Sunday, December 24, 2006

Baada ya mwaka Ikulu: Kikwete anayo furaha?

Baada ya mwaka mmoja Ikulu, Rais Jakaya Kikwete amebakiza miaka mitatu (si minne) madarakani. Anayo furaha aliyokuwa nayo awali? Watanzania wanayo furaha? Ameweza au ameshindwa nini? Bofya hapa tuulizane maswali.

Wednesday, December 20, 2006

Hii ni aibu baada ya miaka 45 ya Uhuru

Hata baada ya miaka 45 ya uhuru, tunashindwa kufanya vitu vidogo kama hivi, kuokoa Watanzania wenzetu! Je, wasio sehemu ya watawala wataokolewa na nani? Aibu!

Sunday, December 17, 2006

Blogu hii bomba!

Tangazo: Unataka kusafiri? Bofya hapa ujue bei ya tiketi ya ndege.

Sunday, December 10, 2006

Hii kali

Sina maelezo. Isome mwenyewe. Tafakari. Halafu jadili.

Mzee wa viwango na kasi anayongwa au anajinyonga?


Siku alipochaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta alijitangaza kuwa spika wa 'viwango na kasi.' Mwaka mmoja baadaye anaweza kujitambulisha kwa maeneno hayo? Anakuwa kinyonga au anajinyonga? Kama hukuridhika soma hii ndefu.

Monday, December 04, 2006

Ahadi za JK zaanza kutekelezwa


Wakati wa kampeni za urais mwaka 2005, JK alisema: "Tanzania Yenye Neema Inawezekana." Aliahidi "kushamirisha demokrasia." Na zaidi ya yote, aliahidi "maisha bora kwa kila Mtanzania" kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Mwaka mmoja umepua tangu aingie madarakani. Haya ndiyo matokeo ya ahadi hizo?

Friday, December 01, 2006

Mbowe na Obasanjo warejea darasani


Wanasiasa hawa wawili, Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania mwaka 2005, Freeman Mbowe, wamefanana katika jambo moja mwaka huu - kurejea shule, kunoa ubongo. Tusisahau Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, naye alijiunga na Chuo Kikuu cha Havard mapema mwaka huu.

Wednesday, November 29, 2006

Kura Za Mzee Wa Kombati Zilikwenda Wapi?


CCM walidai kwamba Mbowe alipata watu wengi kwenye kampeni kwa sababu watu walikwenda kushangaa helikopta. Nikiitazama picha hii naona jambo tofauti. Helikopta ipo uwanjani lakini hawaitazami. Wameiacha nyuma, wanamkodolea macho Mbowe (hayupo pichani). Tazama nyuso zao. Waliofuatilia kampeni zake wanajua hali ilikuwa hivyo kila mkutano wake wa kampeni Oktoba - Desemba 2005. Tazama mmoja wa washindani wake. Nimesikia watu wakijiuliza. Nami najiuliza. Na sasa nawauliza nyie wasomaji. Tuulizane. Hivi kura za Mbowe zilikwenda wapi?

Tuesday, November 21, 2006

Tazama Ubunifu


Rafiki yangu mmoja aitwaye Alex Kaija amenitumia picha hii. Nimemuuliza alikoipata akasema naye ametumiwa. Hamjui aliyeitengeneza. Nimevutiwa na ubunifu wake; nikaona vema niwashirikishe wasomaji wa blogu hii. Mnasemaje?

Sunday, November 19, 2006

Unasemaje juu ya vitisho vya Lowassa?


Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amekuwa akitumia mabavu kukabiliana na wananchi wanaomkosoa, hasa magazetini. Makala HII imemuonya na kumtahadharisha juu ya athari za ubabe huo; hasa kwa mtu ambaye tayari ameshaonyesha nia ya kuwania urais baada ya Jakaya Kikwete. Una maoni gani?

Wednesday, November 08, 2006

Mbunge Huyu Ana Hoja, Asikilizwe


HII ni sehemu tu ya upungufu wa katiba ya nchi yetu ambayo tunaendelea kusisitiza kuwa iandikwe upya ili iendane na matakwa ya sasa. Kwa nini tulazimishane kuongozana kwa matakwa ya miaka 50 iliyopita? Kwa nini hatuoni kwamba na kizazi hiki kina mchango wake katika kukua kwa taifa?

Monday, November 06, 2006

Kifo cha Saddam Hussein


Hajafa, lakini mazingira yanaonyesha kuwa atakufa. Unasemaje kuhusu hukumu dhidi yake? Soma maoni ya "dunia," sifa zake na historia yake.

Thursday, November 02, 2006

Anaharibu hapa anahamishiwa pale

Kuna sababu za msingi za serikali yetu kuwalinda maofisa wanaofuja pesa zetu kwa kuwahamisha badala ya kuwachukulia hatua? Soma hapa kwanza, halafu utoe maoni.

Monday, October 30, 2006

Prof.Shivji na uandishi wetu

"...Hardly any one(including journalists themselves) takes journalism seriously, let alone with commitment." (Issa Shivji; Intellectuals at the hill, pg. 176). Soma nukuu kamili katika bolgu ya Maggid

Johnson Mbwambo je?

Anaandika kwa unyenyekevu mkubwa. Lakini hoja yake ni kali kweli kweli. Anajua kuna wanaotumiwa bila kujua. Anawajua. Anawaonea huruma; ama wao au vizazi vyao. Angependa wajitambue, wajirudi sasa. Warudi kazini kwao. Ni mpole, makini na muwazi. Msome. Huyu hapa.

Wednesday, October 25, 2006

Hata Wakubwa Wanaweza Kushitakiwa

Hivi kama kila Rais Mstaafu angechunguzwa na kushughulikiwa kama huyu hapa, Afrika ingeweza kupiga hatua gani katika mapambano dhidi ya rushwa? Hatua hiyo ingekomesha wizi na kuboresha maisha ya wananchi? Je, sisi Tanzania hatuna viongozi wanaotuibia wakiwa madarakani? Tuwafanyeje wanapostaafu?

Tuesday, October 24, 2006

CCM ukwasi mtupu, watumishi njaa kali


Posho za wakubwa ni mara 300 ya mishahara ya watumishi. Kama wakubwa wameshiba na wadogo wanalia njaa, kuna lolote litakalofanyika? SOMA hapa uone adha za watumishi waaminifu wa CCM, na majibu ya wakubwa wao kuhusu hatima yao. Madereva wa chama nao waja juu. Nadhani wanajiuliza. Bosi wao Yusuf Makamba, anapata manono katika mshahara wa Ubunge, Ukatibu Mkuu wa CCM na masurufu ya safari anayojilipa. PATA uhondo.

Bilioni za kichumi au kisiasa?

Unasemaje kuhusu bilioni moja za Kikwete kila mkoa? Kumbuka huyu ni mchumi na mwanasiasa. Katika uamuzi huu anafanya uchumi au siasa? Toa maoni. Wenzako wameshaanza.

Monday, October 23, 2006

Walimu mavumbini, wanafunzi wanaozwa


Haya jamani. Ona shule zetu zilivyo, miaka 45 baada ua uhuru. Yameenea nchi nzima. Wakubwa wanajisifu, na wanayataja na haya kama mafanikio ya MMEM. Haya yanatokea pia kwingine katika hali tofauti. Hata Dar es Salaam yapo, mita chache kutoka nyumbani na ofisini kwa Rais, Ikulu. Na hili la wanafunzi kujisaidia vichakani katika karne ya 21 tunaizungumziaje? Eti na ukosefu wa VYOO unasababisha shule kufungwa; huku baadhi ya walimu wakiiba fedha za MMEM. Huko Musoma, wanafunzi 600 wanasota. Ndiyo maana hata wazazi hawaamini kwamba watoto wao wasiojua hata kuandika majina yao wameshinda mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kwenda sekondari. Tuko makini kweli? Si hivyo tu. Wazee hawa maskini, wamefungwa jela kwa sababu serikali imeshindwa kujenga shule, na inawalazimishwa wachangie hata kama hawana pesa!

Uhamisho dhidi ya mabadiliko ya mawaziri

Tuulizane: Ni mabadiliko ya Baraza la Mawaziri au uhamisho. Wadau wanasemaje? Imalizie kwa kusoma hapa.

Natamani waandishi wote wangekuwa hivi

Kama waandishi wote wangekuwa hivi, ni hoja gani imebaki bila kujengwa? Ni nani angethubutu kuchezea taaluma yao? Ni nani angejaribu kuwaweka kwenye kiganja chake na kuwadhalilisha? Ni nani angewakuta wakimshambulia anayewatetea? Lakini upande mwingine unasema, kama waandishi wote wangekuwa hivi, tungewezaje kutofautisha pumba na mchele. Hakika, huwezi kuthubutu kumweka Deus Jovin katika kundi la pumba. Labda kama hujasoma hoja yake hii.

Sunday, October 08, 2006

Tunafaidi joto la kukumbatiwa; Tanzania inafaidi nini?

Na Ansbert Ngurumo, Hull University, UK

NAANDIKA kumpa pole Rais Jakaya Kikwete kwa yaliyompata kutoka gazeti la Kenya wiki inayomalizika leo.


Nimesoma kwenye mtandao kwamba gazeti moja la Kenya limechapisha katuni inayoonyesha waandishi wa habari wa Tanzania wakimlamba miguu Rais Kikwete. Nimeiona katuni hiyo.


Nimesoma pia habari juu ya taarifa ya Ikulu kwamba Rais wetu na wasaidizi wake wamesononeshwa na katuni hiyo. Nimesoma pia kwamba Rais hatajibu lolote kuhusu katuni hiyo.


Nakubaliana na rais wangu kwa mambo mawili. Walioandika na kuchora katuni hiyo si Watanzania. Ni Wakenya. Na si Wakenya wote, wala si magazeti yote ya Kenya.


Hivyo Rais amefanya jambo jema kutojiingiza katika malumbano nao. Si wananchi wake.


Maana hata sisi tumekuwa tukiona magazeti yetu yanawachora viongozi wengine wa Afrika na sehemu mbalimbali za dunia. Yanawachora kadiri mitazamo yetu juu yao inavyokuwa wakati huo.


Na michoro hiyo haina masilahi yoyote ya kisiasa. Ina malengo mbalimbali ya kitaaluma. Inalenga kuburudisha wasomaji. Wakati mwingine inaleta ujumbe mpya - inaelimisha. Wakati mwingine inafikirisha.


Na katika kufanya hivyo, inafurahisha au inaudhi. Kwa mfano, kuna watu wamefurahia katuni hiyo kwa kuwa wanaamini kwamba waandishi wa Tanzania wanalamba miguu ya wakubwa. Wapo.


Wapo walioifurahia kwa sababu tu ya kufurahia ubunifu wa mchoraji. Wapo. Wengine wameifurahia kwa sababu wanapenda utani. Na wameona mtu aliyejitokeza kumtania rais wa nchi!


Wengine wameichukia. Si kwa sababu nyingine yoyote, bali kwa kuwa imemgusa na kumsema rais. Basi! Hawataki aguswe.


Wengine wameichukia kwa sababu wamesikia mwenyewe aliyechorwa ameichukia. Wanachukia pamoja naye.


