Monday, May 29, 2006

Anna Senkoro ameangukia pua


WIKI iliyopita, mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania, aliyeshiriki kwenye kinyang'ayiro cha kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Anna Senkoro, kupitia chama cha TPP-Maendeleo, ametangaza kwamba anakihama chama hicho. Tayari amerejesha kadi yake kwa viongozi wa TPP-Maendeleo. Hakuna anayejua kama anaacha siasa au chama. Lakini wachambuzi wameanza kujadili. Hapa chini upo uchambuzi wa Nikita Naikata, mwandishi wa safu ya NASIKITIKA katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili ukurasa wa 10, Mei 28, 2006. SOMA, TOA MAONI.

NASIKITIKA kutosikitika kwamba Anna Senkoro, mwanamke wa kwanza nchini kugombea kiti cha urais, ameamsha mikono na kusema, “yamekwisha!”
Ya kwake yalijulikana mapema. Anna anasema hataki tena siasa za chama chake. Anasema amerudisha kadi. Anasema hajaamua aende chama gani baada ya hapa.
Anna analiza. Anasema, hata hivyo, kwamba hatakwenda chama chochote cha upinzani kwa kuwa alipokuwa amelazwa hospitalini hakuna kiongozi wa upinzani aliyekwenda kumwona.
Anna alikuwa mgombea urais kutoka chama kidogo cha mtu mmoja mwenye madaraka makubwa – PPT-Maendeleo cha Peter Kuge Mziray.
Katikati ya kampeni, Anna alianza kulalamika. Hana fedha za ruzuku za kuendeshea kampeni. Huku bosi wake kichama, Mwenyekiti Mziray akitangaza hadharani kwamba yeye anamuunga mkono mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Haijulikani na labda haitajulikana hivi karibuni, kwa nini PPT-Maendeleo waliweka mgombea urais wakati mwenyekiti wake anapiga debe kwa ajili ya mgombea wa CCM.
Inawezekana basi kwamba mwenyekiti wa PPT-Maendeleo alijua mapema kwamba mgombea wake hashindi. Kwa hiyo alikuwa na ajenda nyingine.
Na kuonyesha kwamba chama ni cha Mziray, hakuna aliyenyoosha kidole kupinga msimamo wake wa kuwa CCM na PPT-Maendeleo kwa wakati mmoja na hasa wakati wa uchaguzi.
Bila shaka ajenda ya PPT ilikuwa ya viongozi wa vyama vingine pia. Kwani baadhi ya vyama vya upinzani viliweka wagombea urais katika mbio za mwaka 2005 ambao hata wao – wagombea na viongozi wao, walijua hawaendi kuleta chochote!
Kulikuwa na fununu kwamba vyama vya upinzani vingepata fedha za kuendeshea kampeni kutoka serikalini na asasi ya Demokrasi ya Uholanzi.
Kwa msingi huo, chama kinachoweka mgombea urais kingekuwa na fungu kubwa la mgawo. Kwa hiyo kugombea likawa suala la “Nenda tu ugombee ili tupate fedha na utangaze chama chetu…”
Ndivyo Anna alivyoingia ulingoni. Mwanamke wa kwanza Mtanzania kugombea urais katika uchaguzi mkuu.
Mwanamke wa kwanza kutoka chama kichanga cha siasa nchini, kisichokuwa na uongozi makini wala mwelekeo unaoeleweka, kugombea urais.
Mwanamke wa kwanza, kuamua kujitupa tu au kutupwa kwenye kinyang’anyiro alichojua au ambacho hakujua nguvu zake, na katikati ya kukurukakara, mwenyekiti wake akamwambia kwamba asilolome sana, vinginevyo atamfukuza uanachama.
Hakuna maelezo ya kitaaluma, lakini mchoko wa kampeni, vitisho vya kufukuzwa uanachama, kudharaulika mbele ya wenye mali na fedha nyingi za kuendesha kampeni kwa rushwa iitwayo “takrima,” bila shaka vilichangia Anna kuugua baada ya uchaguzi.
Kilichoongeza uchungu la labda kulegeza zaidi mishipa ya Anna, ni matokeo ya uchaguzi – kiwango cha kura alizopata, hata kama tangu mwanzo aliamini kuwa hatakuwa rais wa Tanzania.
Nasikitika kwamba sasa Anna Senkoro ameamsha mikono na kuaga chama chake. Bali anasema mambo kadhaa yenye kuhitaji uchambuzi mdogo.
Anna anasema aligombea urais ili kuwahimiza wanawake nchini kujitokeza kuwania nafasi za juu ya kuchaguliwa na kuongoza.
Je, Anna alikuwa anajua kwamba chama alimogombea hakikuwa chama cha washindi? Anataka kusema kwamba wanawake wachukue mfano wake wa “kujitupa” tu bila uchambuzi wa chama kipi kinaweza kuwa chombo cha kusafiria?
Je, anataka wanawake wawe wanachomoka majumbani mwao na kujitangaza kugombea urais au ubunge kupitia chama chochote kile kilichopo alimradi wanataka uongozi?
Je, anataka wanawake waamini kwamba hata bila kujiandaa na kuandaliwa, bila kuwa na chama chenye uongozi thabiti na sera na hata mvuto wa hoja, basi wajitose tu?
Anna anasema lengo lake kubwa lilikuwa kuwapa changamoto wanawake kujitokeza kujaribu BAHATI yao katika siasa. Nasikitika sana kwamba hii sasa siyo siasa, ni BINGO – patapotea!
Anna anasema hajaamua kwenda chama kingine. Hii ina maana anataka kuingia chama kingine. Amesema hatakwenda vyama vya upinzani kwa kuwa alipokuwa mgonjwa hawakwenda kumwona.
Sasa kila mmoja anaona kwamba ama Anna ataanzisha chama chake, atajiunga na ambacho hakijaanzishwa au atakwenda CCM. Je, hilo nalo ni fundisho la Anna ambalo anataka wanawake waige?
Nasikitika kwamba hakuna cha kuiga kwa Anna Senkoro. Kama funzo tu, ni kujifunza kuacha kufanya aliyofanya. Basi!
Kama PPT-Maendeleo na uongozi wake, Anna hakuwa na dira katika chama chake na kitaifa. Yeye ni tunda la fukuto. Kasi ya mchomoko wake haikuwa na jipya, na kama wengine wa aina yake, ameangukia pua.
Nasikitika hakuna wa kumwiga Anna Senkoro.

