Friday, August 18, 2006

Madaraka ya wanasiasa ni bora kuliko maisha yetu?

Na Ansbert Ngurumo, Toronto

NIKIWA Jijini Toronto, Canada wiki hii, nimekutana na watu wengi mno. Walionigusa zaidi ni watu wawili – Ruby Yang na Thomas Lennon.

Ruby na Thomas ni watengeneza filamu. Hawa ni wanahabari. Wametengeneza filamu inayoonyesha jinsi kutokujali kwa serikali ya China kulivyowasababishia wananchi wengi kupata virusi vya UKIMWI, wakati serikali ikisisitiza kwamba hakuna UKIMWI nchini humo.

Ilikuwa hivi: Miaka ya 1980 na 1990, Wachina walihamasihwa kuuza damu yao kwa vituo vya kukusanyia damu vilivyoanzishwa na serikali ili wapate pesa. Umaskini! Vituo vilivyonunua damu yao viliiuza kwa wenye makampuni na viwanda vya kutengenezea dawa.
Damu nyingine ilizungushwa na kutunzwa katika maabara za hospitali ili itumike kwa wananchi waliohitaji kuongezewa damu. Vifaa walivyotumia havikuwa safi. Na si kila damu ilikuwa safi au salama.

Tangazo kwenye redio na televisheni lilisema: “Nyosha mkono wako, vumilia maumivu kidogo ya sindano; ukunje tena; tayari umeshajipatia Yuan 50.”

Matokeo yake, wananchi waliambukizana UKIMWI. Wazazi wakafa. Watoto wadogo wakabaki yatima. Umaskini ukaongezeka. Serikali kimya!

Likaja tatizo la ziada. Kwa desturi, wachina hawazungumzi mambo yao hadharani. Vyombo vya habari havipewi fursa pana ya kufichua masuala kama hayo. Kuna ugandamizaji mkubwa wa uhuru wa habari. Na watawala wanafurahia hali hiyo.

Ndipo Ruby na Thomas, wakaamua kufanya jambo moja – kutengeneza filamu, ambayo ingekuwa kichocheo cha kusema ukweli ambao serikali haitaki kuusikia. Wakaenda katika jimbo moja la Yingzhou, lililokuwa limeathirika zaidi.

Wakatumia waandishi wachache wenyeji na wanataaluma wengine. Wakatengeneza filamu kali, ambayo sasa imepata tuzo kadhaa za kimataifa. Na imeilaimisha serikali kukubali ukweli!

Filamu hiyo (Damu ya Jimbo la Yingzhou) inaonyesha maisha ya shida ya watoto wa vijiji maskini katika jimbo la Anhui Province. Wanakutana na mambo mawili. Tamaduni zinawazuia kusema ukweli. Na unyanyapaa unaifanya jamii, hata ndugu wa karibu, wawatenge watoto hawa. Hata salamu hawapewi. Kisa? Kila mtu anadhani akiwasaidia naye ataambukizwa. Kifo kinabisha hodi mchanan kutwa. Kila mtu anaona. Hakuna aliye tayari kusaidia. Kisa? Woga wa kifo!

Watengeneza filamu wanaingia kijijini. Wanasalimiana na watoto. Kwa mara ya kwanza, watoto hao wanapata mtu wa kuwashika mkono na kuwagusa!

Mhusika mkuu katika filamu hiyo ni motto aitwaye Gao Jun. Yu mkimya kabisa. Hata akisemseshwa hajibu, hadi mwishoni mwa filamu! Kimya hicho kinawakilisha dhuluma na adha ya raia wengi wasio na mahali pa kusemea katika nchi yao, huku wakigandamiza na maisha duni, matokeo ya uamuzi mbaya wa watawala.

Kutokana na uamuzi huo mbaya, wajanja walianzisha vituo bandia vya kununua damu. Baada ya muda mfupi, maelfu ya wakulima maskini katika jimbo la Henan, walikuwa wameambukiza UKIMWI.

