Sunday, January 28, 2007

Sheria ikichelewa wananchi wafanyeje?


Na Ndimara Tegambwage

JESHI la polisi limedhihirisha kwamba sheria iko nyuma kuliko mahitaji na matakwa ya wananchi. Hii ni katika matumizi ya pikipiki kwa ajili ya usafirishaji abiria kibiashara.
Wiki iliyopita, Kamishna Msaidizi wa Polisi. Esaka Mugasa, aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi imepiga marufuku matumizi ya pikipiki kubeba abiria kibiashara.
Amesema wanaotaka kufanya biashara ya kubeba abiria kwa kutumia pikipiki, wasubiri hadi sheria iliyopo itakapobadilishwa na kuruhusu usafirishaji wa aina hiyo kibiashara.
Harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba pikipiki zitaendelea kubeba abiria lakini walio nazo wasionekane wanatoza nauli. Labda wasionekane kukaa foleni wakisubiri wateja. Labda wasiwe na “vijiwe” maalum wanapoegesha kusubiri abiria.
Vinginevyo si rahisi kuzuia mtu kusimamisha pikipiki, kusema anakokwenda na majadiliano juu ya gharama yakafanyika wakati wakiondoka. Si rahisi pia kuwaambia wananchi wenye kuhitaji usafiri kuacha kutumia pikipiki wakati hakuna usafiri mbadala.
Muhimu hapa ni: Sheria inabadilika lini? Nani anataka sheria hiyo ibadilike? Nani atahakikisha inabadilishwa mapema au haraka ili kukidhi mahitaji ya wenye pikipiki na wanaohitaji usafiri? Nani anajali?
Kamishna Mugasa anasema pikipiki zinazozuiwa kubeba abiria ni zile zenye magurudumu mawili na zile zenye magurudumu matatu ambazo zinajulikana kama “bajaji.”
Usafirishaji abiria kibiashara kwa kutumia pikipiki una umri wa zaidi ya miaka 10 katika sehemu mbalimbali nchini. Mjini Bukoba, walianza vijana wawili waliochochewa na biashara hiyo inavyoendeshwa jijini Kampala, Uganda.
Haikutokana na wingi wa pikipiki. Pikipiki nyingi zimenunuliwa baada ya vijana kuona kwamba ni ajira yenye uhakika, na imesaidia kuinua kipato chao binafsi na kaya zao.
Mugasa anaongelea pikipiki; chombo cha moto. Lakini kuna baisikeli; chombo cha “nguvu ya nyonga.” Chombo hiki pia kiliwahi kushambuliwa na polisi na watendaji katika serikali za mitaa.
Sasa tujadili: Nikiwa mjini Bukoba, niliona mwanaume wa umri upatao miaka 30 akiwa na baisikeli, na kwenye baisikeli hiyo amefunga maiti ya mtoto wa kaka yake aliyefia hospitali kuu ya mkoa. Alikuwa akienda kilometa 18 nje ya mji.
Samson Katalibawa hayupo peke yake. Wengine wanabeba wagonjwa na maiti kwenye baisikeli. Wanabeba wafiwa na wanabeba majeneza. Wanabeba ndugu na marafiki zao. Wanabeba mizigo. Ni mchanganyiko wa biashara na huduma ya bure.
Samson Katalibawa alibeba maiti kwenye baisikeli kwa kuwa familia yao haikuwa na fedha za kukodi gari. Hapa ni lazima watumie akili kukabiliana na mazingira yaliyopo.
Ni hali hiyohiyo ambayo imefanya watu wabuni matumizi ya pikipiki yenye magurudumu mawili. Ni ubunifu huohuo uliofanya watu wabuni ujenzi wa bodi ya pikipiki yenye magurudumu matatu.
Na hapa si ubunifu tu. Hoja kuu ni mahitaji kwanza. Kunakuwa na haja ya usafiri. Usafiri uliopo unakuwa hautoshi lakini pia, ghali. Watu wengi wanataabika sana. Inajitokeza haja ya kubuni kitu kipya kitakachokidhi mahitaji ya wanaohangaika.
Ndipo unaona bajaji. Hizi bajaji, nyumbani kwao ni India, nchi yenye watu wapatao bilioni moja na milioni mia moja au mbili (1.2 bilioni). Bajaji inabeba watu wawili nyuma na dreva. Bado mnaweza kujibana na kuingia watatu, pale usafiri unapokuwa mgumu sana.