Wapo walioichukia kwa kuamini kwamba imesema uongo. Wanasema imemdhalilisha Rais. Wanaongeza kuwa imewadhalilisha waandishi wa habari. Wapo.


Bila shaka sitakosea nikisema katika kundi hili wamo waandishi wenyewe. Maana tunajua kwamba wengi wetu, ingawa tunaandika na kuchambua mambo ya wengine kila siku, hatufurahii uchambuzi wa wengine juu yetu kama hautusifii.


Ni hulka ya kibinadamu. Kila mtu anataka asemwe vizuri. Hulka hii ndiyo inayowapa haki waliochukia pamoja na rais wetu.


Lakini wengine hawakuchukia wala kufurahi. Wameguswa tu na hoja ya mchoraji. Wanaweza kukuza mjadala mpya, na kumwambia Rais Kikwete na wasaidizi wake kwamba baada ya kuchukia watafute tafsiri halisi ya katuni hiyo.


Naamini, kama ilivyowahi kuandikwa na mwandishi mmoja ambaye simkumbuki jina, kwamba haiwezekani watu wote wakawa na tafsiri moja inayofanana juu ya katuni hiyo.


Haiwezekani. Hivyo, inabidi tuvumiliane katika kuelewa ujumbe unaoletwa kwetu kupitia katuni hiyo. Watu wenye akili hawatakosa la kuwaza. Wanaweza kuitumia kuboresha uhusiano kati ya rais au serikali na vyombo vya habari. Uhusiano unalisaidia taifa.


Maana kama wengi wanavyosema, nami naamini katika ukweli huu, uhusiano uliopo sasa kati ya rais na vyombo vyetu vya habari unalenga kuisaidia serikali, si nchi.


Ni uhusiano usiotambua kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola. Na hili halikuanzwa na Kikwete. Amelirithi. Lakini litamgusa zaidi yeye kwa kuwa amejitangaza kuwa rafiki wa vyombo vya habari.


Kwa kauli yake mwenyewe, mara kadhaa, amesema kwamba ana nia ya kushamirisha demokrasia katika Tanzania. Nionavyo mimi, Kikwete hawezi kushamirisha demokrasia bila kuviondoa vyombo vya habari katika utumwa.


Hawezi kushamirisha demokrasia iwapo vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira ya woga. Na anayeogopwa katika hili si mwingine, bali serikali. Hawezi kushamirisha demokrasia bila kuondoa sheria dhalimu ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa miaka zaidi ya 14 sasa; ambazo zinavinyima vyombo vya habari fursa ya kuwa huru na kufanya kazi bila kuogopa matumizi mabaya ya utashi wa wakubwa.


Yawezekana mchoraji wa katuni anajua hali halisi ya uandishi wetu na mazingira yanayotukabili. Anajaribu kuchora uhusiano uliopo kati ya waandishi na rais, anasema wanamlamba miguu.


Nasema hivi, hatumlambi miguu. Lakini simshambulii mchoraji. Ningekuwa naichora mimi ningemweka rais akiwa amewakumbatia waandishi, badala ya kuwaonyesha wakilamba miguu.


Kulamba ni alama tu kama ilivyo kukumbatiwa. Hata kama wapo ambao wangedhani kukumbatiwa ni kuzuri zaidi, sioni tofauti kimantiki.


Ninachoona katika kumbatio ni watu wanaofurahia joto la rais. Ikumbukwe kuwa watu hawa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya kubezwa na rais aliyeondoka. Alikuwa mwandishi, lakini hakutangaza kuwa rafiki yao.


Sana sana, alikuwa akilumbana nao kila alipopata fursa ya kufanya hivyo hadharani. Aliwaita waandishi uchwara. Aliwadharau wazi wazi. Bila shaka nao walimchukia.


Sasa huyu kaja. Amenyoosha mikono yote miwili. Katika mshangao wa ajabu, nao wamenyoosha mikono. Wamekumbatiana. Mh! Joto la rais!


Lakini bahati mbaya, huyu aliyewakumbatia haachii. Hawawezi kutoka. Wanabaki wanacheka. Wanapiga stori. Wanatabasamu. Habari zinapita. Haziandikwi.


Zitaandikwaje wakati mikono imekumbatiwa? Zitaandikwaje wakati zinamhusu aliyekumbatia na kukumbatiwa? Zitaandikwaje wakati kila mmoja anaogopa kutofautiana na mkubwa na kuleta malumbano yanayoweza kupoteza joto hili?


Zitaandikwaje wakati wengi waliokumbatiwa wanadhani jukumu lao ni kumsaidia aliyewakumbatia? Zitaandikwaje wakati baadhi ya ahadi zake hazijatimizwa? Hapo ndipo tulipo.


Lakini swali tusilojiuliza haraka haraka ni hili. Iwapo kila mmoja atataka ‘kumsaidia’ rais kutoka ofisini mwake; nani atamsaidia kutoka nje ya ofisi? Lakini zaidi ni wajibu wetu kumsaidia au kuisaidia nchi? Je, nchi yote inaishia kwa rais na wasaidizi wake?


Lipo swali la ziada. Iwapo kila mtu anataka kuwa mwandishi asiye rasmi wa rais, walioajiriwa kumsaidia rais watafanya kazi gani? Na kazi zetu zitafanywa na nani?


Uongo mbaya, waandishi wetu wengi wanampenda rais wetu. Sidhani kama wapo wanaomchukia.


Lakini lazima tuweke tofauti kati ya kupenda, kushabikia na kushangilia. Na tutofautishe mambo ya kushabikia na ya kushangilia. Tuweke tofauti kati ya kufagilia na kufikirisha.


Hata yeye anahitaji kuelimishwa. Hatuwezi kusema ana akili na uwezo wa kusifiwa kwa kila hatua anayoichukua. Anastahili kukosolewa. Na sisi ndio tungepaswa kuongoza Watanzania wenzetu kwa kumfanya rais wetu awe ‘smart’.


Afike mahali hata anapotaka kuzungumza nasi, ajiandae vizuri. Lakini ameshatujaribu mara kadhaa. Ameshinda.


Ipo mifano mingi, lakini nitatoa michache. Wizara ya Nishati na Madini ilipotangaza uamuzi uliotokana na mjadala kati ya Rais Kikwete na Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, kwamba itailipa serikali sh bilioni tisa ambazo ni dola za Marekani milioni saba, hakuna aliyejitokeza kuhoji kwa nini tulipwe kiasi kidogo mno kutoka kwenye migodi mitatu!


Ama tulisahau au hatukujua kwamba kampuni hiyo iliwahi kufanya mazungumzo na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kukubaliana iwe inalipa dola milioni tano kwa mgodi mmoja wa Bulyanhulu, mwaka 1999.


Maana yake, kama alivyosema mwanaharakati wa mazingira, Tundu Lissu, serikali ya sasa itaambulia dola milioni 2.3 kutoka kila mgodi.


Kama ingebanwa kwa mazungumzo ya awali na Mkapa, kampuni hiyo ingelipa dola milioni 15.


Tumeibiwa mchana. Lakini tulimsifu Rais Kikwete kwa hatua aliyochukua. Ndiyo, tumemsifu rais. Tumefaidi joto la kukumbatiwa. Tanzania imefaidi nini?


Rais alipotoa hotuba mbovu jijini Mwanza mwishoni mwa mwezi Julai kuhusu mapanki na silaha, vyombo vya habari vichache - kumbukumbu zangu zinaonyesha havizidi viwili - vilimkosoa baadaye, na wasaidizi wake walikiri kwamba alikosea.


Lakini lugha iliyotumiwa ilikuwa ya kidiplomasia kwamba alishauriwa vibaya; alikoseshwa. Vilivyobaki vyote vilikuwa vikishangilia jinsi alivyomzodoa mtengeneza filamu. Havikutaka kuzama katika mantiki ya filamu hiyo. Havikutazama maisha halisi ya wakazi wa maeneo husika. Kisa? Viliogopa kupoteza joto la rais. Lakini havikumsaidia.


Karibu kila mwandishi anajua kwamba tatizo tulilo nalo katika Bwawa la Mtera, ambalo linadaiwa kusababisha kukosekana kwa umeme wa kutosha nchini, si ukosefu wa maji. Tunajua bwawa limejaa matope.


Tunajua pia kwamba ubabe wa serikali ndio ulioifanya ikatae ushauri wa kitaalamu kwamba bwawa hilo si mradi wa kuaminika wa kuzalisha umeme.


Tunajisifia kwamba viongozi wetu wanatusikiliza tukiwashauri kupitia vyombo vya habari. Mbona tunaendelea kuimba wimbo wao (wa uongo) kwamba tatizo la Mtera ni ukosefu wa maji?


Ipo dhana, ambayo baadhi yetu hatukubaliani nayo kivitendo, kwamba baadhi ya habari haziandikiki. Ipo dhana pia kwamba baadhi ya wakubwa hawaandikiki.


Na wanaosema hivi wanakiri kwamba: “Mkapa licha ya ubabe wake, alikuwa anaandikika, halafu anajibu mapigo… Sumaye pia alikuwa anaandikika, wala hafuatilii kuwasumbua waandishi.”


Ni ujumbe mzito kwa serikali inayowapenda wanahabari, inayowazungumzia vizuri jukwaani, lakini haiboreshi mazingira ya kisera na kisheria kwa ajili yao kufanya kazi kitaaluma. Inaogopa nini?


Nasi wenyewe tunaipa jeuri, kiburi na ubabe tunapokaa na kunyoosha mikono bila kufanya lolote kuikumbusha, kuikemea, kuihoji na kuisumbua.


Tuseme ukweli. Kama ‘Katuni ya Kikwete’ ingetumika katika gazeti lolote nchini, lingekuwa limefungiwa; maana wenzetu hawajajifunza kuvumilia wanapokosolewa. Inawezekana hawajikosoi pia?

Uchambuzi huu unapatikana pia katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Oktoba 8, 2006 na katika tovuti www.freemedia.co.tz Wasiliana na mwandishi kwa simu +447904159823 au barua pepe ansbertn@yahoo.com

Thursday, September 28, 2006

Bora mwanafalsafa asiyeridhika au nguruwe aliyeridhika?

Na Ansbert Ngurumo, Hull University, UK

“UNAWEZA kujua kwa hakika kwamba mtu fulani anakupenda? Utakuwa na uhakika gani? Unaweza kujua watu wengine wanawaza nini au wanahisi nini wasipokwambia?

Au hata wakikwambia utajuaje kwa hakika kwamba walichokwambia ndicho wanachowaza au wanachohisi? Kwa msingi huo, tunaweza kujua jambo lolote kwa hakika kabisa?

Tuna maanisha nini tunaposema kwamba jambo fulani ni kweli? Je, ni jambo gani linalowapatia wanasiasa haki ya kutumia mamlaka na madaraka yao jinsi wafanyavyo?

Je, ipo serikali yoyote duniani inayozingatia na kutenda haki kwa watu wake? Zaidi ya hayo, nini mana ya haki?

