Saturday, December 19, 2009

Sindiketi za watawala

Maswali Magumu wiki hii: Baada ya miaka takribani 15 ya mtandao, baada ya kuonja madhara yake, sasa watawala wameunda sindiketi. Tuwasaidieje?

Thursday, December 17, 2009

Wakubwa waumbuliwa na vitu vidogo vidogo

Rais George W. Bush aliumbuliwa na mlango. Baadaye aliumbuliwa na kiatu. Gordon Brown na Al Gore waliumbuliwa na mlango.

Monday, December 14, 2009

Waitaliano wambonda Waziri Mkuu wao

Nilipoandika kujadili tukio la msafara wa Rais Jakaya Kikwete kurushiwa mawe mkoani Mbeya, mwandishi mmoja aliandika kunijibu akisema, 'Ansbert, rais hapigwi mawe.' Hata hivyo, tayari rais alikuwa ameshapigwa mawe! Lakini wakati ule sikujua pia kwamba wapo wenzetu ambao wameshavuka enzi za mawe, sasa wanarusha hata makonde kwa 'marais' wao. Tazama Waitaliano walimvyomtwanga na kumtoa damu Waziri Mkuu wao, Silvio Berlusconi. Nadhani dunia ya kisiasa inabadilika kwa kasi ya ajabu!

Monday, December 07, 2009

Kwanini tuchague jiwe?

Imerudiwa kutoka Desemba 23, 2007.

Sunday, November 29, 2009

Sunday, November 22, 2009

Chafya ya Rais Mkapa

Ole wao Mkapa akipiga chafya!

Sunday, November 01, 2009

Pinda kaishitaki Ikulu; wabunge wataishinda?


WIKI hii Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameichongea Ikulu kwa Watanzania - bila kujua. Kauli yake kwamba Ikulu ndiyo imeiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) iwahoji wabunge kwa kile kinachoitwa 'posho mbili,' inazua maswali ya msingi juu ya nia ya Ikulu kubuni hila za kuua mjadala wa kitaifa juu ya serikali na Richmond.

Ni kielelezo cha uwezo mdogo wa serikali kimkakati kutumia TAKUKURU kuwaandama wabunge wale wale wanaoituhumu TAKUKURU hiyo hiyo. Taifa liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu na ufisadi wa watawala; maazimio ya Bunge kuhusu Richmond hayajatekelezwa; taifa linasubiri taarifa ya serikali kuhusu suala hili, kumbe wao wanaleta utoto wa 'posho mbili' zao?

Nani amewaruhusu Ikulu na TAKUKURU kupachika ajenda dhaifu katika nafasi ya ajenda kuu? Nani amewaruhusu kuandama wabunge wale wale ambao katika mjadala wa kashfa ya Richmond ndio waliopendekeza kigogo wa TAKUKURU achukuliwe hatua?

Hivi mtu akikutuhumu na wewe ukamtuhumu unakuwa mtu safi kuliko yeye, na unapata nguvu ya kumchukulia hatua? Ikulu na TAKUKURU wanadhani njia sahihi ya kujisafisha ni kuwaandama wanaoituhumu TAKUKURU na Richmond yao?

TAKUKURU ambayo haikuona ufisadi wa Richmond kulipwa milioni 152 kwa siku, tena bila kuzalisha umeme; TAKUKURU ambayo haikujua suala la EPA hadi lilipoibuliwa Bungeni; TAKUKURU ambayo haikujua wizi wa Deep Green Finance: TAKUKURU iliyoshindwa kushughulikia ufisadi katika ununuzi wa rada na ndege ya rais; TAKUKURU iliyoshindwa kuona ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa Kiwira; TAKUKURU inayoshindwa kuchunguza upotevu wa mabilioni ya pesa za Watanzania katika miradi michafu ya vigogo (orodha ni ndefu), ndiyo hii inayoona uchungu wa shilingi 50,000 za posho ya wabunge?

Hata kama posho hizo zina utata, watu wenye akili na uchungu na taifa wanaweza kuruhusu suala hili lifunike mjadala wa ufisadi wa Richmond? Huu ndiyo uwezo na upeo wa Ikulu na TAKUKURU kulinda watu wasiozidi wanne na Richmond yao kwa kunyamazisha na kutisha wanaohoji ufisadi huo?

Watu hawa wanajua kuwa ipo siku wataondoka Ikulu au TAKUKURU? Wanajua kuwa kuna maisha baada ya hila zao hizi za kisiasa au wanadhani watafia katika ofisi hizo ili tusiwahoji? Baada ya Ikulu kulinda na kusaidia watuhumiwa wengine wa Richmond kustaafu kwa heshima, inaona hii ndiyo njia mwafaka ya kuiondoa TAKUKURU katika matope ya Richmond? Hivi wanadhani kwamba hata kama wabunge wakiogopa wakanyamaza, wakaacha kuihoji serikali juu ya Richmond, vigogo hawa wanakuwa watumishi safi mbele ya umma na dhamiri zao wenyewe?

Mkakati huu wa Ikulu na TAKUKURU si uhuni mwingine uliovuka mipaka kwa serikali inayoongozwa na wale wale waliotuambia majuzi kuwa hawana nia ya kuwaziba midomo wabunge? Tusikilize kauli zao au tutazame matendo yao?

Hivi serikali inadhani watu pekee wenye akili wako Ikulu na TAKUKURU, kiasi cha kutupangia ajenda dhaifu ndani ya ajenda kuu, na kutarajia sisi tufuate upepo wao wa kisiasa na kucheza ngoma yao 'isiyokesha?'

Kama huu ndiyo mtiririko wetu wa kufikiri, viko wapi vipaumbele vya kitaifa? Ni haki tupotoshwe na propaganda za Ikulu na TAKUKURU, tuanze kuwajadili na kuwazomea wabunge ambao wamegundua janja hii ya Ikulu na TAKUKURU, wakawa jasiri kugoma na kutoa kauli thabiti?

Ni lini taifa hili litaacha kulea na kuenzi ukondoo, likatukuza ushujaa hata kama ni wa wachache wanaoweza kuwaambia watawala "hapana?"

Katika wakati ambapo taifa zima liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu ya watawala hao hao, tuache kujadili athari za Richmond tujadili posho mbili za wabunge? Kama walikuwa na nia njema na suala hili si wangelitafutia nafasi yake baada ya kuturidhisha na utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu Richmond?

Mbona tunajua kuwa hata rais mwenyewe na mawaziri wake wanaposafiri mikoani na kwingine wanapewa takrima hizo hizo na wenyeji wao? Ni Ikulu na TAKUKURU ipi itamchunguza rais?

Ni haki Watanzania wanyimwe fursa ya kujua hatima ya Richmond kwa ajili ya kuridhisha matakwa ya Ikulu na TAKUKURU kabla wakosaji wa TAKUKURU hawajawajibishwa?

Tumefika mahali ambapo serikali inatukuza na kulinda vigogo na Richmond yao kuliko maisha ya Watanzania milioni 40?

Wala Pinda hakuhitaji kusisitiza maagizo ya Ikulu kwa TAKUKURU, kabla hajatueleza nani aliiagiza TAKUKURU kuisafisha Richmond. Tunachojua ni kwamba TAKUKURU ipo chini ya ofisi ya rais. Hivyo, Ikulu na TAKUKURU ni kitu kimoja. Pinda anaweza kutusaidia kujibu Ikulu, TAKUKURU na Richmond ni vitu vingapi?

Hivi Pinda anadhani tumesahau kauli yake kwamba suala la hatua za serikali dhidi ya mkurugenzi wa TAKUKURU liko mbele ya rais linafanyiwa kazi? Kumbe ndiyo kazi yenyewe hii? Na Pinda anadhani ameipa Ikulu sifa?

Je, vitisho hivi vya Ikulu na TAKUKURU kwa wabunge ndiyo tafsiri ya kauli ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwamba yeye na Rais Jakaya Kikwete wametoka mbali hawawezi kutenganishwa?

Au ndiyo tafsiri ya kauli ya Lowassa, muda mfupi kabla ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka jana, alipowaonya wabunge akisema 'sote hapa ni wanasiasa, tukiamua kushughulikiana nani atabaki?'

Au ndiyo utekelezaji wa kauli ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hosea, alipobanwa na wabunge katika moja ya semina alizowaandalia katika hoteli ya Whitesands, Dar es Salaam, wakamhoji kwa nini hajawajibika kutokana na uzembe wa ofisi yake katika sakata la Richmond, naye akakasirika na kusema atawashughlikia wao kwanza?