Ghafla, jimbo hilo pekee likasemekana kuwa miongoni mwa watu 280,000 waliouza damu yao, 25,000 walikuwa wameambukizwa virusi miaka ya mwanzo ya 90.

Juzi tukiwa Toronto, mwanaharakati Chi Heng, aliyeanzisha asasi yenye makao makuu Hong Kong kwa ajili ya kupambana na maambukizi yaUKIMWI, alisema China sasa ina watu wapatao milioni moja wenye virusi vya UKIMWI. Wachina wengi walioambukizwa ni wakazi wa vijijini. Huu ni UKIMWI wa kisiasa.

Nguyu ya filamu ya Damu ya Jimbo la Yingzhou nayo ilijadiliwa. Kila mtu aliyesikia habari zao alisifia jitihada za watengenezajiw a filamu hiyo, kwamba zimeibadilisha serikali na jamii ya China. Usiri, urasimu na vitisho vya serikali vilikuwa tishio kwa uhai wa watoto hao.

Sasa wanaishi kwa matumaini. Wanahabari hawa waliona bora wavunje urafiki na serikali ili kuokoa maisha ya masikini na wanyonge, wapiga kura wanaouza damu yao kununua UKIMWI kwa sababu ya umaskini.

Ruby na Thomas, walivunja ukuta wa urasimu na utamaduni, wakatumia taaluma yao kuonyesha uzalendo wao, huku serikali ikiwabeza kwamba wanaichafulia jina katika jumuiya ya kimataifa.

Juzi walipokuwa wakijadili nguvu ya filamu yao, waliifananisha na ya mapanki, - Darwin’s Nighmare ya Hubert Sauper; wakasema ni filamu jasiri inayowatetea wananchi maskini dhidi ya ubabe wa sera mbovu za wanasiasa na matajiri wa ndani na nje.

Wanakemea uzembe wa serikali zetu. Wanataka wanasiasa wasahau kwanza madaraka yao, wakumbatie maisha ya wananchi wao.

Soma vizuri tamko la wabunge wetu kuhusu filamu ya mapanki. Wanafanya kazi kama watu ambao hawakuchaguliwa na wananchi, bali wameteuliwa na rais. Wanadhani lazima wakubaliane naye kwa kila kitu, hata kinachowadhuru wananchi.

Wabunge wetu wanakwepa hoja. Hawaoni wala hawakubali kwamba utandawazi ndilo tatizo. Hawasemi kwamba sera yetu ya uwekezaji ndilo tatizo. Hawakubali kwamba umaskini wa wananchi wetu ndio unawafanya walishwe vitu vya ovyo ovyo.

Zaidi ya hayo, tamko lao na lile la Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanafichua pia siri bila kutamka bayana, kwamba sasa wako tayari kuingilia taaluma ya habari. Wanadharau kazi na taaluma za wengine; wanatukuza vyeo vyao.

Wanawabeza waandishi wa Tanzania kwamba ‘wamepotosha’ hotuba ya rais.
Hawajui kwamba waandishi hawa ni watoto wa wananchi wale wale maskini wanaolishwa mapanki, yaliyooza na yasiyooza.

Hawajui kwamba waandishi nao wana macho, pua, masikio na milango mingine ya fahamu wanayoitumia kuandika habari zao. Wanasiasa wetu wanataka kujenga dhana potofu kwamba waandishi ni makarani wa wanasiasa!

