Monday, January 29, 2007

Kamera ya X-ray kuvua watu nguo

Iwapo Kamera hii itatumika kudhibiti ugaidi, kama STORI hii inavyosema, basi tutakuwa kama vile tunatembea uchi.

Kikwete vua ngozi ya Mkapa uwe shujaa


Na Ansbert Ngurumo, Hull

TUNAMPENDA rais wetu, lakini hatupendi baadhi ya tabia zake. Ndiyo maana tunamwambia haya. Ndiyo maana namuuliza maswali. Namwandama? Hapana! Nimuulize nani?

Maana, kama ningekuwa na swali moja tu, nikaulizwa nimtaje mtu mmoja katika Tanzania nzima ambaye, ikibidi awe wa mwisho kufa – kabla yangu – ili aulizwe swali hilo, nimgemtaja rais. Ndiyo! Rais Jakaya Kikwete, chaguo la mtandao, ‘mtu wa watu,’ chaguo la mwisho la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nimeandika maneno hayo hapo juu makusudi. Kuna waliowahi kumwita ‘chaguo la Mungu.’ Wakaleta hisia za ubaguzi na mgawanyiko miongoni mwa Watanzania. Maswali yakaibuka. ‘Kama huyu ni chaguo la Mungu, wengine ni chaguo la shetani?’ Maneno kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu yalisemwa kwa mara ya kwanza na Padri mmoja pale Manzese, Dar es Salaam; anaitwa Mapunda, ‘Tunda Kanisa.’ Bila shaka aliyasema kwa ushabiki, hakutumwa na Kanisa, maana yeye si msemaji wa Kanisa.

Bahati mbaya, maneno hayo yakasingiziwa kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki! Baadaye ilijulikana kuwa kundi kubwa la maaskofu hao, na katika umoja wao bila kusema rasmi, walishatekwa na mtandao wa Kikwete, kwa jina la CCM, kumuunga mkono Kikwete. Leo baada ya mwaka mmoja na ushehe, wanajutia ushabiki wao kwa Kikwete? Ndiye huyu waliyemtarajia? Ni kweli alikuwa chaguo la Mungu au la mtandao?

Nitaeleza kidogo kwa nini nasisitiza chaguo la mtandao! Yaliyotokea ndani ya CCM tunayajua. Chama hakikuwa na chaguo, bali makundi ya wanachama na ya viongozi yalikuwa na ‘machaguo’ yao. Kikwete alikuwa wa mtandao, ambao uliyapiku makundi mengine, na baadaye kumhalalisha Kikwete kwa wana CCM wote.

Ndivyo alivyopata sifa nyingi baadaye. Hata waliokuwa hawamwamini ndani ya chama wakaongoza katika kuimba: “Nina imani na Kikwete, iya , iya, iya…Kikwete kweli….” Pole pole, akawa chaguo la mwisho la CCM. Wakamnadi kama chaguo la watu. Na waliosimamia uchaguzi wakatueleza kwamba ameshinda uchaguzi; akawa rais wetu ‘mwenye mvuto.’

Sina shaka mvuto huo bado anao. Hata juzi alipokuwa hapa nchini Uingereza kwa safari ya kikazi, alishuhudia umati wa Watanzania waliokusanyika kumlaki, kumsalimia, kuteta naye na kumuuliza maswali. Ubalozi wa Tanzania nchini hapa ulifanya maandalizi makubwa ya kuwakusanya Watanzania wengi. Walifika. Pichani kulia, Rais Kikwete akiwa na mkewe na viongozi wengine, anawahutubia Watanzania katika ukumbi wa hoteli ya Churchhill, London.

Waliokuwapo hawajaacha kusimulia badhi ya mambo yaliyojitokeza; kwamba ukumbi uliopangwa haukutosha. Viti viliongezwa. Rais mwenyewe alichelewa kwa dakika zipatazo 45 (kama alivyokuwa akifanya akiwa waziri). Baadhi wanahoji: “kumbe urais haujambadilisha?”

Wanakumbuka hotuba yake ndeeeefu (kuhusu karibu kila kitu alichofikiria kuhusu Tanzania). Wengine wanasema ilikuwa ndefu mno bila sababu. Wanakumbuka nyimbo za CCM zilizoporomoshwa ukumbini, na baadhi ya washiriki ‘waliovalishwa’ sare za chama na kupewa bendera za CCM. Aliyewapa nani? Balozi wa Tanzania nchini Uingereza! Kwani ulikuwa mkutano wa CCM? Wanajua wao.

Kilichowaudhi? Hotuba ndefu iliyomaliza muda wote aliokuwa amepangiwa Rais Kikwete kuzungumza na Watanzania. Badala ya kuzungumza nao, akawahutubia. Hilo liliwaudhi Watanzania waliokuwapo. Hotuba ya dakika 90 ya nini?

Wakosoaji wake wanadai alifanya hivyo ili kukwepa maswali. Na kweli, hakuna Mtanzania aliyeuliza swali. Alipomaliza kuzungumza, akasema muda wake umekwisha, na kwamba wenyeji wake walikuwa wamempangia ratiba nyingine ya kukutana na Waziri anayeshugulika na masuala ya Afrika.

Alijua wana maswali – na ndiyo maana wanasema aliyakwepa. Maana aliwaaambia kuwa wenye maswali wayatunze hadi tarehe 17 Februari 2007 atakaporejea Uingereza kwa ziara nyingine yenye ratiba nafuu. Kikwete huyo! Akaondoka ukumbini, kwenda katika kikao hicho cha kikazi.

Watanzania walisikitika baadaye walipogundua – baada ya muda mfupi – kuwa hakwenda kukutana na waziri huyo, bali alikua katika mechi ya soka kati ya Tottenham Hotspurs na Newcastle. Walisikitika!

Licha ya baadhi ya wapenzi wake, ubalozini na nje ya ubalozi, kutetea kitendo hicho cha rais Kikwete, wakisema asingeacha kwenda kwa kuwa alikuwa amepangiwa na wenyeji wake; wakosoaji wamekuwa wakisema – hadi leo- kwamba wenyeji wa rais hawampangii rais kwenda kwenye starehe ambazo hajaziomba au hajaziafiki.