Pinda alidhani akisema TAKUKURU imetumwa na Ikulu wabunge wote wangeogopa na kutakatifuza makosa ya watawala? Je, hii si dalili kwamba serikali inaficha udhaifu na uchafu wa Ikulu kwa kutumia TAKUKURU kuwatisha wanaohoji kilichopo nyuma ya pazia?

Na hapa ndipo tunapowageuzia kibao wabunge wenyewe. Tuliwaambia, tukawashauri mapema wakati serikali ilipoleta muswada wa kubadili Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kuwa TAKUKURU; tukasema taasisi hii haiwezi kufanya kazi ya kudhibiti wala kuzuia rushwa kama itaendelea kuwa chini ya ofisi ya rais.

Tulijua kwamba ofisi ya rais nayo inahitaji kuchunguzwa na kudhibitiwa, na kuwa serikali haitaki kuiondoa ofisi hiyo chini ya rais ili kuwalinda ama rais mwenyewe, au wasaidizi wake au rafiki zake au jamaa zake iwapo watakumbwa na masuala yanayohitaji mkono wa TAKUKURU.

Tulipendekeza iundwe chini ya chombo kinachojitegemea ili kiweze kusaidia kumulika kote kote bila woga wala upendeleo. Lakini dhamira ya serikali ilipitishwa na wabunge wale wale waliojifanya wanakipenda sana chama chao (CCM) kuliko taifa.

Katika hili la sasa, wabunge hawa wanaopambana na TAKUKURU wanapaswa kujua kwamba wanapambana na nguvu nyingine nyuma yake. Wataweza kuishinda? Je, wananchi watabariki hila za Ikulu na TAKUKURU?

Je, wabunge wetu sasa wameanza kuelewa hekima yetu ya kuiondoa TAKUKURU ofisini kwa rais? Maana hekima ya kawaida inatujulisha kuwa si marais wote watakuwa waadilifu. Wabunge wanajua mchezo unaochezwa na watawala, maana baadhi yao walikuwamo katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kilichomchachafya na kumtisha Sitta na wenzake.

Viongozi wale wale wa vikao vya NEC ndio hao hao wanaoituma TAKUKURU iwarudie kina Sitta kwa hila mpya. Si wamalize sula la Richmond kwanza tuone jeuri yao? Je, wabunge wataweza kuinyamazisha Ikulu na TAKUKURU?

Watawala wanadhani wabunge na wananchi hawajui walengwa wanaotafutwa na wanaolindwa katika sakata hili? Hivi Ikulu haiwezi kuwa imara bila kuwakumbatia mafisadi?

MAKALA hii inapatikana pia katika tovuti ya TanzaniaDaima

Friday, October 30, 2009

Wednesday, October 28, 2009

Sasa tumejua, tatizo ni rais

Baada ya Rais Jakaya Kikwete kukiri kwamba wasaidizi wake walimshauri apumzike akakataa, ndiyo sababu akazidiwa hadharani pale Mwanza, sasa kumeibuka hoja mpya. Je, kama rais anadiriki kuwapuuza wasaidizi wake katika suala nyeti la afya yake, nao wananywea; atawezaje kuwasikiliza wasaidizi na washauri wake katika masuala ya uchumi, siasa, usitawi wa jamii na mengine? Si inawezekana rais ana washauri wazuri wa mambo mengi tu lakini hawasikilizi? Hii si sehemu ya ushahidi kwamba rais ndiye tatizo?

Wednesday, October 14, 2009

Tunayojivunia ndiyo haya?

Kwa mazingira haya ya elimu tunajivunia sera zilizopo na utekelezaji wake?

Sunday, October 11, 2009

JK akianguka tena daktari wake atasemaje?

SI vema kudhani kwamba viongozi wetu hawawezi kuumwa. Lakini ndivyo madaktari wa Rais Jakaya Kikwete wanavyotaka tuamini. Kwani wanadhani wakisema rais anaumwa tutamnyanyapaa? Kwani yeye si binadamu tu? Taarifa yao kwa umma, ambayo inakanusha tetesi za rais kuumwa, wakati yeye anazidiwa hadharani, si dalili kwamba wenyewe wanamnyanyapaa? Hili ndilo swali gumu la wiki hii. SOMA HAPA.

Thursday, October 01, 2009

Hotuba ya Mke wa Gordon Brown

Msikilize na mtazame Sarah Brown akimpigia debe mumewe, ingawa maji ya kisiasa yako shingoni mwa mumewe. Hotuba yake inaweza kuwavutia wanachama wa Labour. Je,itawashawishi wapigakura waliokwishachukia na kuamua kuleta mabadiliko?

Sunday, September 20, 2009

Salaam za Eid El Fitr 2009


Asalaam Aleykum Waislamu wote, popote pale mlipo. Hongera kwa kuhitimisha mfungo wa Ramadhani. Nakutakieni amani na heri ya Eid El Fitr.

Sunday, September 13, 2009

Rais Kikwete amefanikiwa kujidanganya


BAADA ya kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete akijaribu kujibu maswali ya wananchi katika televisheni, huku nikijua kuwa hizo ni propaganda za kisiasa kuelekea 2010, nimeridhika kwamba hajamndanganya mtu yeyote bali yeye mwenyewe. Kwanini? Soma hapa.

Friday, September 04, 2009

Zitto Kabwe ataweza?

Zitto Kabwe ameamua kuwania uongozi wa juu kabisa wa chama chake, na tayari amekiri kwamba si mwa msukumo wake binafsi. Je, ataweza? Soma hapa Ukishamaliza hiyo unaweza kujikumbusha na hili pia.

Saturday, August 08, 2009

Tunamsafisha Kikwete kwa majitaka?

WATU wote wenye akili timamu wanajua kuwa Ikulu imemkashifu Rais Jakaya Kikwete katika jitihada za kumtetea na kumlinda dhidi ya ufisadi wa Richmond. Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, wiki iliyopita, kwamba Rais Kikwete hakuhusika kabisa na mchakato wa kuipatia kampuni ya kitapeli, Richmond Development (LLC), tenda ya kufua umeme wa dharura, ni jaribio jingine dhaifu la kuthubutu kumsafisha rais kwa majitaka. Ndiyo hoja yangu katika Maswali Magumu wiki hii.

Tuesday, August 04, 2009

Tujadili migogoro ya Sitta


MISUKOSUKO ya kisiasa inayompata Spika wa Bunge, Samuel Sitta, imetokana na mambo haya. SOMA hapa ujadili.

Thursday, July 23, 2009

Your girlfriends at a birthday party

Would you invite your 17 ex-girfriends at your birthday party? Well, Simon Cowell has!

Wednesday, July 22, 2009

Migiro opens School of Journalism


United Nations Deputy Secretary General Asha-Rose Migiro (R) recently officiated at the opening ceremony of the School of Journalism and Mass Communication at the Univeristy of Dar es Salaam. Left is Dr. Bernadeta Killian, the dean of the School leading her chief guest and other invitees into the event venue. (Photo by courtesy of IPP Media)

Sunday, July 12, 2009

Ujumbe wa Obama kwa Afrika

Rais wa Marekani, Barack Obama, ametoa ujumbe mzito kwa watawala wa Afrika. Ni ujumbe mzuri, ingawa una upungufu wake, ambao nitaujadili baadaye wiki hii.

Saturday, July 11, 2009

Obama anatazama nini?


Macho ya Rais Barack Obama yanatazama nini? Ndiye pekee anayeweza kujua. Lakini haituzuii kufuatilia na kujadili.

Friday, July 10, 2009

Swali gumu kwa Obama

Msome Erick Kabendera akimweleza Rais Barack Obama juu ya kile ambacho Afrika inahitaji kutoka kwake.

Obama na Papa Benedict XVI wakubali kutofautiana


Rais wa Marekani Barack Obama amemtembelea Papa Benedict XVI, na wawili hao wamekubaliana na kutofautiana katika masuala ya msingi. Wasome hapa. Na kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, mke wa rais, Michelle Obama amevaa vazi linalofunika haswa mwili wake.

Thursday, July 09, 2009

Saturday, July 04, 2009

Mahakama ya Kadhi: Ahadi nzito iliyoshindikana

IWAPO hoja ya Mahakama ya Kadhi Mkuu itafika mahali pa kuwakosanisha na kuwagombanisha Waislamu na Wakristo wa Tanzania, mgogoro huo utakuwa umesababishwa na woga wa watawala wetu. Kwa vipi? Soma Maswali Magumu wiki hii.

Sarah Palin abwaga manyanga


Sarah Palin, aliyekuwa mgombea mwenza wa John McCain kutoka chama cha Republican, Marekani, ametangaza kustaafu wadhifa wa Meya wa Alaska mwezi huu. Pata habari yenyewe.

