Sunday, November 29, 2009

Sunday, November 22, 2009

Chafya ya Rais Mkapa

Ole wao Mkapa akipiga chafya!

Sunday, November 01, 2009

Pinda kaishitaki Ikulu; wabunge wataishinda?


WIKI hii Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameichongea Ikulu kwa Watanzania - bila kujua. Kauli yake kwamba Ikulu ndiyo imeiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) iwahoji wabunge kwa kile kinachoitwa 'posho mbili,' inazua maswali ya msingi juu ya nia ya Ikulu kubuni hila za kuua mjadala wa kitaifa juu ya serikali na Richmond.

Ni kielelezo cha uwezo mdogo wa serikali kimkakati kutumia TAKUKURU kuwaandama wabunge wale wale wanaoituhumu TAKUKURU hiyo hiyo. Taifa liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu na ufisadi wa watawala; maazimio ya Bunge kuhusu Richmond hayajatekelezwa; taifa linasubiri taarifa ya serikali kuhusu suala hili, kumbe wao wanaleta utoto wa 'posho mbili' zao?

Nani amewaruhusu Ikulu na TAKUKURU kupachika ajenda dhaifu katika nafasi ya ajenda kuu? Nani amewaruhusu kuandama wabunge wale wale ambao katika mjadala wa kashfa ya Richmond ndio waliopendekeza kigogo wa TAKUKURU achukuliwe hatua?

Hivi mtu akikutuhumu na wewe ukamtuhumu unakuwa mtu safi kuliko yeye, na unapata nguvu ya kumchukulia hatua? Ikulu na TAKUKURU wanadhani njia sahihi ya kujisafisha ni kuwaandama wanaoituhumu TAKUKURU na Richmond yao?

TAKUKURU ambayo haikuona ufisadi wa Richmond kulipwa milioni 152 kwa siku, tena bila kuzalisha umeme; TAKUKURU ambayo haikujua suala la EPA hadi lilipoibuliwa Bungeni; TAKUKURU ambayo haikujua wizi wa Deep Green Finance: TAKUKURU iliyoshindwa kushughulikia ufisadi katika ununuzi wa rada na ndege ya rais; TAKUKURU iliyoshindwa kuona ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa Kiwira; TAKUKURU inayoshindwa kuchunguza upotevu wa mabilioni ya pesa za Watanzania katika miradi michafu ya vigogo (orodha ni ndefu), ndiyo hii inayoona uchungu wa shilingi 50,000 za posho ya wabunge?

Hata kama posho hizo zina utata, watu wenye akili na uchungu na taifa wanaweza kuruhusu suala hili lifunike mjadala wa ufisadi wa Richmond? Huu ndiyo uwezo na upeo wa Ikulu na TAKUKURU kulinda watu wasiozidi wanne na Richmond yao kwa kunyamazisha na kutisha wanaohoji ufisadi huo?

Watu hawa wanajua kuwa ipo siku wataondoka Ikulu au TAKUKURU? Wanajua kuwa kuna maisha baada ya hila zao hizi za kisiasa au wanadhani watafia katika ofisi hizo ili tusiwahoji? Baada ya Ikulu kulinda na kusaidia watuhumiwa wengine wa Richmond kustaafu kwa heshima, inaona hii ndiyo njia mwafaka ya kuiondoa TAKUKURU katika matope ya Richmond? Hivi wanadhani kwamba hata kama wabunge wakiogopa wakanyamaza, wakaacha kuihoji serikali juu ya Richmond, vigogo hawa wanakuwa watumishi safi mbele ya umma na dhamiri zao wenyewe?

Mkakati huu wa Ikulu na TAKUKURU si uhuni mwingine uliovuka mipaka kwa serikali inayoongozwa na wale wale waliotuambia majuzi kuwa hawana nia ya kuwaziba midomo wabunge? Tusikilize kauli zao au tutazame matendo yao?

Hivi serikali inadhani watu pekee wenye akili wako Ikulu na TAKUKURU, kiasi cha kutupangia ajenda dhaifu ndani ya ajenda kuu, na kutarajia sisi tufuate upepo wao wa kisiasa na kucheza ngoma yao 'isiyokesha?'

Kama huu ndiyo mtiririko wetu wa kufikiri, viko wapi vipaumbele vya kitaifa? Ni haki tupotoshwe na propaganda za Ikulu na TAKUKURU, tuanze kuwajadili na kuwazomea wabunge ambao wamegundua janja hii ya Ikulu na TAKUKURU, wakawa jasiri kugoma na kutoa kauli thabiti?

Ni lini taifa hili litaacha kulea na kuenzi ukondoo, likatukuza ushujaa hata kama ni wa wachache wanaoweza kuwaambia watawala "hapana?"

Katika wakati ambapo taifa zima liko gizani kwa sababu ya maamuzi mabovu ya watawala hao hao, tuache kujadili athari za Richmond tujadili posho mbili za wabunge? Kama walikuwa na nia njema na suala hili si wangelitafutia nafasi yake baada ya kuturidhisha na utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu Richmond?