Wanasema ana haki ya kufurahi kama binadamu wengine, hasa kwa kuwa yeye anajulikana ni mpenzi wa soka. Lakini si soka lililomleta Uingereza. Na alipewa fursa ya kuchagua kati ya kuwa na Watanzania kwa walau dakika nyingine 15 ili wamhoji maswali, yeye alichagua mpira!

Ilisikika baadaye kuwa kesho yake alipata fursa ya kujumuika kwa muda wa kutosha na wana CCM waishio London. Alijua hawa wasingekuwa na maswali muhimu bali nyimbo na tenzi. Maana kwao, yanapofika matendo, CCM kwanza, Tanzania baadaye!

Ikumbukwe kuwa wananchi hao waliokusanyika pale walitoka sehemu mbalimbali za Uingereza. Si wote wanaoishi London. Rais angekwenda uwanjani, lakini angewapa muda wa kuzungumza naye na kumuuliza maswali. Alikuwa na uwezo wa kutoa hotuba fupi. Aliirefusha kama mkakati wa kuwakimbia. Na baadhi yao bado wanahoji. Alitaka kuficha nini? Au kuna uhusiano na hili sakata la rada? Maana ni wiki hiyo hiyo limezuka akiwa London.

Alipohojiwa na vyombo vya habari vya huku, Rais wetu akaonyesha ushabiki wa ununuzi huo wa rada. Anasema ilikuwa ya lazima. Lugha ile ile ya mawaziri wetu Bungeni! Akazungumzia kukerwa na bei ya rada hiyo. Hakukerwa na ‘dili’ ya ununuzi wake. Hakukerwa na taarifa za rushwa. Walau hakuonyesha kukerwa.

Sasa, baadhi ya hao aliowakimbia London, wanahoji. Rais wetu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati rada inanunuliwa, alichangiaje katika upatikanaji wa ‘dili’ hiyo? Alipata nini?

Kwa nini asichunguzwe sambamba na rais aliyekuwapo; mwanasheria mkuu wa serikali aliyekuwapo; gavana wa benki kuu; waziri wa fedha; waziri wa mawasiliano na uchukuzi; maofisa wa juu jeshini; na wengine wanaohisiwa kuhusika, ama moja kwa moja au kwa mzunguko?

Maswali haya yanaulizwa miongoni mwa Watanzana huku Uingereza, na kituo kimojawapo cha redio ya kwenye mtandao wa kompyuta kilichopo Marekani kimerusha kipindi kirefu kuhusu sakata hilo.

Sasa kinachojadiliwa pia ni kulindana kunakojitokeza ndani ya serikali yetu. Mnyororo wa uhusiano kati ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa na hii ya nne ya Kikwete, hauwezi kuleta manufaa kwa Wanzania. Unamnyima rais ujasiri wa kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa. Anaogopa asichukue hatua ambayo ikichunguzwa, naye atahusishwa kwa kuwa alishiriki katika ngazi fulani.

Mashabiki na wapenzi wa Kikwete wanaona sakata hili la rada linamgusa Mkapa. Wanataka wananchi na dunia nzima imwangalie Mkapa na watu wake. Wanasahau kwamba wakiitwa watu wake, Kikwete atakuwamo. Bado wana imani kwamba Kikwete anaweza kuwachukuliwa hatua wakubwa walioshiriki.

Wanakumbuka, na bado wanaamini kauli zilizokuwa zinasambazwa na wanamtandao, kwamba wanataka kuwaondoa wazee hawa – tena baadhi yao waliwaita “hii mijitu” – ili kujenga Tanzania mpya. Wanaona Kikwete na washirika wake wa sasa wana nguvu za kuchukua hatua nzito na kurejesha heshima ya serikali, na kukinusuru CCM kutoka kwenye shutuma za kuwa Chama Cha Majambazi. Watanzania hawa wanawaamini viongozi wetu wa sasa.

Mimi nasema, “ndiyo tunawaamini, lakini wanaaminika? Wanajiaminisha? Wanaamini kwamba Tanzania yenye neema inawezekana. Nami naamini hivyo, lakini nauliza, “itawezekana chini ya mfumo huu na kwa utaratibu huu?” Baadhi yao wanaamini kwamba Kikwete anaweza kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Nami nayataka; nayatamani maisha hayo. Ila sioni kama yanakuja. Sioni maandalizi. Sioni tofauti, bali marudio. Wapo walioamini kauli za wanamtandao, waliojiaminisha kwa Watanzania kwa ‘kumkandia’ Mkapa; na kwamba muarobaini wa matatizo ya Watanzania ni Kikwete. Leo wana jeuri ya kusema hivyo?

Kikwete ninayemuona ni huyu. Ni Mkapa mwingine katika sura tofauti. Na Kwa kuwa alijipatia umaarufu kwa kujitofautisha na akina Mkapa jukwaani, ajue kwamba hawezi kukubalika zaidi na kuaminika kwa Watanzania hadi hapo atakapojitofautisha kwa vitendo. Kikwete wetu amevaa ngozi ya Mkapa. Si aivue tumwone shujaa?

Uchambuzi huu umechapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28. 01. 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu +447828696142 na barua pepe ansbertn@yahoo.com.

Shilpa aliyebaguliwa aibuka mshindi Big Brother UK


Unamjua Shilpa Shetty, mwigizaji maarufu wa Bollywood ya India? Mtazame hapo pichani kushoto. Ndiye mshindi wa mwaka 2007 wa Big Brother, Uingereza. Baada ya masaibu yaliyomkuta, sasa ameibuka kidedea. Soma habari zake HAPA.