Na kwa tabia ya wanasiasa wetu, kama wangekuwa Wachina, wangekuwa wamewafungia watengeneza filamu ya damu eti wanadhalilisha nchi yao, wanatumiwa na watu wasioitakia mema nchi yao. Kwa wanasiasa wetu, nchi ni ya watawala. Kila anayegusa heshima na maslahi watawala anaambiwa haitakii mema nchi yetu! Anaambiwa si mzalendo. Tutabadilika lini?

ansbertn@yahoo.com +255 744 607553 www.ngurumo.blogspot.com

Makala hii inapatikana pia katika www.freemedia.co.tz

Mwisho

Saturday, August 12, 2006

Tunampenda rais wetu, hatukubali makosa yake

Na Ansbert Ngurumo, Toronto

JUMAPILI hii nipo mbali na nyumbani kwa shughuli nyingine ya msingi kitaifa, lakini nimedhani kwamba ipo haja ya kukamilisha hoja yangu niliyoianza wiki iliyopita, na ambayo sasa imegeuka mjadala wa kitaifa.

Nilipoandika kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwezi uliopita, nilijadili suala la mapanki na ukahaba kidogo. Kwa makusudi kabisa, niliacha suala la silaha.

Wengi waliosoma uchambuzi wangu walitoa maoni yao kwa ujumbe mfupi wa simu na kwa barua pepe. Zaidi ya watu 30 waliungana nami kwamba Rais Kikwete alipotoshwa. Tena wengine walikuwa wakali hata kusema nilikuwa mwoga, nikashindwa kusema Rais alidanganya taifa!

Wengine walitumia lugha ya utani kwamba katika Chama Cha Mapinduzi, mwenyekiti hakosei; hata akisema jambo ambalo wanajua si kweli, watapiga makofi kumshangilia, na hata ikibidi wataandamana kushangilia.

Yawezekana walikuwa wakijadili yaliyojitokeza jijini Mwanza, baada ya viongozi waandamizi wa CCM kuwakusanya wanachama waandamane kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete. Kilichowashtua wananch wengi baada ya hapo ni kubaini kwamba wakati Rais Kikwete anahutubia Watanzania kuhusu ‘ubaya’ wa filamu ya Hubert Sauper juu ya mapanki, wananchi wengi waliomsikia walikuwa hawajaiona.

Ndiyo maana makundi kadhaa ya wananchi yamekuwa yakihaha kuitafuta filamu hiyo, waione. Sasa unajiuliza: Hawa walioandamana kuunga mkono hotuba ya Rais wetu walikuwa wanaunga mkono jambo gani? Sitashangaa kwamba hata aliyewahamasisha na aliyepokea maandamano yao walikuwa hawajaona filamu hiyo!

Wapo wengine walionitumia ujumbe mfupi wa vitisho na matusi, kwamba nawapotosha wasomaji, huku mmojawapo akihoji: “Unamkosoa rais wewe? Huogopi kufa?”

Nilijaribu kuwajibu baadhi yao, na baada ya kubadilishana hoja, wengine walionekana kuelewa, na kukiri kuwa ushabiki wao kwa Kikwete ndilo tatizo. Hawataki kuona akichafua rekodi yake ya kisiasa. Nikamuuliza mmoja wao: “Sasa mbona nyie mashabiki wake ndio mnamchafua? Tambua kwamba huwezi kumsafisha rais kwa kutetea udhaifu wake, bali kwa kutetea maudhui na mikakati inayoteteka.”

Nimekuwa nawaza, najihoji. Hii ndiyo Tanzania tunayotaka kujenga? Tunajenga taifa la watu wanaokubali chochote ambacho wakubwa wanasema na kupitisha, hata bila kudadisi? Na bado tunajidai kwamba tuna ‘taifa hai?’

Huu ndiyo ukereketwa? Je, wasingeandamana ingempunguzia nini Rais Kikwete? Au bado tunaendelea kuamini kwamba fikra za mwenyekiti, hata kama ni potofu lazima zisifiwe na zidumishwe?

Kwa hakika, kwa sababu watu wengi walikuwa hawajaiona filamu hiyo, wakiwamo wabunge wetu, Rais Kikwete amejikuta akiipigia debe filamu aliyodhamiria kuipiga vita. Na kwa kuwa aliozungumza nao walikuwa hawajaiona, ujumbe aliotuma siku hiyo siyo utakaozingatiwa baadaye kila mmoja akishaiona filamu hiyo.