Tunaposema jambo fulani ni sahihi au si sahihi tunakuwa tunaonyesha kukubali au kukataa? Uadilifu una maana yoyote? Je ni zaidi ya usahihi na makosa?

Hivi kuna Mungu? Je, hoja zinazojengwa kuthibitika uwepo wa Mungu zina nguvu yoyote? Zinaridhisha? Je, wazo au dhana ya uwepo wa Mungu inakubalika katik akili ya kibinadamu?

Muda ni nini? Una umbile au hulka gani? Muda unaweza ‘kusafiri’ kutoka sehemu moja hadi nyingine?

Mimi ni nini? Ni jambo gani linanifanya mimi niwe mtu yule yule kama nilivyokuwa miaka kadhaa, tuseme 10 au 20 iliyopita?

Utu wangu ni akili yangu? Je akili ni nini? Kuna tofauti kati ya akili na ubongo?

Ni bora kuwa mwanafalsafa asiyeridhika au kuwa nguruwe aliyeridhika?

Uliwahi kuhisi kwamba mara nyingi mambo mengi huishia pale mambo mazuri yanapoanzia au yanapokaribia kujitokeza? Ulishatambua kwamba kunamambo ambayo huwa tunazuiwa kufanya hata kabla hatujafikiria kuyafanya?

Unajua kwamba kunamambo ambayo ulifundishwa au kulelewa usiyahoji? Au wewe ni mmoja wa watu ambao hupokea na kuamini ‘busara’ ya wakubwa tu bila kujipa mwanya wa kuitilia shaka?

Falsafa ni somo ambalo kiini chake ni kuhoji na kuhoji. Katika falsafa, kuhiji hakuwekewi vikwazo hata kidogo, bali kunapaliliwa. Katika falsafa, hakuna jambo hata moja lisilohojiwa. Hata Mungu anahojiwa.

Kwa sababu hiyo, hata wanafalsafa wenyewe hujiuliza kama wanajua maana ya falsafa. Na hata inapotolewa, hawakubaliani kuhusu jibu linalopatikana.

Kama unapenda kuchimba masuala na kwenda ndani kabisa kwa kuhoji na kudadidisi ili kujua misingi ya masuala hayo, basi utafurahia somo hili la falsafa.”

Aya zote hizo zilizotangulia si zangu. Si mawazo yangu. Ni kauli iliyonikaribisha katika Chuo Kikuu cha Hull, Uingereza, wiki iliyopita. Yameandikwa katika jarida ambalo kila mwanafunzi wa falsafa chuoni hapa anakabidhiwa.

Ni maandalizi kwa kozi ya falsafa katika miaka michache ijayo, kwa wanaoanza kabisa na wanaojiendeleza kwenye fani hii ya falsafa.

Kozi yetu ina wanafunzi zaidi ya 120. Nayo imegawanyika katika kozi nyingine ndogo ndogo kulingana na masomo wanayochagua pamoja na falsafa. Wapo wanaosoma falsafa pekee. Wapo wanaochanganya masomo mengine.

Katika darasa langu la fasafa, siasa na uchumi, tumo wanafunzi 24. Hadi sasa mwafrika ni mmoja. Kuna wasichana wawili.

Kijumla, chuo kina wanafunzi wapatao 16,000. Zaidi ya 200 ni wanafunzi wa ‘kimataifa’ kutoka nchi 107 duniani kote. Waliobaki ni Waingereza. Ukiondoa Uingereza, nchi nyingine yenye wanafunzi wengi chuoni ni China.

Kila unakopita utakutana na Mchina. Kama si Mchina atakuwa Mkorea, Mjapani, Muhindonesia, Mtaiwani au Mmalaysia. Ni wengi.

Juzi wanafunzi wote wa falsafa tulikuwa na hafla ya kwanza ya kujuana na kubadilisha mawazo. Katika watu zaidi ya 100 sikumwona Mchina hata mmoja.

Nikamuuliza mmoja wa walimu wetu: inakuwaje kuna Wachina wengi katika chuo hiki, karibnu kila mahali, isipokuwa katika kozi ya falsafa?

Alijibu: “Unajua, kozi hii haiwafai Wachina. Ningeshanga kama wangekuwa hapa. Unajua kwa nini? Hawa wanatoka katika jamii ya watu wanaotii sana mamlaka. Si watu wanaohoji. Siasa na tamaduni zao ni wa jamii inayoogopa kuhoji, tawala zinazoogopa kuhojiwa. Sana sana, nadhani Wajapani sasa wataingia, kwa kuwa siasa zao zinaanza kuchangamka.”

Siku hiyo hiyo, nikiwa natazama vipindi vya televisheni hapa Uingereza, ikarushwa sehemu fupi ya mahojiano kati ya mwandishi na Jenerali Perves Musharraf, kiongozi wa Pakistan.

“Osama bin Laden yuko wapi?” mwandishi akahoji. Musharraf alichanganyikiwa ghafla. Akashtushwa na swali, zikapita sekunde kadhaa kabla hajajibu, watu wakacheka, na mwandishi akatabasamu, halafu Musharraf akapata neon la kusema kuhusu Osama bin Laden.

Mmoja wa wale niliokaa nao akashangaa swali la mwandishi. Nani huyo anauliza swali hilo? Kumbe naye alipigwa butwaa. Hakuzoea kusikia wakubwa wakiulizwa maswali ya kushtukizwa.

Ni Mtanzania ambaye amezoea kuona wanasiasa (hasa watawala) na waandishi wa habari wakisuguana mabega, wakinywa bia, soda au kahawa na kupanga habari za kuandika.

Sikuhangaika kujadili lolote naye. Lakini nilipata hisia kali kwamba waandishi wa nyumbani kwetu hawaoni kwamba kuhoji na kudadisi kila jambo ni sehemu ya kazi yao. Sisi hatuanzii kwenye kutilia shaka, kuhoji, kudadisi na kuchimba.

Sisi tunaogopa wakubwa, mithili ya Wachina niliozungumzia hapo juu. Sisi tumezoea kumwaga sifa kila kukicha hata kwa jambo linaloleta shaka kwa rais wa kawaida, ilimradi limesemwa na kiongozi.

Sisi tunaandika habari zinazonukuu maneno au kauli za wakubwa. Hatuzunguki na kwenda nyuma ya kauli za wakubwa hao. Sisi tunaogopa kupoteza urafiki na wakubwa. Tunaogopa kufokewa na kutishwa. Ndiyo maana hatuulizi maswali magumu.

Ndiyo maana wanasiasa watawala hawatuheshimu. Ndiyo maana wanatututumia. Ndiyo maana wanatudanganya. Ndiyo maana na jamii inaanza ‘kutuona tu tofauti.’ Ndiyo maana nasi tunaingizwa kirahisi katika ufisadi. Ndiyo maana tunashindwa kushinikiza mabadiliko.

Tumeridhika na majibu mepesi. Na wanaotuzunguka wameshatambua uwezo wetu, wanaweza kutuambia lolote. Wameshajiaminisha kwamba hatutawahoji, hata wakitudanganya. Nadhani wanaamini kwamba tumefika hapo kwa kuwa hatujui. na wamegundua kwamba tumeridhika. Tumetekeleza wajibu wetu. Kama nilivyowahi kuandika katika safu hii, tumeacha kazi yetu, tunafanya kazi yao. Hatuwajibiki.

Ni kweli si lazima wote tuwe wanafalsafa kitaaluma. Lakini tuwe wanafalsafa kwa hulka. Tuhoji na kuhoji na kuhoji. Swali lizae jibu, na jibu lizae swali. Baada ya hapo tutaheshimiana. Ndipo tutafanya kazi ya kujenga nchi kama watu wazima, wenye akili.

Ansbert Ngurumo ni mhariri mwanzilishi wa gazeti hili, aliye masomoni Uingereza. Anapatikana kwa barua pepe ansbertn@yahoo.com simu +447904159823

Friday, August 18, 2006

Madaraka ya wanasiasa ni bora kuliko maisha yetu?

Na Ansbert Ngurumo, Toronto

NIKIWA Jijini Toronto, Canada wiki hii, nimekutana na watu wengi mno. Walionigusa zaidi ni watu wawili – Ruby Yang na Thomas Lennon.

Ruby na Thomas ni watengeneza filamu. Hawa ni wanahabari. Wametengeneza filamu inayoonyesha jinsi kutokujali kwa serikali ya China kulivyowasababishia wananchi wengi kupata virusi vya UKIMWI, wakati serikali ikisisitiza kwamba hakuna UKIMWI nchini humo.

Ilikuwa hivi: Miaka ya 1980 na 1990, Wachina walihamasihwa kuuza damu yao kwa vituo vya kukusanyia damu vilivyoanzishwa na serikali ili wapate pesa. Umaskini! Vituo vilivyonunua damu yao viliiuza kwa wenye makampuni na viwanda vya kutengenezea dawa.
Damu nyingine ilizungushwa na kutunzwa katika maabara za hospitali ili itumike kwa wananchi waliohitaji kuongezewa damu. Vifaa walivyotumia havikuwa safi. Na si kila damu ilikuwa safi au salama.

Tangazo kwenye redio na televisheni lilisema: “Nyosha mkono wako, vumilia maumivu kidogo ya sindano; ukunje tena; tayari umeshajipatia Yuan 50.”

Matokeo yake, wananchi waliambukizana UKIMWI. Wazazi wakafa. Watoto wadogo wakabaki yatima. Umaskini ukaongezeka. Serikali kimya!

Likaja tatizo la ziada. Kwa desturi, wachina hawazungumzi mambo yao hadharani. Vyombo vya habari havipewi fursa pana ya kufichua masuala kama hayo. Kuna ugandamizaji mkubwa wa uhuru wa habari. Na watawala wanafurahia hali hiyo.

Ndipo Ruby na Thomas, wakaamua kufanya jambo moja – kutengeneza filamu, ambayo ingekuwa kichocheo cha kusema ukweli ambao serikali haitaki kuusikia. Wakaenda katika jimbo moja la Yingzhou, lililokuwa limeathirika zaidi.

Wakatumia waandishi wachache wenyeji na wanataaluma wengine. Wakatengeneza filamu kali, ambayo sasa imepata tuzo kadhaa za kimataifa. Na imeilaimisha serikali kukubali ukweli!

Filamu hiyo (Damu ya Jimbo la Yingzhou) inaonyesha maisha ya shida ya watoto wa vijiji maskini katika jimbo la Anhui Province. Wanakutana na mambo mawili. Tamaduni zinawazuia kusema ukweli. Na unyanyapaa unaifanya jamii, hata ndugu wa karibu, wawatenge watoto hawa. Hata salamu hawapewi. Kisa? Kila mtu anadhani akiwasaidia naye ataambukizwa. Kifo kinabisha hodi mchanan kutwa. Kila mtu anaona. Hakuna aliye tayari kusaidia. Kisa? Woga wa kifo!

Watengeneza filamu wanaingia kijijini. Wanasalimiana na watoto. Kwa mara ya kwanza, watoto hao wanapata mtu wa kuwashika mkono na kuwagusa!

