Sunday, October 08, 2006

Tunafaidi joto la kukumbatiwa; Tanzania inafaidi nini?

Na Ansbert Ngurumo, Hull University, UK

NAANDIKA kumpa pole Rais Jakaya Kikwete kwa yaliyompata kutoka gazeti la Kenya wiki inayomalizika leo.


Nimesoma kwenye mtandao kwamba gazeti moja la Kenya limechapisha katuni inayoonyesha waandishi wa habari wa Tanzania wakimlamba miguu Rais Kikwete. Nimeiona katuni hiyo.


Nimesoma pia habari juu ya taarifa ya Ikulu kwamba Rais wetu na wasaidizi wake wamesononeshwa na katuni hiyo. Nimesoma pia kwamba Rais hatajibu lolote kuhusu katuni hiyo.


Nakubaliana na rais wangu kwa mambo mawili. Walioandika na kuchora katuni hiyo si Watanzania. Ni Wakenya. Na si Wakenya wote, wala si magazeti yote ya Kenya.


Hivyo Rais amefanya jambo jema kutojiingiza katika malumbano nao. Si wananchi wake.


Maana hata sisi tumekuwa tukiona magazeti yetu yanawachora viongozi wengine wa Afrika na sehemu mbalimbali za dunia. Yanawachora kadiri mitazamo yetu juu yao inavyokuwa wakati huo.


Na michoro hiyo haina masilahi yoyote ya kisiasa. Ina malengo mbalimbali ya kitaaluma. Inalenga kuburudisha wasomaji. Wakati mwingine inaleta ujumbe mpya - inaelimisha. Wakati mwingine inafikirisha.


Na katika kufanya hivyo, inafurahisha au inaudhi. Kwa mfano, kuna watu wamefurahia katuni hiyo kwa kuwa wanaamini kwamba waandishi wa Tanzania wanalamba miguu ya wakubwa. Wapo.


Wapo walioifurahia kwa sababu tu ya kufurahia ubunifu wa mchoraji. Wapo. Wengine wameifurahia kwa sababu wanapenda utani. Na wameona mtu aliyejitokeza kumtania rais wa nchi!


Wengine wameichukia. Si kwa sababu nyingine yoyote, bali kwa kuwa imemgusa na kumsema rais. Basi! Hawataki aguswe.


Wengine wameichukia kwa sababu wamesikia mwenyewe aliyechorwa ameichukia. Wanachukia pamoja naye.


Wapo walioichukia kwa kuamini kwamba imesema uongo. Wanasema imemdhalilisha Rais. Wanaongeza kuwa imewadhalilisha waandishi wa habari. Wapo.


Bila shaka sitakosea nikisema katika kundi hili wamo waandishi wenyewe. Maana tunajua kwamba wengi wetu, ingawa tunaandika na kuchambua mambo ya wengine kila siku, hatufurahii uchambuzi wa wengine juu yetu kama hautusifii.


Ni hulka ya kibinadamu. Kila mtu anataka asemwe vizuri. Hulka hii ndiyo inayowapa haki waliochukia pamoja na rais wetu.


Lakini wengine hawakuchukia wala kufurahi. Wameguswa tu na hoja ya mchoraji. Wanaweza kukuza mjadala mpya, na kumwambia Rais Kikwete na wasaidizi wake kwamba baada ya kuchukia watafute tafsiri halisi ya katuni hiyo.


Naamini, kama ilivyowahi kuandikwa na mwandishi mmoja ambaye simkumbuki jina, kwamba haiwezekani watu wote wakawa na tafsiri moja inayofanana juu ya katuni hiyo.


Haiwezekani. Hivyo, inabidi tuvumiliane katika kuelewa ujumbe unaoletwa kwetu kupitia katuni hiyo. Watu wenye akili hawatakosa la kuwaza. Wanaweza kuitumia kuboresha uhusiano kati ya rais au serikali na vyombo vya habari. Uhusiano unalisaidia taifa.


Maana kama wengi wanavyosema, nami naamini katika ukweli huu, uhusiano uliopo sasa kati ya rais na vyombo vyetu vya habari unalenga kuisaidia serikali, si nchi.


Ni uhusiano usiotambua kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola. Na hili halikuanzwa na Kikwete. Amelirithi. Lakini litamgusa zaidi yeye kwa kuwa amejitangaza kuwa rafiki wa vyombo vya habari.


Kwa kauli yake mwenyewe, mara kadhaa, amesema kwamba ana nia ya kushamirisha demokrasia katika Tanzania. Nionavyo mimi, Kikwete hawezi kushamirisha demokrasia bila kuviondoa vyombo vya habari katika utumwa.