Lakini hoja nyingine ambayo imejadiliwa kidogo mno ni mbinu aliyotumia rais kuzungumzia suala hilo. Jukwaa alilotumia – wananchi wa Mwanza – halikuwa sahihi. Lingekuwa jukwaa sahihi kama angekuwa anafanya uamuzi mgumu na mkubwa wa kuzuia minofu ya samaki wetu kupelekwa Ulaya. Wananchi wangeona wamepatiwa ukombozi. Kilichowafanya Watanzania wengi sasa ‘walumbane na rais’ baada ya kusikia hotuba yake, ni hicho. Hawapingi nia yake, bali mbinu yake. Na wengi hawamlaumu yeye binafsi bali wasaidizi wake wanaomwandalia anayoyasoma na kuyasema mbele ya umma.

Lakini hilo haliwazuii kumwambia kwamba kama angetaka kutoa ujumbe mzito kuhusu mapanki hayo, angeyasemea huko alikokuwa – Ulaya – ambako anadai alikutana na mtengenezaji wa filamu hiyo. Dunia nzima ingemtambua Kikwete ni nani, na uzito wa hoja zake ungepokelewa na wale aliowalenga.

Kwamba hakufanya hivyo akiwa kule, ni ushahidi tosha kwamba lipo jambo ama hakuielewa au aliliogopa. Aliogopa kushushuliwa kwamba anaingilia uhuru wa mawazo ya wanahabari ambao amekuwa akijidai kuwatetea.

Aliogopa kuulizwa na kuhojwa juu ya vibali vya serikali iliyomruhusu mtengeneza filamu kufanya kazi yake baada ya kukagua rasimu ya maudhui ya kazi yake. Aliogopa kuambiwa ukweli kwamba samaki wake wamejaa katika masoko ya Ulaya wakati wananchi wanaambulia vichwa na mifupa, huku wengine wakiokota vilivyooza kwenye mitaro au madampo kwa sababu ya umaskini.

Aliogopa kuulizwa serikali yake inafanya nini kurekebisha hali hiyo. Nadhani hakuwa na majibu ya maswali hayo. Aliogopa ujasiri wa waandishi wa Ulaya ambao hawana nia ya kujipendekeza wala hawaogopi kubanwa na sheria yoyote ya Tanzania kama tulivyo sisi. Maana kama si unyonge wetu, hata pale pale Mwanza waandishi wetu walipaswa kumvaa na kumuuliza maswali mazuri na kuandika stori yenye uzito kuliko kutegemea hotuba yake tu.

Kwamba wamekuwapo waandishi wachache wasiomwonea aibu wala huruma Rais Kikwete katika hili ni ushahidi mwingine wa udhaifu wetu aliotaka kuutumia kusema asemayo akijua tutaandika vivyo hivyo.

Kwamba limekuwapo kundi la watu wake wa karibu linalothubutu kututisha na kutukemea sisi tusiocheza ngoma ya rais, ni ushahisi mwingine wa mambo mawili. Kwanza, wanategemea kutumia kalamu zetu na akili zetu kufanya kazi ya wasaidizi wake; labda kwa kutoamini kwamba wasaidizi wao wanaweza kuandika uchambuzi mbadala na kufunika kazi zetu.

Pili, ni dalili kwamba utawala wa Kikwete unaanza kuingiliwa na kirusi cha vitisho kwa watu wenye mawazo mbadala na waandishi wanaokosoa, kinyume cha ahadi na majigambo yake kufanikisha uhuru wa kujieleza na kuwasialiana.

Ni ishara pia kwamba baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete wanamuundia mabomu bila kujua, na wanataka kuyatetea bila hoja, bali kwa mabavu. Kwa bahati mbaya, inawezekana ameteua wasaidizi wanaomwogopa na wasio wabunifu, wasioweza kumwambia ukweli hata akikosea, na wasioweza kuomba radhi wakikosea.

