Thursday, September 28, 2006

Bora mwanafalsafa asiyeridhika au nguruwe aliyeridhika?

Na Ansbert Ngurumo, Hull University, UK

“UNAWEZA kujua kwa hakika kwamba mtu fulani anakupenda? Utakuwa na uhakika gani? Unaweza kujua watu wengine wanawaza nini au wanahisi nini wasipokwambia?

Au hata wakikwambia utajuaje kwa hakika kwamba walichokwambia ndicho wanachowaza au wanachohisi? Kwa msingi huo, tunaweza kujua jambo lolote kwa hakika kabisa?

Tuna maanisha nini tunaposema kwamba jambo fulani ni kweli? Je, ni jambo gani linalowapatia wanasiasa haki ya kutumia mamlaka na madaraka yao jinsi wafanyavyo?

Je, ipo serikali yoyote duniani inayozingatia na kutenda haki kwa watu wake? Zaidi ya hayo, nini mana ya haki?

Tunaposema jambo fulani ni sahihi au si sahihi tunakuwa tunaonyesha kukubali au kukataa? Uadilifu una maana yoyote? Je ni zaidi ya usahihi na makosa?

Hivi kuna Mungu? Je, hoja zinazojengwa kuthibitika uwepo wa Mungu zina nguvu yoyote? Zinaridhisha? Je, wazo au dhana ya uwepo wa Mungu inakubalika katik akili ya kibinadamu?

Muda ni nini? Una umbile au hulka gani? Muda unaweza ‘kusafiri’ kutoka sehemu moja hadi nyingine?

Mimi ni nini? Ni jambo gani linanifanya mimi niwe mtu yule yule kama nilivyokuwa miaka kadhaa, tuseme 10 au 20 iliyopita?

Utu wangu ni akili yangu? Je akili ni nini? Kuna tofauti kati ya akili na ubongo?

Ni bora kuwa mwanafalsafa asiyeridhika au kuwa nguruwe aliyeridhika?

Uliwahi kuhisi kwamba mara nyingi mambo mengi huishia pale mambo mazuri yanapoanzia au yanapokaribia kujitokeza? Ulishatambua kwamba kunamambo ambayo huwa tunazuiwa kufanya hata kabla hatujafikiria kuyafanya?

Unajua kwamba kunamambo ambayo ulifundishwa au kulelewa usiyahoji? Au wewe ni mmoja wa watu ambao hupokea na kuamini ‘busara’ ya wakubwa tu bila kujipa mwanya wa kuitilia shaka?

Falsafa ni somo ambalo kiini chake ni kuhoji na kuhoji. Katika falsafa, kuhiji hakuwekewi vikwazo hata kidogo, bali kunapaliliwa. Katika falsafa, hakuna jambo hata moja lisilohojiwa. Hata Mungu anahojiwa.

Kwa sababu hiyo, hata wanafalsafa wenyewe hujiuliza kama wanajua maana ya falsafa. Na hata inapotolewa, hawakubaliani kuhusu jibu linalopatikana.

Kama unapenda kuchimba masuala na kwenda ndani kabisa kwa kuhoji na kudadidisi ili kujua misingi ya masuala hayo, basi utafurahia somo hili la falsafa.”

Aya zote hizo zilizotangulia si zangu. Si mawazo yangu. Ni kauli iliyonikaribisha katika Chuo Kikuu cha Hull, Uingereza, wiki iliyopita. Yameandikwa katika jarida ambalo kila mwanafunzi wa falsafa chuoni hapa anakabidhiwa.

Ni maandalizi kwa kozi ya falsafa katika miaka michache ijayo, kwa wanaoanza kabisa na wanaojiendeleza kwenye fani hii ya falsafa.

Kozi yetu ina wanafunzi zaidi ya 120. Nayo imegawanyika katika kozi nyingine ndogo ndogo kulingana na masomo wanayochagua pamoja na falsafa. Wapo wanaosoma falsafa pekee. Wapo wanaochanganya masomo mengine.

Katika darasa langu la fasafa, siasa na uchumi, tumo wanafunzi 24. Hadi sasa mwafrika ni mmoja. Kuna wasichana wawili.

Kijumla, chuo kina wanafunzi wapatao 16,000. Zaidi ya 200 ni wanafunzi wa ‘kimataifa’ kutoka nchi 107 duniani kote. Waliobaki ni Waingereza. Ukiondoa Uingereza, nchi nyingine yenye wanafunzi wengi chuoni ni China.