Mhusika mkuu katika filamu hiyo ni motto aitwaye Gao Jun. Yu mkimya kabisa. Hata akisemseshwa hajibu, hadi mwishoni mwa filamu! Kimya hicho kinawakilisha dhuluma na adha ya raia wengi wasio na mahali pa kusemea katika nchi yao, huku wakigandamiza na maisha duni, matokeo ya uamuzi mbaya wa watawala.

Kutokana na uamuzi huo mbaya, wajanja walianzisha vituo bandia vya kununua damu. Baada ya muda mfupi, maelfu ya wakulima maskini katika jimbo la Henan, walikuwa wameambukiza UKIMWI.

Ghafla, jimbo hilo pekee likasemekana kuwa miongoni mwa watu 280,000 waliouza damu yao, 25,000 walikuwa wameambukizwa virusi miaka ya mwanzo ya 90.

Juzi tukiwa Toronto, mwanaharakati Chi Heng, aliyeanzisha asasi yenye makao makuu Hong Kong kwa ajili ya kupambana na maambukizi yaUKIMWI, alisema China sasa ina watu wapatao milioni moja wenye virusi vya UKIMWI. Wachina wengi walioambukizwa ni wakazi wa vijijini. Huu ni UKIMWI wa kisiasa.

Nguyu ya filamu ya Damu ya Jimbo la Yingzhou nayo ilijadiliwa. Kila mtu aliyesikia habari zao alisifia jitihada za watengenezajiw a filamu hiyo, kwamba zimeibadilisha serikali na jamii ya China. Usiri, urasimu na vitisho vya serikali vilikuwa tishio kwa uhai wa watoto hao.

Sasa wanaishi kwa matumaini. Wanahabari hawa waliona bora wavunje urafiki na serikali ili kuokoa maisha ya masikini na wanyonge, wapiga kura wanaouza damu yao kununua UKIMWI kwa sababu ya umaskini.

Ruby na Thomas, walivunja ukuta wa urasimu na utamaduni, wakatumia taaluma yao kuonyesha uzalendo wao, huku serikali ikiwabeza kwamba wanaichafulia jina katika jumuiya ya kimataifa.

Juzi walipokuwa wakijadili nguvu ya filamu yao, waliifananisha na ya mapanki, - Darwin’s Nighmare ya Hubert Sauper; wakasema ni filamu jasiri inayowatetea wananchi maskini dhidi ya ubabe wa sera mbovu za wanasiasa na matajiri wa ndani na nje.

Wanakemea uzembe wa serikali zetu. Wanataka wanasiasa wasahau kwanza madaraka yao, wakumbatie maisha ya wananchi wao.

Soma vizuri tamko la wabunge wetu kuhusu filamu ya mapanki. Wanafanya kazi kama watu ambao hawakuchaguliwa na wananchi, bali wameteuliwa na rais. Wanadhani lazima wakubaliane naye kwa kila kitu, hata kinachowadhuru wananchi.

Wabunge wetu wanakwepa hoja. Hawaoni wala hawakubali kwamba utandawazi ndilo tatizo. Hawasemi kwamba sera yetu ya uwekezaji ndilo tatizo. Hawakubali kwamba umaskini wa wananchi wetu ndio unawafanya walishwe vitu vya ovyo ovyo.

Zaidi ya hayo, tamko lao na lile la Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanafichua pia siri bila kutamka bayana, kwamba sasa wako tayari kuingilia taaluma ya habari. Wanadharau kazi na taaluma za wengine; wanatukuza vyeo vyao.

Wanawabeza waandishi wa Tanzania kwamba ‘wamepotosha’ hotuba ya rais.
Hawajui kwamba waandishi hawa ni watoto wa wananchi wale wale maskini wanaolishwa mapanki, yaliyooza na yasiyooza.

Hawajui kwamba waandishi nao wana macho, pua, masikio na milango mingine ya fahamu wanayoitumia kuandika habari zao. Wanasiasa wetu wanataka kujenga dhana potofu kwamba waandishi ni makarani wa wanasiasa!

Na kwa tabia ya wanasiasa wetu, kama wangekuwa Wachina, wangekuwa wamewafungia watengeneza filamu ya damu eti wanadhalilisha nchi yao, wanatumiwa na watu wasioitakia mema nchi yao. Kwa wanasiasa wetu, nchi ni ya watawala. Kila anayegusa heshima na maslahi watawala anaambiwa haitakii mema nchi yetu! Anaambiwa si mzalendo. Tutabadilika lini?

ansbertn@yahoo.com +255 744 607553 www.ngurumo.blogspot.com

Makala hii inapatikana pia katika www.freemedia.co.tz

Mwisho

Saturday, August 12, 2006

Tunampenda rais wetu, hatukubali makosa yake

Na Ansbert Ngurumo, Toronto

JUMAPILI hii nipo mbali na nyumbani kwa shughuli nyingine ya msingi kitaifa, lakini nimedhani kwamba ipo haja ya kukamilisha hoja yangu niliyoianza wiki iliyopita, na ambayo sasa imegeuka mjadala wa kitaifa.

Nilipoandika kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwezi uliopita, nilijadili suala la mapanki na ukahaba kidogo. Kwa makusudi kabisa, niliacha suala la silaha.

Wengi waliosoma uchambuzi wangu walitoa maoni yao kwa ujumbe mfupi wa simu na kwa barua pepe. Zaidi ya watu 30 waliungana nami kwamba Rais Kikwete alipotoshwa. Tena wengine walikuwa wakali hata kusema nilikuwa mwoga, nikashindwa kusema Rais alidanganya taifa!

Wengine walitumia lugha ya utani kwamba katika Chama Cha Mapinduzi, mwenyekiti hakosei; hata akisema jambo ambalo wanajua si kweli, watapiga makofi kumshangilia, na hata ikibidi wataandamana kushangilia.

Yawezekana walikuwa wakijadili yaliyojitokeza jijini Mwanza, baada ya viongozi waandamizi wa CCM kuwakusanya wanachama waandamane kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete. Kilichowashtua wananch wengi baada ya hapo ni kubaini kwamba wakati Rais Kikwete anahutubia Watanzania kuhusu ‘ubaya’ wa filamu ya Hubert Sauper juu ya mapanki, wananchi wengi waliomsikia walikuwa hawajaiona.

Ndiyo maana makundi kadhaa ya wananchi yamekuwa yakihaha kuitafuta filamu hiyo, waione. Sasa unajiuliza: Hawa walioandamana kuunga mkono hotuba ya Rais wetu walikuwa wanaunga mkono jambo gani? Sitashangaa kwamba hata aliyewahamasisha na aliyepokea maandamano yao walikuwa hawajaona filamu hiyo!

Wapo wengine walionitumia ujumbe mfupi wa vitisho na matusi, kwamba nawapotosha wasomaji, huku mmojawapo akihoji: “Unamkosoa rais wewe? Huogopi kufa?”

Nilijaribu kuwajibu baadhi yao, na baada ya kubadilishana hoja, wengine walionekana kuelewa, na kukiri kuwa ushabiki wao kwa Kikwete ndilo tatizo. Hawataki kuona akichafua rekodi yake ya kisiasa. Nikamuuliza mmoja wao: “Sasa mbona nyie mashabiki wake ndio mnamchafua? Tambua kwamba huwezi kumsafisha rais kwa kutetea udhaifu wake, bali kwa kutetea maudhui na mikakati inayoteteka.”

Nimekuwa nawaza, najihoji. Hii ndiyo Tanzania tunayotaka kujenga? Tunajenga taifa la watu wanaokubali chochote ambacho wakubwa wanasema na kupitisha, hata bila kudadisi? Na bado tunajidai kwamba tuna ‘taifa hai?’

Huu ndiyo ukereketwa? Je, wasingeandamana ingempunguzia nini Rais Kikwete? Au bado tunaendelea kuamini kwamba fikra za mwenyekiti, hata kama ni potofu lazima zisifiwe na zidumishwe?

Kwa hakika, kwa sababu watu wengi walikuwa hawajaiona filamu hiyo, wakiwamo wabunge wetu, Rais Kikwete amejikuta akiipigia debe filamu aliyodhamiria kuipiga vita. Na kwa kuwa aliozungumza nao walikuwa hawajaiona, ujumbe aliotuma siku hiyo siyo utakaozingatiwa baadaye kila mmoja akishaiona filamu hiyo.

Lakini hoja nyingine ambayo imejadiliwa kidogo mno ni mbinu aliyotumia rais kuzungumzia suala hilo. Jukwaa alilotumia – wananchi wa Mwanza – halikuwa sahihi. Lingekuwa jukwaa sahihi kama angekuwa anafanya uamuzi mgumu na mkubwa wa kuzuia minofu ya samaki wetu kupelekwa Ulaya. Wananchi wangeona wamepatiwa ukombozi. Kilichowafanya Watanzania wengi sasa ‘walumbane na rais’ baada ya kusikia hotuba yake, ni hicho. Hawapingi nia yake, bali mbinu yake. Na wengi hawamlaumu yeye binafsi bali wasaidizi wake wanaomwandalia anayoyasoma na kuyasema mbele ya umma.

Lakini hilo haliwazuii kumwambia kwamba kama angetaka kutoa ujumbe mzito kuhusu mapanki hayo, angeyasemea huko alikokuwa – Ulaya – ambako anadai alikutana na mtengenezaji wa filamu hiyo. Dunia nzima ingemtambua Kikwete ni nani, na uzito wa hoja zake ungepokelewa na wale aliowalenga.

Kwamba hakufanya hivyo akiwa kule, ni ushahidi tosha kwamba lipo jambo ama hakuielewa au aliliogopa. Aliogopa kushushuliwa kwamba anaingilia uhuru wa mawazo ya wanahabari ambao amekuwa akijidai kuwatetea.

Aliogopa kuulizwa na kuhojwa juu ya vibali vya serikali iliyomruhusu mtengeneza filamu kufanya kazi yake baada ya kukagua rasimu ya maudhui ya kazi yake. Aliogopa kuambiwa ukweli kwamba samaki wake wamejaa katika masoko ya Ulaya wakati wananchi wanaambulia vichwa na mifupa, huku wengine wakiokota vilivyooza kwenye mitaro au madampo kwa sababu ya umaskini.

Aliogopa kuulizwa serikali yake inafanya nini kurekebisha hali hiyo. Nadhani hakuwa na majibu ya maswali hayo. Aliogopa ujasiri wa waandishi wa Ulaya ambao hawana nia ya kujipendekeza wala hawaogopi kubanwa na sheria yoyote ya Tanzania kama tulivyo sisi. Maana kama si unyonge wetu, hata pale pale Mwanza waandishi wetu walipaswa kumvaa na kumuuliza maswali mazuri na kuandika stori yenye uzito kuliko kutegemea hotuba yake tu.

Kwamba wamekuwapo waandishi wachache wasiomwonea aibu wala huruma Rais Kikwete katika hili ni ushahidi mwingine wa udhaifu wetu aliotaka kuutumia kusema asemayo akijua tutaandika vivyo hivyo.

