Saturday, January 30, 2010

Ngoma ya Dodoma ichezewe Unguja?

Dare s Salaam

WANAOTILIA shaka hoja yetu ya muda mrefu kuwa Tanzania inakabiliwa na ombwe la uongozi, watazame kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.

Chama tawala kinaendelea kumeguka. Mwenyekiti hajui aunge mkono kundi gani katika mmeguko huo.

Anaitisha vikao vikuu vya chama, wasaidizi wake wanamgomea, naye anaviahirisha. Wabunge wa chama tawala wanamgomea Waziri Mkuu (mwenyekiti wao) wakipinga muswada wa gharama za uchaguzi. Chama tawala kinaweweseka na kutishwa na “chama hewa” cha CCJ, ambacho kimekwua gumzo nchi nzima kwa wiki nzima, ingawa hakijasajiliwa.

Hiki ni chama ambacho kimekufa kabla ya kuzaliwa, maana wenye chama chao wamekosa ujasiri wa kujitambulisha na chama chao. Wamekikana.

Lakini CCM imekiogopa mno kiasi cha kusambaza waraka nchi nzima kuwaonya wanachama wake dhidi ya CCJ; huku ikijua ifika kuwa wanachama wa CCJ ndio hao hao wa CCM!

Chama imara, chenye uongozi imara, kisingepata kizunguzungu kwa hisia za kuundwa kwa chama kingine. Lakini CCM kimetudhihirishia kwamba nguvu pekee inayokipa uhai ni dola.

CCM bila dola – bila majeshi, bila tume za uchaguzi, bila serikali na taasisi nyingine zinazokitegemeza – hakipo.

Yanayokitikisa CCM ni mengi, hata nguvu ya chama chenyewe upande wa Zanzibar, ambayo sasa imeakisi nguvu halisi ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Rais Karume ametunisha msuli, CCM (Bara) imenywea; Serikali ya Muungano imenyong’onyea. Na kwa hali ya kisiasa ya sasa nchini, tunaweza kusema kwamba walau sasa Karume ameonyesha maana ya kuwa rais wa nchi.

Rais wa nchi ni yule anayesimama kidete kutetea kwa nguvu zote masilahi ya watu wake, hata ikibidi atofautiane na wenzake.

Rais Karume ameona bora kutofautiana na viongozi wenzake wa Muungano, iwapo kwa kufanya hivyo, ataweza kutetea maslahi ya kile kinachomfanya aitwe rais.

Katika miezi miwili iliyopita, Karume amekuwa na utambuzi wa ajabu wa nguvu na umuhimu wake katika siasa za Tanzania. Amekohoa, wenzake wa Bara wamepata mafua!

Ameamua kuwa muasi. Sasa wao wanamuita msaliti. Lakini hakuanza leo. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa usaliti wa Karume ulianzia Butiama, mwanzoni mwa mwaka 2008, alipoathiri mwelekeo wa hoja ya serikali ya mseto Zanzibar; akapendekeza isitekelezwe bila kura ya maoni.

CCM, ambayo ilikuwa imeshaafikiana na Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kamati ya mwafaka, kwamba iwepo serikali ya mseto Zanzibar, ilinywea na kuimba wimbo wa Karume.

Kwa hiyo hata sasa hivi, (wapinzani wa Karume) wanapojitapa kwamba wanafuata maazimio ya Butiama, ukweli ni kwamba wanafuata mapendekezo ya Karume. Na yeye anayasisitiza maazimio hayo kwa sababu ni zao la maoni yake. Hajapoteza!

Bahati mbaya Karume alichelewa kutambua nguvu yake. Siku zote alijiona yeye ni makamu mwenyekiti wa CCM, Visiwani. Alisahau kwamba yeye ni rais, kiongozi wa nchi.

Wengine tunadhani kwamba kilichomfanya awe mnyonge ni mchakato wa kisiasa uliomfikisha Ikulu. Haukuwa mchakato sahihi, wala haukuwa huru na wa haki. Alijua kuna walioshinda na waliotawala. Yeye alikuwa kwenye kundi la watawala, lakini hakuwa katika kundi la washindi.

