Saturday, August 12, 2006

Tunampenda rais wetu, hatukubali makosa yake

Na Ansbert Ngurumo, Toronto

JUMAPILI hii nipo mbali na nyumbani kwa shughuli nyingine ya msingi kitaifa, lakini nimedhani kwamba ipo haja ya kukamilisha hoja yangu niliyoianza wiki iliyopita, na ambayo sasa imegeuka mjadala wa kitaifa.

Nilipoandika kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwezi uliopita, nilijadili suala la mapanki na ukahaba kidogo. Kwa makusudi kabisa, niliacha suala la silaha.

Wengi waliosoma uchambuzi wangu walitoa maoni yao kwa ujumbe mfupi wa simu na kwa barua pepe. Zaidi ya watu 30 waliungana nami kwamba Rais Kikwete alipotoshwa. Tena wengine walikuwa wakali hata kusema nilikuwa mwoga, nikashindwa kusema Rais alidanganya taifa!

Wengine walitumia lugha ya utani kwamba katika Chama Cha Mapinduzi, mwenyekiti hakosei; hata akisema jambo ambalo wanajua si kweli, watapiga makofi kumshangilia, na hata ikibidi wataandamana kushangilia.

Yawezekana walikuwa wakijadili yaliyojitokeza jijini Mwanza, baada ya viongozi waandamizi wa CCM kuwakusanya wanachama waandamane kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete. Kilichowashtua wananch wengi baada ya hapo ni kubaini kwamba wakati Rais Kikwete anahutubia Watanzania kuhusu ‘ubaya’ wa filamu ya Hubert Sauper juu ya mapanki, wananchi wengi waliomsikia walikuwa hawajaiona.

Ndiyo maana makundi kadhaa ya wananchi yamekuwa yakihaha kuitafuta filamu hiyo, waione. Sasa unajiuliza: Hawa walioandamana kuunga mkono hotuba ya Rais wetu walikuwa wanaunga mkono jambo gani? Sitashangaa kwamba hata aliyewahamasisha na aliyepokea maandamano yao walikuwa hawajaona filamu hiyo!

Wapo wengine walionitumia ujumbe mfupi wa vitisho na matusi, kwamba nawapotosha wasomaji, huku mmojawapo akihoji: “Unamkosoa rais wewe? Huogopi kufa?”

Nilijaribu kuwajibu baadhi yao, na baada ya kubadilishana hoja, wengine walionekana kuelewa, na kukiri kuwa ushabiki wao kwa Kikwete ndilo tatizo. Hawataki kuona akichafua rekodi yake ya kisiasa. Nikamuuliza mmoja wao: “Sasa mbona nyie mashabiki wake ndio mnamchafua? Tambua kwamba huwezi kumsafisha rais kwa kutetea udhaifu wake, bali kwa kutetea maudhui na mikakati inayoteteka.”

Nimekuwa nawaza, najihoji. Hii ndiyo Tanzania tunayotaka kujenga? Tunajenga taifa la watu wanaokubali chochote ambacho wakubwa wanasema na kupitisha, hata bila kudadisi? Na bado tunajidai kwamba tuna ‘taifa hai?’

Huu ndiyo ukereketwa? Je, wasingeandamana ingempunguzia nini Rais Kikwete? Au bado tunaendelea kuamini kwamba fikra za mwenyekiti, hata kama ni potofu lazima zisifiwe na zidumishwe?

Kwa hakika, kwa sababu watu wengi walikuwa hawajaiona filamu hiyo, wakiwamo wabunge wetu, Rais Kikwete amejikuta akiipigia debe filamu aliyodhamiria kuipiga vita. Na kwa kuwa aliozungumza nao walikuwa hawajaiona, ujumbe aliotuma siku hiyo siyo utakaozingatiwa baadaye kila mmoja akishaiona filamu hiyo.