Kwamba limekuwapo kundi la watu wake wa karibu linalothubutu kututisha na kutukemea sisi tusiocheza ngoma ya rais, ni ushahisi mwingine wa mambo mawili. Kwanza, wanategemea kutumia kalamu zetu na akili zetu kufanya kazi ya wasaidizi wake; labda kwa kutoamini kwamba wasaidizi wao wanaweza kuandika uchambuzi mbadala na kufunika kazi zetu.

Pili, ni dalili kwamba utawala wa Kikwete unaanza kuingiliwa na kirusi cha vitisho kwa watu wenye mawazo mbadala na waandishi wanaokosoa, kinyume cha ahadi na majigambo yake kufanikisha uhuru wa kujieleza na kuwasialiana.

Ni ishara pia kwamba baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete wanamuundia mabomu bila kujua, na wanataka kuyatetea bila hoja, bali kwa mabavu. Kwa bahati mbaya, inawezekana ameteua wasaidizi wanaomwogopa na wasio wabunifu, wasioweza kumwambia ukweli hata akikosea, na wasioweza kuomba radhi wakikosea.

Kwa ukosefu wao wa ubunifu wanatumia mbinu zile zile zilizotumiwa na watangulizi wao katika miaka zaidi ya 40 iliyopita. Na wanafanya hivyo wakiwa karibu mno na rais, huku wakiwa wa kwanza kila siku kumsikia akizungumzia ari mpya ambayo wenyewe hawana. Wanatumia nguvu ya kizamani huku yeye akisisitiza nguvu mpya.

Tukubali. Tukiri makosa tuweze kujenga taifa. Rais amekoseshwa. Naye amekosea. Alipaswa kuukema utandawazi si mpiga filamu wa mapanki. Alipaswa kuwapa wananchi matumaini ya kutumia raslimali zao kujiendeleza.

Maandamano, vitisho na ghiliba zinazotumiwa na wasaidizi wake vinamchafua rais mwenyewe. Na wapo wanaonza kusema sasa kwamba anawatumia wasaidizi wake kichini chini kunyamazisha sauti zinazomkosoa na kumpinga. Hili nalo, asipolipinga kimkakati na kuliweka sawa, litamchafua.

Bahati mbaya aliyonayo rais wetu wa sasa, hapati fursa ya kujua watu wake wanamsemaje. Hakuzoea kusemwa hadharani. Kwa miaka 10 mfululizo amekuwa akisifiwa. Amekaa mbali na msuguano na jamii ya Watanzania akiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Siasa zinazowahusu wananchi moja kwa moja zimekaa mbali naye; ndiyo maana ilimuwia rahisi kufanya kampeni ya urais bila kipingamizi kikubwa.

Lakini sasa akubali kwamba amerejea nyumbani. Akubali udhaifu wake na kuukosoa pale utakapobainika. Ajue, na wasaidizi wake wajue pia, kwamba yeye si mungu. Ni binadamu wa kawaida, anaweza kukosea. Watamsamehe, watamwelewa na kazi itaendelea kama kawaida.

Ajue, na akubali, kwamba wengi wanaomkosoa hawana ugomvi binafsi naye. Wanataka atambue kuwa yeye ni raia nambari wani. Lazima asugue na kung’arisha kauli zake kwa niaba ya Watanzania. Wanampenda rais wao na nchi yao. Lakini hawapendi, wala hawakubali makosa yake.

ansbertn@yahoo.com www.ngurumo.blogspot.com

Makala hii inapatikna pia katika www.freemedia.co.tz

Sunday, August 06, 2006

Kikwete wa Dodoma si yule yule wa Mwanza?

GHAFLA, Rais Jakaya Kikwete amewashtua Watanzania kwa kuzungumzia kwa ukali filamu ya Darwin’s Nightmare iliyoandaliwa na raia wa Ufaransa, Hubert Sauper. Ameikemea na kuishutumu kwa mambo mengi, lakini Watanzania aliokuwa anwaambia hawajawahi kuiona! Pili, amepotosha ukweli kwamba wakazi wa Mwanza hawali mapanki, na kwamba hakuna ukahaba. Ukionoa wanaCCM wa Mwanza walioandaliwa na viongozi wa chama na serikali kuandamana kumuunga mkono Rais na kumlaani Sauper, Watanzania wanaojua hali halisi na wasiogubikwa na ushabiki wa CCM wamemwambia Rais Kikwete ukweli kwamba amechemsha. Yafuatayo ndiyo niliyomwambia kupitia safu ya Maswali Magumu katika gazeti la Tanzania Daima, Jumapili, Agosti 06, 2006. ENDELEA.
RAFIKI yangu mmoja ameniambia kwamba katika kipindi cha miezi takriban minane ambayo Rais Jakaya Kikwete amekaa madarakani, amekutana na Kikwete wawili tofauti.
Wa kwanza ni Kikwete taifa, kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dodoma, Desemba mwaka jana (2005). Wa pili ni yule aliyehutubia Watanzania kupitia kwa wazee wa Mkoa wa Mwanza, mwanzoni mwa wiki hii.
Kikwete wa kwanza alikuwa mahiri wa kuzungumza. Aligusa maisha halisi na mtarajio ya wasikilizaji wake, hata wasio Watanzania. Alizungumza yale ambayo kwa huluka na mazoea, si kauli ya viongozi wetu wakuu tuliowazoea, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kikwete huyu wa kwanza ni mtu wa watu, kiongozi wa Watanzania wote, anayejua matatizo yaliyowasumbua kwa muda mrefu, na ambaye ameahidi kufanya kila anachoweza kuyaondoa, na kuwaletea maisha bora.
Ni Kikwete anayewapa Watanzania matumaini makubwa. Ni Kikwete aliyejua kuchanganya maneno matamu yaliyokolezwa na hoja kadhaa alizoazima kutoka kwa wapinzani, kuonyesha kwamba yu tayari kukosoa yaliyowashinda watangulizi wake.
Yule alikuwa Kikwete tishio la wanaosemekana kutumia vibaya madaraka yao, waliotafuta kujineemesha badala ya kuwaneemesha Watanzania. Wa kwanza alikuwa Kikwete msema kweli.
Kikwete wa pili, huyu wa Mwanza, hakuwa mkweli sana. Hakuwa msema kweli. Hotuba yake haikuwa na mvuto kwa wasikilizaji wote. Hakuwa Kikwete mwenye uso wa tabasamu. Alinuna. Alionya na kulaani.
Hotuba yake haikuwa na maneno matamu tuliyozoea. Haikuwa na ahadi. Huyu hakuwa Kikwete wa wananchi. Alikuwa Kikwete Rais wa nchi.
Ni Kikwete ambaye hakueleweka kwa baadhi ya wasikilizaji wake. Aliwachanganya. Kilichomfanya awachanganye wasikilizaji wake ni msisitizo usio wa kawaida, huku akikemea waandaaji wa filamu ya Darwin’s Nightmare, kwamba wakazi wa Mwanza hawali vichwa vya samaki, na kwamba jiji lao halina makahaba!
Akashindilia hoja yake kwa kusema wanaosema mapanki yanaliwa na kwamba kuna ukahaba Mwanza ni waongo na wazandiki!
Wanaojua ukweli wa hali halisi ya Mwanza, alikokuwa, wakashindwa kusema rais ameongopa; wakasema ameshauriwa vibaya, amepotoshwa. Ila hawakusema kwamba alipopotoshwa, hakupotoka! Hawakusema kwamba alipodanganywa, hakuwadanganya Watanzania.
Sana sana, walianza kujiuliza: Nani amemlazimisha rais kusema maneno haya? Kuna msukumo gani nyuma yake? Je, hili ni tatizo kubwa la kitaifa ambalo ilikuwa alizungumzie?
Je, ndiyo sababu iliyomfanya apumzikie Mwanza, siku chache baada ya kutoka kwenye matibabu Ulaya? Si angesubiri kwanza akatembelea mitaa kadhaa, akatembelea masoko na kuona hali halisi kabla hajahutubia taifa?
Sasa kama rais anasemeshwa uongo, watu hawa wanaojua ukweli watamwona vipi baadaye, hata akisema jambo lililo kweli? Na kama ameshasema yeye, nani atarudi baadaye kurekebisha kauli ya rais, kwamba alikuwa ameteleza kwa kuwa ulimi hauna mfupa?
Wengine walifika mahali pa kusema: “Kumbe hata Kikwete anaweza kuongopa?” Nikawauliza: “Kwani nyie mnamwonaje? Yeye si binadamu kama nyie?”
Lakini hoja kuu hapa ni kwamba kusema uongo ni kosa. Na adhabu yake inafahamika. Nani atamwadhibu Kikwete? Kwa kuwa aliyesema uongo ni rais, hakuna mtu wa kumwadhibu, lakini yeye ana uwezo wa kuwaadhibu waliomsababishia kusema uongo. Basi afanye hivyo, na ajifunze kutokusoma kila kitu wanachomwandikia.
Ajue pia namna ya kuchuja ukweli katika mapendekezo anayoletewa na wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo mawaziri. Maana tayari zipo dalili kwamba baadhi yao wamejiingiza katika kashfa, ambazo wanamsukumia yeye azibariki bila kujua, kulinda masilahi yao binafsi.
Hawa wote wanaomdanganya ni wateule wake. Kama anawaamini kwa asilimia 100, huku wakimdanganya, anatarajia Watanzania wamwamini yeye kwa asilimia 100? Sana sana watasema ama aliwateua bila kujua, kwa hiyo anadanganywa kwa bahati mbaya; au tukubali kwamba lao ndilo lake, anajua kinachoendelea lakini anafanya hivi kulinda masilahi fulani.
Kwa mfano, hili la Mwanza limeleta hisia kwamba Rais Kikwete amebanwa na ‘wahisani wake’ akanushe tuhuma zilizo katika mkanda huo, ili kusafisha sura na jina la Tanzania. Akakosea mbinu.
Wakati anasisitiza kuwaita wazandiki waliotengeneza filamu hiyo, wapo Watanzania waliokuwa sokoni kununua mapanki hayo. Wengine walikuwa maeneo ya Igoma wanaokota yaliyotupwa kwenye dampo.
Wengine walikuwa wameshika pua kuzuia harufu mbaya ya mapanki wakati gari likipita katika mitaa ya jiji kwenda kumwaga mapanki hayo. Wengine walikuwa kiwandani wanalangua lori la mapanki hayo ili baadaye wayakaushe na kuwauzia wanunuzi wa Mwanza na kwingineko.
Mkoani Kagera, raia walikuwa wanakimbizana na polisi kujibu walikopata samaki waliokutwa nao; maana wenye haki ya kuvua samaki si wananchi bali wenye vibali maalumu au wenye viwanda!
Wakati huo huo, mabinti wadogo waliohitimu darasa la saba, na dada zao wakubwa – wengine ni wasomi kwenye vyuo – walikuwa wanahitimisha muda wao wa kulala, kujiandaa na kibarua kigumu usiku katika mitaa ya katikati ya jiji.
Baadhi ya wanaume waliomsikia ndio wateja wa kina dada hao. Nadhani nao walimkejeli usiku huo kwa kufanya maasi yasiyosemeka.
Hawa wote walishindwa kusema, lakini waliona kiongozi mkuu wa nchi amepotoka, hasemi ukweli.
Naamini kwamba baada ya wananchi wa Mwanza kumkosoa rais kupitia vyombo vya habari, amediriki kutuma wasaidizi wadogo kuona ukweli wa maisha ya Watanzania.
Sasa wanasubiri awachukulie hatua waliomkosesha. Wanasubiri kuona kama atakuwa muungwana na kusahihisha kauli yake, huku akiweka mikakati ya kuondoa kero hizo.
Akifanya hivyo, anaweza kupunguza makali ya hisia za Watanzania wanaomweka katika kundi la watu wanaoweza kupinda ukweli. Atasaidia pia kuifanya jamii ijue kwamba bado Kikwete ni mmoja.
Na huyo mmoja hatapatikana hadi wa kwanza atakapomuua wa pili. Vinginevyo, tukubaliane kwamba Watanzania wataamua wamwamini na kumfuata Kikwete mmojawapo; wa Dodoma au wa Mwanza.

