ALIPOULIZWA na waandishi wa habari mapema mwaka huu juu ya habari kwamba watu wanne waliouawa na polisi jijini Dar es Salaam hawakuwa majambazi bali wafanyabiashara, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Abdallah Zombe, aliwataka wananchi wasiingilie kazi ya polisi. Alisisitiza:
"Upolisi ni taaluma kama nyingine. Unasmomewa. Sisi ndio tunaweza kusema fulani ni jambazi au la..."
Sasa wenye taaluma yao, wakiongozwa na Jaji Kipenka Musa, wametoa taarifa ya tume inayoonyesha kuwa waliouawa hawakuwa majambazi. Askari polisi 15 wamehusishwa na mauaji hayo ya kikatili na uporaji wa mamilioni ya shilingi.
Zombe ameumbuka. Wananchi wanahoji: "Taaluma yake ni ipi sasa?" Taarifa zinasema naye yuko chini ya ulinzi, anahojiwa, huku akisubiri kuvuliwa vyeo vyake ili ashitakiwe kwa makosa yake, ingawa vyanzo vya kipolisi vimesema hatashitakiwa kwa mauaji, bali kwa 'makosa mengine.'
Lililo wazi ni kwamba wananchi wanaonekana kuchukizwa na kitendo cha Zombe kutopelekwa mahakamani Jumapili 20.02.2006 pamoja na askaro polisi wanne waliokwisha kamatwa.
Nashangaa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, anatoa kauli za kupinga taarifa za vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa Zombe. Watu wanajua kwamba alikwisharudishwa mkukumkuku kutoka Rukwa alikokuwa amepelekwa kuwa RPC; wanajua kuwa amekuwa akihojiwa makao makuu ya polisi; lakini Tibaigana anasema Zombe hajatiwa mbaroni, wala hahusiki!
Anaficha nini? Sasa kama hajatiwa mbaroni, katiwa wapi? Tibaigana hajaeleza Zombe yuko wapi? Anamkingia kifua? Vyovyote itakavyokuwa, Zombe keshakuwa Zombe, na wananchi wanataka serikali imzombe, haki itendeke! Vinginevyo, tutasema bado serikali inaendekeza kulindana.
Tunahitaji kujua kwa sababu hatujui; na hatuwezi kujua kama hatujui kwamba hatujui...Hatutajua chochote iwapo hatutahoji na kudadisi. Na kadiri tunavyojua, ndivyo tunavyogundua kwamba hatujui...
Tuesday, February 21, 2006
Wednesday, February 15, 2006
Nimerejea ulingoni
WAPENDWA wanablogu, nilipotokomea sikuaga, kwa sababu haikuwa nia yangu kujitenga nanyi. Sasa nimerejea. Kwa muda nilikuwa mafichoni. Baadhi ya walionikosa kwenye blogu walitumia njia nyingine za kuwasiliana nami, wakahoji kama niko uhamishoni! Hata bila kujibu nilikuwa wapi, nafurahi kuwatangazia maswahiba wote kwamba sasa nimo ulingoni. Nimefurahi kuwakuta wanablogu wapya, kina Jeff Msangi (niliyemuathiri binafsi kuingia kwenye blogu) wakiwa wanatamba. Picha za Muhidin Issa Michuzi zimekuwa kivutio kingine. Hoja tekenyo za Reginald Simon zimekuwa kiburudisho kikubwa, bila kusahau hoja nyeti za painia Ndesanjo Macha. Nakiri kwamba nilikosa mengi katika muda niliokuwa mbali na wanablogu. Yawezekana pia nimewanyima machache kadhaa niliyokuwa nayo. Tafadhari mnisamehe. Sasa nimerejea.
Thursday, February 09, 2006
Picha iliyowaponza Tanzania Daima Hii Hapa
NOVEMBA 6, 2005 Gazeti la Tanzania Daima lichapishwalo na Free Media Ltd ya Dar es Salaam, lilikuwa na habari na makala nzito juu ya kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar wiki hiyo uliomrejesha Rais Amani Karume madarakani. Mbele ya gazeti kulikuwa na picha hii. Gazeti liliuzwa hadi likaisha. Walilenga kuchekesha, wakanunisha wakubwa. Walitumaini wako huru, wakajikuta mahabusu. Soma hapa. Na dunia nzima ilitambua ubabe wa serikali ya Tanzania. Ona!
Subscribe to:
Posts (Atom)
- Ansbert Ngurumo
- Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'