Sunday, January 28, 2007

Karume ndiye mwenye ufunguo Zanzibar


Na Ndimara Tegambwage

ZANZIBAR yaweza kuwa chimbuko jingine la “kuchafuka kwa hali ya hewa kisiasa,” ambako kulimfukuzisha urais, Aboud Jumbe.
Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa anataka kumaliza kile anachokiita “mpasuko” wa kisiasa katika visiwa ya Unguja na Pemba na kwamba hataki mwanachama yeyote wa chama chake, CCM awe kikwazo.
Hili ni kama apizo. Kwanza Rais Kikwete amesema na kurudia kwamba amedhamiria kumaliza “tatizo la Zanzibar.” Lakini katika apizo anasema hataki mtu yeyote kumchafulia.
Amesema atakayejiingiza na kujaribu kuzuia juhudi za kuleta ufumbuzi, atafukuzwa uanachama wa CCM. Si kawaida kwa rais kutumia vitisho vya aina hiyo katika suala linalohusu utatuzi wa mgogoro.
Kikwete alisema kama rais, lakini amevaa kofia ya mwenyekiti pia wa CCM. Je, inawezekana ni uenyekiti wake unaofanya atishie kumvua mtu uanachama au kuna jambo la nyongeza? Je, wenye nafasi ya kutibua ufumbuzi ni wale wa CCM peke yao?
Je, inawezekana rais au mwenyekiti wa CCM amegundua kuwa mpasuko wa Zanzibar umeletwa na kulelewa na viongozi wa CCM au wanachama wake, na si wananchi kwa ujumla au wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi – CUF? Kwa nini rais atishie kumvua uanachama, mtu au tuseme kiongozi yeyote wa CCM?
Kwa kuzingatia hali ya Zanzibar, ufunguo wa mgogoro ulioghubika nchi hiyo, ni Rais Aman Karume. Kulainika kwake kunaweza kufanya mgogoro uyeyuke na kukamia kwake kunaweza kufanya hata juhudi za Rais Kikwete kukwama.
Mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya CCM na CUF, yakiongozwa na makatibu wake wakuu, Yusufu Makamba na Maalim Seif, ni hatua ya kukamilisha kile ambacho Rais Kikwete ameishaandaa.
Bila shaka Kikwete atakuwa ameandaa kwa ushirikiano na Rais Karume. Vinginevyo ameandaa na wahasimu wa Karume ndani ya CCM na huko huko visiwani. Hili linajitokeza katika sura mbili.
Kwanza, ni ukaidi wa CUF kwamba hata sasa hawatambui ushindi wa Karume na hawako tayari kuingia katika muwafaka wa tatu. Hili linaonyesha CUF wanaweza kuwa wameona mzani unaelemea upande upi na wanataka kutumia karata yao kufanikisha majadiliano ya sasa.
Kwani Karume, kama Rais Mstaafu, Salmin Amour, hajatimiza matakwa yote ya muwafaka wa pili kati ya CCM na CUF na huenda akatoka madarakani bila kuutekeleza wote.
Pili, ni jinsi Yusufu Makamba alivyokwenda Zanzibar. Katika mazingira ambayo inasemekana Naibu Katibu Mkuu wake, Salehe Ramadhani Feruzi “alimkimbia,” bila shaka kuna mambo ambayo hayaendi sawa katika mpangilio wa kumaliza mpasuko.
Feruzi, pamoja na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, ni miongoni mwa marafiki wakubwa wa Rais Karume. Kutokuwepo kumlaki Makamba, uwanja wa ndege na ofisini, kunaashiria upinzani, aghalabu wa chinichini, wa kile ambacho Makamba na Kikwete wanajaribu kunadi.
Habari zisizothibitishwa zinasema pamoja na ujumbe wa Makamba kwa viongozi wa CCM Zanzibar na CUF, alibeba pia vitisho vingi kwa Rais Karume, zikiwemo shutuma hapa na pale, ili kumlainisha na kuzuia upinzani kwa hoja za Kikwete.
Hata hivyo, hiyo ni hali iliyotegemewa. Karume hawezi kukubali haraka kufanya kazi na mahasimu wake; lakini hawezi kuasi uamuzi wa chama chake. Yote mawili ni shubiri kooni.
Rais Kikwete anajua yote haya mawili. Anajua hali inayomkabili Karume ikiwa ni pamoja na upinzani mkubwa ndani ya CCM kutoka kwa waliokuwa wakimuunga mkono au walioshindana naye kuwania uteuzi wa kugombea urais mwaka 2005.
Katika hali hii, nani, kama si Rais Karume, ambaye Kikwete alimlenga, pale alipotishia kwamba atakayekuwa kizingiti katika kuleta ufumbuzi atafukuzwa uanachama CCM?
Kwani uanachama wa CCM unawauma sana viongozi na “wakubwa” wengine, ambao huweza kupoteza nafasi zao za uongozi, hata urais wa Karume, kuliko wanachama wa kawaida.
Wachunguzi wa siasa za CCM wanasema kilichompata Jumbe kinaweza kumpata Karume iwapo atakaidi mapendekezo ya Kikwete. Kwanza kwa kutangaza hali ya kuchafuka kwa siasa, ambazo hakika zilichafuka tangu zamani, na pili kutafuta njia ya kumweka kando kupitia Dodoma.
Rais Aman Karume alipigiwa kampeni kubwa Dodoma na Kikwete na wenzake, mwaka 2000 kwa tiketi ya vijana. Vikao vyote vya juu ya CCM vilizizima kwa kampeni za “kijana Zanzibar” na kwamba chaguo pekee alikuwa Aman Karume.
Leo hii, wakati Rais Kikwete anataka kuondoa kile alichoita mpasuko Zanzibar, si tu anahitaji, bali pia analazimika kupata, ushirikiano wa “ndugu yake katika siasa za ujana za 2000.
Lakini iwapo ushirikiano hautapatikana, na iwapo Kikwete na Karume hawatakuwa na msimamo mmoja, uwezekano wa Kikwete kumtosa Karume, tena pale Dodoma, kupitia vikao vya CCM, uko wazi kabisa.
Wachambuzi wa siasa wanauliza iwapo Kikwete anaweza kumtosa Karume ili kumaliza mgogoro, ambao kumalizika kwake kunaweza kuondoa CCM madarakani huko Zanzibar na huenda kuwa njia pekee ya kuimarisha upinzani Tanzania bara.
Kwa kila hali, na hata bila kuanza kwa majadiliano ya kina, mwenye uwezo wa kuleta ufumbuzi wa haraka Zanzibar ni Rais Aman Karume. Huo ndio ufunguo.
Kinyume cha hayo, Kikwete ana uwezo, kupitia Dodoma, kuweka mazingira yatakayozaa shutuma na hata kashfa, na hatimaye kujiuzulu au kufukuzwa kwa Karume katikati ya vilio na aibu. Lakini yote kwa faida ya nani?
Kuchafuka au kutochafuka kwa siasa; kufukuzwa au kujiuzulu kwa Karume; jawabu sahihi kwa mgogoro wa Zanzibar ni kuheshimu kauli ya umma. Kuacha kuchezea maamuzi ya wananchi katika sanduku la kura.
Uadilifu ukitinga, haki ikatendeka, aliyeshinda ataingia ikulu; aliyeshindwa atasubiri wakati wake bila kelele wala mikwaruzo.

ndimara@yahoo.com

Sheria ikichelewa wananchi wafanyeje?


