Sunday, July 01, 2007

Buriani Amina Chifupa; umekwenda kishujaa




Na Ansbert Ngurumo, Hull
1.
Amina Mpakanjia;
Nani asiyekujua?
Nani hajakusikia?
Nani hakukutambua?

2.
Eti umetukimbia?
Sikubali nakataa;
Nani kakuondoa?
Lipi umemfanyia?

3.
Amina, mi siamini;
Kwamba tena sikuoni;
Haraka hiyo ya nini?
Wakimbia ‘fanya nini?

4.
Najua hukuwa radhi;
Kwenda chini ya aridhi;
Yatoka wapi maradhi;
Bila idhini ya Kadhi?

5.
Bado ulikuwa dogo;
Miongoni mwa vigogo;
Yako marefu malengo;
Sasa wayapa kisogo.

6.
Umekwenda kwa lazima;
Siku zote tutasema;
Umeondoka mapema;
Nani amekusukuma?

7
Mungu ndiye anajua;
Kwanini watangulia;
Ameshindwa kuzuia;
Majonzi ya Tanzania.


8
Kama angetuuliza;
Nani kumtanguliza;
We tusingekupoteza;
Kura tungezipunguza.


9
Si wewe mwenye hatia;
Ulopaswa tangulia;
Wapo walokuvizia;
Sasa umewakimbia!

10.
Wapo waliokubeza;
Mwenyewe ukanyamaza;
Pole pole ukaanza;
Hadi wao kushangaza.

11.
Kisomo chako kidogo;
Si kama chao vigogo;
Kiliyabeba magogo;
Kuwaachia usongo.

12.
Woga ‘liweka pembeni;
Na nchi yako usoni;
Lionekana makini;
Kama vile wa zamani.

13.
Vijana uliwawaza;
Hata wale wasocheza;
Sumbawanga hadi Mwanza;
Ulisema: ‘hawa kwanza.’

14.
Soka ulishangilia;
Timu yetu saidia;
Nguvu kuiongezea;
Us’okuja shuhudia.

15.
Watoto ulitetea;
Kama mama asilia;
Ulijua Tanzania;
Hao yawategemea.

16.
Yatima ‘lisaidia;
Tumaini ‘liwatia;
Wagonjwa ‘lisalimia;
Wote uliwawazia.


17.
Tabasamu lilijaa;
Huruma lilichochea;
Urembo ulitumia;
Wengi kuwahudumia.

18.
‘Liitwa Mama shughuli;
Kwa kazizo mbalimbali;
Hata kuwapamba wali;
Mambo yako kali kali.

19.
Kikwete anauliza;
Sitta huyo kanyamaza;
Chifupa amepoteza;
Nani ‘tambembeleza?

20.
Wapo ul’oshambulia;
Kwa haki nakutetea;
Mihadarati bugia;
Hukutaka kusikia

21.
Nyota yako iliwaka;
Hata kwa wasoitaka;
Haya sasa umetoka;
Lije walilolitaka?

22.
Sadaka uliyotoa;
Sote tunaitambua;
Hata walokusumbua;
Hili watalijutia.

23.
Hatuwezi simangana;
Sasa twafarijiana;
Ila twaweza ‘onyana;
Hata kushauriana.

24.
Amina umetoroka;
Waacha moto wawaka;
Umejitoa sadaka;
Tutakayoikumbuka.

25.
Twajua ‘metangulia;
Sote tutaelekea;
Ila moja twatambua;
Umekwenda kishujaa!

26.
Umekimbia kwa kasi;
Kuliko hata ya fisi;
Vijana watakumisi;
Wabunge hata na sisi.

27.
Kina mama wanalia;
Mwenzao wakumbukia;
Wasanii nao pia;
Nyimbo wanakuimbia.

29.
Maisha yako twakiri;
Ni mafupi na ya heri:
Marefu yaliyo shari;
Umeachia wapori.

30.
Tulia na Malaika;
Pale atapokuweka;
Tabasamu cheka cheka;
Yametimu, yamefika.

31.
Ukiukuta mpira;
Cheza na Hawa na Sara;
Shambulia mduara;
Hata mbinguni, ahera.

32.
Mpakanjia na mwana;
Baba na Mama Amina;
Kubali ya Maulana;
Itikieni: Amina.

3 comments:

Anonymous said...

Ansbert kazi nzuri sana ya tenzi hii.... hongera
Simon

Mjengwa said...

Shairi limenikuna hili Ansbert!
Sikupati kwa simu, kulikoni?
/Maggid

Anonymous said...

Shairi murua. Linaibua hisia nyingi. Hongera Ngurumo!

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'