Wednesday, June 21, 2006

Watoto wa takrima wakongwe, jengo jipya

Na Nikita Naikata

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wabunge wa Tanzania kuwa nadhifu na makini ili wafanane na jengo jipya la Bunge la Jamhuri ya Muungano lililogharimu sh. milioni 31. Huku baadhi yao wakijiandaa kukubaliana na rais, mchambuzi NIKITA NAIKATA anasema wabunge ni watoto wa takrima, wakongwe wasio na jipya katika jengo jipya! Soma hapa chini.

SITAKI kuambiwa kwamba kwa kuwa sasa kuna jengo jipya la Bunge, pale Dodoma, basi fikra za wabunge zitakuwa mpya pia.
Sitaki kabisa kushawishiwa, hata na Rais Jakaya Kikwete, kwamba wabunge watakuwa wapya kifikra kwa kuwa watakuwa wanatumia jengo jipya la Bunge lililogharimu mabilioni ya shilingi.
Nasema hivyo kwa kuwa bunge si jengo. Bunge ni watu waliochaguliwa, kwa njia halali au hata kwa hila, kuwa wawakilishi wa wananchi katika Baraza la Kutunga Sheria.
Historia inaonyesha kwamba kumekuwapo na wawakilishi wa wananchi ambao hawakuwahi kuchaguliwa kwa kura za “nipe nikupe” ambao walifanya uwakilishi wa maana zaidi kuliko hawa wa leo.
Nyakati ndizo ziliamua nani awe mwakilishi. Ni matakwa ya nyakati yaliyoathiri fikra zao. Ni historia iliyotoa majukumu kwa waliotokea kuwa wawakilishi bora.
Na hao walitokea kwenye vibanda. Walikaa katika nyumba za kawaida na kupitisha uamuzi mzuri uliolenga kunufaisha jamii.
Bali mazingira yanabadilika. Uwezo umeongezeka. Nyenzo za kufanyika kazi zimeongezeka. Mahitaji mapya katika nyakati mpya yameongezeka pia kwa kiwango kikubwa.
Hivyo, kuwa na jengo jipya la Bunge, lenye ofisi za wabunge, vifaa, nafasi pana ya kumwezesha mbunge kupumua vizuri na kupata taarifa zaidi, ni mambo muhimu katika nyakati tulizomo.
Lakini jengo zuri la kisasa la Bunge haliwezi hata kuhusishwa na fikra nzuri wala bora. Sitaki hata kodogo kushawishiwa hivyo! Kuna sababu nyingi. Hapa tuangalie chache zifuatazo.
Kwanza, wabunge hawana upya wowote. Wengi, hasa katika uchaguzi uliopita, wameingia bungeni kwa njia ya takrima. Rushwa!
Takrima ni rushwa iliyohalalishwa na bunge kwa kuitungia sheria. Wenye fedha, wakatumie fedha zao, kwa madai ya kukirimu wananchi wapiga kura, na kujizolea kura za kuwapeleka waliko.
Upya wa watoto wa takrima uko wapi? Fikra mpya na bora, katika “nipe nikupe” zitatoka wapi? Kuna uzuri gani katika mashindano ya kukatana shingo kwa hela na hila na mshindi atakuwaje na fikra sahihi za wananchi aliowahonga?
Jengo jipya lililojaa sehemu kubwa ya waliopatikana kwa hongo iliyohalalishwa na jengo la zamani, litakuwaje chemchemi ya fikra nzuri? Sitaki kusikia!
Pili, kinachofanya jengo kuwa la maana ni wale waliomo, nia na shabaha zao na kazi zinazofanyika humo. Nini basi kinafanyika katika jengo jipya?
Uchaguzi mkuu hadi uchaguzi mkuu mwingine, chama kimoja – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kimeendelea kuzoa kura (si kushinda) kwa hila na ujanja.