ansbertn@yahoo.com +255744607553

Mkala hii inapatikana pia katika www.freemedia.co.tz

Monday, July 03, 2006

Uteuzi wa Makamba CCM una matundu

BAADA YA MWENYEKITI WA CCM, JAKAYA KIKWETE, KUMTEUA YUSUFU MAKAMBA KUWA KATIBU MKUU BADALA YA PHILLIP MANGULA, WATU WENGI WAMESHINDWA KUFICHA HISIA ZAO KUHUSU UTEUZI HUO. HAPA, MWANDISHI Kanku Gambire WA SAFU YA NASIKITIKA KATIKA GAZETI LA Tanzaia Daima, anachambua uteuzi huo, akiwalinganisha Makamba na Mangula. SOMA

NASIKITIKA kwamba uteuzi wa Yusufu Makamba kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) una matundu.
Hadi hapo Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete atakapoamua kutoa hadharani nini hasa sababu ya kumteua Makamba kuwa Katibu Mkuu, kila mwenye kujua siasa za Tanzania atabakia kupapasa.
Ni kupapasa haswa! Kwani Katibu Mkuu aliyeondolewa, Philip Mangula na Yusufu Makamba, hawawezi kulinganishwa na sifa zao angalu kushabihiana katika nyanja mbalimbali.
Mangula ni mtendaji wa kirasimu; anayejali na kuheshimu kanuni na taratibu. Makamba ni mwanasiasa mwenezi wa wazo la mkubwa wake hata kama mantiki yake ni ndogo sana.
Mangula ni mwanasiasa anayeshikilia usimamizi wa taratibu na anayeegemea andiko. Makamba ni msema chochote ili kukabiliana na hali yoyote iliyojitokeza ikiwa ni pamoja na kukana au kukiri jambo lolote ili kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.
Mangula anajipa muda kufikiri na kutafuta ufumbuzi wa jambo wenye kukubalika kwa mantiki kuu. Makamba ni maarufu kwa “uchochezi” unaolenga kudhoofisha misuli ya mlengwa.
Mangula ana uwezo na uzoefu wa kusimamia utatuzi wa mgogoro hata kama ni kwa ujanja na ghiliba za chama chake kikubwa. Makamba anaagukia kwenye matumizi ya dola na viotisho.
Katika hili, ni vigumu kufikiria jinsi Makamba angefanya kazi ya uwakilishi wa chama chake katika kutafuta usuluhishi kati ya CCM na CUF na kuzaliwa kwa muwafaka.
Makamba ni mwelekezaji wa utekelezaji wa matakwa ya chama chake kwa kadri alivyoelewa jambo. Mangula, pamoja na kuwa mwelekezaji, ni muumbaji wa taratibu asiyesubiri kuwekewa mifumo ya kutekeleza.
Mangula siyo msemaji sana bali mzingatiaji wa mwelekeo wa chama chake. Makamba ni moto wa kiangazi; mwanasiasa katika maana ya uanasiasa pokopoko ambao mara nyingi hukariri uadilifu wa chama usioonekana kwa macho ya wengi.
Makamba na Mangula ni watumishi wa CCM ambao uaminifu wao katika chama hauhitaji kutiliwa mashaka. Bali Mangula ana chembechembe za kujiamini na hata kuwa na msimamo hasi, wakati Makamba ni mfuasi wa kile alichoambiwa na “bwana mkubwa.”
Makamba ni maarufu kwa kumimina nahau za Kiswahili wakati akiongea na kuchagiza hadhira yake – ile sehemu ya kazi ya mwenezi wa chama ambayo Kikwete amemnyima.
Mangula ni mtawala anayeongea machache lakini mwenye king’ang’anizi kwa kauli za awali na misimamo ya chama hadi hapo atakaposhurutishwa kuwa tofauti.
Makamba ni mwoga wa kitu kipya kama alivyoonyesha wakati wa kuweka jiwe la msingi la uwanja mpya wa mpira jijini Dar es Salaam, mbele ya rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Makamba alilalama na kukiri pia kwamba yeye hawezi kasi mpya na akaonyesha kuwa huenda akatupwa nje ya duara la siasa iwapo wachagizaji wa “kasi mpya” wataingia madarakani.
Wakati inawezekana kabisa kwamba hiyo inaweza kuwa ghiliba, kwa kuzingatia uhusiano uliopo kati ya Makamba na Rais Kikwete na nafasi yake ya sasa, hapa kuna mwanasiasa asiye na soni kwa lolote alisemalo – la kweli, la kuficha ukweli au la kubabaisha.
Kwa upande mwingine, Mangula ana uwezo wa kuchukua maamuzi na kujiegemeza kwa “kundi” lake na kuonyesha hivyo.
Kila chama duniani huwa na makundi. Makundi hayo huwa na mawazo mbalimbali na wakati mwingine kukinzana lakini kwa shabaha ya kunoa chama na si kukidhoofisha au kukiua.
Wakati Makamba ana woga wa kuwa na kambi katika chama na kuwa wazi juu ya hilo, Mangula amewahi kuhusishwa na kambi na hakukana. Labda huo ndio mwanzo wa jino kulegea na hatimaye kung’olewa.
Mwisho: Viwango vyao vya elimu ya darasani havilinganishiki. Hapa Makamba yuko nyuma. Umiliki na usimamizi thabiti wa shughuli za utendaji ndani ya chama unahitaji umahiri utokanao na elimu pana na si wingi wa mikutano ya hadhara.
Unaweza kusema iwe na iwavyo, kwani CCM ni chama changu? Na hivyo ndivyo nisemavyo. Lakini kusaidia wana-CCM kufikiri na kutafakari ni moja ya sababu za kusikitika kwangu leo hii.

kankugambile@yahoo.com

Wednesday, June 21, 2006

Watoto wa takrima wakongwe, jengo jipya

Na Nikita Naikata

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wabunge wa Tanzania kuwa nadhifu na makini ili wafanane na jengo jipya la Bunge la Jamhuri ya Muungano lililogharimu sh. milioni 31. Huku baadhi yao wakijiandaa kukubaliana na rais, mchambuzi NIKITA NAIKATA anasema wabunge ni watoto wa takrima, wakongwe wasio na jipya katika jengo jipya! Soma hapa chini.

SITAKI kuambiwa kwamba kwa kuwa sasa kuna jengo jipya la Bunge, pale Dodoma, basi fikra za wabunge zitakuwa mpya pia.
Sitaki kabisa kushawishiwa, hata na Rais Jakaya Kikwete, kwamba wabunge watakuwa wapya kifikra kwa kuwa watakuwa wanatumia jengo jipya la Bunge lililogharimu mabilioni ya shilingi.
Nasema hivyo kwa kuwa bunge si jengo. Bunge ni watu waliochaguliwa, kwa njia halali au hata kwa hila, kuwa wawakilishi wa wananchi katika Baraza la Kutunga Sheria.
Historia inaonyesha kwamba kumekuwapo na wawakilishi wa wananchi ambao hawakuwahi kuchaguliwa kwa kura za “nipe nikupe” ambao walifanya uwakilishi wa maana zaidi kuliko hawa wa leo.
Nyakati ndizo ziliamua nani awe mwakilishi. Ni matakwa ya nyakati yaliyoathiri fikra zao. Ni historia iliyotoa majukumu kwa waliotokea kuwa wawakilishi bora.
Na hao walitokea kwenye vibanda. Walikaa katika nyumba za kawaida na kupitisha uamuzi mzuri uliolenga kunufaisha jamii.
Bali mazingira yanabadilika. Uwezo umeongezeka. Nyenzo za kufanyika kazi zimeongezeka. Mahitaji mapya katika nyakati mpya yameongezeka pia kwa kiwango kikubwa.
Hivyo, kuwa na jengo jipya la Bunge, lenye ofisi za wabunge, vifaa, nafasi pana ya kumwezesha mbunge kupumua vizuri na kupata taarifa zaidi, ni mambo muhimu katika nyakati tulizomo.
Lakini jengo zuri la kisasa la Bunge haliwezi hata kuhusishwa na fikra nzuri wala bora. Sitaki hata kodogo kushawishiwa hivyo! Kuna sababu nyingi. Hapa tuangalie chache zifuatazo.
Kwanza, wabunge hawana upya wowote. Wengi, hasa katika uchaguzi uliopita, wameingia bungeni kwa njia ya takrima. Rushwa!
Takrima ni rushwa iliyohalalishwa na bunge kwa kuitungia sheria. Wenye fedha, wakatumie fedha zao, kwa madai ya kukirimu wananchi wapiga kura, na kujizolea kura za kuwapeleka waliko.
Upya wa watoto wa takrima uko wapi? Fikra mpya na bora, katika “nipe nikupe” zitatoka wapi? Kuna uzuri gani katika mashindano ya kukatana shingo kwa hela na hila na mshindi atakuwaje na fikra sahihi za wananchi aliowahonga?
Jengo jipya lililojaa sehemu kubwa ya waliopatikana kwa hongo iliyohalalishwa na jengo la zamani, litakuwaje chemchemi ya fikra nzuri? Sitaki kusikia!
Pili, kinachofanya jengo kuwa la maana ni wale waliomo, nia na shabaha zao na kazi zinazofanyika humo. Nini basi kinafanyika katika jengo jipya?
Uchaguzi mkuu hadi uchaguzi mkuu mwingine, chama kimoja – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kimeendelea kuzoa kura (si kushinda) kwa hila na ujanja.
Kikiwa madarakani, kimeweka na kusimamia utaratibu unaoendeleza hodhi ya siasa nchini. Kwa mfano, kwa kutumia wingi wa wabunge wake, kimekataa kuruhusu mfumo wa uwakilishi wa uwiano.
Kukataa uwakilishi wa uwiano ni kukubali kutawala kwa mabavu. Tuchukue mfano wa jimbo lenye wapiga kura 60,000 ambako wagombea wawili wamepata kura 28,786 na mwingine 28,999 na huyu wa pili aliyepata kura 213 zaidi ndiye anatangazwa mshindi.
Hakika huu si ushindi wa faraja. Huu ni ubunge unaopwaya. Zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura katika jimbo wanakuwa wamekukataa lakini kwa mujibu wa sheria mbovu, unakuwa mbunge kwa shinikizo tu.
Kuna uhusiano gani kati ya fikra hizi juu ya uwakilishi na jengo jipya la bunge? Je, jengo litabadili fikra hizo au litazisimamia zaidi katikati ya viyoyozi imara na nuru kuu ya taa za kisasa?
Tatu, si siri kwamba wabunge wa CCM wana tabia ya kuunga mkono kila hoja ya serikali hata kama wanajua kwamba inapwaya na hata kuwa na madhara makubwa kwa wananchi baadaye.
Hili linafanywa kinafiki ili kulinda maslahi ya chama chao kinachoongoza serikali. Je, unafiki na usaliti wa wananchi kwa njia hiyo unaweza kubadilishwa na jengo jipya?
Nne, serikali “imekubaliana” na uamuzi wa mahakama wa kufuta sheria iliyoruhusu rushwa iitwayo takrima. Lakini huko ni kufuta kipengele kwenye vitabu. Si kuacha kutoa rushwa kwa maelezo mengine.
Je, mara moja jengo jipya limefanya wabunge wawe wanaharakati wa kweli wa kusambaza taarifa za kupinga takrima iliyowapeleka bungeni au wataendelea kutoa chini ya jina jingine?
Tano, jengo jipya lina uhusiano gani na mabadiliko ya taratibu za bunge katika kupokea miswada? Uzoefu ni kwamba serikali ndiyo imekuwa ikipeleka miswada bungeni. Kwa maana nyingine, serikali imekuwa ikitafuta msaada wa bunge wa kutawala inavyotaka.
Miswada binafsi ya wabunge imekuwa haba na pale ilipopita, ilikuwa ya kujikomba kwa serikali na kujitafutia umaarufu wa binafsi miongoni mwa watawala.
Jengo jipya lina uwezo wa kuchochea miswada ya binafsi? Linaweza kuondoa hodhi ya taratibu za kupeleka miswada na kuamsha akili ya kukubali hoja badala ya kuangalia muswada umeletwa na nani na kutoka kambi ipi?
Sita, bunge bado limejaa fikra kwamba wabunge wa upinzani ni walalamishi tu na hupinga kila kitu. Fikra hizo huwafanya wabunge wa CCM kuwaona wale wa upinzani kuwa hawawezi.
Mkondo wa fikra za hawawezi umetapakaa kila kona ya utawala kiasi kwamba asiye mwana-CCM hapewi nafasi hata kwenye bodi ya shirika la umma! Je, fikra hizo mbovu zitaondoshwa na mng’aro wa jengo jipya la bunge?
Kuna mengi ambayo wabunge, na hasa wabunge kutoka CCM, wamebeba kutoka jengo la zamani hadi jipya. Serikali pia imebeba fikra hizo hizo na kuziingiza kwenye jengo lililojengwa kwa mabilioni.
Sitaki kuambiwa kwamba jengo litaleta fikra mpya. Jengo, na huu ndiyo ukweli mweupe, litaimarisha fikra kongwe na chafu zilizoasisiwa kulinda maslahi ya waliomo serikalini.