Imemchukua miaka tisa (9) kujiamini na kutumia urais wake kutetea Wazanzibari. Katika miaka tisa iliyopita, ngoma ilikuwa inapigwa Dodoma, Karume anaichezea Zanzibar.

Sasa ameshtuka. Ameamua ngoma ya Wazanzibari ipigwe na kuchezewa Unguja! Ametuma ujumbe mzito kwa CCM na serikali. Wenye akili wameshaupokea; kwamba si haki na si sahihi kwa CCM kumchukulia Karume kama wanavyomchukulia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Pius Msekwa, au Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

CCM (Muungano) ilipoandaa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu Wazanzibari wakagoma ikaahirisha, na baadaye ikaandaa kikao cha dharura Karume na wenzake wakagoma kuhudhuria, ikaahirisha tena; imedhihirisha kwamba haiwezi kwenda bila nguvu ya Karume.

Sisi siri kwamba kama Karume angehudhuria vikao hivyo, wenzake wa Bara wangevitumia (kwa wingi wao na ubabe wa kihistoria) kumbana na kumwadabisha.

Kwa hatua yake ya sasa, ya kuwagomea na kuitisha kikao maalumu huko Zanzibar, amethibitisha kwamba ana uwezo wa kuzichonga siasa za Zanzibar zikawa tofauti na jinsi ambavyo wenzake wasio Wazanzibari wanataka ziwe.

Amewafungua macho wana CCM wenzake wa Zanzibar kwamba wakiamua, wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika taifa lao. Sasa wametambua, na wamedhihirisha kwamba wao si mkoa ndani ya Tanzania, bali ni taifa ndani ya taifa.

Wana serikali yao; katiba yao; bendera yao; Bunge (Baraza la Wawakilishi) lao; tume yao ya uchaguzi; wimbo wao wa taifa.

Utaifa huu wa Zanzibar ndiyo uliowafanya Karume na hasimu wake mkuu kisiasa, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kukutana na kujadili mustakabali wa taifa lao.

Kwa Karume na Maalim Seif, Uzanzibari wao ni muhimu kuliko Utanzania wao. Imesemwa mara nyingi, na sasa wao wamethibitisha, kwamba linapofika suala la maslahi ya Zanzibar, CUF na CCM ni kitu kimoja.

Kwao, maendeleo ya Zanzibar, kwa muda mrefu, yameathiriwa na kile wanachokiita “ukoloni wa Bara.” Hawa ni watu wanaopigana kujinasua kwenye “ukoloni” wa Serikali ya Muungano.

Ndiyo maana Karume na Maalim Seif wameungana sasa. Kwao, Zanzibar kwanza; Tanzania baadaye.

Si hilo tu, lakini pia wanazingatia ukweli kuwa Wazanzibari wasipoamua kushughulikia matatizo yao wenyewe, wakiamua kuwaachia wabara wayamalize kwa niaba yao, hayatakoma.

Wamechoka kuendesha siasa za Zanzibar kutoka Dodoma; maana wanaweza kufanya hivyo wakiwa Unguja.

Rais Karume aliingia madarakani kwa nguvu, jeuri na aibu. Sasa anajiandaa kuondoka madarakani kwa heshima na utukufu uliowashinda watangulizi wake.

Watafiti na wachambuzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar wanajua na wamesema mara kadhaa kwamba Rais Karume aliupata urais wake bila ushindi utokanao na wingi wa kura halali.

Sasa amepata ushindi dhidi ya nguvu kongwe za CCM zitokazo katika Serikali ya Muungano (Bara), na ameanza kushinda hila za wasaidizi wake na washindani wake wa Zanzibar wanaohaha kumrithi baadaye mwaka huu.

Karume huyu hawezi kuendeshwa kwa maazimio yanayotokana na ushawishi au nguvu ya hoja za akina Msekwa au Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba. Kwake, hawa nao ni sehemu ya “wakoloni” hao wa Muungano.

Ndiyo maana wanaojua siasa za Zanzibar wanakiri kwamba kama Karume asingekuwa nyuma ya ajenda ya CUF kutaka katiba irekebishwe, kuanzishwe serikali ya mseto na mchakato huo usimamiwe na Karume mwenyewe, wana CCM katika Baraza la Wawakilishi wasingeunga mkono hoja ya chama hicho cha upinzani.