Kila unakopita utakutana na Mchina. Kama si Mchina atakuwa Mkorea, Mjapani, Muhindonesia, Mtaiwani au Mmalaysia. Ni wengi.

Juzi wanafunzi wote wa falsafa tulikuwa na hafla ya kwanza ya kujuana na kubadilisha mawazo. Katika watu zaidi ya 100 sikumwona Mchina hata mmoja.

Nikamuuliza mmoja wa walimu wetu: inakuwaje kuna Wachina wengi katika chuo hiki, karibnu kila mahali, isipokuwa katika kozi ya falsafa?

Alijibu: “Unajua, kozi hii haiwafai Wachina. Ningeshanga kama wangekuwa hapa. Unajua kwa nini? Hawa wanatoka katika jamii ya watu wanaotii sana mamlaka. Si watu wanaohoji. Siasa na tamaduni zao ni wa jamii inayoogopa kuhoji, tawala zinazoogopa kuhojiwa. Sana sana, nadhani Wajapani sasa wataingia, kwa kuwa siasa zao zinaanza kuchangamka.”

Siku hiyo hiyo, nikiwa natazama vipindi vya televisheni hapa Uingereza, ikarushwa sehemu fupi ya mahojiano kati ya mwandishi na Jenerali Perves Musharraf, kiongozi wa Pakistan.

“Osama bin Laden yuko wapi?” mwandishi akahoji. Musharraf alichanganyikiwa ghafla. Akashtushwa na swali, zikapita sekunde kadhaa kabla hajajibu, watu wakacheka, na mwandishi akatabasamu, halafu Musharraf akapata neon la kusema kuhusu Osama bin Laden.

Mmoja wa wale niliokaa nao akashangaa swali la mwandishi. Nani huyo anauliza swali hilo? Kumbe naye alipigwa butwaa. Hakuzoea kusikia wakubwa wakiulizwa maswali ya kushtukizwa.

Ni Mtanzania ambaye amezoea kuona wanasiasa (hasa watawala) na waandishi wa habari wakisuguana mabega, wakinywa bia, soda au kahawa na kupanga habari za kuandika.

Sikuhangaika kujadili lolote naye. Lakini nilipata hisia kali kwamba waandishi wa nyumbani kwetu hawaoni kwamba kuhoji na kudadisi kila jambo ni sehemu ya kazi yao. Sisi hatuanzii kwenye kutilia shaka, kuhoji, kudadisi na kuchimba.

Sisi tunaogopa wakubwa, mithili ya Wachina niliozungumzia hapo juu. Sisi tumezoea kumwaga sifa kila kukicha hata kwa jambo linaloleta shaka kwa rais wa kawaida, ilimradi limesemwa na kiongozi.

Sisi tunaandika habari zinazonukuu maneno au kauli za wakubwa. Hatuzunguki na kwenda nyuma ya kauli za wakubwa hao. Sisi tunaogopa kupoteza urafiki na wakubwa. Tunaogopa kufokewa na kutishwa. Ndiyo maana hatuulizi maswali magumu.

Ndiyo maana wanasiasa watawala hawatuheshimu. Ndiyo maana wanatututumia. Ndiyo maana wanatudanganya. Ndiyo maana na jamii inaanza ‘kutuona tu tofauti.’ Ndiyo maana nasi tunaingizwa kirahisi katika ufisadi. Ndiyo maana tunashindwa kushinikiza mabadiliko.

Tumeridhika na majibu mepesi. Na wanaotuzunguka wameshatambua uwezo wetu, wanaweza kutuambia lolote. Wameshajiaminisha kwamba hatutawahoji, hata wakitudanganya. Nadhani wanaamini kwamba tumefika hapo kwa kuwa hatujui. na wamegundua kwamba tumeridhika. Tumetekeleza wajibu wetu. Kama nilivyowahi kuandika katika safu hii, tumeacha kazi yetu, tunafanya kazi yao. Hatuwajibiki.

Ni kweli si lazima wote tuwe wanafalsafa kitaaluma. Lakini tuwe wanafalsafa kwa hulka. Tuhoji na kuhoji na kuhoji. Swali lizae jibu, na jibu lizae swali. Baada ya hapo tutaheshimiana. Ndipo tutafanya kazi ya kujenga nchi kama watu wazima, wenye akili.

Ansbert Ngurumo ni mhariri mwanzilishi wa gazeti hili, aliye masomoni Uingereza. Anapatikana kwa barua pepe ansbertn@yahoo.com simu +447904159823

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'