Lakini hoja nyingine ambayo imejadiliwa kidogo mno ni mbinu aliyotumia rais kuzungumzia suala hilo. Jukwaa alilotumia – wananchi wa Mwanza – halikuwa sahihi. Lingekuwa jukwaa sahihi kama angekuwa anafanya uamuzi mgumu na mkubwa wa kuzuia minofu ya samaki wetu kupelekwa Ulaya. Wananchi wangeona wamepatiwa ukombozi. Kilichowafanya Watanzania wengi sasa ‘walumbane na rais’ baada ya kusikia hotuba yake, ni hicho. Hawapingi nia yake, bali mbinu yake. Na wengi hawamlaumu yeye binafsi bali wasaidizi wake wanaomwandalia anayoyasoma na kuyasema mbele ya umma.

Lakini hilo haliwazuii kumwambia kwamba kama angetaka kutoa ujumbe mzito kuhusu mapanki hayo, angeyasemea huko alikokuwa – Ulaya – ambako anadai alikutana na mtengenezaji wa filamu hiyo. Dunia nzima ingemtambua Kikwete ni nani, na uzito wa hoja zake ungepokelewa na wale aliowalenga.

Kwamba hakufanya hivyo akiwa kule, ni ushahidi tosha kwamba lipo jambo ama hakuielewa au aliliogopa. Aliogopa kushushuliwa kwamba anaingilia uhuru wa mawazo ya wanahabari ambao amekuwa akijidai kuwatetea.

Aliogopa kuulizwa na kuhojwa juu ya vibali vya serikali iliyomruhusu mtengeneza filamu kufanya kazi yake baada ya kukagua rasimu ya maudhui ya kazi yake. Aliogopa kuambiwa ukweli kwamba samaki wake wamejaa katika masoko ya Ulaya wakati wananchi wanaambulia vichwa na mifupa, huku wengine wakiokota vilivyooza kwenye mitaro au madampo kwa sababu ya umaskini.

Aliogopa kuulizwa serikali yake inafanya nini kurekebisha hali hiyo. Nadhani hakuwa na majibu ya maswali hayo. Aliogopa ujasiri wa waandishi wa Ulaya ambao hawana nia ya kujipendekeza wala hawaogopi kubanwa na sheria yoyote ya Tanzania kama tulivyo sisi. Maana kama si unyonge wetu, hata pale pale Mwanza waandishi wetu walipaswa kumvaa na kumuuliza maswali mazuri na kuandika stori yenye uzito kuliko kutegemea hotuba yake tu.

Kwamba wamekuwapo waandishi wachache wasiomwonea aibu wala huruma Rais Kikwete katika hili ni ushahidi mwingine wa udhaifu wetu aliotaka kuutumia kusema asemayo akijua tutaandika vivyo hivyo.

Kwamba limekuwapo kundi la watu wake wa karibu linalothubutu kututisha na kutukemea sisi tusiocheza ngoma ya rais, ni ushahisi mwingine wa mambo mawili. Kwanza, wanategemea kutumia kalamu zetu na akili zetu kufanya kazi ya wasaidizi wake; labda kwa kutoamini kwamba wasaidizi wao wanaweza kuandika uchambuzi mbadala na kufunika kazi zetu.

Pili, ni dalili kwamba utawala wa Kikwete unaanza kuingiliwa na kirusi cha vitisho kwa watu wenye mawazo mbadala na waandishi wanaokosoa, kinyume cha ahadi na majigambo yake kufanikisha uhuru wa kujieleza na kuwasialiana.

Ni ishara pia kwamba baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete wanamuundia mabomu bila kujua, na wanataka kuyatetea bila hoja, bali kwa mabavu. Kwa bahati mbaya, inawezekana ameteua wasaidizi wanaomwogopa na wasio wabunifu, wasioweza kumwambia ukweli hata akikosea, na wasioweza kuomba radhi wakikosea.

Kwa ukosefu wao wa ubunifu wanatumia mbinu zile zile zilizotumiwa na watangulizi wao katika miaka zaidi ya 40 iliyopita. Na wanafanya hivyo wakiwa karibu mno na rais, huku wakiwa wa kwanza kila siku kumsikia akizungumzia ari mpya ambayo wenyewe hawana. Wanatumia nguvu ya kizamani huku yeye akisisitiza nguvu mpya.