Na kama kuna ujumbe CCM inapaswa kuupata kutoka kwenye uamuzi wa baraza kuridhia hoja ya CUF ni mmoja – kwamba umma wa Wazanzibari sasa unaandaliwa kwa kura ya maoni itakayokuwa kama watakavyo watawala.

Ndiyo maana baadhi yetu tunaiona serikali ya mseto Zanzibar inakuja. Ndiyo tafsiri ya kauli ya Karume kwamba rais kutoka Pemba si dhambi. Ndiyo maana naye sasa ana ujasiri wa kuimba wimbo ule ule wa wapinzani, wa muda mrefu, kuwa mafuta ya Zanzibar (kama yapo) yasiwe suala la Muungano.

Wala hatulalamiki, maana huu ni uamuzi uliochelewa. Zanzibar yenye amani haiwezi kuongozwa kwa siasa za ubabe, jeuri, vinyongo na visasi. Wala haiwezi kuwa chini ya chama kimoja tu, maana hata wanaotangazwa kuwa wameshindwa wanakuwa na karibu nusu ya kura zote zilizopigwa.

Lakini kuna jambo ambalo CUF wanalisisitiza; kwamba baada ya miaka 10 madarakani, Rais Karume hana tena uchu wa madaraka. Amekua, ameongoka na yuko tayari kutambua na kutimiza matakwa ya Wazanzibari.

Yupo tayari kuwaunganisha Wazanzibari na kustaafu kwa mbwembwe. Anatafuta ushujaa ambao rais yeyoye mpya atakayeingia madarakani angependa kuutafuta baada ya miaka 10 Ikulu.

Kwa hiyo, ni vema Karume anayemaliza na mwenye nia, apewe fursa (ya walau miezi 6 hadi miaka miwili) asimamie utekelezaji wa makubaliano yake na Maalim Seif.

Katiba irekebishwe, sheria za uchaguzi zirekebishwe, tume ya uchaguzi irekebishwe, wapiga kura wandikishwe upya (vema) na kadhalika. Baada ya hapo, uitishwe uchaguzi huru na wa haki; atakayeshinda amkaribishe aliyeshindwa (maana itakuwa kwa asilimia ndogo tu) waunde serikali ya mseto.

Mwisho wa yote, Karume atastaafu kama shujaa; na Wazanzibari watakuwa wameanza siasa mpya za ushindani usio na uhasama. Nani asiyeitaka Zanzibar ya namna hii?

Ni wazi, wapo baadhi wanaonufaika na siasa za Zanzibar kwa jinsi zilivyo leo. Wapo pia wanaojiandaa kugombea urais baada ya Karume, na wasingependa kuendeleza urithi wa Karume na Maalim Seif.

Kete yao ni moja. Iwapo Karume ataondoka bila kuyaingiza kwenye mfumo mazungumzo yake na Maalim Seif, yatafutika siku ya kwanza ya utawala mpya, naye ataishi maisha ya kula pensheni ya aibu.

Hadi sasa, Karume, kwa hiki kidogo alichofanya, amekuwa shujaa mbele ya Watanzania wengi. Amefuta aibu ya muda mrefu, na amevaa ujasiri wa ajabu unaojitokeza kwa sura ya uasi na usaliti.

Akitaka kuupoteza ushujaa wake huu, alegeze kamba, apoteze nia, awasikilize wanaomsonga kutoka Bara na visiwani. Aatapoteza ushujaa na heshima yake binafsi, na ataitokomeza amani ya Zanzibar ambayo sasa iameanza kuchanua.

Wakristo wanaamini kwamba kama Yuda asingemsaliti Yesu, kile wanachokiita ukombozi wao kisingepatikana. Yawezekana Karume pia amegundua kwamba asipomsaliti Rais Jakaya Kikwete na CCM yake, ukombozi wa Wazanzibari hautapatikana.

Kwa nini asiasi kama amegundua kuwa wakubwa hawana nia njema na Zanzibar? Na kama tunataka ukombozi wa Zanzibar, kwa nini tusimsaidie Karume kuwadhibiti “wahuni” wa Bara wanaohaha kumzuai asiasi zaidi?

ansbertn@yahoo.com +255 653 172 665

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'