Na Ndimara Tegambwage

JESHI la polisi limedhihirisha kwamba sheria iko nyuma kuliko mahitaji na matakwa ya wananchi. Hii ni katika matumizi ya pikipiki kwa ajili ya usafirishaji abiria kibiashara.
Wiki iliyopita, Kamishna Msaidizi wa Polisi. Esaka Mugasa, aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi imepiga marufuku matumizi ya pikipiki kubeba abiria kibiashara.
Amesema wanaotaka kufanya biashara ya kubeba abiria kwa kutumia pikipiki, wasubiri hadi sheria iliyopo itakapobadilishwa na kuruhusu usafirishaji wa aina hiyo kibiashara.
Harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba pikipiki zitaendelea kubeba abiria lakini walio nazo wasionekane wanatoza nauli. Labda wasionekane kukaa foleni wakisubiri wateja. Labda wasiwe na “vijiwe” maalum wanapoegesha kusubiri abiria.
Vinginevyo si rahisi kuzuia mtu kusimamisha pikipiki, kusema anakokwenda na majadiliano juu ya gharama yakafanyika wakati wakiondoka. Si rahisi pia kuwaambia wananchi wenye kuhitaji usafiri kuacha kutumia pikipiki wakati hakuna usafiri mbadala.
Muhimu hapa ni: Sheria inabadilika lini? Nani anataka sheria hiyo ibadilike? Nani atahakikisha inabadilishwa mapema au haraka ili kukidhi mahitaji ya wenye pikipiki na wanaohitaji usafiri? Nani anajali?
Kamishna Mugasa anasema pikipiki zinazozuiwa kubeba abiria ni zile zenye magurudumu mawili na zile zenye magurudumu matatu ambazo zinajulikana kama “bajaji.”
Usafirishaji abiria kibiashara kwa kutumia pikipiki una umri wa zaidi ya miaka 10 katika sehemu mbalimbali nchini. Mjini Bukoba, walianza vijana wawili waliochochewa na biashara hiyo inavyoendeshwa jijini Kampala, Uganda.
Haikutokana na wingi wa pikipiki. Pikipiki nyingi zimenunuliwa baada ya vijana kuona kwamba ni ajira yenye uhakika, na imesaidia kuinua kipato chao binafsi na kaya zao.
Mugasa anaongelea pikipiki; chombo cha moto. Lakini kuna baisikeli; chombo cha “nguvu ya nyonga.” Chombo hiki pia kiliwahi kushambuliwa na polisi na watendaji katika serikali za mitaa.
Sasa tujadili: Nikiwa mjini Bukoba, niliona mwanaume wa umri upatao miaka 30 akiwa na baisikeli, na kwenye baisikeli hiyo amefunga maiti ya mtoto wa kaka yake aliyefia hospitali kuu ya mkoa. Alikuwa akienda kilometa 18 nje ya mji.
Samson Katalibawa hayupo peke yake. Wengine wanabeba wagonjwa na maiti kwenye baisikeli. Wanabeba wafiwa na wanabeba majeneza. Wanabeba ndugu na marafiki zao. Wanabeba mizigo. Ni mchanganyiko wa biashara na huduma ya bure.
Samson Katalibawa alibeba maiti kwenye baisikeli kwa kuwa familia yao haikuwa na fedha za kukodi gari. Hapa ni lazima watumie akili kukabiliana na mazingira yaliyopo.
Ni hali hiyohiyo ambayo imefanya watu wabuni matumizi ya pikipiki yenye magurudumu mawili. Ni ubunifu huohuo uliofanya watu wabuni ujenzi wa bodi ya pikipiki yenye magurudumu matatu.
Na hapa si ubunifu tu. Hoja kuu ni mahitaji kwanza. Kunakuwa na haja ya usafiri. Usafiri uliopo unakuwa hautoshi lakini pia, ghali. Watu wengi wanataabika sana. Inajitokeza haja ya kubuni kitu kipya kitakachokidhi mahitaji ya wanaohangaika.
Ndipo unaona bajaji. Hizi bajaji, nyumbani kwao ni India, nchi yenye watu wapatao bilioni moja na milioni mia moja au mbili (1.2 bilioni). Bajaji inabeba watu wawili nyuma na dreva. Bado mnaweza kujibana na kuingia watatu, pale usafiri unapokuwa mgumu sana.
Sasa polisi hawataki pikipiki ya magurudumu mawili na bajaji, kubeba abiria kibiashara. Wanasema wasubiri sheria ibadilishwe ndipo waanze biashara.
Kwa sasa wenye vyombo hivyo, na hata baisikeli, wanaweza “kufa kwa muda,” kutokana na njaa inayowakabili, na “kufufuka” pale sheria itakapokuwa imetungwa na kuwaruhusu kufanya biashara na kuweza kuishi na kujitafutia maisha.
Tunachokiona hapa ni polisi kutumia sheria ya matajiri kuua masikini. Kama huna usafiri binafsi au huna nauli inayotozwa katika magari, basi huna haki ya kusafiri kwa chombo chochote isipokuwa miguu.
Hii yaweza pia kuwa makusudi; kwamba miongoni mwa wenye mabasi na magari madogo ya taxi, ni maofisa wa polisi na viongozi wa kisiasa ambao wanaona ushindani utakuwa mkubwa na pato lao litapungua.
Inawezekana pia amri hii ikatokana na upofu unaokabili watendaji wengi nchini. Wengi wanakwenda kwa mwendo wa “sokoleke,” kwani hawana nyenzo za kuwasaidia kufikiri, isipokuwa kwa kusukumwa tu.
Nchini India, ambako ndiko nyumbani kwa bajaji, kuna usafiri ufuatao: Kuna usafiri wa ndege (tena aina mbalimbali), kuna treni, mabasi, magari madogo tunayoita taxi (saluuni na yale ya aina ya kombi).
Usafiri mwingine ni ule wa pikipiki (magurudumu mawili); kuna bajaji, baisikeli, mikokoteni inayovutwa na tembo, ng’ombe, vihongwe na wanyama wengine; kuna mikokoteni inayovutwa au kusukumwa na binadamu, kuna machela. Acha bwana! Kuna watu wanaotaka wakubebe mgongoni wapate riziki yao.
Haya mambo ya usafiri wa India, na hasa mijini, ukiyaangalia bila nyenzo, utadhani ni yale ya “dunia uwanja wa fujo.” Sivyo. Na kama tutakubali kuwa dunia ni uwanja wa fujo, basi ni fujo hiyo ya walionacho, inayosababisha mazingira magumu na umuhimu wa kila mmoja kutafuta bila kusubiri ajira ya rais.
Hali hiyo haiko India peke yake. Nchi zote za Asia zina mitindo hiyo ya usafiri, na serikali na polisi wake, hawaingilii ili kutibua na hatimaye kuleta karaha na vifo kutokana na ghadhabu na njaa.
Mitindo hiyo iko pia katika nchi za Amerika Kusini. Mitindo hiyo imeanzishwa Afrika kwa kasi. Hii haina maana kwamba ndiyo maendeleo. Hapana. Ni mitindo inayodhihirisha mifumo ya uchumi katika nchi hizo.
Wakati rais ananunua ndege isiyoweza kutua kwenye uwanja wenye vumbi, watu wake wanabeba maiti kwenye baisikeli. Huo ndio mfumo wa Tanzania. Upe jina unalotaka.
Kuna utajiri wa kisambe, wizi wa kimasomaso na umasikini uliokithiri. Katika hali hii inazuka mifumo ya usafiri kama ilivyo kwa mifumo mingine ya kujisetiri au kijikimu.
Tatizo hapa ni kwamba, watawala na polisi wao, wanaingilia na kusema, hata huko katika kujikimu, katika njia binafsi ambazo masikini wamejiundia ili wasife leo, sharti wafuate sheria za wenye-nacho au waache njia zao za kujikimu mpaka hapo sheria itakapozitambua.
Hatua hii inaharakisha kifo cha masikini. Inaziba mifereji ya kufikiri na fursa za ubunifu. Watawala wanaoheshimu watu wao, hutafuta njia mbadala na kuziba mfereji wa uhai kwa kisingizio cha sheria.Hapa ndipo tunasema, sheria ikichelewa, wananchi waendelee; sheria itawakuta njiani na kuhalalisha wanachofanya. Na hiyo ni kama ni lazima. Basi!

