Saturday, December 04, 2010

Elimu yetu kikwazo kwa Tanzania tuitakayo

ASASI binafsi inayoitwa UWEZO Tanzania, Mei mwaka (2010) huu ilifanya utafiti juu ya maendeleo ya elimu katika vijiji 1,140 kwenye wilaya 38, ikahoji watoto 42,033 wa shule za msingi, wenye umri kati ya miaka mitano (5) na 16, katika kaya 22,800. Matokeo ya utafiti huo, ambayo yalitangazwa rasmi Septemba 2010, kwa kifupi, yaliibua masuala yafuatayo:

1. Katika watoto watano wanaohitimu elimu elimu ya msingi (Darasa la Saba), mmoja anaweza hawezi kusoma Kiswahii cha darasa la pili.
2. Nusu ya watoto wanaohitimu Elimu ya Msingi (Darasa la Saba) hawawezi kusoma Kiingereza.
3. Katika watoto 10 wanaohitimu darasa la Saba, watatu hawawezi kufanya hesabu (hisabati) ya darasa la pili.
4. Asilimia 70 ya wanafunzi wa shule za msingi hawajui kusoma Kiswahili kwa ufasaha.
5. Hadi darasa la tatu, watoto saba kati ya 10 hawawezi kusoma Kiswahili cha msingi.
6. Watoto tisa kati ya 10 hawawezi kusoma Kiingereza cha msingi.
7. Watoto wanane kati ya 10 hawawezi kufanya hisabati za msingi.


Jambo la kukumbuka: Elimu ya Msingi ndiyo msingi wa maisha ya kila Mtanzania. Bila msingi huu, mtoto hawezi kusonga mbele kupata elimu ya sekondari au ya chuo kikuu. Hata asipoipata ya sekondari, hataweza kujiwezesha kwa lolote kwa sababu hatakuwa na stadi muhimu za kukabiliana na maisha yake pale alipo. Kumbuka kuwa Watanzania walio wengi wana elimu ya Darasa la Saba.

Maswali muhimu: Je, kwa kiwango hiki cha elimu, serikali inawatendea haki watoto wetu? Kwa elimu hii, tutaweza kujikomboa kutoka kwenye umaskini? Je, elimu hii itatuwezesha kushindana na kukabiliana na changamoto za kimataifa? Je, kwa viwango hivi, tutaipataje Tanzania tuitakayo? Tujadili.

4 comments:

Ansbert Ngurumo said...

Nyongeza: Taasisi ya Mo Ibrahim ilifanya utafiti mwaka huu kuhusu elimu katika nchi za Afrika. Tanzania ilishika nafasi ya 47 kati ya 50

Anonymous said...

Nyongeza: Tafiti mbili zilizofanywa kwa wanafunzi wa darasa la 2 na la 3 katika shule za msingi 10 zilizopo vijijini Wilayani Bagamoyo hivi karibuni [Ngorosho, 2010a, 2010b]zinaonesha kuwa asilimia 29 walishindwa kutambua sauti katika maneno ya Kiswahili. Sauti za lugha ndizo basic foundation katika kujua kusoma na kuandika.

Stella said...

Hapa ndipo kichekesho kinapotokea. Kuna mahali Tanzania inapewa nishani kwa kuendeleza elimu na hapa Taasisi hii inatoa uhalisia wa maendeleo ya elimu kuwa nchi hii ni ya nne kutoka mwisho. Hao waliopatia Tanzania nishani si ni kebehi tupu? Viongozi wetu nao wakatangaza kwa mbwembwe kuwa tumeboresha elimu hadi kupewa nishani.

Ni vema viongozi wa elimu nchini wakazingatia matokeo ya tafiti nyingi zinazofanywa humu nchini ambazo ninaamini zinaonesha picha halisi ya maendeleo ya elimu kwa watoto wetu.

Nakala ya baadhi ya tafiti hizo ziko kwenye mtandao, mashuleni, nahata katika ofisi za elimu za wilaya. Matokeo ya tafiti hizi yatumike kuboresha elimu, nahasa ya msingi.

Anonymous said...

sio kwamba serikali yetu haijui ukweli uliomo kwenye tafiti hizi wanajua vizuri sana na ndo maana hauwezi kuwakuta watoto wao kwenye hizi shule walizomo watoto wetu. Wanachokifanya ni kutekeleza kwa umakini mkakati wao wa "wapumbaze uzidi kuwatawala."

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'