CCM madarakani huko Zanzibar na huenda kuwa njia pekee ya kuimarisha upinzani Tanzania bara.
Kwa kila hali, na hata bila kuanza kwa majadiliano ya kina, mwenye uwezo wa kuleta ufumbuzi wa haraka Zanzibar ni Rais Aman Karume. Huo ndio ufunguo.
Kinyume cha hayo, Kikwete ana uwezo, kupitia Dodoma, kuweka mazingira yatakayozaa shutuma na hata kashfa, na hatimaye kujiuzulu au kufukuzwa kwa Karume katikati ya vilio na aibu. Lakini yote kwa faida ya nani?
Kuchafuka au kutochafuka kwa siasa; kufukuzwa au kujiuzulu kwa Karume; jawabu sahihi kwa mgogoro wa Zanzibar ni kuheshimu kauli ya umma. Kuacha kuchezea maamuzi ya wananchi katika sanduku la kura.
Uadilifu ukitinga, haki ikatendeka, aliyeshinda ataingia ikulu; aliyeshindwa atasubiri wakati wake bila kelele wala mikwaruzo.

ndimara@yahoo.com

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'