Kwa ukosefu wao wa ubunifu wanatumia mbinu zile zile zilizotumiwa na watangulizi wao katika miaka zaidi ya 40 iliyopita. Na wanafanya hivyo wakiwa karibu mno na rais, huku wakiwa wa kwanza kila siku kumsikia akizungumzia ari mpya ambayo wenyewe hawana. Wanatumia nguvu ya kizamani huku yeye akisisitiza nguvu mpya.

Tukubali. Tukiri makosa tuweze kujenga taifa. Rais amekoseshwa. Naye amekosea. Alipaswa kuukema utandawazi si mpiga filamu wa mapanki. Alipaswa kuwapa wananchi matumaini ya kutumia raslimali zao kujiendeleza.

Maandamano, vitisho na ghiliba zinazotumiwa na wasaidizi wake vinamchafua rais mwenyewe. Na wapo wanaonza kusema sasa kwamba anawatumia wasaidizi wake kichini chini kunyamazisha sauti zinazomkosoa na kumpinga. Hili nalo, asipolipinga kimkakati na kuliweka sawa, litamchafua.

Bahati mbaya aliyonayo rais wetu wa sasa, hapati fursa ya kujua watu wake wanamsemaje. Hakuzoea kusemwa hadharani. Kwa miaka 10 mfululizo amekuwa akisifiwa. Amekaa mbali na msuguano na jamii ya Watanzania akiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Siasa zinazowahusu wananchi moja kwa moja zimekaa mbali naye; ndiyo maana ilimuwia rahisi kufanya kampeni ya urais bila kipingamizi kikubwa.

Lakini sasa akubali kwamba amerejea nyumbani. Akubali udhaifu wake na kuukosoa pale utakapobainika. Ajue, na wasaidizi wake wajue pia, kwamba yeye si mungu. Ni binadamu wa kawaida, anaweza kukosea. Watamsamehe, watamwelewa na kazi itaendelea kama kawaida.

Ajue, na akubali, kwamba wengi wanaomkosoa hawana ugomvi binafsi naye. Wanataka atambue kuwa yeye ni raia nambari wani. Lazima asugue na kung’arisha kauli zake kwa niaba ya Watanzania. Wanampenda rais wao na nchi yao. Lakini hawapendi, wala hawakubali makosa yake.

ansbertn@yahoo.com www.ngurumo.blogspot.com

Makala hii inapatikna pia katika www.freemedia.co.tz

Sunday, August 06, 2006

Kikwete wa Dodoma si yule yule wa Mwanza?