nikitanaikata@yahoo.com

Monday, May 29, 2006

Anna Senkoro ameangukia pua


WIKI iliyopita, mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania, aliyeshiriki kwenye kinyang'ayiro cha kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Anna Senkoro, kupitia chama cha TPP-Maendeleo, ametangaza kwamba anakihama chama hicho. Tayari amerejesha kadi yake kwa viongozi wa TPP-Maendeleo. Hakuna anayejua kama anaacha siasa au chama. Lakini wachambuzi wameanza kujadili. Hapa chini upo uchambuzi wa Nikita Naikata, mwandishi wa safu ya NASIKITIKA katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili ukurasa wa 10, Mei 28, 2006. SOMA, TOA MAONI.

NASIKITIKA kutosikitika kwamba Anna Senkoro, mwanamke wa kwanza nchini kugombea kiti cha urais, ameamsha mikono na kusema, “yamekwisha!”
Ya kwake yalijulikana mapema. Anna anasema hataki tena siasa za chama chake. Anasema amerudisha kadi. Anasema hajaamua aende chama gani baada ya hapa.
Anna analiza. Anasema, hata hivyo, kwamba hatakwenda chama chochote cha upinzani kwa kuwa alipokuwa amelazwa hospitalini hakuna kiongozi wa upinzani aliyekwenda kumwona.
Anna alikuwa mgombea urais kutoka chama kidogo cha mtu mmoja mwenye madaraka makubwa – PPT-Maendeleo cha Peter Kuge Mziray.
Katikati ya kampeni, Anna alianza kulalamika. Hana fedha za ruzuku za kuendeshea kampeni. Huku bosi wake kichama, Mwenyekiti Mziray akitangaza hadharani kwamba yeye anamuunga mkono mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Haijulikani na labda haitajulikana hivi karibuni, kwa nini PPT-Maendeleo waliweka mgombea urais wakati mwenyekiti wake anapiga debe kwa ajili ya mgombea wa CCM.
Inawezekana basi kwamba mwenyekiti wa PPT-Maendeleo alijua mapema kwamba mgombea wake hashindi. Kwa hiyo alikuwa na ajenda nyingine.
Na kuonyesha kwamba chama ni cha Mziray, hakuna aliyenyoosha kidole kupinga msimamo wake wa kuwa CCM na PPT-Maendeleo kwa wakati mmoja na hasa wakati wa uchaguzi.
Bila shaka ajenda ya PPT ilikuwa ya viongozi wa vyama vingine pia. Kwani baadhi ya vyama vya upinzani viliweka wagombea urais katika mbio za mwaka 2005 ambao hata wao – wagombea na viongozi wao, walijua hawaendi kuleta chochote!
Kulikuwa na fununu kwamba vyama vya upinzani vingepata fedha za kuendeshea kampeni kutoka serikalini na asasi ya Demokrasi ya Uholanzi.
Kwa msingi huo, chama kinachoweka mgombea urais kingekuwa na fungu kubwa la mgawo. Kwa hiyo kugombea likawa suala la “Nenda tu ugombee ili tupate fedha na utangaze chama chetu…”
Ndivyo Anna alivyoingia ulingoni. Mwanamke wa kwanza Mtanzania kugombea urais katika uchaguzi mkuu.
Mwanamke wa kwanza kutoka chama kichanga cha siasa nchini, kisichokuwa na uongozi makini wala mwelekeo unaoeleweka, kugombea urais.
Mwanamke wa kwanza, kuamua kujitupa tu au kutupwa kwenye kinyang’anyiro alichojua au ambacho hakujua nguvu zake, na katikati ya kukurukakara, mwenyekiti wake akamwambia kwamba asilolome sana, vinginevyo atamfukuza uanachama.
Hakuna maelezo ya kitaaluma, lakini mchoko wa kampeni, vitisho vya kufukuzwa uanachama, kudharaulika mbele ya wenye mali na fedha nyingi za kuendesha kampeni kwa rushwa iitwayo “takrima,” bila shaka vilichangia Anna kuugua baada ya uchaguzi.
Kilichoongeza uchungu la labda kulegeza zaidi mishipa ya Anna, ni matokeo ya uchaguzi – kiwango cha kura alizopata, hata kama tangu mwanzo aliamini kuwa hatakuwa rais wa Tanzania.
Nasikitika kwamba sasa Anna Senkoro ameamsha mikono na kuaga chama chake. Bali anasema mambo kadhaa yenye kuhitaji uchambuzi mdogo.
Anna anasema aligombea urais ili kuwahimiza wanawake nchini kujitokeza kuwania nafasi za juu ya kuchaguliwa na kuongoza.
Je, Anna alikuwa anajua kwamba chama alimogombea hakikuwa chama cha washindi? Anataka kusema kwamba wanawake wachukue mfano wake wa “kujitupa” tu bila uchambuzi wa chama kipi kinaweza kuwa chombo cha kusafiria?
Je, anataka wanawake wawe wanachomoka majumbani mwao na kujitangaza kugombea urais au ubunge kupitia chama chochote kile kilichopo alimradi wanataka uongozi?
Je, anataka wanawake waamini kwamba hata bila kujiandaa na kuandaliwa, bila kuwa na chama chenye uongozi thabiti na sera na hata mvuto wa hoja, basi wajitose tu?
Anna anasema lengo lake kubwa lilikuwa kuwapa changamoto wanawake kujitokeza kujaribu BAHATI yao katika siasa. Nasikitika sana kwamba hii sasa siyo siasa, ni BINGO – patapotea!
Anna anasema hajaamua kwenda chama kingine. Hii ina maana anataka kuingia chama kingine. Amesema hatakwenda vyama vya upinzani kwa kuwa alipokuwa mgonjwa hawakwenda kumwona.
Sasa kila mmoja anaona kwamba ama Anna ataanzisha chama chake, atajiunga na ambacho hakijaanzishwa au atakwenda CCM. Je, hilo nalo ni fundisho la Anna ambalo anataka wanawake waige?
Nasikitika kwamba hakuna cha kuiga kwa Anna Senkoro. Kama funzo tu, ni kujifunza kuacha kufanya aliyofanya. Basi!
Kama PPT-Maendeleo na uongozi wake, Anna hakuwa na dira katika chama chake na kitaifa. Yeye ni tunda la fukuto. Kasi ya mchomoko wake haikuwa na jipya, na kama wengine wa aina yake, ameangukia pua.
Nasikitika hakuna wa kumwiga Anna Senkoro.

kankugambile@yahoo.com

Sunday, May 21, 2006

Nimeshinda Mauti

NILIPOWAELEZA baadhi ya rafiki zangu walicheka, wengine wakatania kwamba aliyeshinda mauti ni Yesu Kristo tu, kwa vile, kama waaminivyo Wakristo, ndiye alikufa halafu akafufuka. Lakini ukweli ni kwamba tangu Mei Mosi hadi Mei 15, 2006 nilikuwa hoi, kitandani.

Kwa siku tano za kwanza, nililala nyumbani kwangu nikiwa natumia dawa nilizopewa hospitali. Nilikuwa nasumbuliwa na Malaria INAYOKATAA DAWA, ambayo vijidudu vyake vilikuwa ngangari kinoma; ikabidi nirudishwe hospitali Mei 6, baada ya kumaliza dozi nzima ya Arinate.

Nililazwa katika hospitali ya Dk. K.K. Khan, katikati ya jiji la Dar es Salaam, nikatundikiwa dripu 39 (tisa za Quinine na 30 za antibiotics). Kichwa kilinitwanga kwelikweli kwa siku 10 mfululizo.

Nakumbuka mara ya mwisho niliugua mwaka 1981. Lakini mara hii ilikuwa hatari zaidi. Nashukuru nimepona, nimerejea katika kundi la wanablogu wenzangu. Kumbuka, MBINGUNI (maana nisingekwenda motoni) hakuna BLOGU. Ndiyo maana nimechomoa!

Tuesday, April 04, 2006

Serikali Kusomesha Waandishi

MALUMBANO kati ya waandishi na Dk. Harrison Mwakyembe, na kati yake na serikali kupitia Bunge, juu ya wajibu wa serikali kusomesha waandishi sasa yamepata mwelekeo. Soma stori hii hapa chini:

SERIKALI imekubali ushauri wa Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwasomesha waandishi wa habari na kutunga sheria zinazolinda taaluma na maslahi yao.