Sunday, June 28, 2009

Michael Jackson: Skendo Tupu


Tumesikia na kusoma mengi mazuri ya Mfalme wa Pop, hayati Michael Jackson. Hapa kuna skendo za maisha yake ya nyumbani - yeye na pesa, watoto, ndugu, marafiki na majirani - zinazosimuliwa na mlezi wa watoto wake, Grace. Soma mwenyewe hapa.

Saturday, June 27, 2009

Serikali inataka kulikoroga jeshi letu?Serikali imeamua kulipaka jeshi letu matope ya ufisadi, kulifanya ngao ya ufisadi wa vigogo, huku ikisisitiza kwamba ni kwa maslahi na usalama wa taifa. Je, inajua madhara yake? Ni haki kulitumia jeshi letu kulinda matumbo machafu ya wanasiasa? Huu ndio mjadala wa Maswali Magumu wiki hii.

Wednesday, June 24, 2009

Ijue Nguvu ya Sikio lako la Kulia

Ijue nguvu ya sikio lako na kulia na jinsi ya kulitumia la mwenzio katika mawasiliano. Soma hapa.

Tuesday, June 23, 2009

Uingereza wapata Spika mpinzani

Baada ya Spika wa awali kujiuzulu kwa kashfa, Bunge la Uingereza limechagua Spika mpya John Bercow (46) ambaye anatoka chama cha upinzani cha Conservative. Mtazame hapa akitambulishwa na kutambuliwa rasmi baada ya kupata baraka za Malkia; na hapa akikubali majukumu ya kazi yake mpya n akuwashukuru wabunge. Hizi hapa ni hotuba za viongozi wa vyama vikuu Bungeni: 1. Waziri Mkuu , Gordon Brown (Labour). 2. Kiongozi wa Upinzani , David Cameron (Conservative). 3. Kiongozi wa chama cha upinzani , Nick Clegg( Lib Dem). Msikilize Spika mpya akimnanga mbunge mzee aliyekataa kumuunga mkono kwa kigezo cha umri. Huu ndiyo utaratibu wa kumpata Spika wao.

Sunday, June 21, 2009

Rostam Mbunge Bubu
Imedhihirika kwamba miongoni mwa wabunge wote (319) wa Tanzania yupo mmoja, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (pichani kulia), ambaye hajawahi kuuliza swali Bungeni wala kuchangia katika mjadala wa jambo lolote katika vikao vya Bunge kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo (Desemba 2005-Juni 2009. ) Je, anatumia ubunge wake kufanya nini? Pitia orodha ya wabunge bubu wa Tanzania, utoe maoni yako.

Thursday, June 18, 2009

Hukumu muhimu kwa wanablogu: Kublogu na siri haviendani

Kama ulitaka kublogu na kutunza siri, fikiri upya. Hukumu hii inawanyanganya wanablogu haki ya kuwa na siri kwa sababu kazi yao si yao binafsi bali ya jamii. Soma hapa.

Saturday, June 13, 2009

Yajue manono ya Ronaldo

Umeipata hii ya kipato cha Ronaldo? Atakuwa analipwa paundi 55 (karibu 110,000/=) kila dakika, hata kama yuko usingizini. Soma habari kamili hapa.