Sasa polisi hawataki pikipiki ya magurudumu mawili na bajaji, kubeba abiria kibiashara. Wanasema wasubiri sheria ibadilishwe ndipo waanze biashara.
Kwa sasa wenye vyombo hivyo, na hata baisikeli, wanaweza “kufa kwa muda,” kutokana na njaa inayowakabili, na “kufufuka” pale sheria itakapokuwa imetungwa na kuwaruhusu kufanya biashara na kuweza kuishi na kujitafutia maisha.
Tunachokiona hapa ni polisi kutumia sheria ya matajiri kuua masikini. Kama huna usafiri binafsi au huna nauli inayotozwa katika magari, basi huna haki ya kusafiri kwa chombo chochote isipokuwa miguu.
Hii yaweza pia kuwa makusudi; kwamba miongoni mwa wenye mabasi na magari madogo ya taxi, ni maofisa wa polisi na viongozi wa kisiasa ambao wanaona ushindani utakuwa mkubwa na pato lao litapungua.
Inawezekana pia amri hii ikatokana na upofu unaokabili watendaji wengi nchini. Wengi wanakwenda kwa mwendo wa “sokoleke,” kwani hawana nyenzo za kuwasaidia kufikiri, isipokuwa kwa kusukumwa tu.
Nchini India, ambako ndiko nyumbani kwa bajaji, kuna usafiri ufuatao: Kuna usafiri wa ndege (tena aina mbalimbali), kuna treni, mabasi, magari madogo tunayoita taxi (saluuni na yale ya aina ya kombi).
Usafiri mwingine ni ule wa pikipiki (magurudumu mawili); kuna bajaji, baisikeli, mikokoteni inayovutwa na tembo, ng’ombe, vihongwe na wanyama wengine; kuna mikokoteni inayovutwa au kusukumwa na binadamu, kuna machela. Acha bwana! Kuna watu wanaotaka wakubebe mgongoni wapate riziki yao.
Haya mambo ya usafiri wa India, na hasa mijini, ukiyaangalia bila nyenzo, utadhani ni yale ya “dunia uwanja wa fujo.” Sivyo. Na kama tutakubali kuwa dunia ni uwanja wa fujo, basi ni fujo hiyo ya walionacho, inayosababisha mazingira magumu na umuhimu wa kila mmoja kutafuta bila kusubiri ajira ya rais.
Hali hiyo haiko India peke yake. Nchi zote za Asia zina mitindo hiyo ya usafiri, na serikali na polisi wake, hawaingilii ili kutibua na hatimaye kuleta karaha na vifo kutokana na ghadhabu na njaa.
Mitindo hiyo iko pia katika nchi za Amerika Kusini. Mitindo hiyo imeanzishwa Afrika kwa kasi. Hii haina maana kwamba ndiyo maendeleo. Hapana. Ni mitindo inayodhihirisha mifumo ya uchumi katika nchi hizo.
Wakati rais ananunua ndege isiyoweza kutua kwenye uwanja wenye vumbi, watu wake wanabeba maiti kwenye baisikeli. Huo ndio mfumo wa Tanzania. Upe jina unalotaka.
Kuna utajiri wa kisambe, wizi wa kimasomaso na umasikini uliokithiri. Katika hali hii inazuka mifumo ya usafiri kama ilivyo kwa mifumo mingine ya kujisetiri au kijikimu.
Tatizo hapa ni kwamba, watawala na polisi wao, wanaingilia na kusema, hata huko katika kujikimu, katika njia binafsi ambazo masikini wamejiundia ili wasife leo, sharti wafuate sheria za wenye-nacho au waache njia zao za kujikimu mpaka hapo sheria itakapozitambua.
Hatua hii inaharakisha kifo cha masikini. Inaziba mifereji ya kufikiri na fursa za ubunifu. Watawala wanaoheshimu watu wao, hutafuta njia mbadala na kuziba mfereji wa uhai kwa kisingizio cha sheria.Hapa ndipo tunasema, sheria ikichelewa, wananchi waendelee; sheria itawakuta njiani na kuhalalisha wanachofanya. Na hiyo ni kama ni lazima. Basi!

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'