Katika majibu ya maandishi kwa mbunge huyo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammad Seif Khatib, amesema serikali itaandaa programu ya kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari yanayolenga elimu ya juu.

“Majukumu makubwa ya wizara katika programu hiyo ni kuratibu upatikanaji wa misaada kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na ya muda mrefu ndani na nje ya nchi.

“Katika programu hiyo, wamiliki wa vyombo vya habari watatakiwa kuandaa orodha za wanahabari wanaohitaji mafunzo, na kuchangia gharama za mafunzo hayo.”

Kwa sababu hiyo, waziri alisema serikali itaandaa rasimu ya sheria inayotekeleza maelekezo ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003.

Kwa majibu wa maelezo ya waziri, sheria hiyo itaunda chombo ambacho kitalinda na kutetea taaluma na maadili ya habari.

Serikali pia imesema itaandaa programu ya mafunzo yatakayowawezesha waandishi kubobea katika maeneo maalumu.

“Lengo la programu hii ni kuipatia serikali sekta ya habari wanahabari wenye taaluma za uchumi, kilimo, uhasibu, sheria, utamaduni na michezo,” alisema waziri.

Majibu ya Seif Khatib kwa Dk. Mwakyembe ni sehemu ya majibu mengine yanayotolewa na serikali kwa hoja za wabunge kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Katika hoja yake ya msingi, kwenye kikao cha pili cha bunge kilichopita, Dk. Mwakyembe alishauri serikali iweke utaratibu wa kuwasomesha waandishi ndani na nje ya nchi, itenge walau nafasi 10 hadi 20 kwa mwaka (kuanzia mwaka huu), ili waandishi nao wapate fursa ya kujiendeleza kielimu na kubobea katika taaluma yao kama walivyo wanataaluma wengine.

Alisema hatua hiyo itapunguza baadhi ya manung’uniko yanayotokana na makosa ya kitaaluma, na kuongeza ujuzi na uelewa katika masuala yanayoandikwa.

Alijenga hoja kwa kusisitiza kwamba baadhi ya waandishi wanafanya kazi hiyo bila kuwa na elimu ya kutosha, na kwamba ni wajibu wa serikali kuwawezesha ili viwango vyao vya elimu viendane na mahitaji ya kitaaluma na zama tulizomo.

Alitoa mfano wa serikali ya Uganda ambayo ilipitisha sheria kuwalazimisha waandishi wasome walau hadi kiwango cha shahada moja; akasema ingawa uamuzi huo uliwatesa na ulilalamikiwa mwanzoni, umekuwa wa manufaa kwa waandishi wa Uganda na jamii yao kwa ujumla.

Aliishauri serikali isilazimike kuchukua uamuzi mgumu kama huo, lakini ianze pole pole kutoa nafasi na kuzilipia katika vyuo vikuu ndani na nje ya nchi. Dk. Mwakyembe alipendekeza kwamba jukumu hili lisiwe la wamiliki wa vyombo vya habari, bali la serikali.

Hoja hiyo haikuwapendeza baadhi ya waandishi; wakadai kwamba mbunge huyo ana jeuri ya usomi, amewatukana kwa kusema hawajasoma vizuri. Baadhi walimuunga mkono wakasema ipo haja ya serikali kuwasomesha waandishi kwa sababu kihistoria imewatelekeza.

Alipoitembelea wizara husika wiki kadhaa zilizopita, Rais Jakaya Kikwete, alichochea hoja kwa kumshauri waziri aweke utaratibu wa kuwaendeleza waandishi kitaaluma.

Wednesday, March 15, 2006

Nani anasema JK hayawezi?


Mwanablogu Reginald Simon Miruko ndiye kanitumia picha hii. Miss Personality, Witness Manwingi, ambaye alikuwa mwakilishi wa Tanzania katika shindano la kumtafuta Miss Tourism wa Dunia mwaka 2006 anasalimia Rais Jakaya Kikwete wakiwa wamekumbatiana. Wote wanatabasamu, wanapendeza na wameshikana VIZURI! Au nimeshindwa kuitafsiri barabara?

Monday, March 13, 2006

Kikwete, CCM na mapato haramu

MAJUZI, Rais Jakaya Kikwete alikutana na 'wafadhili' wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jijini Dar es Salaam, waliokisaidia kupata pesa za kampeni mwaka 2005. Katikakuzungumza nao, Kikwete alisisitiza mambo mawili. Kwanza, aliwaomba wana CCM wasilewe ushindi walioupata mwaka 2005, badala yake wajiandae kwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Hii ni changamoto nzuri kutoka kw amtu anayetarajiwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho katikati ya mwaka huu. Pili, aliwaasa wanachama wenzake waanze kutafakari namna ya kupata MAPATO HALALI kwa ajili ya kampeni. Hili ndilo linazua maswali, hasa kwa kuwa limesemwa sasa baada ya chama kushinda kwa nguvu kubwa ya pesa, huku kikiwa kinashutumiwa kusaidiwa na matajiri kadhaa wanaojihusisha na ujambazi. Je, Kikwete anakiri kwamba ameingia madarakani kwa kutumia pesa haramu? Na je, vyanzo haali vikikosekana, au kama havitatosha, CCM itapataje ushindi? Au itarudi kule kule?! TUJADILI.

Monday, March 06, 2006

Waandishi katika mjadala mzito


KUNA mjadala umeibuka. Ulianzia Bungeni Dodoma, katika kikao cha pili cha Bunge hilo, cha Februari 2006. Mwandishi wa zamani, ambaye sasa ni mwanasheria na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, alichokoza nyuki pale alipojenga hoja kwamba Bunge liazimie kuibana serikali iwasomeshe waandishi kwa kuwa baadhi yao, kama si wengi wao, hawana elimu ya kutosha, uandishi unabadilika na kukua kila mara na kwamba jukumu hili hawawezi kuachiwa wamiliki wa vyombo vya habari. Alitumia kila msamiati aliodhani kwamba ungemsaidia kujenga hoja na kuonyesha kwamba KUNA TATIZO. Maskini Dk. Mwakyembe, hakujua kwamba alikuwa anachokoza nyuki. Waandishi walichukia, na wengi wao sasa wamekuwa wakimshambulia magazetini kwa madai kwamba aliwatukana kuwaambia hawajasoma.Baadhi yao wanataka awaombe radhi. Wengine wamefikia hata kuazimia kutokuandika habari zake. Nawe u miongoni mwao? Una maoni gani? Soma hapa kwanza, upate maoni yangu. Soma na hii hapa.

Tuesday, February 21, 2006

Taaluma ya Zombe ni ipi?

ALIPOULIZWA na waandishi wa habari mapema mwaka huu juu ya habari kwamba watu wanne waliouawa na polisi jijini Dar es Salaam hawakuwa majambazi bali wafanyabiashara, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Abdallah Zombe, aliwataka wananchi wasiingilie kazi ya polisi. Alisisitiza:

"Upolisi ni taaluma kama nyingine. Unasmomewa. Sisi ndio tunaweza kusema fulani ni jambazi au la..."

Sasa wenye taaluma yao, wakiongozwa na Jaji Kipenka Musa, wametoa taarifa ya tume inayoonyesha kuwa waliouawa hawakuwa majambazi. Askari polisi 15 wamehusishwa na mauaji hayo ya kikatili na uporaji wa mamilioni ya shilingi.

Zombe ameumbuka. Wananchi wanahoji: "Taaluma yake ni ipi sasa?" Taarifa zinasema naye yuko chini ya ulinzi, anahojiwa, huku akisubiri kuvuliwa vyeo vyake ili ashitakiwe kwa makosa yake, ingawa vyanzo vya kipolisi vimesema hatashitakiwa kwa mauaji, bali kwa 'makosa mengine.'

Lililo wazi ni kwamba wananchi wanaonekana kuchukizwa na kitendo cha Zombe kutopelekwa mahakamani Jumapili 20.02.2006 pamoja na askaro polisi wanne waliokwisha kamatwa.

Nashangaa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, anatoa kauli za kupinga taarifa za vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa Zombe. Watu wanajua kwamba alikwisharudishwa mkukumkuku kutoka Rukwa alikokuwa amepelekwa kuwa RPC; wanajua kuwa amekuwa akihojiwa makao makuu ya polisi; lakini Tibaigana anasema Zombe hajatiwa mbaroni, wala hahusiki!

Anaficha nini? Sasa kama hajatiwa mbaroni, katiwa wapi? Tibaigana hajaeleza Zombe yuko wapi? Anamkingia kifua? Vyovyote itakavyokuwa, Zombe keshakuwa Zombe, na wananchi wanataka serikali imzombe, haki itendeke! Vinginevyo, tutasema bado serikali inaendekeza kulindana.

Wednesday, February 15, 2006

Nimerejea ulingoni

WAPENDWA wanablogu, nilipotokomea sikuaga, kwa sababu haikuwa nia yangu kujitenga nanyi. Sasa nimerejea. Kwa muda nilikuwa mafichoni. Baadhi ya walionikosa kwenye blogu walitumia njia nyingine za kuwasiliana nami, wakahoji kama niko uhamishoni! Hata bila kujibu nilikuwa wapi, nafurahi kuwatangazia maswahiba wote kwamba sasa nimo ulingoni. Nimefurahi kuwakuta wanablogu wapya, kina Jeff Msangi (niliyemuathiri binafsi kuingia kwenye blogu) wakiwa wanatamba. Picha za Muhidin Issa Michuzi zimekuwa kivutio kingine. Hoja tekenyo za Reginald Simon zimekuwa kiburudisho kikubwa, bila kusahau hoja nyeti za painia Ndesanjo Macha. Nakiri kwamba nilikosa mengi katika muda niliokuwa mbali na wanablogu. Yawezekana pia nimewanyima machache kadhaa niliyokuwa nayo. Tafadhari mnisamehe. Sasa nimerejea.

Thursday, February 09, 2006

Picha iliyowaponza Tanzania Daima Hii Hapa


NOVEMBA 6, 2005 Gazeti la Tanzania Daima lichapishwalo na Free Media Ltd ya Dar es Salaam, lilikuwa na habari na makala nzito juu ya kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar wiki hiyo uliomrejesha Rais Amani Karume madarakani. Mbele ya gazeti kulikuwa na picha hii. Gazeti liliuzwa hadi likaisha. Walilenga kuchekesha, wakanunisha wakubwa. Walitumaini wako huru, wakajikuta mahabusu. Soma hapa. Na dunia nzima ilitambua ubabe wa serikali ya Tanzania. Ona!

Saturday, January 14, 2006

Limekuja Lenyewe, Hili Hapa


KILE zilichoshindwa timu zetu za soka, Coca-Cola imeweza: kulileta kombe la dunia Tanzania. Walau imetuwezesha kuliona, kulishika, kulinusa na kupiga nalo picha. Walau hili tumeliweza! Sijui uwezo wetu ndo umeishia hapo, au tumehamasika!
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'