Sunday, June 07, 2009

Vijana CCM Bukoba acheni kujikomba

VIJANA wa leo wanafanyaje siasa tofauti na vijana wa zamani? Vijana waliosoma, wenye elimu (walau wenye makaratasi yanayoonyesha hivyo) wanafanyaje siasa tofauti na wale ambao hawakupata bahati ya kuelimika kama wao?
Wakilinganishwa na vijana waliowatangulia, vijana wa leo wana vipaumbele gani vilivyo bora? Na wakilinganishwa na wazee wa leo, vijana wa leo wanaonyesha matumaini gani ya kuwa na uzee mwema hapo baadaye?
Je, Tanzania yetu hii tukiikabidhi kwa vijana hawa tulionao, itakuwa salama zaidi kuliko ilivyo leo mikononi mwa wazee wanaong’ang’ania ujana? Je, wanaowabeza vijana wa Tanzania, wana haki ya kufanya hivyo? Au kuna sampuli ya vijana wanaosababisha bezo linalowaumiza vijana wote?
Je, Umoja wa Vijana wa CCM una haki tena ya kujiona wao ndio wawakilishi wa fikra, tabia na mwelekeo halisi wa vijana wa Tanzania? Je, vijana wa Tanzania, kwa ujumla wao, wanaonyesha jeuri, ujuzi, umakini, nguvu, upeo, wepesi, udadisi, moyo wa kujituma na wa harakati kuliko waliowatangulia?
Mfumo wetu wa elimu na malezi, umetulelea vijana wenye sifa hizo au umetufyatulia vibaraka na wapambe wa mfumo uliopo walio wepesi kunyanyaswa, kupuuzwa na kutumiwa kwa maslahi ya walio madarakani, hata kwa kuteketeza maslahi ya taifa la kesho?
Je, dhana ya taifa la kesho ipo kweli, au maisha yote yanakamilika na kumalizika leo tu? Kama kesho ipo, ni nani anabaki kuwa mlinzi wa hiyo kesho?
Nimejiuliza maswali haya na mengine baada ya kusikia kilichotokea Bukoba Mjini wiki hii, ambapo Umoja wa Vijana wa CCM, umetoa hundi ya shilingi milioni moja (1,000,000/-) kumlipia Rais Jakaya Kikwete kiasi anachohitaji kuchukulia fomu ya kugombea tena urais mwaka 2010.
Wamempa pia Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Sued Kagasheki, hundi ya laki moja (100,000/-) ili aweze kulipia fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM mwaka 2010.
Najua kampeni zinazoendelea ndani ya CCM. Siwaonei wivu Rais Kikwete na Balozi Kagasheki. Naelewa pia kwamba vijana hao wametoa michango hiyo kama hamasa ya kisiasa. Ni kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010.
Lakini najiuliza, hizi ndizo siasa zinazowafaa watu wanaojiita vijana katika karne ya 21? Kwa staili hii, wao wanajifanya watu wa kuiga au wa kuigwa? Hii ndiyo sampuli ya vijana wa Bukoba? Wanaleta aibu au sifa kwa vijana wenzao kimkoa na kitaifa?
Hii dhana ya kumchangia pesa rais inatokana na nini? Ni kwamba Rais Kikwete ni mhitaji wa pesa kwa kiwango hicho cha kutegemea misaada ya kuchangiwa au kupewa? Je, vijana hawa wana fedha nyingi za kugawa hata kwa Rais Kikwete?
Je, vijana hawa wamejitosheleza au wana miradi mikubwa kiasi kwamba pesa hiyo inatokana na faida kubwa waliyopata, na sasa wameamua kutoa mchango kwa ‘maskini Kikwete na Kagasheki?’
Ni kweli kwamba katika bajeti yao ya mwaka huu pesa hiyo ilitengwa kwa ajili ya kununulia fomu ya Rais Kikwete mwaka ujao? Ni kweli Rais Kikwete alihitaji kuchangiwa milioni moja na kundi kama hili? Je, hii pesa ni ya vijana hao au wamepewa ili wafanyie mbwembwe na harakati za kisiasa?
Najua kinachofanyika hapa ni kampeni; ni propaganda; ni mbwembwe; ni kujitangaza. Lakini hii ndiyo staili ambayo inawafaa vijana wetu, tena baadhi yao wasomi? Je, siasa za namna hii zitatuendeleza?
Je, CCM Bukoba imeendelea, imeridhika na ina ziada ya pesa kiasi cha kutoa misaada kwa wengine wanaohitaji, nje ya mkoa, akiwamo rais?
Vijana hawa hawa ambao wamekuwa wanakinga bakuli kwa Mbunge wao, ambao baadhi yao wamekuwa wakitumika kumsifia mchana na kumshambulia usiku, leo wamepata wapi jeuri ya pesa ya kumsaidi yeye badala ya kukarabati majengo ya ofisi zao zilizochakaa na kuweka mikakati ya kuboresha vipato vya watendaji katika ofisi zao?
Balozi Kagasheki amekuwa akitumia fedha zake nyingi kufadhili miradi mbalimbali katika jimbo lake. Vijana hawa waliwahi kumchangia katika kufadhili mradi gani kwa ajili ya maendeleo ya wakazi wa Bukoba?
Jambo moja ni wazi. Hatuwezi kuwapangia matumizi ya pesa za chama. Lakini tunaweza kuwashauri. Kwa sehemu kubwa, matumizi kama haya yanaonyesha udhalili wa wahusika; na yanawafanya waonekane wanajikomba kwa maslahi finyu ya kisiasa.
Nisingehoji sana kama pesa hizi zingetolewa na jumuiya isiyo ya vijana. Wala nisingewasema sana kama zingekwenda kwa watu wanaozihitaji, ambao wanataka kugombea ubunge au urais lakini vipato vyao haviwawezeshi kupata viwango hivyo vya pesa.
Wapo wananchi wanataka kugombea ubunge, lakini wanatengwa na mfumo unaothamini pesa kuliko utu. Baadhi yao wangeweza kuwa wawakilishi wazuri tu, lakini kwa kuwa hawana pesa ya kununua fomu na kuhonga wakati wa kampeni, wanatupwa nje ya ulingo wa siasa.
Kama vijana hawa wangewatambua watu wa aina hii, wakawapa hamasa kwa kuwachangia pesa, tungeona wamefanya jambo la maana. Lakini pia, vijana ndio wangetarajiwa kukisaidia chama chao kuondoa taratibu kongwe na za kibaguzi zinazoleta matabaka kwenye chama chao na katika taifa kwa ujumla.
Badala ya kukaa tu na kuabudu mifumo hii, vijana wangekuwa wabunifu na jasiri zaidi kwa kuwashawishi wazee kuondokana na mifumo mikongwe ndani ya chama.
Zaidi ya hayo, vijana hawa ndio wangepaswa kukikosoa chama, kukipa changamoto ndani na nje ya vikao, kukitetemesha na kukitikisa ili kirejee katika misingi ya chama cha wakulima na wafanyakazi; chama cha mlalahoi, Mtanzania mlipa kodi; chama wa waadilifu na watu wenye uchungu na nchi hii.
Sifa wanazomwaga kwa viongozi walioshindwa kazi, ni dalili tosha kwamba vijana wenyewe wamezeeka kabla ya wakati wao; wamegeuka wachafuzi na wakorogaji wa siasa za Tanzania; wamekuwa waviziaji na wazengeaji wa vyeo vya kuteuliwa; wanajikomba na kujidhalilisha; wanatanguliza maslahi yao finyu.
Duniani kote, uhai na maendeleo ya taifa hutegemea zaidi vijana; si tu kwa misuli yao bali hasa kwa akili na ubunifu, ujasiri na moyo wa kuthubutu kubadilisha mazoea.
Lakini sehemu kubwa ya vijana wa Tanzania, hasa wenye nafasi katika mfumo wa utawala wan chi hii, wanashangilia mazoea ya muda mrefu, na yaliyochoka na kuchokwa hata na baadhi ya walioyaasisi. Kuna tatizo gani?
Tunapowaza kutengeneza sera za maendeleo yetu, tunalenga mustakabali wa taifa miaka 30 na zaidi ijayo. Hapa tunazungumzia kizazi kijacho – watoto na wajukuu wetu. Tunazungumzia urithi tutakaowaachia watoto tunaowazaa leo na watoto wao.
Hatuwazi kutafuna na kuteketeza kila kilichopo leo, kana kwamba tunawakomoa wale tuliowatangulia kuzaliwa. Uchungu na ugomvi wa baadhi yetu na watawala, tunapojadili uoza na ufisadi wao, unatokana na fikra hii kwamba walio madarakani na wapambe wao, wameendekeza dhana ya kukomoa kizazi kijacho.
Laiti vijana wa leo wangejua kuwa ni jukumu lao kuwazuia watawala na kudhibiti ukomoaji huu unaoendelea kulitafuna taifa lililojaliwa raslimali nyingi mno, lakini linasifika duniani kote kwa amani na utulivu katikati ya umaskini uliokithiri.
Wanaotusifu wana sababu zao. Si zetu. Sifa za watu wa nje hazileti chakula mezani kwetu. Hazilipi kodi ya nyumba; hazitujengei shule wala hazitulipii karo ya watoto wetu. Hazitibu wagonjwa wetu.
Lakini sifa hizo zinalegeza mioyo yetu, na zinawahakikishia wanaotusifu fursa ya kutumia raslimali zetu kuendeleza mataifa yao; kuwawekea hazina vijana na watoto wa mataifa yao kwa kutumia jasho la vijana na watoto wetu. Ni wajibu wetu, hasa vijana wa leo wa Tanzania, kusema, ‘hapana!’
Si sifa ya kujivunia kwa watawala wetu kumeza ndoani za mataifa makubwa, huku wakivikwa vilemba vya ukoka na kutunukiwa tuzo na shahada za bure ili waendelee kutengeneza na kuchonga mirija mirefu, mikubwa na imara zaidi ya kuhamishia utajiri wa nchi zetu kwa wakoloni wapya, wababe wa utandawazi.
Ni jukumu la vijana kuhakikisha kuwa ujana wao na wa watoto wao haunyonywi na vijana wa wakoloni weusi au weupe au wowote wale, kwa kisingizio chochote kile.
Tukubali, tukatae; kesho ni ya vijana. Lakini kesho hiyo hiyo inaanza leo, na inatengenezwa na leo yetu.
Bahati mbaya, sioni kama vijana wenyewe wanatambua hilo au wanahangaika kuitengeneza kesho hiyo, au kuwazuia waharibifu wa leo yetu inayoleta maangamizi ya kesho yao. Kama wapo hawatoshi.
Kwa sababu ya kasumba za muda mrefu na propaganda za kisiasa zilizodumaza uwezo wa wananchi kufikiri; kwa sababu ya mfumo wa elimu ya kunakiri na kukariri; wananchi wetu wengi, vijana wakiwamo, wamekuwa mateka wa mifumo ambayo wangepaswa kusimama kidete kuihoji, kuipinga na kuiangusha.
Sina ugomvi na utendaji wa Balozi Kagasheki katika jimbo lake. Ni mmoja wa wabunge wachache wanaotumia raslimali zao binafsi kuendeleza majimbo yao. Lakini hii siyo siasa tunayotaka kujenga. Si kazi ya mtu mmoja kuwajenga wananchi milioni mbili madaraja, madarasa, barabara, nyumba za kuishi, miradi ya maji na afya, kuwanunulia magari ya wagonjwa, na kadhalika.
Tunahitaji siasa endelevu, ambazo zinakiwezesha chama na serikali ya wakati huo kuweka mifumo ya utendaji kazi, hata kama mbunge mwenyewe hachaguliwi tena au anajiuzulu. CCM Bukoba Mjini wamekuwa wakimsaliti mna kumzunguka Kagasheki, wakijua upinzani mkuwa alio nao dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Kama kuna msaada walipaswa kumpa, si pesa; sila ki moja. Huu ni uhuni, ni matusi. Kagasheki nahitaji nguvu na umoja wa kichama, ushirikiano katika kujenga mikakati ya maendeleo na ushindani wa kistaarabu; mifumo endelevu ya kuleta maendeleo ya wana Bukoba.
Kama walitaka kusaidia, basi hiyo laki moja wangemchangia mwanachama mwingine anayetaka kuchuana na Kagasheki ndani ya chama, lakini ha uwezo wa kuipata. Tungewaita mashujaa, wanademokrasia wanaokua na vijana wa kutegemewa na taifa zima.
Kwa uapnde mwingine, tungewaona mashujaa kama miongoni mwao angejitokeza kiaja anayetaka kuchukua fomu kuchuana na Rais Kikwete katika kugombea urais mwaka kesho, kwa sababu sote tunajua kwamba katika miaka mitatu hii iliyopita, mambo yamemuwia magumu!
Tunajua ugumu wa kupambana na rais aliye madarakani. Si lazima umshinde, lakini ni vema kuandika historia kwamba vijana wa Tanzania wana uwezo kukataa kusifia kasoro na udhaifu wa wakubwa.
Wana CCM wenye akili, ambao hawaridhiki na utendaji wa serikali ya awamu ya nne, lakini hawana ujasiri wa kutosha kuwanyooshea wakubwa kidole, wananyamaza. Sawa ni waoga, lakini ni bora kuliko kujidhalilisha!
Naomba nieleweke. Vijana wote hawawezi, na hawapaswi kuwa na msimamo mmoja; au kuwa katika chama kimoja; au kuwa nje ya chama. Lakini wanaotaka kumsaidia rais au nchi yao, wanaweza kufanya hivyo ndani ya chama kwa kukipa changamoto na kukibadilisha ili kiendane na zama zao.
Wanaweza kufanya kazi nzuri tu bila kutumia kama mihuri ya maamuzi ya wakubwa. Wanaweza kuingiza nguvu mpya ya kiakili na kimwili katika chama, na kukipa mwelekeo mpya ulio imara.
Siasa za kutafuta maslahi kwa kujikomba na kumwaga sifa zisizostahili ni siasa dhalili zinazoweza kufanywa na wale tu ambao wanatambua kuwa nafsi zao hazina thamani, wala utu wao hauna nafasi, na ni kivuli tu, mbele ya nafsi za wakubwa.
Kuishi, kula na kufanikiwa kwao kunategemea fadhila, uteuzi na huruma ya wakubwa. Hizi si siasa za kufanywa na vijana. Na kwa hili, tuwaulize vijana hawa wa CCM Bukoba: ‘ipo wapi jeuri, ujuzi, umakini, nguvu, upeo, wepesi, udadisi wao kisiasa?’ Tukubaliane. Wametudhalilisha

Thursday, June 04, 2009

Obama awaahidi Waislamu 'mwanzo mpya'


Kama hukuweza kusikiliza hotuba ya Rais Barack Obama, jijini Cairo, Misri, kuhusu 'mwanzo mpya' kati ya Marekani na Waislamu duniani kote, bonyeza hapa usikilize alichosema. Hata kama ulimsikia, unaweza kurudia kuisikiliza hotuba nzima, ukajikumbusha kile alichoita changamoto sita zinazoikabili dunia kwa sasa.

