Sunday, August 06, 2006

Kikwete wa Dodoma si yule yule wa Mwanza?

GHAFLA, Rais Jakaya Kikwete amewashtua Watanzania kwa kuzungumzia kwa ukali filamu ya Darwin’s Nightmare iliyoandaliwa na raia wa Ufaransa, Hubert Sauper. Ameikemea na kuishutumu kwa mambo mengi, lakini Watanzania aliokuwa anwaambia hawajawahi kuiona! Pili, amepotosha ukweli kwamba wakazi wa Mwanza hawali mapanki, na kwamba hakuna ukahaba. Ukionoa wanaCCM wa Mwanza walioandaliwa na viongozi wa chama na serikali kuandamana kumuunga mkono Rais na kumlaani Sauper, Watanzania wanaojua hali halisi na wasiogubikwa na ushabiki wa CCM wamemwambia Rais Kikwete ukweli kwamba amechemsha. Yafuatayo ndiyo niliyomwambia kupitia safu ya Maswali Magumu katika gazeti la Tanzania Daima, Jumapili, Agosti 06, 2006. ENDELEA.
RAFIKI yangu mmoja ameniambia kwamba katika kipindi cha miezi takriban minane ambayo Rais Jakaya Kikwete amekaa madarakani, amekutana na Kikwete wawili tofauti.
Wa kwanza ni Kikwete taifa, kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dodoma, Desemba mwaka jana (2005). Wa pili ni yule aliyehutubia Watanzania kupitia kwa wazee wa Mkoa wa Mwanza, mwanzoni mwa wiki hii.
Kikwete wa kwanza alikuwa mahiri wa kuzungumza. Aligusa maisha halisi na mtarajio ya wasikilizaji wake, hata wasio Watanzania. Alizungumza yale ambayo kwa huluka na mazoea, si kauli ya viongozi wetu wakuu tuliowazoea, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kikwete huyu wa kwanza ni mtu wa watu, kiongozi wa Watanzania wote, anayejua matatizo yaliyowasumbua kwa muda mrefu, na ambaye ameahidi kufanya kila anachoweza kuyaondoa, na kuwaletea maisha bora.
Ni Kikwete anayewapa Watanzania matumaini makubwa. Ni Kikwete aliyejua kuchanganya maneno matamu yaliyokolezwa na hoja kadhaa alizoazima kutoka kwa wapinzani, kuonyesha kwamba yu tayari kukosoa yaliyowashinda watangulizi wake.
Yule alikuwa Kikwete tishio la wanaosemekana kutumia vibaya madaraka yao, waliotafuta kujineemesha badala ya kuwaneemesha Watanzania. Wa kwanza alikuwa Kikwete msema kweli.
Kikwete wa pili, huyu wa Mwanza, hakuwa mkweli sana. Hakuwa msema kweli. Hotuba yake haikuwa na mvuto kwa wasikilizaji wote. Hakuwa Kikwete mwenye uso wa tabasamu. Alinuna. Alionya na kulaani.
Hotuba yake haikuwa na maneno matamu tuliyozoea. Haikuwa na ahadi. Huyu hakuwa Kikwete wa wananchi. Alikuwa Kikwete Rais wa nchi.
Ni Kikwete ambaye hakueleweka kwa baadhi ya wasikilizaji wake. Aliwachanganya. Kilichomfanya awachanganye wasikilizaji wake ni msisitizo usio wa kawaida, huku akikemea waandaaji wa filamu ya Darwin’s Nightmare, kwamba wakazi wa Mwanza hawali vichwa vya samaki, na kwamba jiji lao halina makahaba!
Akashindilia hoja yake kwa kusema wanaosema mapanki yanaliwa na kwamba kuna ukahaba Mwanza ni waongo na wazandiki!
Wanaojua ukweli wa hali halisi ya Mwanza, alikokuwa, wakashindwa kusema rais ameongopa; wakasema ameshauriwa vibaya, amepotoshwa. Ila hawakusema kwamba alipopotoshwa, hakupotoka! Hawakusema kwamba alipodanganywa, hakuwadanganya Watanzania.
Sana sana, walianza kujiuliza: Nani amemlazimisha rais kusema maneno haya? Kuna msukumo gani nyuma yake? Je, hili ni tatizo kubwa la kitaifa ambalo ilikuwa alizungumzie?
Je, ndiyo sababu iliyomfanya apumzikie Mwanza, siku chache baada ya kutoka kwenye matibabu Ulaya? Si angesubiri kwanza akatembelea mitaa kadhaa, akatembelea masoko na kuona hali halisi kabla hajahutubia taifa?
Sasa kama rais anasemeshwa uongo, watu hawa wanaojua ukweli watamwona vipi baadaye, hata akisema jambo lililo kweli? Na kama ameshasema yeye, nani atarudi baadaye kurekebisha kauli ya rais, kwamba alikuwa ameteleza kwa kuwa ulimi hauna mfupa?