Mbona tunajua kuwa hata rais mwenyewe na mawaziri wake wanaposafiri mikoani na kwingine wanapewa takrima hizo hizo na wenyeji wao? Ni Ikulu na TAKUKURU ipi itamchunguza rais?

Ni haki Watanzania wanyimwe fursa ya kujua hatima ya Richmond kwa ajili ya kuridhisha matakwa ya Ikulu na TAKUKURU kabla wakosaji wa TAKUKURU hawajawajibishwa?

Tumefika mahali ambapo serikali inatukuza na kulinda vigogo na Richmond yao kuliko maisha ya Watanzania milioni 40?

Wala Pinda hakuhitaji kusisitiza maagizo ya Ikulu kwa TAKUKURU, kabla hajatueleza nani aliiagiza TAKUKURU kuisafisha Richmond. Tunachojua ni kwamba TAKUKURU ipo chini ya ofisi ya rais. Hivyo, Ikulu na TAKUKURU ni kitu kimoja. Pinda anaweza kutusaidia kujibu Ikulu, TAKUKURU na Richmond ni vitu vingapi?

Hivi Pinda anadhani tumesahau kauli yake kwamba suala la hatua za serikali dhidi ya mkurugenzi wa TAKUKURU liko mbele ya rais linafanyiwa kazi? Kumbe ndiyo kazi yenyewe hii? Na Pinda anadhani ameipa Ikulu sifa?

Je, vitisho hivi vya Ikulu na TAKUKURU kwa wabunge ndiyo tafsiri ya kauli ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwamba yeye na Rais Jakaya Kikwete wametoka mbali hawawezi kutenganishwa?

Au ndiyo tafsiri ya kauli ya Lowassa, muda mfupi kabla ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka jana, alipowaonya wabunge akisema 'sote hapa ni wanasiasa, tukiamua kushughulikiana nani atabaki?'

Au ndiyo utekelezaji wa kauli ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hosea, alipobanwa na wabunge katika moja ya semina alizowaandalia katika hoteli ya Whitesands, Dar es Salaam, wakamhoji kwa nini hajawajibika kutokana na uzembe wa ofisi yake katika sakata la Richmond, naye akakasirika na kusema atawashughlikia wao kwanza?

Pinda alidhani akisema TAKUKURU imetumwa na Ikulu wabunge wote wangeogopa na kutakatifuza makosa ya watawala? Je, hii si dalili kwamba serikali inaficha udhaifu na uchafu wa Ikulu kwa kutumia TAKUKURU kuwatisha wanaohoji kilichopo nyuma ya pazia?

Na hapa ndipo tunapowageuzia kibao wabunge wenyewe. Tuliwaambia, tukawashauri mapema wakati serikali ilipoleta muswada wa kubadili Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kuwa TAKUKURU; tukasema taasisi hii haiwezi kufanya kazi ya kudhibiti wala kuzuia rushwa kama itaendelea kuwa chini ya ofisi ya rais.

Tulijua kwamba ofisi ya rais nayo inahitaji kuchunguzwa na kudhibitiwa, na kuwa serikali haitaki kuiondoa ofisi hiyo chini ya rais ili kuwalinda ama rais mwenyewe, au wasaidizi wake au rafiki zake au jamaa zake iwapo watakumbwa na masuala yanayohitaji mkono wa TAKUKURU.

Tulipendekeza iundwe chini ya chombo kinachojitegemea ili kiweze kusaidia kumulika kote kote bila woga wala upendeleo. Lakini dhamira ya serikali ilipitishwa na wabunge wale wale waliojifanya wanakipenda sana chama chao (CCM) kuliko taifa.

Katika hili la sasa, wabunge hawa wanaopambana na TAKUKURU wanapaswa kujua kwamba wanapambana na nguvu nyingine nyuma yake. Wataweza kuishinda? Je, wananchi watabariki hila za Ikulu na TAKUKURU?

Je, wabunge wetu sasa wameanza kuelewa hekima yetu ya kuiondoa TAKUKURU ofisini kwa rais? Maana hekima ya kawaida inatujulisha kuwa si marais wote watakuwa waadilifu. Wabunge wanajua mchezo unaochezwa na watawala, maana baadhi yao walikuwamo katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kilichomchachafya na kumtisha Sitta na wenzake.

Viongozi wale wale wa vikao vya NEC ndio hao hao wanaoituma TAKUKURU iwarudie kina Sitta kwa hila mpya. Si wamalize sula la Richmond kwanza tuone jeuri yao? Je, wabunge wataweza kuinyamazisha Ikulu na TAKUKURU?

Watawala wanadhani wabunge na wananchi hawajui walengwa wanaotafutwa na wanaolindwa katika sakata hili? Hivi Ikulu haiwezi kuwa imara bila kuwakumbatia mafisadi?

MAKALA hii inapatikana pia katika tovuti ya TanzaniaDaima
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'