Friday, January 26, 2007

Ndesamburo: Taarifa ndiyo silaha ya rushwa


Mahojiano kati ya Mheshimiwa Philemon NDESAMBURO, Mbunge wa Moshi Mjini na mwandishi wa habari Ndimara Tegambwage, siku 10 baada ya Ndesamburo kujiuzulu kutoka Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka, hapo 10 Januari 2007. Ndesamburo alijiuzulu kutokana na madai kwamba wabunge wamehongwa katika suala la madai ya Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi dhidi ya Adam Kighoma Malima, Mbunge wa Mkuranga, Pwani. Sababu nyingine aliyotoa ni kwamba utawala (executive) unaingilia Bunge.


Swali: Wakati ukiongea na waandishi wa habari juu ya kujiuzulu kwako, ulisema kwamba una umri mkubwa, zaidi ya miaka 70. Je, kwa umri huu bado unaweza kushiriki mapambano dhidi ya rushwa?
Jibu: Nani amekwambia kuwa umri ni kikwazo? Niliwaambia waandishi wa habari kwamba hata nikifa, nimeishazidi miaka 70. Basi. Ni umri mkubwa lakini siyo kwamba sina uwezo wa kuchukua maamuzi; tena hapa ndipo nastahili kuwa jasiri zaidi katika kukataa rushwa au tendo lolote la kifisadi.
Kupambana na rushwa, kwanza ni dhamira, na pili, ni hatua mahsusi za kukataa kutoa au kupokea rushwa; kukataa kuhusishwa na rushwa na kufanya kila unaloweza kuzuia kitendo cha rushwa. Hapa suala la umri linatoka wapi?
Swali: Bado niko kwenye umri. Nasema ungeanza mapema harakati hizi. Siyo leo. Na kwa msingi huo hakutakuwepo wa kuziendeleza kwani umri wako sasa ni mkubwa.
Jibu
: Kupambana kunahitaji kuanzia pale ulipo. Kuanzia pale ulipopata fursa. Nasema suala la uzee haliingii hapa. Wenye umri mkubwa watafanya kile wanachoweza kwa wakati wao. Wataachia wengine wanaowafuata na vizazi vingine.
Hata hivyo, siyo mimi niliyeanzisha mapambano dhidi ya rushwa. Wananchi wengi hawataki rushwa. Kuna asasi mbalimbali ambazo zimekuwa zikipambana na rushwa. Zilianza zamani. Mimi sikuanzisha chochote. Nilisema kuna madai kwamba wabunge wamehongwa. Madai yenye shina katika ofisi kubwa ya serikali – Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa kuwa nami nilikuwa mmoja wa wanaoshughulikia shauri muhimu katika Kamati, nikasema sikupokea rushwa, na kwa msingi huo, hata kama wenzangu watakaa kimya, mimi siwezi kubaki kwenye Kamati na kuyapa nguvu madai ya rushwa. Nikajiuzulu.
Swali: Lakini hayo yalikuwa madai tu. Kwa nini usingesubiri uthibitisho?
Jibu:
Uthibitisho kutoka kwa nani? Unataka kuleta mambo ya rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Alikuwa akisema kwamba wanaomtuhumu mtu kula rushwa sharti waje na uthibitisho. Nakwambia, kwa utaratibu huo, hutakamata mtu. Tuhuma peke yake ni msingi wa kutosha wa kufanyia uchunguzi. Sasa kama hutaki hata kufanya uchunguzi, ina maana unaneemesha rushwa, hata kama hukupokea rushwa.
Katika suala langu hili, msingi mkubwa ni kwamba aliyesema kuna rushwa ni Waziri Mkuu. Huyu ni mtu mzima. Hawezi kuchomoka na kusema tu. Lazima awe na uhakika. Ni kiongozi katika serikali inayosema inapambana na rushwa na imeamua kwamba, hata ushahidi wa kimazingira ni muhimu katika kukabiliana na rushwa. Kwa hiyo, siyo sahihi kupuuza kauli ya Waziri Mkuu. Siyo sahihi kukataa kufanya uchunguzi. Siyo sahihi kuendelea kuwa katika Kamati ambayo hata Waziri Mkuu anajua wajumbe wake wametuhumiwa kula rushwa.
Swali: Sasa unadhani vita hii unayochochea ukiwa uzeeni itasimamiwa na nani?
Jibu
: Nimekwambia kuna asasi nyingi zinazopambana na rushwa. Kuna taratibu kadhaa za serikali zikiwa pamoja na sheria mpya inayopelekwa bungeni hivi karibuni. Sijasema nimejitwisha jukumu lote. Mimi naitikia pale nilipo; na wewe na mwingine afanye vivyo hivyo huko alipo. Ni jukumu la kila mmoja. Bali kuna kitu kimoja muhimu. Nacho ni hiki:
Kuna haja ya kuweka kwenye mitaala ya shule za msingi hadi vyuo vya juu, mafunzo juu ya rushwa. Wajue rushwa ni nini? Aina za rushwa. Mifumo ya rushwa. Nani wanadai rushwa, nani wanatoa rushwa na nani wanapokea rushwa. Kwa nini kuna rushwa? Mazingira gani yanarutubisha rushwa? Madhara ya rushwa kwa mtu, jamii na utawala.
Haya ni muhimu kujulikana kwa kila mmoja, tangu utotoni, ili kuandaa jeshi kubwa la kupambana na rushwa. Ukianzia darasa la nne unajua rushwa ni nini na ukajenga chuki dhidi ya rushwa, utakulia katika mapambano ya kweli ya kuondoa kansa hii.
Hapa utakuwa umewapa watoto na vijana, pamoja na jamii kwa ujumla, misingi ya kukataa kufanyiwa vitendo vya rushwa. Chuki itazaa ujasiri na watapinga rushwa.
Swali: Lakini hiyo itamaliza
Jibu: Sikiliza kwanza. Fikiria hali hii. Mtoto akue akijua kwamba rushwa inamkosesha au inampunguzia huduma za kijamii; inamwondolea haki ya kutoa mawazo na kushiriki kikamilifu katika jamii; inadhoofisha utawala; inajenga mazingira ya mifarakano na hatimaye chuki na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Huyo mtoto atakuwa imara sana katika mapambano dhidi ya rushwa. Ni vema elimu hii ianze mapema.
Nazungumzia elimu inayoweza kusaidia kuonyesha uhusiano kati ya uduni wa maisha ya wananchi na mabilioni ya fedha yanayochukuliwa kwa njia ya mikataba feki au katili. Uhusiano kati ya ukosefu wa elimu na wizi wa mali ya umma. Uhusiano kati ya kushamiri kwa ghafla kwa biashara mbalimbali, ikiwa pamoja na biashara ya madawa ya kulevya (mihadarati), na fedha haramu ambazo hazitoki kwenye mzunguko halali na wa kawaida wa fedha katika nchi.