Hawezi kushamirisha demokrasia iwapo vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira ya woga. Na anayeogopwa katika hili si mwingine, bali serikali. Hawezi kushamirisha demokrasia bila kuondoa sheria dhalimu ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa miaka zaidi ya 14 sasa; ambazo zinavinyima vyombo vya habari fursa ya kuwa huru na kufanya kazi bila kuogopa matumizi mabaya ya utashi wa wakubwa.


Yawezekana mchoraji wa katuni anajua hali halisi ya uandishi wetu na mazingira yanayotukabili. Anajaribu kuchora uhusiano uliopo kati ya waandishi na rais, anasema wanamlamba miguu.


Nasema hivi, hatumlambi miguu. Lakini simshambulii mchoraji. Ningekuwa naichora mimi ningemweka rais akiwa amewakumbatia waandishi, badala ya kuwaonyesha wakilamba miguu.


Kulamba ni alama tu kama ilivyo kukumbatiwa. Hata kama wapo ambao wangedhani kukumbatiwa ni kuzuri zaidi, sioni tofauti kimantiki.


Ninachoona katika kumbatio ni watu wanaofurahia joto la rais. Ikumbukwe kuwa watu hawa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya kubezwa na rais aliyeondoka. Alikuwa mwandishi, lakini hakutangaza kuwa rafiki yao.


Sana sana, alikuwa akilumbana nao kila alipopata fursa ya kufanya hivyo hadharani. Aliwaita waandishi uchwara. Aliwadharau wazi wazi. Bila shaka nao walimchukia.


Sasa huyu kaja. Amenyoosha mikono yote miwili. Katika mshangao wa ajabu, nao wamenyoosha mikono. Wamekumbatiana. Mh! Joto la rais!


Lakini bahati mbaya, huyu aliyewakumbatia haachii. Hawawezi kutoka. Wanabaki wanacheka. Wanapiga stori. Wanatabasamu. Habari zinapita. Haziandikwi.


Zitaandikwaje wakati mikono imekumbatiwa? Zitaandikwaje wakati zinamhusu aliyekumbatia na kukumbatiwa? Zitaandikwaje wakati kila mmoja anaogopa kutofautiana na mkubwa na kuleta malumbano yanayoweza kupoteza joto hili?


Zitaandikwaje wakati wengi waliokumbatiwa wanadhani jukumu lao ni kumsaidia aliyewakumbatia? Zitaandikwaje wakati baadhi ya ahadi zake hazijatimizwa? Hapo ndipo tulipo.


Lakini swali tusilojiuliza haraka haraka ni hili. Iwapo kila mmoja atataka ‘kumsaidia’ rais kutoka ofisini mwake; nani atamsaidia kutoka nje ya ofisi? Lakini zaidi ni wajibu wetu kumsaidia au kuisaidia nchi? Je, nchi yote inaishia kwa rais na wasaidizi wake?


Lipo swali la ziada. Iwapo kila mtu anataka kuwa mwandishi asiye rasmi wa rais, walioajiriwa kumsaidia rais watafanya kazi gani? Na kazi zetu zitafanywa na nani?


Uongo mbaya, waandishi wetu wengi wanampenda rais wetu. Sidhani kama wapo wanaomchukia.


Lakini lazima tuweke tofauti kati ya kupenda, kushabikia na kushangilia. Na tutofautishe mambo ya kushabikia na ya kushangilia. Tuweke tofauti kati ya kufagilia na kufikirisha.


Hata yeye anahitaji kuelimishwa. Hatuwezi kusema ana akili na uwezo wa kusifiwa kwa kila hatua anayoichukua. Anastahili kukosolewa. Na sisi ndio tungepaswa kuongoza Watanzania wenzetu kwa kumfanya rais wetu awe ‘smart’.


Afike mahali hata anapotaka kuzungumza nasi, ajiandae vizuri. Lakini ameshatujaribu mara kadhaa. Ameshinda.


Ipo mifano mingi, lakini nitatoa michache. Wizara ya Nishati na Madini ilipotangaza uamuzi uliotokana na mjadala kati ya Rais Kikwete na Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, kwamba itailipa serikali sh bilioni tisa ambazo ni dola za Marekani milioni saba, hakuna aliyejitokeza kuhoji kwa nini tulipwe kiasi kidogo mno kutoka kwenye migodi mitatu!


Ama tulisahau au hatukujua kwamba kampuni hiyo iliwahi kufanya mazungumzo na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kukubaliana iwe inalipa dola milioni tano kwa mgodi mmoja wa Bulyanhulu, mwaka 1999.


Maana yake, kama alivyosema mwanaharakati wa mazingira, Tundu Lissu, serikali ya sasa itaambulia dola milioni 2.3 kutoka kila mgodi.


Kama ingebanwa kwa mazungumzo ya awali na Mkapa, kampuni hiyo ingelipa dola milioni 15.