Sunday, May 31, 2009

Thursday, May 28, 2009

Ferguson akiri kuzidiwa kete

Kwa kauli yake na wachezaji wake, na jinsi sote tulivyoshuhudia, Barcelona ndiyo timu bora. Soma hapa

Friday, May 01, 2009

Bibi harusi mfupi sana


Unamjua bibi harusi mfupi sana ambaye ilibidi apande kiti ili aweze kumbusu mumewe mara baada ya kufunga ndoa? Habari yenyewe hii hapa.

Mtoto jiniasi kuliko wote


Mtoto huyu Elise Tan Roberts ana umri wa miaka miwili tu, lakini anaonekana kuwa na kiwango kikubwa mno cha uwezo kiakili - ambacho wenzetu wanaita IQ - na amekuwa mtoto jiniasi mwenye umri mdogo kuliko wote. Anajua makao makuu ya 'karibu kila nchi' duniani. Anapoulizwa hapotezi muda kufikiri, bali anaporomosha jibu kama 'hana akili nzuri.' Mtazame kidogo hapa akihojiwa, naye akimhoji ripota.

Thursday, April 30, 2009

Tuesday, April 28, 2009

Ni Messi au Ronaldo?

Wapenzi wa soka mnasemaje kuhusu kijana huyu Lionel Messi wa Barcelona? Kiwango chake kiko juu sana. Hebu mtazame hapa kwa dakika nne tu, halafu uamue kama wanaomlinganisha na Cristiano Ronaldo wa Manchester United wanamtendea haki.

Friday, April 24, 2009

Mengi anamsaidia Rais Kikwete?

Mwenyekiti Mtenadaji wa IPP, Reginald Mengi, amelipuka na kuwasha moto mpya dhidi ya mafisadi. Kama ilivyokuwa kwa Dk. Willibrord Slaa aliyetangaza orodha ya mafisadi kwa sifa, vyeo na majina yao Septemba mwaka juzi, Mengi naye amethubutu kutaja majina matano tu ya wale aliowaita mapapa wa ufisadi nchini. Ni wazi, wengine tuliwajua mapema, walishatajwa walishanong'onwa, wana tuhuma nzito lakini kwa sababu zinazojulikan kwa watawala, mafisadi hao hawashitakiki. Baadhi yao wako mahakamani wanashitakiwa kwa ufisadi.

Wapo watu wanaombeza Mengi kwa tamko hili; na wapo wanaomuunga mkono. Wote hao, pamoja na Mengi, tutawajadili baadaye. Lakini kijumla ni kwamba, kwa maslahi yoyote yale, Mengi amethubutu. Je, unataka kuwajua 'Mapapa wa 'Mengi?' Hawa hapa. Hawa wamemnukuu lakini wakaogopa kutaja majina. Na yeye anasema kwa kauli yake hiyo anamsaidia Rais Kikwete kupambana na ufisadi. Ni kweli? Sehemu ya pili hii hapa.

Wednesday, April 22, 2009

Jacob Zuma ashinda urais Afrika Kusini

Afrika Kusini walipoingia katika uchaguzi wa rais na viongozi wengine wa kitaifa, kama kawaida, wananchi waligawanyika katika makundi, na walitoa maoni yao. Soma hapa. Baada ya kura kupigwa, chama tawala (ANC) kilipata ushindi mnono. Tazama Rais Mtarajiwa Jacob Zuma anavyoburudika na wapambe wake jukwaani kushangilia ushindi.

Monday, April 20, 2009

DECI, dini na siasa

Tathmini yangu fupi ni kwamba sakata la kampuni ya DECI inayoendesha upatu limechukua muda mrefu kwa kuwa wamiliki walimau kutumia dini kuhujumu wananchi maskini huku wakijificha katika kivuli cha siasa zetu. Ndiyo maana waliweza kusitawi kwa miaka mitatu bila kuguswa na vyombo vya usalama wa taifa. Walipata imani ya umma na ulinzi wa dola usio rasmi. Sasa wameshtukiwa, lakini tazama suala hili linavyojaa utata na kuchukua muda mrefu kutekelezwa. Ni dini na siasa ulingoni. Sijui wewe unasemaje.

Friday, April 17, 2009

Jogoo wa shamba kawika mjini London

Mama huyu mwanakijiji Susan Boyle amekuwa gumzo. Inawezekana wakati wewe utamtazama na kumsikiliza hapa utakuwa mtu wa milioni 17 ndani ya wiki moja. Chema kimejiuza; na jogoo wa shamba amewika mjini. Msome, msikilize; huyu hapa.

Wednesday, April 15, 2009

Watoto wa Nyerere na Amini wakutanishwa

Tanzania na Uganda zilipoingia vitani (1978-79) haikuwa vita ya kifamilia, lakini BBC imefanya jitihada za kuwakutanisha watoto wawili wa waliokuwa marais wa nchi hizo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Iddi Amin Dada. Watoto wao, Madaraka na Jaffari wamekutana kijijini Butiama, na hizi hapa ndizo kauli zao. Kumbukumbu muhimu.

Sunday, April 05, 2009

Eti Malkia hakumbatiwi?

Michelle Obama alivunja mwiko akamkumbatia Malkia Elizabeth II, naye akamkumbatia. Wala hajakatika mikono. Ona hapa!

Saturday, April 04, 2009

Urithi wa siku 1200 za Kikwete Ikulu

Bado hajamaliza, lakini tayari Rais Jakaya Kikwete amekwangua siku 1202 akiwa Ikulu. Kwa kuwa dalili zinaonyesha ameshaanza kujiandalia ngwe ya pili, tujiulize: hizo alizomaliza zimewaachia Watanzania urithi gani? Tujadili.

Friday, April 03, 2009

Vituko vya kidiplomasia vya Berlusconi


Wapo viongozi wa nchi wanaofahamika kwa vituko vya kidiplomasia. Kwa Ulaya, nadhani Waziri wa Italia, Silvio Berlusconi, anaongoza. Mwaka 2005 aliiudhi serikali ya Finland kwa 'mizaha ya kitoto' aliyomfanyia rais Tarja Halonen. Mwaka mmoja baadaye aliingia kwenye mgogoro na serikali ya China baada ya kudai kwamba chini ya utawala wa Mao Zedong, Wachina walikuwa 'wanachemsha watoto wachanga.' Kuna wakati aliwahi kuangusha kichwa cha mimbari mbele ya Rais George Bush na waandishi wa habari. Aliwahi kutoa kauli tete juu ya rangi ya ngozi ya Barack Obama, mara alipochaguliwa Novemba mwaka 2008 kuwa rais wa Marekani. Mwaka jana alimchezea Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, mchezo ule ujulikanao kama 'hide-and-seek.' Hata juzi akiwa jijini London kwenye mkutano wa G20, Berlusconi alipayuka hadharani akimuita Rais Obama mara baada ya kupiga picha ya pamoja na Malikia wa Uingereza, Elizabeth II, jambo ambalo hata malkia mwenyewe anasemekana hakulipenda! Ikumbukwe kuwa huko nyuma aliwahi kujikuta kwenye mzozo na Wajerumani kwa utani wa KINAZI dhidi ya mbunge mmoja wa Ujerumani. Aliwahi pia kumsifia waziri Mkuu wa Denmark kuwa ni handsome kuliko viongozi wote wa Ulaya! Hata majuzi katika mkutano wa NATO alichelewesha ufunguzi wa mkutano huo baada ya kuganda kwenye simu nje ya ukumbi, huku mmoja wa wenyeji wa mkutano, Merkel, akimsubiri bila mafanikio. Mtazame hapa. Una kituko kingine cha Berlusconi au kigogo yeyote? Kwa Afrika ni kiongozi gani 'anasifika' kwa vituko vya kidiplomasia?