Ulitaka kuuliza iwapo hatua hizi zitamaliza rushwa? Sizungumzii kumaliza. Nazungumzia kuzuia na kupunguza. Hatua hizi zitakuwa zimepunguza rushwa kwa kiasi kikubwa na zimejenga msingi mkubwa wa kuchukia na kupambana na rushwa.
Swali: Kuna madai ya kupokea rushwa katika mikataba mingi nchini. Mbona hujajiuzulu ubunge kwa tuhuma hizo?
Jibu:
Sijaona popote ambako Bunge, kwa ujumla wake limehusika katika kupitisha mikataba yenye rushwa ndani yake. Hakuna tuhuma dhidi ya Bunge. Bali kuna matakwa ya wabunge na Kamati za Bunge ya kutaka kujua undani wa mikataba iliyoingiwa na serikali. Haya ni matakwa sahihi.
Swali: Ikitokea zikaletwa tuhuma kwamba Bunge zima limehongwa ili lipitishe muswada au mkataba fulani, utajiuzulu ubunge ili kulinda uadilifu wako binafsi? Je, hiyo itakuwa imemsaidia nani?
Jibu
: Labda nianze na hilo la pili, kwamba nikijiuzulu nitakuwa nimemsaidia nani. Na mimi nauliza: Je, nikibaki mbunge na kushiriki ufisadi, nitakuwa namsaidia nani? Hakuna ninayemsaidia. Ninanyonga kila mtu; kila mwananchi.
Lakini hebu turudi kwenye swali la msingi. Siyo rahisi kuhonga Bunge zima. Ni rahisi kuhonga watu wachache ambao watatumia nafasi zao kushawishi wabunge wengine, na bila kuwaambia ukweli wote kuhusu mradi wa ufisadi. Nasubiri kupinga hilo kama litatokea, na kama nitapata taarifa. Mimi siyo mtu wa kutumika hivihivi.
Unafahamu ndugu yangu, hatua zozote ambazo mbunge atatumia, ikiwa ni pamoja na kujiuzulu, ni nyenzo tu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi, watawala na dunia nzima. Ni ushahidi wa kukataa kuwa sehemu ya ufisadi. Sasa ngoja niseme: Nasema nikigundua kuna ufisadi, nitajiuzulu. Na hii haitakuwa kwa uadilifu wa binafsi, bali kwa uadilifu wa wote wasiotaka rushwa; wasioamini katika rushwa na wanaopinga ufisadi.
Kitu muhimu hapa ni kutambua kuwa Bunge ni chombo cha wananchi cha uwakilishi. Kina nafasi yake kama nguzo mojawapo ya dola. Kina hadhi yake inayotokana na ridhaa ya wananchi waliotupeleka humo. Hivyo ni sahihi kabisa kulinda hadhi yake ili kiendelee kuheshimika na kufanya kazi zake.
Kwa hiyo ninapojiuzulu, kama nilivyofanya, kutoka kwenye Kamati, nimelinda haki za bunge. Nimelinda hadhi na heshima yake. Nilifanya hivyo, pamoja na sababu nilizotaja hapo awali, ili kuendelea kulipa Bunge heshima linayostahili.
Swali: Kuna taarifa kwamba madai ya Mbunge Adam Kighoma Malima hayakuwa na hadhi ya kusikilizwa na Bunge bali mahakama; maana anadai kukashifiwa. Hilo mliliona kabla hujajiuzulu?
Jibu
: Sasa hayo ni mambo ya kumuuliza Spika, Mheshimiwa Samuel Sitta. Siyo mimi. Au jaribu kwa wajumbe wengine. Ninachojua ni kwamba kuna utaratibu wa kufanya kazi katika Kamati, na mwisho wa kazi kila kitu kitawekwa wazi. Bali kunapotokea kikwazo cha kufanya kazi mliyopewa, ndipo unashughulikia kikwazo; kama nilivyofanya.
Swali: Lakini mimi najua kwamba Kamati haina uwezo wa kushughulikia kashfa na kama waliita wataalam wa kuwasaidia watakuwa waliwaambia hilo.
Jibu: Kama unajua hivyo, basi unajua hivyo. Mimi siwezi kukuzuia kujua unavyojua.
Swali: Lakini unakubaliana nami kuwa hivyo ndivyo ilivyo?
Jibu
: Kwa nini unataka nikubaliane na wewe?
Swali: Nataka kujua kama umenielewa na unakubaliana nami au una uelewa tofauti. Hili ni suala la kisheria na wewe ni mtunga sheria.
Jibu: Nakumbuka ulipotaka kunihoji uliniambia kwamba utashughulikia suala la kujiuzulu kwangu kutoka kwenye Kamati. Na katika kujiuzulu kwangu hakuna popote ninapojadili mambo ya ndani ya Kamati. Nadhani hilo swali siyo mahali pake hapa. Hata hivyo nina mawazo binafsi juu ya mambo mengi, siyo hilo peke yake.
Swali: Kamati haikuwaita Waziri Mkuu Edward Lowassa wala Reginald Mengi, watu muhimu katika madai yako…
Jibu: Siyo hivyo. Kamati haikuzingatia maelezo yangu kuhusu madai ya rushwa. Haikuyashughulikia. Ingeyashughulikia, lazima watu hao wawili wangehojiwa; popote pale walipo.
Swali: Unataka kusema, kwa kufanya hivyo, Kamati haikulinda hadhi ya Bunge?
Jibu: Nasema haikulishughulikia. Wewe na yeyote yule, mnaweza kujazia hapo. Kama haikulishughulikia, basi ilifanyaje?
Swali: Haikulinda hadhi ya bunge.
Jibu:
Huyo ni wewe. Muulize na mwingine. Mimi sina hukumu kwa yeyote. Nasema baada ya tuhuma kwamba wabunge wamehongwa, dhamira yangu iliniongoza katika kutaarifu wenzangu; na kulipokuwa na kusita, nikajiondoa kwenye Kamati. Basi.
Swali: Ili watu waweze kuchukia na kupinga rushwa, wanahitaji taarifa. Wanahitaji kujua serikali inafanya nini na wapi; imefanyaje hayo inayoyafanya. Kama serikali haikubali kutoa taarifa, je, wananchi watawezaje kupinga rushwa?
Jibu
: Hilo siyo katika rushwa peke yake. Ni katika mwenendo mzima wa serikali na idara zake. Wananchi wanahitaji kujua serikali inafanya nini. Wananchi wanapaswa kuwa wasimamizi wa serikali yao kupitia bunge na asasi za kijamii. Kama wananchi watakuwa hawapati taarifa kamili na sahihi juu ya utendaji wa serikali, basi hawawezi kuisimamia, kama vile ambavyo hawawezi kuiwajibisha.
