Monday, August 30, 2010

Slaa akata anga Morogoro

LEO Dk. Willlibrod Slaa alikuwa mkoani Morogoro, katika wilaya za Mikumi na Mvomero. Mikutano imefana. Amesisitiza haja ya Morogoro kuwa na wabunge wa upinzani ili kuongeza uwajibikaji katika halmashauri za mkoa huu, na katika nchi nzima kupitia Bunge; na kudhibiti wizi wa fedha za umma.

Akiwa Mikumi, alimlipua mwenyekiti wa kamati ya kampeni za CCM, Abdulahman Kinana, akisema kigogo huyo ana mkono katika biashara chafu za makampuni ya meli; akamtaka ajielekeze katika masuala ya kitaifa badala ya kumwandama yeye (Slaa). Akasisitiza kwamba ana ushahidi wa kauli zake, kwani hana historia ya kukurupuka.

Kauli hiyo ya Dk. Slaa inakuja siku moja baada ya Kinana kujibu mapigo ya makada wa Chadema, hasa Mabere Marando, ambao waliwataja hadharani vigogo wanaohusika na ufisadi mkubwa, huku CCM ikilalamika kwamba chama hicho cha upinzani kinatoa matusi.

Katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za Chadema, Marando alisema vigogo waliohusika na wizi wa EPA ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Rostam Azizi na Edward Lowassa, akasema waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi ni dagaa wanaoonewa ili kuficha madhambi ya wahusika wenyewe wa ufisadi.

Juzi Kinana alijitokeza na kumbeza Dk. Slaa, kwamba anatumia lugha ya matusi kwenye kampeni kinyume cha makubaliano waliyosaini. Dk. Slaa jana alisema mtu akiiba anaitwa mwizi; na kwamba kumwita hivyo si matusi.

Wednesday, August 25, 2010

Helikopta ya Kikwete yashindwa kutua


MWANABIDII mmoja, Leila Abdul, ameripoti kuwa helikopta inayombeba mgombea urais kupitia CCM Jakaya Kikwete, leo majira ya saa 10 imeshindwa kutua Ngara, mkoani Kagera, kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri. Kwa sababu hiyo, mkutano uliopaswa kufanyika wilayani hapo uliahirishwa hadi kesho

"Kutokana na hali hiyo imembidi mwenyekiti wa CCM wilayani Ngara Hellena Adrian alilazimika kuwataarifu wananchi kuwa mkutano huo hautafanyika ikiwa ni majira ya saa 11:30 jioni na kueleza kuwa badala yake mkutano huo utafanyika kesho majira ya saa 2: 00, na kubainisha kuwa Kikwete amelazimika kusafiri kwa magari," aliandika Leila, katika waraka uliosambazwa kwa wanabidii wote.

Msafara wa Kikwete waua mtoto

HABARI zilizoifikia blogu hii jana jioni zinasema gari moja aina ya Land Cruiser VX, T 181 BJP, lililokuwa katika msafara wa Rais Jakaya Kikwete, jana liligonga na kuua mtoto pala pale, eneo la Izigo, Muleba, mkoani Kagera. Hata hivyo, wahusika katika msafara huo wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM walisema gari lililoua halikuwa katika msafara. Baadaye ilidhihirika kuwa gari hilo lilikuwa limeutangulia msafara wa JK; na lilibeba vifaa vya kampeni vya CCM. Dereva wa gari hilo alishikiliwa na kuhojiwa na polisi mkoani Kagera, lakini jitihada za kupata mamlaka husika kufafanua ajali hiyo hazikufanikiwa. Tutaendelea kuifuatilia. Mwaka 2000 msafara wa aliyekuwa mgombea wa CCM, Rais Benjamin Mkapa, ulia mtu mkoani Mwanza. Waandishi walioambatana naye waliamriwa wasiandike habari hiyo kabisa. Walibaki kusimulia kwa midomo baada ya kampeni!

Saturday, August 21, 2010

Kikwete aanguka tena jukwaani


Tumpe pole Rais Jakaya Kikwete. Ameanguka jukwaani, Jangwani Dar es Salaam, siku ya ufunguzi wa kampeni yake. Niliwahi kuwauliza madaktari wa rais, walipotoa taarifa ya ugonjwa wa rais, wakasema hataanguka tena. Nikasema, iwapo ataanguka tena, watatuambia nini? Nadhani hapa kuna tatizo kubwa. Tumwombee, na tumshauri Rais Kikwete.