Thursday, April 02, 2009

Maazimio ya kina Obama haya hapa

Wakubwa wa nchi 20 kubwa duniani wamemaliza mkutano wao jijini London na wamekubaliana misingi kadhaa katika kuinua na kumarisha uchumi. Hii hapa. Tazama na hapa. Na mtazame mwenyeji wao, Gordon Brown, akifunga mkutano huo na Rais Barack Obama akitoa majumuisho mbele ya waandishi wa habari.

Wednesday, April 01, 2009

Obama atua LondonRais wa Marekani Barack Obama yupo London akiwa na mkewe Michelle kushiriki mkutano wa nchi 20 zenye nguvu zaidi kiuchumi. Huyu hapa akishuka kwenye ndege yake na kuelekea kwenye 'chopa' kwenda Ubalozi wa Marekani nchini Uingereza. Hizi hapa ndizo mbwembwe zinazoambatana na msafara wa 'kiranja wa marais' duniani (wapo katika picha ya pamoja chini kulia).

Matukio mengine: Obama, Gordon Brown na waandishi wa habari. Obama na 'Kwini.' Obama na vigogo wengine 19. Siasa za tabasamu za wake wa wakubwa (tazama picha hapo juu kushoto) na video kadhaa zinazoonyesha harakati za Michelle akiwa London - Cheki hapa na hapa. Brown akifungua mkutano. Baada ya mkutano Obama alikwenda Ufaransa, Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya. Muone hapa akimudu jukwaa mbele ya umma Ufaransa.

Sunday, March 22, 2009

Buriani Jade Goody

MSANII maarufu wa runinga nchini Uingereza, Jade Goody, aliyekuwa anasumbuliwa na Kansa, ambaye aliolewa (shukrani zake hapa) na kubatizwa pamoja na watoto wake wawili, ameaga dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili 22, 03, 2009. Mwanamuziki Darren Hayes amemsindikiza Jade kwa kibao cha I miss you . Humjui Jade Goody? Maelezo haya yanaweza kukusaidia kumfahamu. Alijiandalia mazishi yake mwenywe, na alitaka yawe ya kifahari, iwe hafla ya kusherehekea maisha yake mafupi ya miaka 27, hata kama yatapambwa na machozi ya baadhi ya baadhi ya waombolezaji. Apumzike kwa amani!

Tusaidiane kuepusha ugaidi huu

UGAIDI gani huo? Soma hapa. Na hii je uliipata?

Saturday, March 21, 2009

Rajoelina: Mimi ni rais

Madagascar ina kiongozi mpya Andry Rajoelina (34) ambaye ameapishwa Machi 21, 2009 baada ya kuiangusha serikali ya Marc Ravalomanana. Naona wamepuuza vitisho na kemeo la SADC na AU; na ingawa hata mabalozi wamesusa hafla ya kuapishwa kwake, habari ndiyo hiyo. Rajoelina anasema, 'nimeshakuwa rais.'

Papa Benedicto XVI na Kondomu

KAULI ya hivi majuzi ya Papa Benedicto XVI kupinga matumizi ya kondomu katika vita ya UKIMWI imezua mjadala mpya, huku wengine wakimlaani kwamba anakwamisha mafanikio ya jitihada za kupambana na maambukizi ya UKIMWI na kwamba hakupaswa kutoa kauli hiyo. Wengine wamemkosoa kwamba si kweli kwamba matumizi ya kondomu yanaongeza kasi ya maambukizi ya UKIMWI kwa sababu taarifa za kitafiti zinaonyesha umuhimu wa kondomu katika kuzuia maambukizi. Hata hivyo, taarifa hizo hizo zinadai kwamba kinga ya kutumia kondomu si ya asilimia 100.

Lakini Papa ni kiongozi wa dini, na ujumbe wake unazingatia maadili yanayosimamiwa na madhehebu ya imani yake. Kama huo ndiyo msimamo wa kanisa lake, tulitarajia aseme nini? Ahubiri nini? Asiposema hayo aliyosema atakuwa Papa tena? Na kama kondomu haizuii kwa asilimia 100 Papa amekosea nini?

Tuesday, March 17, 2009

Wananchi wachukua Ikulu Madagascar

Ndo hivyo! Rais Marc Ravalomanana wa Madagascar ameondolewa madarakani. Alipewa muda aondke mwenyewe kwa hiari, akashindwa kusoma alama za nyakati. Sasa yametimia! Jeshi limeingilia kati, na aliyekuwa kiongozi wa upinzani, Andry Rajoelina (34) kaingia Ikulu. Ona hapa eti wanaondoa mapepo ya Ravalomanana Ikulu!

Lucy Kibaki kashika hatamu au mpini?

Ukisikia mke kushika hatamu, Mke wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya amedhihirisha hilo. Hakika huyu ameshika zaidi ya hatamu - ameshika mpini; mumewe ameshika makali. Lakini si wapimane ubavu kimya kimya, katika faragha? Kwa nini wanamwaga mtama mbele ya kuku wengi? Ndiyo maana nasema wote wawili wamenichefua. Bofya hapa ucheke kwa furaha au hasira.

Saturday, March 14, 2009

Uongozi unaoahirisha majukumu utafanikiwa?

Waislamu wameibuka tena wanataka serikali itekeleze ahadi yake juu ya Mahakama ya Kadhi. Nilishawashauri, na nilisisitiza hivyo katika makala yangu mojawapo ya Novemba mwaka jana. Nasisitiza kuwa wasipowabana wakubwa ahadi hii nayo itayeyuka kama lilivyo suala la Mwafaka wa Zanzibar. Vyovyote itakavyokuwa, litawatesa wakubwa ifikapo 2010.

Friday, March 13, 2009

Wapime watawala wetu kwa swali hili dogo

UKITAKA kujua uwezo au udhaifu wa viongozi wetu waulize maswali. Wala yasiwe magumu. Maswali mepesi tu yanatosha kuonyesha uwezo na upeo wao. Bonyeza hapa utazame na kusikiliza swali dogo lilivyogaragaza wakubwa katika mjadala wa masuala ya kiuchumi.

Monday, March 09, 2009

Watawala wetu mitumba ya kisiasa?

Ni vema TANESCO imejitoa katika biashara chafu ya ununuzi wa genereta mitumba za Dowans. Lakini king'ang'anizi cha serikali kufanya biashara ya mitumba hii, na kauli ya kukata tamaa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Dk. Idris Rashid baada ya wabunge kumjia juu, vinaweza kupata tafsiri nyingi tata kama wanavyosema wananchi. Mi najiuliza: Wenzetu hawa wanang'ang'ania mitumba kwa sababu wamezoea siasa za mitumba, nao ni wanasiasa mitumba?

Kabumbu: Kumbukumbu Muhimu

Wapenzi wa soka mtakaoweza kutazama mechi hizi, nawaletea kumbukumbu za mechi chache muhimu za Kombe la Dunia. Mnaweza kuanza na hii iliyochenzwa na akina PELE mwaka 1970 muone Brazil ilivyoichapa Italia; usipitwe na bao la 'Mkono wa Mungu' lililofungwa na Maradona katika fainali za mwaka 1986; itazame mechi bora kati ya Brazil na Ufaransa mwaka 1986; fuatilieni tathmini fupi ya Kombe la Dunia mwaka 1998 na kifafa cha Ronaldo de Lima.

Linki hizo hapo zinafunguka vema kwa walio Uingereza. Walio nje ya Uingereza nao wanaweza kutumia lakini inabidi wajipatie proxy server ya bure ya UK na wawe na kaufundi kiasi ka kuifiksi. Wale walio Marekani, kama wanatumia Intaneti yenye kasi kubwa wanaweza kufaidi uhondo huu kupitia ESPN360. Vinginevyo, nenda Yahoo World Cup Coverage.

Monday, March 02, 2009

CNN wailetea Afrika programu mpya

MWEZI huu wa Machi 2009, kituo maarufu cha Televisheni cha CNN International kinaanzisha programu mpya kwa Afrika itakayojishughulisha na kutangza masuala ya kitamaduni, michezo na biashara ya bara letu katika mtazamo mpya. Habari kamili hii hapa.

Sunday, March 01, 2009

Michelle Obama rasmi


Hii ndiyo picha rasmi ya Michelle Obama iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Februari 27, 2009. (AP Photo/The White House, Joynce N. Boghosian).