Suala la kupatikana kwa taarifa za utendaji wa serikali ni muhimu sana. Bila taarifa huwezi kuhoji; huwezi kupendekeza; huwezi kukataa kitu bila kukielewa; huwezi kuunga mkono chochote. Sharti upate taarifa. Hivi sasa kuna sauti nyingi juu ya mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari. Nadhani kilio chao ni hicho. Wanataka vyombo vya habari na wananchi wapate taarifa ili waweze kuisimamia vizuri serikali. Kinyume cha hayo hawatakuwa na mchango wowote katika usimamizi.
Lakini hili linahusu rushwa pia. Bila taarifa juu ya mapato ya serikali na juu ya mifumo ya bajeti na matumizi ya serikali, rushwa itakaa pembeni ikichekelea kwa kuwa wengi hawajui kinachotendeka.
Iwapo wananchi, ambao ni wasimamizi wakuu wa serikali yao, watabaki gizani, juu ya sera na mipango ya serikali katika maeneo yote, basi hawataweza kuihoji serikali. Hawataisimamia. Lakini vilevile hawataweza kuipongeza kwa kazi nzuri hapa na pale, kwa kuwa hawana taarifa.
Nakubaliana nawe kwamba serikali inapaswa kuweka wazi taarifa zake. Bila uwazi rushwa itaota mizizi. Ukosefu wa taarifa juu ya mwenendo wa serikali na watendaji wake; na ukosefu wa taarifa juu ya mikataba kati ya serikali na makampuni na mashirika ya ndani na nje, huchochea rushwa kwa kiwango kikubwa.
Rushwa hufanyika gizani, kwenye uficho, pembeni. Hata kama itakuja kujulikana baadaye, wahusika hukutana na kupeana gizani. Kwa hiyo, kama hakuna uwazi juu ya mikataba, juu ya mapato ya serikali kutokana na madini, vito vingine vya thamani na maliasili za nchi, basi hesabu za mapato hazitafahamika kwa wananchi. Hapo ndipo rushwa itaota mizizi.
Swali: Uliwahi kupewa adhabu na Bunge kwa kile kilichoitwa “kushindwa kuthibitisha kauli” zako bungeni. Leo, baada ya kujiuzulu kutoka kwenye Kamati, kuna walioanza kukushutumu kwa kile wanachoita “kuingiza siasa” bungeni. Unahusishaje matukio haya mawili?
Jibu: Sikiliza bwana. Haya mawili hayana uhusiano bali yote yamenikuta Ndesamburo. Lile la Bunge la 2000-2005 nililithibitisha. Sema hawakukubaliana nami. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alihutubia mikutano mjini Moshi na kuwaambia wafanyabishara, kweupe kabisa, kwamba anayetaka kufanikiwa katika bishara yake, sharti apeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hili nililithibitisha kwa kadri ya uwezo wangu; useme tu kwamba kuna waliokuwa wamelenga kumlinda Waziri Mkuu.
Sasa hili la kujiuzulu kutoka Kamati, kwanza sijui kwa nini unalirudiarudia. Lakini ni hivi: Kwanza, kudai kwamba ninapeleka siasa bungeni, ni kupotoka. Tuko pale bungeni kutokana na utaratibu wa kisiasa. Tumetokana na vyama vya siasa na mfumo maalum wa siasa.
Pili, kazi tunayofanya ni ya kisiasa. Ni siasa ambazo zinaelekeza utawala wa nchi. Ni kukwama kwa siasa ambako kutaliangamiza taifa hili. Sheria zinazotungwa sharti zielekezwe na zijibu hoja kuu ya siasa za nchi. Sasa kusema kwamba Ndesamburo anapeleka siasa bungeni, ama ni kutaka kupotosha watu au ni kutojua kwamba bungeni ndiko hasa mahali pa siasa.
Bali suala la kujiondoa kwenye Kamati halina huyu anatoka chama kipi. Ni suala la uadilifu. Mimi na wenzangu tumetuhumiwa kula rushwa. Mimi sikula rushwa. Sasa kwa nini nisionyeshe kwa vitendo kwamba sikuhongwa? Ni haki yangu.
Swali: Mwenyekiti wa Kamati, anasema ulishiriki zaidi ya asilimia 90 ya vikao, kwa hiyo maamuzi ya mwisho yanakuhusu pia. Unasemaje kuhusu hili?
Jibu: Sina sababu ya kuzozana na mwenyekiti wangu wa zamani. Anaelewa vema nilichosema kuhusu kutohusishwa. Namheshimu mwenyekiti na wajumbe wote. Bali nasema, lile hitimisho; yale maoni ya mwisho ya Kamati, na vyovyote yatakavyokuwa, ambayo yanakata shauri lililokuwa mbele ya Kamati, hakika sikushiriki na sitaki kuhusishwa.
Swali: Kama hivyo ndivyo, kwa nini hukujiuzulu mapema?
Jibu: Hapo ndipo wengine hawataki kuelewa. Nadhani ni makusudi. Na mimi nawauliza: Ni lini nilipata taarifa za wabunge kuhongwa? Unachukua hatua pale unapokuwa umepata taarifa. Kama hukupata taarifa, utachukuaje hatua? Utaendelea kama kawaida. Ukipata taarifa, unatumia taarifa hiyo. Taarifa inaweza kugeuza kabisa mkondo wa fikra na utendaji. Nilichukua hatua pale nilipoambiwa kwamba kuna madai kuwa wabunge wamepokea rushwa. Ningezipata mapema nisingeingia hata kikao cha kwanza. Basi.
Swali: Katika hali zote mbili: kuadhibiwa na Bunge na kujiuzulu; ni mambo yanayoonyesha umekuwa katika misokosuko. Je, unajisikiaje kuwa katika misukosuko ya aina hiyo?
Jibu: Sioni kama ni misukosuko. Naona ni changamoto. Hakuna kinachofanywa kwa maigizo. Kila tukio linakuja kwa njia yake na wakati wake. Nami nayakabili kwa kadri yanavyojitokeza.
Swali: Unadhani kuna wabunge wa CCM ndani na nje ya Kamati yako ya zamani ambao wanakuunga mkono katika hili la kujiondoa kwenye Kamati?
Jibu: Hiyo siyo hoja. Hoja ni kutenda kwa kuamini kwamba unachofanya ni kweli na sahihi. Kwamba unadhihirisha uadilifu wako; kile kilichoko moyoni mwako bila kujali nani anakuunga mkono. Bali naweza kusema kwa uhakika, kwamba kila mwenye nia njema na mwadilifu, ndani au nje ya Bunge, atakuwa anaunga mkono hatua niliyochukua. Je, wewe huungi mkono?

