Wednesday, February 23, 2011

Ni kweli! Tatizo si Dowans, ni serikali

Kwa wanaofuatilia mjadala kuhusu Dowans wiki hii, ndugu yangu Absalom Kibanda ameandika kwenye bidii baada ya kusoma maoni yangu na ya Kitila Mkumbo. Sisi tumesema mwenye tatizo si Dowans bali watawala wetu na washauri wao; maana tunaweza kujikuta tunaacha kupamabana na waliotusababishia matatizo, tunabaki kukabana koo na wawekezaji ambao wameletwa tu - na wao wanatafuta kila upenyo wa kibiashara. Kibanda amefafanua vizuri zaidi hoja hii, nami nikaona niwawekee wasomaji wa blogu hii. Ameandika hivi:

"Kitila/Ansbert

Nimewaelewa, mmetufikirisha. Tunamuacha adui na kumshambulia mhanga. Hiyo ndiyo siri ambayo Kikwete na serikali yake wanaificha. Wanatambua kwamba wao ndiyo wenye makosa, wanatambua kwamba makosa waliyofanya katika mkataba wa Richmond ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo leo. Leo hii wanashangilia chini chini na waziwazi wanapoona waandishi wa habari, wanazuoni na wachambuzi wa mambo wakielekeza mashambulizi yao kwa Dowans wakati ukweli ukiwa bayana kwamba tunaopaswa kuwawajibisha ni viongozi wetu serikalini ambao wameitumia sekta ya nishati na madini kama mtaji wa mapato yao haramu.

Hivi nani hajui kuwa ufisadi kupitia mikataba ya IPTL na Songas ni wa kutisha kuliko ilivyo kwa Dowans. Hivi Watanzania wangapi wanajua kwamba fedha ambazo Taifa hili lilikopwa na Benki ya Dunia tena kwa riba ndizo tuliipa kampuni iliyoanza uwekezaji wa Songas kuwekeza kama mtaji wake wa asilimia 100 halafu baada ya sisi kuwapa mtaji huo kampuni hiyo ikafanikisha uwekezaji huo haramu na leo wanatuuzia umeme na deni la WB tunalipa.

Nani amesahau uharamia wa IPTL ambao ulikaribia kumpokonya maisha (Patrick) Rutabanzibwa aliyejaribu kupinga uwekezaji wake? Nani anaikumbuka ile story ya The Ugly Malaysians iliyoandikwa kueleza siri ya ufisadi wa kutisha ndani ya IPTL. Nani hajui kwamba gharama ambazo serikali inatumia kuigharamia IPTL kwa mwezi mmoja zinaendesha mitambo ya Dowans kwa miezi minne?

Hivi kama tungekuwa tumewekeza katika sekta ya nishati ipasavyo tulikuwa na sababu ya kuwaita wawekezaji wa msimu wa aina ya Dowans, IPTL na Songas? Ni serikali gani kama si hizi za CCM ambazo ndizo zimetufikisha hapa?

Hivi Kikwete ambaye alikaa katika Wizara ya Nishati na Madini kwa miaka mingi akiwa Naibu Waziri na Waziri kamili alifanya nini cha maana kulinusuru taifa na matatizo ya leo? Kama alishindwa akiwa katika wizara mama ataweza akiwa rais? Kwa nini hatulishangai hilo?

Kwa nini hatujiulizi? Iweje akiwa Ikulu ameshindwa kubaini mianya ya ufisadi katika umeme wa dharura wakati yeye mwenyewe akiwa ndiye aliye na siri nzito kuhusu kuwapo kwa IPTL hapa nchini? Mbona viongozi wetu wanatumia wepesi wa Watanzania kusahau kwa manufaa yao?

Ni kwa sababu ya jeuri hiyo ndiyo maana leo anadiriki kusema hawafahamu wamiliki wa Dowans. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana ni yeye aliyewapa baraka AG (Frederick) Werema na (Waziri wa Nishati na Madini) William Ngeleja kutamka kwamba tutawalipa Dowans na baada ya akina Sitta, Mwakyembe na wanaharakati wengine kuibuka na kumtisha akageuka na kusema eti naye ni mmoja wa watu ambao hawapendi Dowans walipwe.

Ni yeye aliwapa baraka awali akina Dk. Idris Rashid na Ngeleja za kutaka serikali inunue mitambo hiyo ya Dowans na halafu joto lilipozidi kupinga msimamo huo akageuka na kusema eti uamuzi wao wa kuachana na nia yao ya kuinunua ilikuwa ni wa kusoma alama za nyakati. Je ni haki kumuacha huyu na serikali yake salama na kumshambulia Adawi na Dowans yake? Tunapaswa kufikiri upya.

Ndiyo maana baadhi yetu tunachelea kuiunga mkono CCM na serikali yake. ndiyo maana huwa nawashangaa baadhi ya viongozi wa upinzani wanapohadaika na kuwaunga mkono wahuni kadhaa wa ndani ya CCM wanaojifanya wazalendo wakati rekodi zilizo wazo zikithibitisha pasipo shaka kwamba hao ni maruhani wanaoifanyia kazi CCM kwa staili ya kuuhadaa umma."

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'