Tukubali. Tukiri makosa tuweze kujenga taifa. Rais amekoseshwa. Naye amekosea. Alipaswa kuukema utandawazi si mpiga filamu wa mapanki. Alipaswa kuwapa wananchi matumaini ya kutumia raslimali zao kujiendeleza.

Maandamano, vitisho na ghiliba zinazotumiwa na wasaidizi wake vinamchafua rais mwenyewe. Na wapo wanaonza kusema sasa kwamba anawatumia wasaidizi wake kichini chini kunyamazisha sauti zinazomkosoa na kumpinga. Hili nalo, asipolipinga kimkakati na kuliweka sawa, litamchafua.

Bahati mbaya aliyonayo rais wetu wa sasa, hapati fursa ya kujua watu wake wanamsemaje. Hakuzoea kusemwa hadharani. Kwa miaka 10 mfululizo amekuwa akisifiwa. Amekaa mbali na msuguano na jamii ya Watanzania akiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Siasa zinazowahusu wananchi moja kwa moja zimekaa mbali naye; ndiyo maana ilimuwia rahisi kufanya kampeni ya urais bila kipingamizi kikubwa.

Lakini sasa akubali kwamba amerejea nyumbani. Akubali udhaifu wake na kuukosoa pale utakapobainika. Ajue, na wasaidizi wake wajue pia, kwamba yeye si mungu. Ni binadamu wa kawaida, anaweza kukosea. Watamsamehe, watamwelewa na kazi itaendelea kama kawaida.

Ajue, na akubali, kwamba wengi wanaomkosoa hawana ugomvi binafsi naye. Wanataka atambue kuwa yeye ni raia nambari wani. Lazima asugue na kung’arisha kauli zake kwa niaba ya Watanzania. Wanampenda rais wao na nchi yao. Lakini hawapendi, wala hawakubali makosa yake.

ansbertn@yahoo.com www.ngurumo.blogspot.com

Makala hii inapatikna pia katika www.freemedia.co.tz

5 comments:

Anonymous said...

Ngurumo naomba namba yako ya simu landline hapo Toronto, ili tukipata nafasi tuwasiliane.

Anonymous said...

Kwanza kabisa nakupongeza kwa mchango wako katika kulielimisha taifa letu juu ya masuala mbalimbali ya jamii. Hongera sana.

Ninakubaliana nawe kuwa filamu hii inajaribu kuifahamisha dunia kwamba utandawazi (Globalization) na swala zima la mfumo mpya wa dunia ndiyo chanzo hasa cha udhalilishaji wa kisasa wa bara letu la Afrika.

Kwa maoni yangu,kimsingi filamu inaonyesha jinsi serikali yetu, inavyotegemea sana biashara ya kuuza rasilimali zetu nje na kutowajali wananchi wake jambo linalopelekea baa la njaa, umaskini, ukahaba, ukimwi, uhalifu na matumizi ya madawa ya kulevya.

Mtengenezaji wa filamu hii anasema ingawa katika filamu hii anazungumzia samaki, lakini angeweza kutengeneza filamu nyingine kama hii kuhusu Sierra Leone, ingawa samaki huko ingekuwa almasi. Angeweza kutengeneza filamu kama hiyo kuhusu Amerika Kusini, ingawa huko samaki ingekuwa ndizi. Na angeweza kutengeneza filamu kama hiyo kuhusu Libya, Nigeria au Angola ingawa huko samaki wangekuwa mafuta.

Na anasema inashangaza jinsi ambavyo mahali popote panapogunduliwa rasilimali kubwa, taratibu wenyeji wanaanza kufa kinyonge, vijana wao wanaishia kuwa ombaomba, na mabinti zao wanakuwa makahaba.

Na serikali haina mikakati yoyote kuboresha hali zao.