Thursday, January 25, 2007

Mjadala wa Muswada wa Habari wazidi kukua


Soma stori ya Majira kutoka Mbeya kuhusu muswada wenye utata ulioandaliwa na waziri Mohammed Seif Khatib (pichani) kunyonga uhuru wa habari Tanzania.

Mjadala wa Muswada wa Uhuru wa Habari wazidi kupamba moto

Ayub Rioba ametoka mafichoni. Amemwaga sumu hapa. Safi kabisa. Isome mwenyewe.

Monday, January 15, 2007

JK mbona unataka kuwanyonga rafiki zako?


Rais Jakaya Kikwete amekuwa akijitambulisha na kutambulishwa kama 'rafiki' wa wanahabari. Ajabu ni kwamba serikali yake inataka kudhibiti habari kijanja, kuficha 'mambo'yake. Ndiyo maana imeshirikiana na baadhi ya wadau wa habari, kuandaa muswada wa utumwa wa habari kwa kisingizio cha kutunga sheria ya uhuru wa habari. Lakini hii siyo iliyokusudiwa na wadau. Juu juu muswada unafanana na uhuru; ndani ni utumwa mtupu. Mwenzetu mmoja, akiakisi sauti za wanaharakati wengi waliogundua janja ya serikali ya Kikwete kunyonga vyombo vya habari, huku yeye akitabasamu, nao wakifurahi, amekataa. Anasema: SITAKI. Hataki nini? Soma mwenyewe; toa maoni.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'