Kifuta machozi cha Richmond

MJADALA na mvutano unaoendelea kuhusu nia ya serikali, kupitia TANESCO, kununua mitambo ya Dowans kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura, unaleta hisia mchanganyiko. Wapo wanaodhani ni mradi makini na halali kwa maslahi ya taifa. Wengine wanashtuka kwa kuwa Dowans ni dada yake Richmond, na wanadhani hii ni janja ya serikali kuwabeba akina Richmond kupitia mlango wa nyuma; kuwapa kifuta machozi kwa yaliyowatokea huko nyuma.

Thursday, February 26, 2009

Obama ahutubia Bunge

Hotuba ya kwanza ya Rais Barack Obama kwa Bunge la Marekani. Hii hapa msikilize.

Sunday, February 22, 2009

Kinamama hawa wanaimba, wanatisha!

Wapenzi wa Classical Music sikilizeni kinadada hawa wanavyoporomosha Soprano kutoka albamu maarufu ya G.F. Handel iitwayo Messiah. Mmoja anaitwa Emma Kirkby katika wimbo wa But Who May Abide Huyu hapa. Mwingine ni Renee Fleming anaimba Rejoice Greatly. Si karama tu, bali pia matokeo ya mazoezi makali ya kuimba. Nimewakubali. Wewe je?

Tunapigwa kwa kuwa tunapigika

Hii ndiyo fasiri yangu ya kipigo cha walimu kutoka kwa DC wilayani Bukoba.

Monday, February 16, 2009

Mikono imekamatwa, ubongo upo kazini

Wapendwa wasomaji, hasa wadau wa Maswali Magumu, nilipotea kwa wiki mbili. Majukumu yalikuwa mengi kiasi, nikashikwa mikono; lakini ubongo ulikuwa kazini. Sasa tutakuwa pamoja tena katika safu yetu na nyinginezo, ikiwamo hii hapa mpya mpya.

Saturday, January 31, 2009

Chozi la Pinda


Baada ya yote yaliyoandikwa na kusemwa, kuhusu kauli ya kuomba radhi na chozi la Waziri Mkuu Mizengo Pinda (pichani juu) akiwa Bungeni wiki hii, bado najiuliza: Amewalilia albino au serikali, au amejililia yeye? Au kuna jambo jingine lililomliza? Kwa kuwa alipotoa kauli tata tulisema ni kauli ya serikali, je kilio hiki cha waziri mkuu ni kilio cha serikali? TUJADILIANE.

Friday, January 23, 2009

Obama: Public service is a privilege

Nakubaliana na msimamo huu kwa asilimia 100. Naamini na viongozi wetu wamejifunza kitu hapa, na kitawasaidia kurejea katika misingi. Hili nalo ni suala nyeti, swali gumu.

Wednesday, January 21, 2009

Dansi la kwanza Ikulu kabla ya kazi
Uchaguzi umekwisha, Rais Barack Obama ananza kazi, lakini kwanza rais mpya na mkewe wanasakata dansi la kwanza kabisa baada ya kuingia Ikulu, muda mfupi kabla ya kufungua ofisi. Tazama miondoko yao hapa.

Tuesday, January 20, 2009

Funzo kutoka kwa Obama
TUTAFAKARI: Miaka miwili iliyopita sidhani kama kuna Mmarekani alidhani kwamba Marekani ingekuwa na rais mweusi sasa. Leo Barack Obama ameruka vihunzi vyote, amevunja miiko yote, amekuwa rais mpya wa Marekani, na kuanza kujenga legasi yake kwa maneno mazito. Historia imeandikwa upya. Sikiliza hotuba yake ya kwanza akiwa rais.
Kwetu Tanzania, bado kuna kasumba kwamba viongozi lazima watoke Chama Cha Mapinduzi, kwa maelezo kuwa wasio wana CCM hawaonekani kuwa na uwezo wa kuongoza - ingawa waliopo ndio wameshathibitisha kwamba wameanza kuishiwa mawazo na uwezo wa kuongoza.
Kwangu mimi, ushindi wa Obama ni ushahidi na funzo tosha kwamba lolote linawezekana katika nchi yetu wakati wowote kuanzia sasa, kama kutakuwa na bidii ya kutosha. Hata wanaobezwa au wasiojulikana, na hata wasiokubalika sasa wanaweza kuiondoa CCM madarakani iwapo watajipanga vema. Najua wahafidhina watabisha kwa kuwa wanajua jambo tu - CCM. Na wanasubiri CCM ndiyo iwaruhusu kufikiri na kuamua vinginevyo.
Wenye akili pana, upeo na fikra angavu zilizofunguka, watapata fursa ya kutafakari na kuona vinginevyo. Baada ya marais 43 weupe, Marekani sasa imepata rais wa 44 mweusi katika mazingira ambayo ubaguzi wa rangi haujatokomezwa kabisa. Watanzania wanahitaji kuwa na marais wangapi wa CCM kabla ya kufanya mabadiliko? Wewe binafsi uko upande gani? Obama amekufunza nini? Jadili.

Sunday, January 18, 2009

Maparoko na Mkapa

SOMA hapa kuhusu kisa cha maparoko wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Friday, January 16, 2009

Nami nimehojiwa

Nimezoea kuhoji na kuandika wengine, sasa nami nimedakwa nakuhojiwa kuhusu umuhimu na maendeleo ya blogu katika Afrika. Soma mahojiano na jarida moja jipya la karne ya 21 lijulikanalo kama RAP21 hapa.

