Ndugu zangu wapigakura wa Muleba,
Pokeeni pongezi za
kipekee kwa kazi nzuri mliyofanya – kuleta ushindi mnono kwenu, kwa wanamageuzi
nchi nzima na kwa chama chenu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ni ninyi, mabibi na
mabwana, mlioleta ushindi katika uchaguzi wa vijiji na vitongoji uliopita
ambamo mmevuna viti vya vijiji vitano na vitongoji 10.
Haya siyo matokeo
yaliyonyesha tu kama mvua ya ghafla; ni matokeo ya mpango mkakati tuliouasisi –
ninyi na mimi – hapo 29 Desemba 2012. Ni matunda ya mafunzo ya uongozi
tuliyofanya katika kata zote 18 za jimbo tangu Februari 2012. Ni ushahidi kwa
ujenzi wa misingi tuliyofanya pamoja katika maeno mbalimbali Muleba Kaskazini
tangu Mei 2012; na Desemba 2012 Muleba Kusini.
Huu ni ushahidi mwanana
wa kazi za wote ambao tulishirikiana kuandaa Kongamano Kuu la Jimbo na mikutano
mikubwa ya hadhara tuliyofanya Septemba 2012 kwenye vituo vya Muhutwe, Kagoma,
Kamachumu, Nyakatanga na Izigo. Bali hatukuwa peke yetu.
Makamanda wengi
wameshiriki kikamilifu katika kuleta ushindi huu wa aina yake. Naomba kuwataja
wachache, kwa niaba ya wengine wote waliokamilisha kazi hii. Kwa leo acha
niwataje Salehe Mashaka, Symphorian Nkokerwa, Robert Rwegasira, Pontian
Kaganda, Oliva Ishebabi, Medard Karwani, Zamda Salum, Emmanuel Mugalura, Joan
Mary Rwegasira, Mzee Pangani, Ismail Bilyomumaisho, Leonigard Bayona na wengine
wengi walioshiriki.
Wapo pia makamanda
kutoka nje ya Muleba ambao tulishirikiana kujenga chama hadi hatua hiyo. Wamo
Godbless Lema, Alphonce Mawazo, John Heche, Kamanda Upendo, Concesta Rwamulaza,
Peter Mweyunge, Renatus Kilongozi, Victor Sherejei, ambao, kwa nyakati tofauti,
tuliwaalika jimboni kufanya kazi na waliitikia bila kusita. Ushindi huu ni wao pia
kama ulivyo kwa wananchi wote wanaotafuta kukata minyororo ya utawala wa CCM.
Nakumbuka siku moja,
ilikuwa Jumamosi, kabla ya kupiga kura, Karwani na Rwegasira mkaharibikiwa
pikipiki mara nne mkitoka Ngenge na Bulyakashaju kwenye mkutano wa mwisho wa
kampeni. Poleni na hongereni!
Nakumbuka Ijumaa jana
yake, katibu wetu wa kata Ngenge –anafahamika kwa jina
la “Kakuru” – alipigwa na kuuawa na watu
wasiojulikana. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
Katika mazingira ambamo
CCM inanyang’anywa vijiji na vitongoji, hata kama ni kimoja; kwetu ni ushindi.
Asitokee hata mtu mmoja kudai kwamba ni ushindi wake. Ni wetu sote. Hongereni
makamanda. Leo hii, hatuhitaji kufanya utafiti mwingine. Hapana! Tayari tumejua
kuwa ushindi utapatikana kwa maandalizi ya umma – ndani ya vyumba vyao; ndani
ya nyumba zao, ndani ya vitongoji na mitaa yao; ndani ya vijiji, kata na wilaya
zao. Hapa ndio kazi imeanza.
Aluta continua!
No comments:
Post a Comment