GHAFLA, Rais Jakaya Kikwete amewashtua Watanzania kwa kuzungumzia kwa ukali filamu ya Darwin’s Nightmare iliyoandaliwa na raia wa Ufaransa, Hubert Sauper. Ameikemea na kuishutumu kwa mambo mengi, lakini Watanzania aliokuwa anwaambia hawajawahi kuiona! Pili, amepotosha ukweli kwamba wakazi wa Mwanza hawali mapanki, na kwamba hakuna ukahaba. Ukionoa wanaCCM wa Mwanza walioandaliwa na viongozi wa chama na serikali kuandamana kumuunga mkono Rais na kumlaani Sauper, Watanzania wanaojua hali halisi na wasiogubikwa na ushabiki wa CCM wamemwambia Rais Kikwete ukweli kwamba amechemsha. Yafuatayo ndiyo niliyomwambia kupitia safu ya Maswali Magumu katika gazeti la Tanzania Daima, Jumapili, Agosti 06, 2006. ENDELEA.
RAFIKI yangu mmoja ameniambia kwamba katika kipindi cha miezi takriban minane ambayo Rais Jakaya Kikwete amekaa madarakani, amekutana na Kikwete wawili tofauti.
Wa kwanza ni Kikwete taifa, kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dodoma, Desemba mwaka jana (2005). Wa pili ni yule aliyehutubia Watanzania kupitia kwa wazee wa Mkoa wa Mwanza, mwanzoni mwa wiki hii.
Kikwete wa kwanza alikuwa mahiri wa kuzungumza. Aligusa maisha halisi na mtarajio ya wasikilizaji wake, hata wasio Watanzania. Alizungumza yale ambayo kwa huluka na mazoea, si kauli ya viongozi wetu wakuu tuliowazoea, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kikwete huyu wa kwanza ni mtu wa watu, kiongozi wa Watanzania wote, anayejua matatizo yaliyowasumbua kwa muda mrefu, na ambaye ameahidi kufanya kila anachoweza kuyaondoa, na kuwaletea maisha bora.
Ni Kikwete anayewapa Watanzania matumaini makubwa. Ni Kikwete aliyejua kuchanganya maneno matamu yaliyokolezwa na hoja kadhaa alizoazima kutoka kwa wapinzani, kuonyesha kwamba yu tayari kukosoa yaliyowashinda watangulizi wake.
Yule alikuwa Kikwete tishio la wanaosemekana kutumia vibaya madaraka yao, waliotafuta kujineemesha badala ya kuwaneemesha Watanzania. Wa kwanza alikuwa Kikwete msema kweli.
Kikwete wa pili, huyu wa Mwanza, hakuwa mkweli sana. Hakuwa msema kweli. Hotuba yake haikuwa na mvuto kwa wasikilizaji wote. Hakuwa Kikwete mwenye uso wa tabasamu. Alinuna. Alionya na kulaani.
Hotuba yake haikuwa na maneno matamu tuliyozoea. Haikuwa na ahadi. Huyu hakuwa Kikwete wa wananchi. Alikuwa Kikwete Rais wa nchi.
Ni Kikwete ambaye hakueleweka kwa baadhi ya wasikilizaji wake. Aliwachanganya. Kilichomfanya awachanganye wasikilizaji wake ni msisitizo usio wa kawaida, huku akikemea waandaaji wa filamu ya Darwin’s Nightmare, kwamba wakazi wa Mwanza hawali vichwa vya samaki, na kwamba jiji lao halina makahaba!
Akashindilia hoja yake kwa kusema wanaosema mapanki yanaliwa na kwamba kuna ukahaba Mwanza ni waongo na wazandiki!
Wanaojua ukweli wa hali halisi ya Mwanza, alikokuwa, wakashindwa kusema rais ameongopa; wakasema ameshauriwa vibaya, amepotoshwa. Ila hawakusema kwamba alipopotoshwa, hakupotoka! Hawakusema kwamba alipodanganywa, hakuwadanganya Watanzania.
Sana sana, walianza kujiuliza: Nani amemlazimisha rais kusema maneno haya? Kuna msukumo gani nyuma yake? Je, hili ni tatizo kubwa la kitaifa ambalo ilikuwa alizungumzie?
Je, ndiyo sababu iliyomfanya apumzikie Mwanza, siku chache baada ya kutoka kwenye matibabu Ulaya? Si angesubiri kwanza akatembelea mitaa kadhaa, akatembelea masoko na kuona hali halisi kabla hajahutubia taifa?
