Friday, November 21, 2014

Kwa heri Asiimwe, Malaika wangu

Ni wakati mgumu sana katika maisha yangu. Si jambo jepesi kufiwa na mtoto. Nafarijika kwa maneno ya wote walionitumia salaam za rambirambi. Hapa chini, najaribu tu kufanya jambo gumu na zito - kuwashirikisha, kwa njia ya tanzia, WASIFU wa binti yangu Asiimwe aliyefariki ghafla mwanzoni mwa mwezi huu:

Asiimwe Wilhelmina alizaliwa tarehe 12/10/2002 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam. Ni mtoto wa tatu, na binti wa pili, katika familia ya Bwana na Bibi Ngurumo.

Babu yake mzaa baba (aliyefariki dunia Mei 15 mwaka huu), Ta Theogenes Ngaiza, ndiye alimpatia jina Asiimwe, maana yake Mungu Ashukuriwe. Katika ubatizo, bibi yake mzaa mama akampatia jina Wilhelmina, lake mwenyewe. Akawa somo wake.

Hadi mwaka jana 2013, Asiimwe alikuwa anasomea katika Shule ya St. Aloysius Girls ya Dar es Salaam. Mwaka huu 2014 mwanzoni, alihamishiwa katika Shule ya St. Joseph Model English Medium, Rutabo, katika darasa la nne.

Jumatatu ya tarehe 10/11/2014 alipaswa kufanya mtihani wa taifa wa Darasa la Nne. Kwa miezi kadhaa kabla na baada ya kuhamia Rutabo, amekuwa katika mafundisho ya Komunyo ya Kwanza, ambayo alitarajia kupokea tarehe 15/11/2014.

Tarehe 06/11/2014 asubuhi, akiwa katika ibada ya misa kwenye Kanisa la Parokia ya  Rutabo, alionekana kupepesuka. Kabla hajaanguka chini, Sista Mlezi alimdaka na kumtoa nje, akamkabidhi kwa walimu wamhudumie.

Walimu waliamua kumpeleka Hospitali ya Ndolage, akapimwa na kugundulika ana Malaria kali na upungufu wa sukari mwilini. Walimlaza na kutoa taarifa kwangu, baba yake.

Kabla ya kuwasili hospitalini, kwa kuwa nilikuwa mbali kidogo, Muleba Mjini, nilipiga simu nyumbani, nikashauri mgonjwa apelekewe chai, kwani nilikuwa nimeelezwa na walezi wake kwamba Asiimwe alipaswa kuwekewa drip ya dawa, lakini mishipa ya damu ilikuwa haipatikani.

Wauguzi walihisi hali hiyo ilitokana na kushuka kwa sukari, na ilihitajika sukari ya nyongeza mwilini ama kwa kunywa chai au glucose au kitu chochote chenye sukari.

Shangazi yake mkubwa aitwaye Francisca, aliandaa na kupeleka chai kwa mgonjwa. Kadiri ya simulizi la shangazi yake, alipowasili alikuta mgonjwa anazungumza, wakasalimiana huku, kadiri ya maelezo ya wauguzi, ameshawekewa drip ya quinine iliyochanganywa na glucose.

Nilipowasili hospitalini baadaye, nilikuta Asiimwe anamalizia drip ya pili ya quinine, na hakunitambua, kwani alionekana kuwa katika usingizi na uchovu mkali. Sote tuliokuwapo tulihisi ni uchovu uliotokana na ukali wa dawa.

Mnamo saa nane (8) usiku wa kuamkia tarehe 07/11/2014, Asiimwe alikata roho akiwa na drip ya tatu ambayo hakuweza kuimalizia.

Taarifa ya kifo chake, kwa mujibu wa daktari, inasema Asiimwe alifariki dunia kutokana na upungufu mkubwa wa sukari mwilini, ujulikanao kama hypoglycemia.

Sista mmoja aliyeishi na Asiimwe kwa karibu, na ambaye alikuwa mwalimu wake wa dini, alimweleza Asiimwe kama mtoto mwenye Sifa ya. Kimalaika. Alipenda sana ibada. Na hata alipotimiza miaka 12, mwezi uliopita, aliomba nimpatie zawadi. Alichagua anunuliwe Biblia Takatifu, ndogo.

Kwa maelezo ya Sista huyu, hiki kilikuwa kitendo kisicho cha kawaida kwa mtoto mdogo kuomba zawadi ya Biblia kutoka kwa mzazi katika siku yake ya kuzaliwa, kwani hata watu wazima wengi hawana, na hawasomi, Biblia; wala wasingechagua Biblia kama zawadi kwenye siku muhimu za maisha yao.

Asiimwe alibahatika kuwa mmoja wa watoto waliokwenda kuhiji Nyakijoga, Mugana, wiki chache zilizopita. Kwa maelezo ya Sista Mlezi, Asiimwe hakuwa kwenye orodha ya awali ya mahujaji kutoka shule hiyo.