Tuesday, January 13, 2009

Tutamkomaza Kikwete

Na Ansbert Ngurumo

NIMEFARIJIKA kwa kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba sasa amekusudia kujitoa mhanga katika vita dhidi ya ufisadi. Hii nayo ni ahadi ya nyongeza ambayo Watanzania watafuatilia utekelezaji wake.
Ameitoa wiki hii katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Dodoma.
Kilichonigusa ni nia ya rais – kujitoa mhanga ili kushinda vita dhidi ya ufisadi. Anajua kwamba ili ashinde vita hii - ili awe mwenzetu - lazima aikane nafsi yake, akubali kubeba ‘msalaba’ wake na kutufuata! Huko ndiko kujitoa mhanga.
Lazima awateme wapambe na maswahiba wake, ambao anajua walihusika katika ufisadi mkubwa unaolisumbua taifa sasa; unaomnyima usingizi.
Lazima ajiweke tayari kwa lolote litakalotokana na hatua yake hiyo, hata kama itabidi wamfitini aukose urais mwaka 2010. Naamini huko ndiko kujitoa mhanga anakozungumzia.
Lazima ajipange na sisi, awe upande wetu, na azingatie matakwa na maslahi yetu dhidi ya wachache wenye nguvu ya pesa chafu na madaraka dhalimu. Lakini anajua matokeo yake. Nguvu hiyo inaweza kumdhuru na kutokomeza ‘utukufu’ wake uliotengenezwa na wale wale anaosema atapambana nao. Huko ndiko kujitoa mhanga.
Maswali yanakuja. Je, ataweza? Maneno yake yatageuka vitendo? Ni kweli amebadilika na kuwa kama sisi? Au hiyo nayo ni kete ya kisiasa kulainishia hisia na akili za Watanzania?
Au ni kampeni zimeanza kiujanjaujanja kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu? Kimsingi, ni yeye tu anayeweza kujibu maswali haya vizuri. Wengine wote watajipendekeza na watashindwa.
Napenda kukiri, na naona fahari, kwamba nimekuwa mmoja wa wananchi waliomwandama Rais Kikwete tangu mwanzo. Taratibu, sote tutaanza kukubaliana kwamba mashambulizi yetu yamemsaidia rais kuliko sifa alizomwagiwa - hata kama hataki kukiri.
Na kama ningepaswa kuorodhesha mambo 10 tu ambayo tumeyatimiza katika miaka mitatu ya serikali ya awamu ya nne, nisingekosa la kusema. Yeye alitaja mafanikio yake; acha na sisi tutaje jinsi tulivyomsaidia.
Kwanza, tumemtoa rais kwenye sifa za vilemba vya ukoka; tukamfanya atambue uwezo na udhaifu wake halisi katika hali halisi ya ugumu wa maisha ya Watanzania na uzito wa kazi inayomkabili. Kauli yake kwamba yuko tayari kujitoa mhanga ina maana kwamba anawajua anaopambana nao. Anajijua uwezo wake, lakini anajua pia udhaifu wake ambao wenzake wanaweza kuutumia kumuumiza. Ulevi wa sifa umeanza kumtoka.
Pili, tumekomesha shamrashamra na majigambo ya ushindi wa kishindo. Walipoanza kushindwa kazi ndipo wakajua maana ya kishindo. Kura za umma ni laana kwa watawala kama hawatimizi ahadi walizotoa kwenye majukwa ya siasa. Siku hizi hata wao wanakiri kwamba mambo yamekuwa magumu. Sasa wanakubaliana na sisi; wameshindwa.
Tatu, tumemtoa tongotongo machoni. Sasa anaona vema matatizo halisi ya wananchi. Ugumu wa maisha ya Watanzania umemfanya rais na wapambe wake wasahau kabisa kaulimbiu ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania.’ Wamekubali kwamba hicho kilikuwa kibwagizo cha uchaguzi. Walikuwa wakishangiliwa sana wakati ule, sasa wakithubutu kuyasema maneno hayo wanazomewa.
Nne, tumemfunza kwa lazima kutofautisha kazi na urafiki. Anawajua wenzake, jasho lililowatoka; pesa waliyochanga; dili walizofanya na kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana. Lakini sasa tumemfikisha mahali anaanza kutambua kwamba ni zamu ya Watanzania kupata ushindi wa kishindo – dhidi ya njama za mafisadi; na kwamba ni zamu yake sasa kujitoa mhanga.
Mafisadi hawa, hasa walio karibu naye, ndio amekuwa akiwaogopa; na yawezekana ndio hao anaowazungumzia anaposema yuko tayari kujitoa mhanga, liwalo na liwe. Kama ataweza hilo, kwanini tumlaumu? Likimshinda kwanini tusimzomee?
Tano, tumemfanya aone kuwa kuna hatari ya CCM kumilikiwa na kununuliwa na matajiri wachache – tena kwa pesa ambayo Baba wa Taifa aliwahi kuiita ‘ya bangi.’ Ni yeye tu anayeweza kuinusuru au kuitosa CCM. Na kwa kuwa ndicho chama kinachoongoza serikali kwasasa, asipokinusuru ataliangamiza taifa.
Sita, tumemfanya alazimike kuzungumza lugha yetu, na kutumia msamiati wetu. Mwaka juzi wakati mawaziri wake na viongozi waandamizi wa CCM wanazunguka mikoani kupinga harakati za wapinzani na wanaharakati dhidi ya ufisadi wa watawala, serikali ilikuwa inapinga dhana hii ya ufisadi. Yeye aliongoza harakati hizo akiziita kelele za mlango.
Na wakati fulani Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, alianzisha ngonjera na mchezo wa maneno juu ya dhana ya ufisadi, akilenga kupuuza, kupunguza makali ya neno na dhana hiyo. Hakuweza.
Lakini sasa na rais (mwenyekiti wa Makamba) anazungumzia mafisadi, tena baadhi yao ni wale wale waliotajwa pamoja naye katika orodha ya iliyoanikwa hadharani pale Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Septemba 15, 2007. Siku hiyo ndipo ilizinduliwa rasmi vita dhidi ya mafisadi; na msamiati huo ukaanza kutumika kwa kishindo kuelezea uoza unaoendekezwa na watawala, unaolikabili taifa letu.
Ni faraja iliyoje kwamba sasa na rais anatumia lugha hiyo hiyo katika kueleza hatua na mikakati ya serikali dhidi ya watu wale wale waliokuwa wanalindwa kwa nguvu zote. Amekiri kiutu uzima kwamba hawezi kushinda nguvu ya umma. Imemshinda, na sasa anatafuta fursa ya kujiunga nayo. Kwa nini tusimpongeze kama anaanza kujisahihisha?
Lakini kujisahihisha huko kusipokuwa kwa dhati kutageuka kitanzi kwake. Maana sasa wananchi wameona na wamejua kwamba naye anajua kinachoendelea na - kama alivyowahi kusema mwaka 2006 - anawajua wanaohusika. Tatizo ni pale anaposema anasubiri ushahidi kuwachukulia hatua.
Lakini mbona ushahidi unapaswa kuwakuta mahamakani? Mbona ushahidi unapaswa kuwa sehemu ya mwenendo wa mashitaka? Atapataje ushahidi asipowafikisha kwenye vyombo vya sheria? Au anataka kutuambia kwamba wote walio mahakamani na magerezani leo ni kwa sababu kesi zao zina ushahidi wa kutosha?
Mbona kuna kesi zimedumu miaka zaidi ya 10 na zinaendelea kupigwa kalenda kwa kisingizo kuwa ushahidi haujakamilika? Kwa nini linapofika suala la kuwatia mbaroni mafisadi, rais anadai kwanza upatikane ushahidi? Kwani kuwatia mbaroni ni sawa na kuwahukumu?
Kwa maoni yangu, hili ni eneo ambao bado hatujamkomboa rais. Bado anarudia kauli alizorithi kwa mtangulizi wake Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye alitumia kauli hii hii kukwepa wajibu wa serikali kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa mbele ya vyombo vya sheria.
Je, Watanzania wataelewa na kukubali urithi huu wa Kikwete kutoka kwa Mkapa? Kama Mkapa alishindwa kuturidhisha kuhusu suala la ushahidi kabla ya kuwakamata wala rushwa, Kikwete ataweza kutulegeza? Na kuna ushirika gani kati yao unaowafanya watudai ushahidi wakati wapelelezi wa kesi ndio wana jukumu la kupekua na kukusanya ushahidi?
Na mbona baadhi ya wananchi walishatangaza kwamba wana ushahidi dhidi ya mafisadi, lakini polisi hawajawahi kuwafuata kuchukua vielelezo hivyo kwa ajili ya kuendelezea upelelezi wao? Hapo ndipo inakuja shaka juu ya umakini wa kauli za wakubwa kuhusu vita dhidi ya ufisadi.
Saba, tumemfanya apunguze safari za nje, akae ofisini. Ameanza kuzoea kwamba kazi hizo si zake tena, bali ni za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Nane, tumemlazimisha kuwagusa baadhi ya vigogo ambao hakuwa amedhamiria waguswe. Serikali ilijua makosa yao mapema sana. Ilikaa kimya hadi ilipoumbuliwa na wapinzani na wanaharakati. Na si hao tu, lakini hawa ndio wamepita kwenye chekecheo la mtandao. Wengine wamebaki juu kwa sababu ni wakubwa kuliko matundu ya chekecheo, lakini si safi kuliko wadogo waliopenya! Hata kama ni hatua ya kisiasa, ni hatua imepigwa.
Tisa, tumemfanya avunje Baraza la Mawaziri na kupunguza idadi ya wizara. Awali, alidhani kwamba ufanisi wa serikali ungetokana na wingi wa mawaziri. ‘Madongo’ yetu yalimfanya atambue kasoro hiyo na akajaribu kuirekebisha.
Kumi, tumemfanya atambue – na sasa ameanza kuonyesha hivyo – kwamba zetu si kelele za mlango. Na hata kama zingekuwa za mlango, hawezi kulala usingizi hadi zitakapokoma! Bado tutaendelea kupiga kelele maana tunajua umuhimu wake.
Tunajivuna kwamba sifa bandia zimeyeyuka mithili ya barafu kwenye jua. Sasa vumbi limeanza kutua. Tunaanza kuishi katika ukweli; katika kushindwa au kuweza. Naamini kwamba katika hili hakuna mtu atakayejitokeza kuomba tumpe ushahidi.
Kwani ni wazi kwamba waliokuwa wanatembea miaka mitatu iliyopita sasa wamekuwa viwete. Waliokuwa wanaona wamekuwa vipofu. Waliokuwa wanasikia sasa ni viziwi. Waliokuwa na shibe sasa wanalia njaa.
Huu ndiyo ukweli unaomsukuma rais aseme anataka kujitoa mhanga. Hawezi kujivunia umaskini, ujinga, njaa na maradhi yanayoongezeka miongoni mwa watu wale wale waliompigia kura za kishindo. Neema za mafisadi – wa awamu ya tatu au ya nne - ni hukumu yake.
Tunachosubiri ni kuona jinsi atakavyojitoa na kuwatoa wengine mhanga. Hapo ndipo tunapopataka.
La msingi ni kwamba taratibu anaanza kuacha kudeka; kwani aliokuwa akiwadekea ndio wamemuangusha. Na ndio hao anaopaswa kuwatumia kujitoa mhanga. Yaani tumeanza kumkomaza; na tutaendelea kumkomaza ili kulijenga taifa.

Saturday, January 03, 2009

Wanataka tuote sugu?

Watawala wanapowatisha wananchi wasihoji, au wasifichue ufisadi, eti kwa kisingizio cha uchochezi, si bure kuna jambo wanaogopa. Na wakati mwingine wanataka wengine tuote sugu. Tukubaliane nao, tunyamaze?
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'