Sunday, May 21, 2006

Nimeshinda Mauti

NILIPOWAELEZA baadhi ya rafiki zangu walicheka, wengine wakatania kwamba aliyeshinda mauti ni Yesu Kristo tu, kwa vile, kama waaminivyo Wakristo, ndiye alikufa halafu akafufuka. Lakini ukweli ni kwamba tangu Mei Mosi hadi Mei 15, 2006 nilikuwa hoi, kitandani.

Kwa siku tano za kwanza, nililala nyumbani kwangu nikiwa natumia dawa nilizopewa hospitali. Nilikuwa nasumbuliwa na Malaria INAYOKATAA DAWA, ambayo vijidudu vyake vilikuwa ngangari kinoma; ikabidi nirudishwe hospitali Mei 6, baada ya kumaliza dozi nzima ya Arinate.

Nililazwa katika hospitali ya Dk. K.K. Khan, katikati ya jiji la Dar es Salaam, nikatundikiwa dripu 39 (tisa za Quinine na 30 za antibiotics). Kichwa kilinitwanga kwelikweli kwa siku 10 mfululizo.

Nakumbuka mara ya mwisho niliugua mwaka 1981. Lakini mara hii ilikuwa hatari zaidi. Nashukuru nimepona, nimerejea katika kundi la wanablogu wenzangu. Kumbuka, MBINGUNI (maana nisingekwenda motoni) hakuna BLOGU. Ndiyo maana nimechomoa!

7 comments:

Anonymous said...

Pole sana Ngurumo, Mwenyezi Mungu hapendi kuona unateseka na amini yote haya ni mapito. Nafurahi kuwa u-mzima na naamini Bwana ataendelea kukulinda kupitia malaika zake. Ningependa tuwe pamoja kupitia tovuti yangu hii www.JamboTanzania.net na naamini ukiwa unatoa mada zako kwenye sehemu ya forum(mijadala) inaweza kupendeza zaidi.
Aidha naweza kukuweka kama Moderator na ukaongoza mijadala yote. Pia niko tayari kukupa email account iwe ngurumo@jambotanzania.net au vyovyote upendavyo. Nimekuwa nikifuatilia makala zako kwa kina na nimevutika sana nazo.Unaweza kwenda forum moja kwa moja kupitia www.jambotanzania.net/forum na ukajisajili. Au unaweza kuwasiliana nami kwa barua pepe kupitia mac@jambotanzania.net au sim +255 741/787 444 649.
Mungu akujaalie hekima zaidi.

John Mwaipopo said...

Urejewe na nguvu na afya tele tele.

Jeff Msangi said...

Nikisema pole nitakuwa kama nakukumbusha yaliyopita.Hivyo nitasema karibu tena na nakutakia afya njema.

mloyi said...

Pole Bwana ngurumo. Ni hali yetu sisi Wa-TZ kusumbuliwa na magonjwa ambayo wenzetu wameyasahau kabisa. Pole sana.
Nategemea hii itakuwa changamoto ya kuandika habari za kupambana na malaria katika ulimwenu huu kwa dhati kabisa.
Najua hali uliyopitia, nakumbuka siku za JKT nilikuwa nasumbuliwa na malaria kila baada ya wiki mbili, hesabu vidonge vingapi nilikunywa! Kama vinamadhara mengine? nimepunguza siku ngapi za maisha yangu?
MALARIA inabidi iondolewe kabisa duniani.

mwandani said...

Pole Ngurumo. Hizo dripu za kwinini niliziramba mwaka 89 - najua jinsi zinavotwanga kichwa.Pole.

Ubarikiwe.

boniphace said...

Ngurumo tulikukosa sana hapa afadhali umekuja maana kinyume chake tungetangaza msiba na kufuta Gazeti Tando lako? Kumbuka sasa kutoa pasword yako kwa mwanao ili ukikimbilia mbinguni siku nyingine Gazeti Tando hili lisife.

Reggy's said...

Pole sana Mr. Ngurumo. malaria ni mbaya kuliko maradhi mengine tunayoogopa sana sasa. lakini usijali kwa bora uzima na umerejea salama. Tulikumiss, na tonaomba, labda kwa ugonjwa pekee, usipotee tena.
Nataka Makene atambue kwamba Gazeti tando hili lisingefungwa, endapo Israel angeamua kufanya vitu vyake. Kwani Hukuandika wosia kulilidhisha kwa mtu? HII NI CHANGAMOTO.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'