Sunday, July 22, 2007

Serikali Kupinduliwa

HABARI hii ilileta kizaazaa kati ya serikali na gazeti la MwanaHALISI Jumatano 18.07.2007. Serikali inagombana na maoni ya wakili na mwanasiasa maarufu, mmoja wa waasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini, Mabere Nyaucho Marando.

Marando anasema serikali inaweza kupinduliwa, iwapo wananchi watajua haki zao.

“Wewe unatumia lugha ya kupindua. Kwa lugha ya kawaida, kupindua ni kutumia nguvu za kijeshi. Lakini yapo mapinduzi mengine yanayowezekana. Ni yale yanayotokana na mwamko wa wananchi,” amesema.

Katika mahojianao maalum na MwanaHALISI juu ya miaka 15 ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, Marando amesema, “Wananchi wana uwezo wa kuipindua serikali kupitia njia halali ya sanduku la kura.”

Akihusisha hasa na madai ya wabunge wa CCM, Job Ndungai na Janet Masaburi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwamba elimu inayotolewa na HakiElimu inaweza kusababisha serikali kupinduliwa, Marando alisema:

“Hili linawezekana kabisa. Kinachohitajika ni mwamko zaidi kwa umma. Wananchi wakipata mwamko, wanaweza kuipundua serikali kwa njia ya kura.
Marando amesema serikali ya sasa imeshindwa kuwajibika na hivyo inaweza kung’olewa kwa nguvu za umma.

Amesema HakiElimu inafanya kazi nzuri na inaifanya vizuri na kwamba vyama vya upinzani havina budi kujifunza kutoka HakiElimu, hasa katika suala la utafiti wa hoja muhimu za haki za binadamu na maslahi ya jamii.

“Unajua, CCM inaumwa ugonjwa wa kusinyaa. Ugonjwa huu huvipata vyama vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu. Chama kikikaa madarakani kwa muda mrefu, kinasinyaa. Kinakuwa na mchoko,” anasema.

Katika mahojiano ambayo yamechapishwa katika toleo hili, Marando anasema, sababu za kuchukia CCM bado zipo, “Hiki bado ni chama cha kidkteta. Matumaini ya wananchi bado yapo, kwamba kuna siku watajikomboa kutoka udikteta huu.”

Kuhusu mafanikio ya upinzanai katika kipindi hiki, Marando anasema, “uwanja wa demokrasia umepanuka. Serikali inachukua hatua, japo kwa kiwango kidogo na bila upinzani serikali ingefanya itakavyo. Siridhiki, lakini angalau tumepata mahali pa kuanzia.”

Alipoulizwa CCM inaweza kujivunia nini katika miaka hiyo, Marando alisema, “Wanaweza kujivunia bahati yao nzuri ya kushikilia madaraka bila kuwa na sababu za msingi za kutawala na kuendelea kubaki madarakani wakati hawastahili kuwapo.”

Marando amesema CCM haina zaidi cha kujivunia, “Labda ujinga wanaowalisha kwa Watanzania kwamba CCM ndiyo baba na ndiyo mama, wakati si kweli. Wanaweza kujivunia pia rushwa ambayo wameifanya kuwa sera ndani ya CCM na serikali yake. Basi!”

Kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kifedha, Marando anasema, ni kweli vyama havina fedha wala wafadhili, “Lakini lazima wafanye kazi hiyo. Waende kwa Watanzania wenzao… kuomba msaada. Hilo ni jukumu lao na hawawezi kulikwepa hata kidogo.”


Soma Mahojiano na Marando

1 comment:

Anonymous said...

Na bado tu. Wataondoka. Zama zimebadilika.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'