Cha kushangaza ni kuwa hata yule kijana aliyeonekana mara kadhaa katika hiyo filamu, mchoraji Jonathan, anaonekana kuelewa vyema chanzo cha matatizo ya wananchi kuliko hata hoa wabunge huko Dodoma, hii inasikitisha sana.

Bwana JK anatakiwa atoe mikakati ya jinsi serikali yake inavyopanga kukabiliana na kurekebisha hali mbaya za wananchi wetu. Sisi hatuko tayari kudanganywa na hilo bunge eti tutumie ukereketwa wetu (our patriotism) kuunga mkono azimio hilo la Bunge kulaani filamu hiyo.

Wananchi hatuko tayari kufanya huo ukasuku na kushangilia kila hotuba zinazotolea na raisi hata kama hoja zake hazina nguvu.
Kwanza yeye kama raisi anatakiwa kutolikubali azimio hilo kwani linatoa picha yenye mtazamo finyu sana wa Wabunge hao.

Leo journalists wa Kitanzania(www.mwanakijiji.podomatic.com) wameweka online interview waliyofanya leo na bwana Sauper na inaonekana bwana Kikwete ameudanganya umma wote. Katika interview hiyo bwana Sauper anakanusha madai kuwa bwana Kikwete aliwahi kumwuliza maswali juu ya filamu hiyo walipokutana kwenye dinner party huko Paris. Bwana Sauper anasema yeye alijitambulisha kwa raisi Kikwete na kumwuliza kama ameishaiona filamu yake na Kikwete alisema kuwa alikuwa hajaiona. Na wakaachana. Cha ajabu, katika hotuba yake ya Mwanza raisi Kikwete alidai kuwa alipokutana na Sauper alimwomba ampe ushahidi juu ya masuala aliyoonyesha katika filamu na eti bwana Sauper alitoroka bila ya kujibu. Sasa jamani kama raisi amefikia hatua ya kuudanganya umma hadharani bila kuwa na aibu yoyote ile, tutafika kweli?

Anonymous said...

Ngurumo, sasa nafurahi kuwa UNDISHI wa habari unarudi kwa baadhi ya magazeti, unajua niliacha kununua na kusoma magazeti maana yote yalikuwa yana chochea MISIFA, Hili lililotokea nilijua kuwa litafika tu ,maana sikutegemea magazeti yote yawe yanalipwa na IKULU kusema mambo chanya ya serilaki, na dalili za media kutupa ukweli sasa zinaanza.
Nikirudi katika hoja msingi, mimi kama ningemtayarishia rais hotuba hiyoo ingekuwa hivi na isingekuwa kuwahutubia wazee wa mwanza bali wafanya biashara wa samaki na wenye viwanda:

Ndugu zangu Wafanyabiashara wa Samaki na Wenye viwanda vya samaki hapa Mwanza, tangu nitwae madaraka nimekwa siku zote silali kushughulikia swala zima la kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.Nimeanza na swala la majambazi na rushwa na sasa nimekuja hapa Mwanza pamoja na mambo mengine lakini kufanyia kazi mikataba mbalimbali hasa katika sekta ya Madini na Soko la Samaki. Ni majuzi nilikuwa kule Ufaransa na Ujerumani katika mchakato wangu niliojipangia wa kujitambulisha kwa viongozi wenzangu baada ya kutwaa madaraka ya kuiongoza nchi hii. Jambo ambalo limenifikirisha na kunihuzunisha ni hili ambalo limenigafanya kuongea nanyi leo, bahati mbaya wawakilishi kutoka machimbo ya Geita na huko Musoma na Shinyanga hawakupelekewa habari mapema, haaidhuru, nyinyi ni wajumbe wao kama wawekezaji na wafanyabiashara. Nikiwa Ufaranza na pia Ujerumani, marais wenzangu wainiuliza juu ya hali ya uchumi wa kanda hii ya Ziwa hususani biashara ya samaki.Kilichowafanya waniulize ni kutokana na Film iliyotengenezwaa mzungu mwenzao anaitwa ehhh, Hurbert. Katika picha hii mambo makuu manne yanajitokeza
Mosi, bishara hii inavyowanufaisha zaidi watu wa Umoja wa Ulaya na kuwaacha Wakazi wa Mwanza hohe hae wakila mapanki, minofu ikipelekwa kwao.
Mbili, umaskini ulioko kanda ya Ziwa pamoja na kuwa maarufu kwa samaki na madini, bado watu hali zao zinatisha na kusababisha makahaba na watoto wa mitaani.
Tatu, swala la ndege kutoka Russia zinazobeba minofu hiyo na kuja na silaha kuleta Afrika, hasa nchi za Maziwa Makuu.
Nne swala la UKIMWI hasa katika vijiji vya wavuvi.
Nilijadilina na wenzangu hao na nikawaambia kuwa bado film hiyo sijaiona,ingawaa kumbe Ulaya imeshaonyeshwa.
Baadaye niliteta na mabalozi wangu wa nchi hizo wakanieleza kweli picha hiyo imeonyeshwa ingawa hawakutoa taarifa kwangu kama Waziri wa wakati ule wa Mambo ya Nchi za nje,nikaona basi nitarishughulikia kiofisi maana nami nahusika kwa namna moja hasa ukizingatia nilikuwa waziri mwenye dhamana ya nchi za nje.
Sasa nilichowaitieni hapa ni kile ambacho mzungu mwenzenu amekifanya, kuonyesha ni kwa jinsi gani nyinyi mnatumia UTANDWAZI kuendelea kutunyonya.Hubert ametoa picha halisi ya jinsi nchi za Ulaya Magharibi zinavyoendeleza unyonyaji kwa wananchi wa nchi zinazoendelea, na hata "Title" ya film hiyo Dwarin's Nightmare"
inatoa taswira ya makuhadi wa soko huria ambao nyinyi ni maajenti wake.Inatoa hali halisi ya mnyonge hana nguvu mpaka mwenye nguvu apende"na kule Pwani kuna methali mgeni aje mwenyeji apone lakini picha hii inatoa kinyume chake, mgeni aje mwenyeji apate shida ama afe. Rais wa Ufaransa alinileza wazi kuwa picha hii imewapa mwanga kutetea zaidi FAIR TRADE katika kikao chao cha Shirika la Biashara la Kimataifa yaani WTO, pia wameona ni wakati muafaka kwa EU kutathimini uhusianao wa kibiasahara kati ya nchi zilizoendelea na hizi zetu kwa kusisitiza haki. Waliniuliza bei ya minofu hapa TZ nilishindwa kueleza maana sijui na mbaya waziri muhusika hakuwepo, eti ni kiasi gani kwa hapa Mwanza(kicheko cha mbali).Haya kule kilo moja ni karibu na Euro 20 ambazo ni sawa karibu TShs.20,000. Niliporudi niliitafuta film hiyo na kujionea hali halisi nikaamua kuja likizo ya kikazi hapa Mwanza. Tangu nifike majuzi,nilitembelea maeneo tajwaa katika film hiyo na kujionea hali halisi, nilikaa na viongozi wa hapa na kujadili kwa kirefu na nikamjulisha Waziri Mkuu a Mwaziri wote na Wabunge na Chama tawala juu ya haya niliyoamua ambayo sikutaka kusubiri kufanya vikaoa nao. Nadhani manakumbuka kuwa nilisema kuna maamuzi makubwa nitayafanya, yataumiza lakini ni kwamanufafa ya Taifa hili amabalo nimeapa kulitumikia.Sasa ninachotaka kusema,kuanzia leo,mikataba yenu ya kuendesha uvuvi na biashara ya samaki inasimamishwa mpaka tuhuma hizi zitakapopata ufumbuzi.Nimeunda Tume amabayo itashirikisha wataalamu mbalimbali wa maswala ya biashara na uchumi kuketi na kuangalia swala hili, pia kufuatilia mauhudhui yaliyomo katika picha hii. Nimemwagiza RPC na vijana wake kuhahikisha kwamba shughuli hizi za uvuvi na usafirishaji wa minofu haziendelei mpaka hapo ufumbuzi utakapo patikana,wavuvi wadogo wadogo wameruhusiwa kuvua kwa ajili ya huduma za soko la ndani , tume pia itaratibu kutembelea vijiji vyote vya uvuvi, viwanda vya samaki na machimbo ya madini.
Kwa wakati huu ningewaomba mbaki nchini ili kutoa ushirikiano kwa tume hiyo, sitaki kutumia lugha kali kwamba hamruhusiwi kutoka nje ya nchi lakini ikibidi nitafanya hivyo.Hatuwezi kuendelea hivi jamani, uwekezaji lazima unufaishe jamii husika na siyo kufanya kile ambacho Ukoloni ulifanya wakati wa kutafuta malighafi kulisha viwanda vya Ulaya.Biashara tunaipenda lakini si ile ya kunufaisha upande mmoja, nitashindwa kuwajibu wapiga kura wangu tukiendelea hivi.Kwa kumalizia nataka mbaki hapa kuona hii picha alafu mtaongea na waandishi wa habari.Mungu Ibariki Tanzania.