Kikiwa madarakani, kimeweka na kusimamia utaratibu unaoendeleza hodhi ya siasa nchini. Kwa mfano, kwa kutumia wingi wa wabunge wake, kimekataa kuruhusu mfumo wa uwakilishi wa uwiano.
Kukataa uwakilishi wa uwiano ni kukubali kutawala kwa mabavu. Tuchukue mfano wa jimbo lenye wapiga kura 60,000 ambako wagombea wawili wamepata kura 28,786 na mwingine 28,999 na huyu wa pili aliyepata kura 213 zaidi ndiye anatangazwa mshindi.
Hakika huu si ushindi wa faraja. Huu ni ubunge unaopwaya. Zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura katika jimbo wanakuwa wamekukataa lakini kwa mujibu wa sheria mbovu, unakuwa mbunge kwa shinikizo tu.
Kuna uhusiano gani kati ya fikra hizi juu ya uwakilishi na jengo jipya la bunge? Je, jengo litabadili fikra hizo au litazisimamia zaidi katikati ya viyoyozi imara na nuru kuu ya taa za kisasa?
Tatu, si siri kwamba wabunge wa CCM wana tabia ya kuunga mkono kila hoja ya serikali hata kama wanajua kwamba inapwaya na hata kuwa na madhara makubwa kwa wananchi baadaye.
Hili linafanywa kinafiki ili kulinda maslahi ya chama chao kinachoongoza serikali. Je, unafiki na usaliti wa wananchi kwa njia hiyo unaweza kubadilishwa na jengo jipya?
Nne, serikali “imekubaliana” na uamuzi wa mahakama wa kufuta sheria iliyoruhusu rushwa iitwayo takrima. Lakini huko ni kufuta kipengele kwenye vitabu. Si kuacha kutoa rushwa kwa maelezo mengine.
Je, mara moja jengo jipya limefanya wabunge wawe wanaharakati wa kweli wa kusambaza taarifa za kupinga takrima iliyowapeleka bungeni au wataendelea kutoa chini ya jina jingine?
Tano, jengo jipya lina uhusiano gani na mabadiliko ya taratibu za bunge katika kupokea miswada? Uzoefu ni kwamba serikali ndiyo imekuwa ikipeleka miswada bungeni. Kwa maana nyingine, serikali imekuwa ikitafuta msaada wa bunge wa kutawala inavyotaka.
Miswada binafsi ya wabunge imekuwa haba na pale ilipopita, ilikuwa ya kujikomba kwa serikali na kujitafutia umaarufu wa binafsi miongoni mwa watawala.
Jengo jipya lina uwezo wa kuchochea miswada ya binafsi? Linaweza kuondoa hodhi ya taratibu za kupeleka miswada na kuamsha akili ya kukubali hoja badala ya kuangalia muswada umeletwa na nani na kutoka kambi ipi?
Sita, bunge bado limejaa fikra kwamba wabunge wa upinzani ni walalamishi tu na hupinga kila kitu. Fikra hizo huwafanya wabunge wa CCM kuwaona wale wa upinzani kuwa hawawezi.
Mkondo wa fikra za hawawezi umetapakaa kila kona ya utawala kiasi kwamba asiye mwana-CCM hapewi nafasi hata kwenye bodi ya shirika la umma! Je, fikra hizo mbovu zitaondoshwa na mng’aro wa jengo jipya la bunge?
Kuna mengi ambayo wabunge, na hasa wabunge kutoka CCM, wamebeba kutoka jengo la zamani hadi jipya. Serikali pia imebeba fikra hizo hizo na kuziingiza kwenye jengo lililojengwa kwa mabilioni.
Sitaki kuambiwa kwamba jengo litaleta fikra mpya. Jengo, na huu ndiyo ukweli mweupe, litaimarisha fikra kongwe na chafu zilizoasisiwa kulinda maslahi ya waliomo serikalini.

nikitanaikata@yahoo.com
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'