Sasa kama rais anasemeshwa uongo, watu hawa wanaojua ukweli watamwona vipi baadaye, hata akisema jambo lililo kweli? Na kama ameshasema yeye, nani atarudi baadaye kurekebisha kauli ya rais, kwamba alikuwa ameteleza kwa kuwa ulimi hauna mfupa?
Wengine walifika mahali pa kusema: “Kumbe hata Kikwete anaweza kuongopa?” Nikawauliza: “Kwani nyie mnamwonaje? Yeye si binadamu kama nyie?”
Lakini hoja kuu hapa ni kwamba kusema uongo ni kosa. Na adhabu yake inafahamika. Nani atamwadhibu Kikwete? Kwa kuwa aliyesema uongo ni rais, hakuna mtu wa kumwadhibu, lakini yeye ana uwezo wa kuwaadhibu waliomsababishia kusema uongo. Basi afanye hivyo, na ajifunze kutokusoma kila kitu wanachomwandikia.
Ajue pia namna ya kuchuja ukweli katika mapendekezo anayoletewa na wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo mawaziri. Maana tayari zipo dalili kwamba baadhi yao wamejiingiza katika kashfa, ambazo wanamsukumia yeye azibariki bila kujua, kulinda masilahi yao binafsi.
Hawa wote wanaomdanganya ni wateule wake. Kama anawaamini kwa asilimia 100, huku wakimdanganya, anatarajia Watanzania wamwamini yeye kwa asilimia 100? Sana sana watasema ama aliwateua bila kujua, kwa hiyo anadanganywa kwa bahati mbaya; au tukubali kwamba lao ndilo lake, anajua kinachoendelea lakini anafanya hivi kulinda masilahi fulani.
Kwa mfano, hili la Mwanza limeleta hisia kwamba Rais Kikwete amebanwa na ‘wahisani wake’ akanushe tuhuma zilizo katika mkanda huo, ili kusafisha sura na jina la Tanzania. Akakosea mbinu.
Wakati anasisitiza kuwaita wazandiki waliotengeneza filamu hiyo, wapo Watanzania waliokuwa sokoni kununua mapanki hayo. Wengine walikuwa maeneo ya Igoma wanaokota yaliyotupwa kwenye dampo.
Wengine walikuwa wameshika pua kuzuia harufu mbaya ya mapanki wakati gari likipita katika mitaa ya jiji kwenda kumwaga mapanki hayo. Wengine walikuwa kiwandani wanalangua lori la mapanki hayo ili baadaye wayakaushe na kuwauzia wanunuzi wa Mwanza na kwingineko.
Mkoani Kagera, raia walikuwa wanakimbizana na polisi kujibu walikopata samaki waliokutwa nao; maana wenye haki ya kuvua samaki si wananchi bali wenye vibali maalumu au wenye viwanda!
Wakati huo huo, mabinti wadogo waliohitimu darasa la saba, na dada zao wakubwa – wengine ni wasomi kwenye vyuo – walikuwa wanahitimisha muda wao wa kulala, kujiandaa na kibarua kigumu usiku katika mitaa ya katikati ya jiji.
Baadhi ya wanaume waliomsikia ndio wateja wa kina dada hao. Nadhani nao walimkejeli usiku huo kwa kufanya maasi yasiyosemeka.
Hawa wote walishindwa kusema, lakini waliona kiongozi mkuu wa nchi amepotoka, hasemi ukweli.
Naamini kwamba baada ya wananchi wa Mwanza kumkosoa rais kupitia vyombo vya habari, amediriki kutuma wasaidizi wadogo kuona ukweli wa maisha ya Watanzania.
Sasa wanasubiri awachukulie hatua waliomkosesha. Wanasubiri kuona kama atakuwa muungwana na kusahihisha kauli yake, huku akiweka mikakati ya kuondoa kero hizo.
Akifanya hivyo, anaweza kupunguza makali ya hisia za Watanzania wanaomweka katika kundi la watu wanaoweza kupinda ukweli. Atasaidia pia kuifanya jamii ijue kwamba bado Kikwete ni mmoja.
Na huyo mmoja hatapatikana hadi wa kwanza atakapomuua wa pili. Vinginevyo, tukubaliane kwamba Watanzania wataamua wamwamini na kumfuata Kikwete mmojawapo; wa Dodoma au wa Mwanza.

ansbertn@yahoo.com +255744607553

Mkala hii inapatikana pia katika www.freemedia.co.tz
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'