Monday, March 31, 2008

Nyerere ataka kijiji, Kikwete mji
Nyerere hakutaka Butiama iwe makao makuu

Na Beldina Nyakeke, Musoma

CHIFU wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi amesema azma ya Rais Jakaya Kikwete kukifanya kijiji cha Butiama kuwa makao makuu ya Wilaya ya Musoma Vijijini, inapingana na mpango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Wanzagi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ukoo wa Burito Nyerere, amesema mpango wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kuifanya Butiama kuwa kijiji cha historia, kinyume na azma hiyo ya Rais Kikwete.

Chifu huyo alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kijijini Butiama hivi karibuni.

Wanzagi alisema kimsingi hapingani na azma ya Rais Kikwete ya kutaka kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya mambo mbalimbali, ikiwamo kukifanya kijiji cha Butiama kuwa makao makuu ya wilaya, lakini akasisitiza kuwa anao ushahidi ingawa si wa maandishi ambao kabla ya kifo chake, Mwalimu Nyerere aliwahi kumweleza nia na madhumuni ya kukifanya kijiji hicho kuwa cha kihistoria.

Alisema katika nia hiyo, Mwalimu Nyerere alipendekeza kijiji cha Kiabakari kilicho jirani na Butiama ndio pawe makao makuu ya wilaya.

Wanzagi alisema endapo serikali itaamua kukifanya kijiji hicho kuwa makao makuu ya wilaya, upo uwezekano wa kuchanganya mila na desturi za makabila mbalimbali kijijini hapo kutokana na muingiliano wa watu watakaohamia katika mji huo hali ambayo Mwalimu Nyerere hakupenda iwepo.

"Ninao ushahidi japo si wa maandishi. Na sijui hata kama Mama (Mama Maria) anajua kuwa mzee hakupeda kijiji cha Butiama kuwa mji. Maana aliniambia kuwa Butiama itakapokuwa mji, basi kutakuwepo na muingiliano wa watu wa makabila mbalimbali na kupoteza uasilia wa kijiji chetu ambapo alitolea mfano jiji la Dar es Salaam, ambalo kutokana na muingiliano wa watu, wenyeji wa pale, yaani wazaramo, wamehama na kusogea nje kabisa ya jiji," alisema.

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mkutano wa NEC, Rais Kikwete alisema ili kumuenzi Mwalimu Nyerere, serikali itakapofikia uamuzi wa kuigawa wilaya ya Musoma Vijijini, Butiama lazima kiwe makao makuu ya wlilaya na kuungwa mkono na mkutano huo na kuiagiza serrikali kufanya haraka kutekeleza pendekezo hilo.

Katika hatua nyingine, Chifu Wanzagi, aliitaka serikali kuwawezesha wakulima kwa kuwapa mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na pembejeo ili kuboresha kilimo.

Habari hii nimeichukua kutoka Tovuti ya Mwananchi kwa sababu za kihistoria. Nimeona ni vema iwekwe mahali ambapo hata tukiitaka kufanyia marejeo tutaipata, maana tovuti ya Mwananchi haitunzi habari zilizopita. - Mhariri.

2 comments:

Anonymous said...

Labda Kikwete anadhani huko ndiko kumuenzi Nyerere

Anonymous said...

Kugeuza miji kuwa vijiji kuna athari kubwa kuliko faida kwa wenyeji. Mfano ni jinsi Jiji la Dar linavyomeza makazi ya watu. Mfano watu walihamia maeneo ya geza ulole na vijij vingine na kufungua mashamba bila kupewa hatimiliki. Leo hii wanafukuzwa kisa ni jiji na ardhi haina makaratasi hivyo serikali huchukua bila fidia ya mali wala shughuli mbadala kwa wakazi. Je mtu anaweza kunza upya kila miaka kumi huku umri ukimpiga kofi. Je hatuwezi kujenga satellite cities zinazotenganishwa na maeneo ambayo watu wanaendelea na shughuli zao za kilimo na kufuga? Mbona wenzetu Ulaya, hususa magharibi hakuna minyororo ya kuta za sementi? Ni ulafi na kuharibu historia. Nitashukuru watu wa Butiama mkikataa kijiji chenu kugeuzwa mji. Angalieni Kung'ombe inavyotaka kumezwa na BUNDA. Si kila kipya ni maendeleo.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'