Anonymous said...

Kuna tatizo la kutokuelewa hapa, pamoja na ushabiki wa kishenzi kwa kisingizio cha Uzalendo. Uzalendo wa kumfichia mtu maradhi yake au wa kuficha mioto yenu wakati moshi unafuka nje na watu wanauona ni UZALENDO WA KISHENZI MNO.
- Hivi unajua kati ya walioandamana wapo wengi ambao hata hotuba ya rais mwenyewe tu walikuwa hawajaisikia?

- Nadhani unajua kuwa wengi wa waliokuwa wameisikia hotuba hiyo pia hawakuwa wameiona filamu yenyewe.

- Hivi ni kwanini Rais kama aliiona akiwa Ufaransa hakuita Press Conference na waandishi wa kule wa kimataifa na akakanusha kulekule maana sifa mbaya imetapakaa kimataifa?

- Hivi kilichomfanya asizungumzie suala hilo nyakati zoooote hizo ni nini wakati mwandishi mmoja aliwahi kuandika kuihusu filamu hiyo na akamwomba rais aagize balozi zetu zishinikize mataifa husika kuitengeneza kuomba radhi? sio kwasababu alijua wazi ni tatizo la kweli? au rais huwa hasomi magazeti siku hizi kwakuwa yameshamfikisha alipotaka?

- Hivi....hivi....hivi... ah!!! Kuna maswali mengi sana ya kujiuliza kwahakika na ambayo yote yanaleta mashaka juu ya kauli za mheshimiwa JK kuhusu filamu ile.

TUACHE UZALENDO WA KISHENZI, UZALENDO WA SUNGURA, KUFICHA KICHWA KATIKA SHIMO AKIAMINI KAJIFICHA MWILI MZIMA.

Anonymous said...

Mheshimiwa Raisi JK tunakuomba ufanye Re-view ya hotuba yako juu ya Filamu ya Darwin's Nightmare. Watanzania wengi hatujaridhika kwa sababu zifuatazo:

1. Hukutoa mwaja kwa watanzania kuweza kuona filamu hiyo matokeo yake tunakuona kama mpotoshaji wa ukweli au mlaghai kwa kutumia ujinga wetu wa kutoijua filamu ya Darwin's Nightmare kwa maslahi binafsi ama kwa makusudi au kwa kudanganywa na wachache tu unaowaamini wewe bila kucambua ukweli wa mambo na hali halisi ilivyo kwa raia wako wanaoumizwa na uwekezaji wa kihuni tulionao kila kona nchini kwetu.

2. Ulipaswa na bado unapaswa kuwabwatukia watengeneza filamu ukiwa huko nje ya nchi ili kuisafisha Tanzania kama kweli imechafuliwa?? Kwani Mwanza ni wantazania ambao pamoja na kuandamana kwao wanaita "Demo" uliwaacha katika giza tororo mpaka leo kuhusu hotuba yako ya Mapanki.

Mungu akusidie kutafakari upya Raisi wetu Mpendwa.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'