kankugambile@yahoo.com

3 comments:

Reggy's said...

Sitaweza kujadili kwa nina juu ya uamuzi wa Anna Senkoro, kwa sababu sijui undani wa sababu zake. Mimi najadili hili la nje: Amekabidhi kadi yake kwa Viongozi wa TPP-Maendeleo. Viongozi wengine wanaohama vyama, hukabidhi kadi zao kwa viongozi wa chama kipya wanachohamia. Huyu amekuwa tofauti, ameamua kufanya tofauti na kukabidhi kadi yake kwa mahasimu wake.

Jeff Msangi said...

Makala safi sana hii.Wanawake wajifunze nini kutoka kwa huyu mama?Nadhani huyu amerudisha nyuma mioyo ya wanawake ambao kwa kumuangalia yeye wangeingia kwenye ulingo wa siasa.Wanawake wanahitajika sana katika kujenga dunia ya leo.

Mija Shija Sayi said...

Anna bado hajanishawishi, bado kabisaaaaa!! bado!

Sikubaliani na sababu alizozitoa, napata picha kwamba kuingia kwake katika kinyang'anyiro hakukuwa ni kwa utashi wake binafsi, sababu kama ingekuwa ni kwa utashi wake lazima angekuwa amejiandaa kwa misukosuko. Siasa ni mapambano kwa hiyo unapoiingia jiandae kupambana. Anna alitakiwa ajue yote haya ya kusalitiwa, ya matokeo kuja kinyume na alivyotegemea, ya kutokutumia muda mwingi na familia, ya kuzomewa na kudhihakiwa...kuugua n.k

Ningependa Anna na viongozi wengine warejee mfano wa uongozi wa mwanafalsa Yesu, pale tunajifunza mambo mengi sana.

Jamani bado hajanishawishi.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'