Thursday, August 19, 2010

Mtikila akosa sifa kugombea urais


Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye alichukua fomu kugombea urais wa Tanzania, ameondolewa kwenye orodha ya wagombea urais. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba Mtikila alikosa sifa. Hakupata wadhamini kutoka mikoa 10 kama sheria inavyotamka. Mtikila aliwasili ofisi za NEC saa 10 jioni, kwa mbwembwe, kabla ya kupata habari mbaya, ambazo hata hivyo, kwa kuwa hakuwa amepata wadhamamini alizitarajia. Katika picha hii, Mtikila alikuwa anahutubia 'umati' ulikusanyika kumsikiliza katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, mwaka 2005 alipogombea urais. Wagombea mwingine ambao hawakutimiza masharti ni Paul Kyara wa SAU na wa Jahazi Asilia na Demokrasia Makini. Mgombea wa Demokrasia Makini na wa NRA hawakutokea kabisa kurejesha fomu.

Wagombea urais waliobaki hadi sasa ni Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA); Prof. Ibrahim Lipumba (CUF); Jakaya Kikwete (CCM); Hashim Rungwe (NCCR-Mageuzi); Mutamwega Mgaywa (TLP); Sahma Dovutwa (UPDP); na Peter Kuga Mziray (APPT-Maendeleo).

Wagombea urais warejesha fomu


Dk. Slaa

CHDM

Chadema

CCM

CCM

CCM

CUF

CUF

CUF

TLP

APPT-Maendeleo

Dini ya Obama yaleta kizaazaa


Wamarekani sasa wamekumbwa na mjadala mpya juu ya dini ya Obama. Kwa vipi? Kwa nini? SOMA hapa.

Tuesday, August 17, 2010

Serikali yatisha Maswali Magumu

JANA niliitwa Ofisi ya Idara ya Habari (MAELEZO) na kuhojiwa, nikiwa na Mhariri Mtendaji, Absalom Kibanda, juu ya ukali wa makala za Maswali Magumu ya Agosti 8, 2010 na ya Agosti 15, 2010, ambayo kwa taarifa nilizonazo yaliikera Ikulu, nayo ikaisakama MAELEZO. Kikao hicho kilishirikisha Mkurugenzi wa Maelezo, Clementi Mshana; Mkurugenzi Msaidizi, Raphael Hokororo na ofisa wa maelezo aitwaye Jovina, aliyekuwa anaandika muhtasari wa mazungumzo yetu. Tulizungumza mengi, lakini katika yote, nakumbuka nukuu ya mmoja wa vigogo hao wa MAELEZO akisema: "Mashujaa wote hawako hai...".

Wednesday, August 11, 2010

Pweza afanya vitu vyake


Wabunifu wameshaanza kufanya vitu vyao kuelekea Uchaguzi Mkuu. Eti na pweza ameshatabiri!

Tuesday, August 10, 2010

Dk. Slaa alazwa


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amelazwa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili. Blogu hii ilizungumza na Dk Slaa hospitalini hapo, akasema alilazwa jana Jumatatu kwa ajili ya matibabu ya mkono wake uliovunjika mfupa wa juu ya kiwiko wiki moja iliyopita. Kwa maelezo yake, alishauriwa na daktari aliyemfunga 'mhogo' (POP) katika hospitali ya Bugando, Mwanza, kwamba alipaswa kurejea hospitali kwa uchunguzi mwanzoni mwa wiki hii. Alikwenda Muhimbili mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jana Jumanne.

Habari za kulazwa kwa Dk. Slaa zilipowafikia mashushushu wa CCM na marafiki wa mafisadi, zilipokelewa kwa hisia za kishabiki, hata baadhi yao wakadiriki kueneza uvumi kwamba Dk. Slaa yu mahututi. Mwenyewe alipozungumza na blogu hii kwa simu alisema: "Siko mahututi. Ni jambo la kawaida, nililazimika kurudi hospitali kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya ziada, ikiwa ni pamoja na kufungua POP."

