Monday, July 03, 2006

Uteuzi wa Makamba CCM una matundu

BAADA YA MWENYEKITI WA CCM, JAKAYA KIKWETE, KUMTEUA YUSUFU MAKAMBA KUWA KATIBU MKUU BADALA YA PHILLIP MANGULA, WATU WENGI WAMESHINDWA KUFICHA HISIA ZAO KUHUSU UTEUZI HUO. HAPA, MWANDISHI Kanku Gambire WA SAFU YA NASIKITIKA KATIKA GAZETI LA Tanzaia Daima, anachambua uteuzi huo, akiwalinganisha Makamba na Mangula. SOMA

NASIKITIKA kwamba uteuzi wa Yusufu Makamba kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) una matundu.
Hadi hapo Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete atakapoamua kutoa hadharani nini hasa sababu ya kumteua Makamba kuwa Katibu Mkuu, kila mwenye kujua siasa za Tanzania atabakia kupapasa.
Ni kupapasa haswa! Kwani Katibu Mkuu aliyeondolewa, Philip Mangula na Yusufu Makamba, hawawezi kulinganishwa na sifa zao angalu kushabihiana katika nyanja mbalimbali.
Mangula ni mtendaji wa kirasimu; anayejali na kuheshimu kanuni na taratibu. Makamba ni mwanasiasa mwenezi wa wazo la mkubwa wake hata kama mantiki yake ni ndogo sana.
Mangula ni mwanasiasa anayeshikilia usimamizi wa taratibu na anayeegemea andiko. Makamba ni msema chochote ili kukabiliana na hali yoyote iliyojitokeza ikiwa ni pamoja na kukana au kukiri jambo lolote ili kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.
Mangula anajipa muda kufikiri na kutafuta ufumbuzi wa jambo wenye kukubalika kwa mantiki kuu. Makamba ni maarufu kwa “uchochezi” unaolenga kudhoofisha misuli ya mlengwa.
Mangula ana uwezo na uzoefu wa kusimamia utatuzi wa mgogoro hata kama ni kwa ujanja na ghiliba za chama chake kikubwa. Makamba anaagukia kwenye matumizi ya dola na viotisho.
Katika hili, ni vigumu kufikiria jinsi Makamba angefanya kazi ya uwakilishi wa chama chake katika kutafuta usuluhishi kati ya CCM na CUF na kuzaliwa kwa muwafaka.
Makamba ni mwelekezaji wa utekelezaji wa matakwa ya chama chake kwa kadri alivyoelewa jambo. Mangula, pamoja na kuwa mwelekezaji, ni muumbaji wa taratibu asiyesubiri kuwekewa mifumo ya kutekeleza.
Mangula siyo msemaji sana bali mzingatiaji wa mwelekeo wa chama chake. Makamba ni moto wa kiangazi; mwanasiasa katika maana ya uanasiasa pokopoko ambao mara nyingi hukariri uadilifu wa chama usioonekana kwa macho ya wengi.
Makamba na Mangula ni watumishi wa CCM ambao uaminifu wao katika chama hauhitaji kutiliwa mashaka. Bali Mangula ana chembechembe za kujiamini na hata kuwa na msimamo hasi, wakati Makamba ni mfuasi wa kile alichoambiwa na “bwana mkubwa.”
Makamba ni maarufu kwa kumimina nahau za Kiswahili wakati akiongea na kuchagiza hadhira yake – ile sehemu ya kazi ya mwenezi wa chama ambayo Kikwete amemnyima.
Mangula ni mtawala anayeongea machache lakini mwenye king’ang’anizi kwa kauli za awali na misimamo ya chama hadi hapo atakaposhurutishwa kuwa tofauti.
Makamba ni mwoga wa kitu kipya kama alivyoonyesha wakati wa kuweka jiwe la msingi la uwanja mpya wa mpira jijini Dar es Salaam, mbele ya rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Makamba alilalama na kukiri pia kwamba yeye hawezi kasi mpya na akaonyesha kuwa huenda akatupwa nje ya duara la siasa iwapo wachagizaji wa “kasi mpya” wataingia madarakani.
Wakati inawezekana kabisa kwamba hiyo inaweza kuwa ghiliba, kwa kuzingatia uhusiano uliopo kati ya Makamba na Rais Kikwete na nafasi yake ya sasa, hapa kuna mwanasiasa asiye na soni kwa lolote alisemalo – la kweli, la kuficha ukweli au la kubabaisha.
Kwa upande mwingine, Mangula ana uwezo wa kuchukua maamuzi na kujiegemeza kwa “kundi” lake na kuonyesha hivyo.
Kila chama duniani huwa na makundi. Makundi hayo huwa na mawazo mbalimbali na wakati mwingine kukinzana lakini kwa shabaha ya kunoa chama na si kukidhoofisha au kukiua.
Wakati Makamba ana woga wa kuwa na kambi katika chama na kuwa wazi juu ya hilo, Mangula amewahi kuhusishwa na kambi na hakukana. Labda huo ndio mwanzo wa jino kulegea na hatimaye kung’olewa.
Mwisho: Viwango vyao vya elimu ya darasani havilinganishiki. Hapa Makamba yuko nyuma. Umiliki na usimamizi thabiti wa shughuli za utendaji ndani ya chama unahitaji umahiri utokanao na elimu pana na si wingi wa mikutano ya hadhara.
Unaweza kusema iwe na iwavyo, kwani CCM ni chama changu? Na hivyo ndivyo nisemavyo. Lakini kusaidia wana-CCM kufikiri na kutafakari ni moja ya sababu za kusikitika kwangu leo hii.

kankugambile@yahoo.com
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'