Wengine walifika mahali pa kusema: “Kumbe hata Kikwete anaweza kuongopa?” Nikawauliza: “Kwani nyie mnamwonaje? Yeye si binadamu kama nyie?”
Lakini hoja kuu hapa ni kwamba kusema uongo ni kosa. Na adhabu yake inafahamika. Nani atamwadhibu Kikwete? Kwa kuwa aliyesema uongo ni rais, hakuna mtu wa kumwadhibu, lakini yeye ana uwezo wa kuwaadhibu waliomsababishia kusema uongo. Basi afanye hivyo, na ajifunze kutokusoma kila kitu wanachomwandikia.
Ajue pia namna ya kuchuja ukweli katika mapendekezo anayoletewa na wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo mawaziri. Maana tayari zipo dalili kwamba baadhi yao wamejiingiza katika kashfa, ambazo wanamsukumia yeye azibariki bila kujua, kulinda masilahi yao binafsi.
Hawa wote wanaomdanganya ni wateule wake. Kama anawaamini kwa asilimia 100, huku wakimdanganya, anatarajia Watanzania wamwamini yeye kwa asilimia 100? Sana sana watasema ama aliwateua bila kujua, kwa hiyo anadanganywa kwa bahati mbaya; au tukubali kwamba lao ndilo lake, anajua kinachoendelea lakini anafanya hivi kulinda masilahi fulani.
Kwa mfano, hili la Mwanza limeleta hisia kwamba Rais Kikwete amebanwa na ‘wahisani wake’ akanushe tuhuma zilizo katika mkanda huo, ili kusafisha sura na jina la Tanzania. Akakosea mbinu.
Wakati anasisitiza kuwaita wazandiki waliotengeneza filamu hiyo, wapo Watanzania waliokuwa sokoni kununua mapanki hayo. Wengine walikuwa maeneo ya Igoma wanaokota yaliyotupwa kwenye dampo.
Wengine walikuwa wameshika pua kuzuia harufu mbaya ya mapanki wakati gari likipita katika mitaa ya jiji kwenda kumwaga mapanki hayo. Wengine walikuwa kiwandani wanalangua lori la mapanki hayo ili baadaye wayakaushe na kuwauzia wanunuzi wa Mwanza na kwingineko.
Mkoani Kagera, raia walikuwa wanakimbizana na polisi kujibu walikopata samaki waliokutwa nao; maana wenye haki ya kuvua samaki si wananchi bali wenye vibali maalumu au wenye viwanda!
Wakati huo huo, mabinti wadogo waliohitimu darasa la saba, na dada zao wakubwa – wengine ni wasomi kwenye vyuo – walikuwa wanahitimisha muda wao wa kulala, kujiandaa na kibarua kigumu usiku katika mitaa ya katikati ya jiji.
Baadhi ya wanaume waliomsikia ndio wateja wa kina dada hao. Nadhani nao walimkejeli usiku huo kwa kufanya maasi yasiyosemeka.
Hawa wote walishindwa kusema, lakini waliona kiongozi mkuu wa nchi amepotoka, hasemi ukweli.
Naamini kwamba baada ya wananchi wa Mwanza kumkosoa rais kupitia vyombo vya habari, amediriki kutuma wasaidizi wadogo kuona ukweli wa maisha ya Watanzania.
Sasa wanasubiri awachukulie hatua waliomkosesha. Wanasubiri kuona kama atakuwa muungwana na kusahihisha kauli yake, huku akiweka mikakati ya kuondoa kero hizo.
Akifanya hivyo, anaweza kupunguza makali ya hisia za Watanzania wanaomweka katika kundi la watu wanaoweza kupinda ukweli. Atasaidia pia kuifanya jamii ijue kwamba bado Kikwete ni mmoja.
Na huyo mmoja hatapatikana hadi wa kwanza atakapomuua wa pili. Vinginevyo, tukubaliane kwamba Watanzania wataamua wamwamini na kumfuata Kikwete mmojawapo; wa Dodoma au wa Mwanza.

ansbertn@yahoo.com +255744607553

Mkala hii inapatikana pia katika www.freemedia.co.tz

1 comment:

Jeff Msangi said...

Ama kweli maswali haya magumu.Kama ni hesabu ningesema ni zile za waendesha roketi.Umenifanya niwaze na kuwazua,nirudi kwenye maswali ambayo swahiba wangu Makene hupenda kuuliza,hivi nani anasema ukweli kuhusu Afrika/Tanzania?

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'