Akiwa Muhimbili, Dk Slaa anaweza ama kufungwa POP jingine au kufanyiwa pia upasuaji mdogo ili kuwezesha mkono kupona haraka. Alisisitiza kwamba kulazwa kwake hakuathiri mchakato wa maandalizi ya kampeni zake; na kwamba alikuwa akifanya kazi kwenye kompyuta yake kama anavyoonekana kwenye picha hii, iliyopigwa na Joseph Senga leo Jumanne jioni katika wodi binafsi, F, hospitalini Muhimbili.

Friday, August 06, 2010

Lipumba achukua fomu za urais


Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) jana alichukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alisema anagombea urais ili kukuza mapambano dhidi ya mafisadi.

Michelle Obama kanogewa Ikulu?


Michelle Obama ameanza kunogewa manono ya Ikulu? Soma HAPA uone jinsi vyombo vya habari vinavyoanza kummulika na kumjadili.

Kikwete aogopa mdahalo tena

KAMA alivyofanya mwaka 2005, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameogopa mdahalo na wagombea urais wenzake kutoka vyama vya upinzani. Taarifa ya Kikwete kuogopa mdahalo huo ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba na Naibu Mkuu wa Kitengo cha propaganda wa CCM, Tambwe Hiza, jana Agosti 05/08/2010, Dar es Salaam. Kikwete anakimbia mdahalo huo wakati maandalizi yakiendelea, huku mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Lipumba na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibrod Slaa wakisisitiza kuwa wanataka mdahalo huo ili wananchi wawapime kwa hoja. Hata hivyo, kukimbia kwa Kikwete hakutazuia mdahalo kuendelea. Wenzake watapewa fursa hiyo adhimu, na iwapo watamjadili in absentia atakuwa amepoteza fursa muhimu sana ya kujenga hoja na kujitetea kwa hoja zinazoelekezwa kwake na chama chake. Mwaka jana, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown wa Uingereza alianza kwa kukataa kushiriki mdahalo (ambao ulifanyika mwaka huu), lakini baadaye alikubali na kushiriki, na alifanya vizuri, ingawa hatimaye hakushinda uchaguzi. Lakini kwa jinsi washindi (Conservative) walivyokosa kura za kutosha kuunda serikali peke yao kama walivyotarajiwa, ni ishara kwamba mdahalo na utendaji wake waktia masuala mengine, hasa uchumi, vilimwinua Brown, akaungwa mkono na sehmu kubwa ya umma uliokuwa unambeza awali. Je, Kikwete ataendelea kuogopa na kupoteza fursa hii?

Dk. Slaa afunika Moshi


Sehemu ya umati wa wakazi wa mji wa Moshi, wakisikiliza hotuba ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa (hayupo pichani), wakati wa mkutano wa kuomba udhamini, kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010. (Picha zote na Joseph Senga)


Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, akihutubia katika mkutano wake wa hadhara wa kuomba kudhaminiwa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010.


Mwenyekiti wa CHADEMA), Freeman Mbowe, akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi, katika mkutano wa hadhara wa kuomba udhamini wa mgombea urais wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Manyema mjini Moshi 05/08/2010.


Msafara wa mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, ukipita katikati ya mji wa Moshi, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa ndege mjini humo, ambako alihutubia mkutano wa hadhara wa kuomba kudhaminiwa, kwenye Uwanja wa Manyema jana, huku ukisindikizwa na helikopta (juu) 05/08/2010.


Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Said Arfi, akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi na vitongoji vyake, katika mkutano wa hadhara wa kuomba udhamini kwa mgombea urais kupitia chama hicho, kwenye Uwanja wa Manyema 05/08/2010.

Wednesday, August 04, 2010

Dk Slaa mjini Mtwara na Songea

Dk. Willibrod Slaa katika msafara uliompokea mjini Songea (04/08/2010)

Dk. Slaa akihutubia wananchi mjini Songea (04/08/2010)

Dk. Slaa, akihutubia wananchi na kuomba udhamini mjini Mtwara (04/08/2010)

Tuesday, August 03, 2010

Dk. Slaa aiteka Mbeya
Picha hizi mbili zinaonyesha sehemu tu ya umati wa wakazi wa Mbeya mjini uliompokea Dk.Willibrod Slaa kumdhamini ili agombee urais 2010 kupitia Chadema (03/08/2010)

Monday, August 02, 2010

Dk. Slaa mgombea urais Chadema 2010Huyu ndiye Dk. Willibrod Slaa, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'