Alipata fursa hiyo baada ya mwanafunzi mmoja kushindwa kwenda kwa sababu za kiafya. Sista akampendekeza Asiimwe ajaze nafasi hiyo.

Katika salaam za pole kwangu baba mzazi, Sista Mlezi alisema pamoja na kwamba alilia sana baada ya kupata taarifa za kifo cha Asiimwe, anaamini kwamba Mungu aliamua kumchukua mtoto huyu mapema ili aungane naye kabisa mbinguni, kabla ya muungano wa kiroho katika Ekaristi Takatifu aliyopaswa kupokea katikati ya mwezi huu.

Alisema, "Asiimwe alikuwa mtoto mwema sana mbele yetu na mbele ya Mungu. Mungu ameamua kumchukua mapema ili asichafuke. Amekuwa mwakilishi, na atakuwa mwombezi wa familia, mbele ya Mungu. Asiimwe alikuwa Malaika. Amewahi kabla ya Komunyo, ili aungane na Mungu kabisa."

Miongoni mwa watu walionipa pole na kuzungumza nami kuwa simu mara baada ya kupata taarifa za kifo cha Asiimwe, ni Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ambaye alisema maneno haya ya faraja:

"Asiimwe alikuwa mtoto wako, lakini alikuwa mtoto wa Mungu zaidi. Mungu alikupa Zawadi hii ukae nayo kwa miaka 12 tu, halafu ameichukua. Usinung'unike, msikate tamaa wala msikufuru; bali kama yasemavyo maandiko, Mshukuruni Mungu kwa kila jambo."

Asiimwe alizaliwa, akabatizwa na akalelewa katika imani Katoliki; na amezikwa katika imani yake hiyo. Alikuwa mtoto mwenye upendo wa pekee kwa kila mtu aliyekutana naye.

Uso wake ulijaa tabasamu. Alikuwa na huruma ya wazi. Siku moja nilipomtembelea shuleni na kutoa pesa ya matumizi kwa ajili yake, aliniuliza kwa upendo na tabasamu usoni, "mbona hujamwachia Sista pesa yoyote? Mpe na yeye, ananitunza vizuri." Kwa ombi hili la Asiimwe, nilimpatia Sista kiasi kidogo cha pesa nilichokuwa nacho!

Alikuwa mchangamfu, mcheshi na mwenye utani kwa watoto wenzake na watu wazima. Mnamo Septemba 02, 2014, nilialikwa kwenye adhimisho la misa ya Shukrani ya Padri Denis Muchunguzi parokiani Rutabo.

Katika hafla iliyofanyika mbele ya Kanisa kwenye viwanja vya Shule ya akina Asiimwe, mtangazaji alinitaka nicheze ngoma ya Kihaya iliyokuwa inapigwa. Nilipoingia tu uwanjani na kuanza kucheza na Ndugu Diocles Rutabana, kama ilivyokuwa imetangazwa, nikistuka kuona Asiimwe akiwa mbele yangu, anacheza ngoma hiyo pamoja nami.

Ndiyo ilikuwa siku ya mwisho niliyomuona akiwa mzima! Kumbe alikuwa ananiaga. Aliniaga kwa tabasamu, kwa furaha!

Tulimlaza salama kwenye makao ya milele, katika makaburi ya familia ya babu zake, Kyamawa, Rwanda, Kamachumu, tarehe 09/11/2014.

Naandika haya kwa masikitiko na uchungu mkubwa sana. Napata kumbukumbu  zinazoumiza moyo wangu. Siwezi kuendelea!

Kwa niaba ya familia,  nawashukuru wote  walioshiriki kumlea, kumfundisha na kumhudumia kwa njia na nyakati mbalimbali katika maisha yake mafupi ya miaka 12 na siku 24.

Nawashukuru pia kwa namna ya pekee wote waliotufariji kwa njia mbalimbali tangu tulipopatwa na msiba huu mzito.

Shukrani za pekee ziwaendee mapadri Faustine Mukyanuzi, Florence Rutaihwa na Johannes Rweyemamu, walioongoza ibada ya mazishi ya Asiimwe; Padri Evodius Mwijage aliyeadhimisha misa ya kuanua matanga, wote walioshirikiana nasi na wanaoendelea kutufariji katika kipindi hiki kigumu.

Katika Ibada ya Misa ya mazishi yake, Padri Mukyanuzi, Paroko wa Rutabo, alisema kwamba katika umri mdogo aliokuwa Asiimwe, ni dhahiri kwamba hakuwa na makosa makubwa mbele ya Mungu.

Akasema misa hiyo, pamoja na kumkumbuka marehemu, itumike kuombea wazazi na familia. Zilitolewa Misa 129 kwa nia hiyo.

Hata hivyo, kwa imani zetu, tunamwombea Asiimwe huko alikotangulia, Mungu amjalie pumziko jema na raha ya milele. Pengo lake haliwezi kuzibwa kamwe.

Tulimpenda sana, lakini Mungu amempenda zaidi. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe!

Kwa heri, Malaika wangu, Asiimwe!


No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'