Tumeibiwa mchana. Lakini tulimsifu Rais Kikwete kwa hatua aliyochukua. Ndiyo, tumemsifu rais. Tumefaidi joto la kukumbatiwa. Tanzania imefaidi nini?


Rais alipotoa hotuba mbovu jijini Mwanza mwishoni mwa mwezi Julai kuhusu mapanki na silaha, vyombo vya habari vichache - kumbukumbu zangu zinaonyesha havizidi viwili - vilimkosoa baadaye, na wasaidizi wake walikiri kwamba alikosea.


Lakini lugha iliyotumiwa ilikuwa ya kidiplomasia kwamba alishauriwa vibaya; alikoseshwa. Vilivyobaki vyote vilikuwa vikishangilia jinsi alivyomzodoa mtengeneza filamu. Havikutaka kuzama katika mantiki ya filamu hiyo. Havikutazama maisha halisi ya wakazi wa maeneo husika. Kisa? Viliogopa kupoteza joto la rais. Lakini havikumsaidia.


Karibu kila mwandishi anajua kwamba tatizo tulilo nalo katika Bwawa la Mtera, ambalo linadaiwa kusababisha kukosekana kwa umeme wa kutosha nchini, si ukosefu wa maji. Tunajua bwawa limejaa matope.


Tunajua pia kwamba ubabe wa serikali ndio ulioifanya ikatae ushauri wa kitaalamu kwamba bwawa hilo si mradi wa kuaminika wa kuzalisha umeme.


Tunajisifia kwamba viongozi wetu wanatusikiliza tukiwashauri kupitia vyombo vya habari. Mbona tunaendelea kuimba wimbo wao (wa uongo) kwamba tatizo la Mtera ni ukosefu wa maji?


Ipo dhana, ambayo baadhi yetu hatukubaliani nayo kivitendo, kwamba baadhi ya habari haziandikiki. Ipo dhana pia kwamba baadhi ya wakubwa hawaandikiki.


Na wanaosema hivi wanakiri kwamba: “Mkapa licha ya ubabe wake, alikuwa anaandikika, halafu anajibu mapigo… Sumaye pia alikuwa anaandikika, wala hafuatilii kuwasumbua waandishi.”


Ni ujumbe mzito kwa serikali inayowapenda wanahabari, inayowazungumzia vizuri jukwaani, lakini haiboreshi mazingira ya kisera na kisheria kwa ajili yao kufanya kazi kitaaluma. Inaogopa nini?


Nasi wenyewe tunaipa jeuri, kiburi na ubabe tunapokaa na kunyoosha mikono bila kufanya lolote kuikumbusha, kuikemea, kuihoji na kuisumbua.


Tuseme ukweli. Kama ‘Katuni ya Kikwete’ ingetumika katika gazeti lolote nchini, lingekuwa limefungiwa; maana wenzetu hawajajifunza kuvumilia wanapokosolewa. Inawezekana hawajikosoi pia?

Uchambuzi huu unapatikana pia katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Oktoba 8, 2006 na katika tovuti www.freemedia.co.tz Wasiliana na mwandishi kwa simu +447904159823 au barua pepe ansbertn@yahoo.com

6 comments:

Maggid Mjengwa said...

Ngurumo,
Nimekusoma gazetini na humu mtandaoni. Kazi nzuri. Vipi masomo huko?
Nitembelee: http://mjengwa.blogspot.com

Ndabuli said...

Ngurumo, hapa kweli umeunguruma,chmbuzi hizi ndio zinaitwa upande mwingine wa sarafu, kunavitu nilikuwa sijavifikiria lakini umenifanya nifikirie. Aksante

Anonymous said...

Mzee Ngrurumo nimeukubali uchambuzi wako kwa mikono miwili, hususan kuhusu mahusiano kati ya rais wa awamu ya nne na vyombo vya habari na pia mahusiano kati ya rais aliyetangulia na waandishi wa habari. Udhaifu wa vyombo vyetu vya habari uko dhahiri sitaki kuuelezea hapa lakini nataka rais wa awamu ya tatu ambaye alidiriki kuwakashifu waandishi wa habari kwa kuwaita waandishi "Uchwara" ni sawa na baba kumtukana mtoto wake kwa kumuita "mbwa", ilhali akijua, mtoto wa mbwa ni "mbwa" na hawezi kuwa kitu kingine! Ahsante, Ndesika nawasilisha!!

Ansbert Ngurumo said...

Aha! Kumbe ni Ndesika! Naona majina yako yote yanaanza na ND. Hivi kwa nini

Uko wpi siku hizi? Unafanya nini 'kubomoa' taifa? Una mipango gani ya baadaye?

Baada ya hapo naomba nichangie kidogo mada yako. Huyo Rais aliyeondoka, nadhani ukimuuliza alimchukia mwandishi gani katika utawala wake, baada ya Ulimwengu ni NGURUMO.

Uongo mbaya, nilimwandama. Si kwa ubaya, bali kwa kutimiza wajibu wangu. Ndiyo ilikuwa njia yangu ya kujenga taifa. Kuwaandama watawala ili watende yaliyo haki, yanayokubalika kwa wananchi. Kama walitenda hayo waliyotenda, tunayodhani kwamba si mazuri sana, wakati tuliwaandama, jaribu kujuliuza ingekuwaje kama tusingefanya lolote.

Kamwe sikmchukia Rais Mkapa. Nilimsumbua kutetea kura niliyompigia. Niliudhika alipotenda kinyume cha matarajio ya wananchi. Nilisikitika alipotamka mambo yanayotia aibu uongozi wake. Katika kutetea' dhamana yake kwetu, nilidhamiria kumkumbusha wajibu wake, na kumwambia mfalme kwamba yu uchi.' Kama hakusikia, si kosa langu.

Wala sikuchukizwa naye alipotuita sisi 'waandishi uchwara.' DEmokrasia tunayoitetea inatupa haki ya kuna mambo yale yale kwa miwani tofauti. Yeye alituona uchwara. Tulibaki tulivyokuwa. Nasi tulimuita majin mengine, alibaki alivyokuwa. Sehemu kubwa ya mchezo iliishia pale. Ndogo ndiyo iliyotuandama, kama serikali zote zilivyo katili dhidi ya waandishi.

Mkapa keshaondoka. Aliyofanya ameyafanya, atawajibika kwayo. Lakini tunaweza kumpia hasa, kwa kuwa ameshamaliza. Mwache apumzike, historia itasimulia kisa chake.

Lakini hapa tulipo si pazuri kabisa. Hawa wakubwa hawasemeki. Hawatishi kwa bunduki wala mapanga, lakini wanatumia 'bongo kuwateka waandishi. Hawamshurutishi mtu, lakini kalamu hazina wino kabisa! Na wanapoandikwa kidogo - ehe!

Wanakuwa wakali kama mbogo, simu zinapigwa kwenye vyumba vya habari au kwa wahariri. Wanalalamika. hawaleti jibu mbadala, lakini wanaonya kijanja. Waandishi wote wanakaribia kuwa 'watumishi' wa viongozi, hasa Rais na Waziri Mkuu. Taaluma inaelekea shimoni!

Na kinachochangia zaidi ni umaskini wetu. Ndiyo unaosababisha woga wetu. Ndiyo unyonge wetu.

Na sasa wameanza kakati wa kununua vyombo vya habari au kuwekeza katika vyombo vingi ili kupunguza makali yake.

Kazi hii inafanywa na SPIN DOCTORS - kina Rostam Aziz. Kwa ustawi wa nchi, kazi hii ni mbaya na chafu kuliko kebehi za Mkapa.

Historia itatuhukumu!

Naomba kuwasilisha.

Shimba said...

What a brain. Kusema kweli wakati mwingine Bw. Ngurumo huwa nakata tamaa kabisa na nchi yetu. Tulitarajia vyombo vya habari ndivyo vitusaidie lakini wapi! Waandishi mko wachache mno.
Mimi bila shaka nadhani tatizo jingine ni lile lile linalowakumba Watanzania wengi; NJAA. Ni njaa hiyo hiyo inayowafanya wapiga kura watoe kura kwa sababu ya chumvi, kanga, tshirt na kofia. Ni njaa ndio inayowafanya waandishi wajipendekeze.
Lakini pia bila kulenga kumdhalilisha yeyote pana tatizo la elimu hapa. Elimu hiyo hiyo inayowakwaza wapiga kura ndio elimu hiyo inayowakwaza waandishi. Kidato cha nne na miezi mitatu pale TSJ, tutategemea nini kwa mtu kama huyu? Elimu yake yote haijamfunza kuwa mchambuzi. Hana elimu yakumwezesha kutoa changamoto kwa mtoa habari n.k Huyu bila shaka ni reporter na si journalist. Tanzania Daima, Raia na machache makini yanaweza kufanya yafanyayo kwa sababu kuna journalists na siyo reporters.
Yote kwa yote makala yako Bw. Ngurumo imenipa faraja ni kuwa tu sijui "watawala wetu huwa wanazipata?"

Anonymous said...

Kwa ni uongo? waandishi wetu wamechoka!!! Hawana jipya..yaani mimi wameshanikera mpaka sina hamu nao.....yaani wao ni kusifia tuu hawato critique yoyote..jamani!! Kaka ile katuni haikuwa na uwongo wa aina yoyote!!!

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'