Monday, January 29, 2007

Kikwete vua ngozi ya Mkapa uwe shujaa


Na Ansbert Ngurumo, Hull

TUNAMPENDA rais wetu, lakini hatupendi baadhi ya tabia zake. Ndiyo maana tunamwambia haya. Ndiyo maana namuuliza maswali. Namwandama? Hapana! Nimuulize nani?

Maana, kama ningekuwa na swali moja tu, nikaulizwa nimtaje mtu mmoja katika Tanzania nzima ambaye, ikibidi awe wa mwisho kufa – kabla yangu – ili aulizwe swali hilo, nimgemtaja rais. Ndiyo! Rais Jakaya Kikwete, chaguo la mtandao, ‘mtu wa watu,’ chaguo la mwisho la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nimeandika maneno hayo hapo juu makusudi. Kuna waliowahi kumwita ‘chaguo la Mungu.’ Wakaleta hisia za ubaguzi na mgawanyiko miongoni mwa Watanzania. Maswali yakaibuka. ‘Kama huyu ni chaguo la Mungu, wengine ni chaguo la shetani?’ Maneno kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu yalisemwa kwa mara ya kwanza na Padri mmoja pale Manzese, Dar es Salaam; anaitwa Mapunda, ‘Tunda Kanisa.’ Bila shaka aliyasema kwa ushabiki, hakutumwa na Kanisa, maana yeye si msemaji wa Kanisa.

Bahati mbaya, maneno hayo yakasingiziwa kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki! Baadaye ilijulikana kuwa kundi kubwa la maaskofu hao, na katika umoja wao bila kusema rasmi, walishatekwa na mtandao wa Kikwete, kwa jina la CCM, kumuunga mkono Kikwete. Leo baada ya mwaka mmoja na ushehe, wanajutia ushabiki wao kwa Kikwete? Ndiye huyu waliyemtarajia? Ni kweli alikuwa chaguo la Mungu au la mtandao?

Nitaeleza kidogo kwa nini nasisitiza chaguo la mtandao! Yaliyotokea ndani ya CCM tunayajua. Chama hakikuwa na chaguo, bali makundi ya wanachama na ya viongozi yalikuwa na ‘machaguo’ yao. Kikwete alikuwa wa mtandao, ambao uliyapiku makundi mengine, na baadaye kumhalalisha Kikwete kwa wana CCM wote.

Ndivyo alivyopata sifa nyingi baadaye. Hata waliokuwa hawamwamini ndani ya chama wakaongoza katika kuimba: “Nina imani na Kikwete, iya , iya, iya…Kikwete kweli….” Pole pole, akawa chaguo la mwisho la CCM. Wakamnadi kama chaguo la watu. Na waliosimamia uchaguzi wakatueleza kwamba ameshinda uchaguzi; akawa rais wetu ‘mwenye mvuto.’

Sina shaka mvuto huo bado anao. Hata juzi alipokuwa hapa nchini Uingereza kwa safari ya kikazi, alishuhudia umati wa Watanzania waliokusanyika kumlaki, kumsalimia, kuteta naye na kumuuliza maswali. Ubalozi wa Tanzania nchini hapa ulifanya maandalizi makubwa ya kuwakusanya Watanzania wengi. Walifika. Pichani kulia, Rais Kikwete akiwa na mkewe na viongozi wengine, anawahutubia Watanzania katika ukumbi wa hoteli ya Churchhill, London.

Waliokuwapo hawajaacha kusimulia badhi ya mambo yaliyojitokeza; kwamba ukumbi uliopangwa haukutosha. Viti viliongezwa. Rais mwenyewe alichelewa kwa dakika zipatazo 45 (kama alivyokuwa akifanya akiwa waziri). Baadhi wanahoji: “kumbe urais haujambadilisha?”

Wanakumbuka hotuba yake ndeeeefu (kuhusu karibu kila kitu alichofikiria kuhusu Tanzania). Wengine wanasema ilikuwa ndefu mno bila sababu. Wanakumbuka nyimbo za CCM zilizoporomoshwa ukumbini, na baadhi ya washiriki ‘waliovalishwa’ sare za chama na kupewa bendera za CCM. Aliyewapa nani? Balozi wa Tanzania nchini Uingereza! Kwani ulikuwa mkutano wa CCM? Wanajua wao.

Kilichowaudhi? Hotuba ndefu iliyomaliza muda wote aliokuwa amepangiwa Rais Kikwete kuzungumza na Watanzania. Badala ya kuzungumza nao, akawahutubia. Hilo liliwaudhi Watanzania waliokuwapo. Hotuba ya dakika 90 ya nini?

Wakosoaji wake wanadai alifanya hivyo ili kukwepa maswali. Na kweli, hakuna Mtanzania aliyeuliza swali. Alipomaliza kuzungumza, akasema muda wake umekwisha, na kwamba wenyeji wake walikuwa wamempangia ratiba nyingine ya kukutana na Waziri anayeshugulika na masuala ya Afrika.

Alijua wana maswali – na ndiyo maana wanasema aliyakwepa. Maana aliwaaambia kuwa wenye maswali wayatunze hadi tarehe 17 Februari 2007 atakaporejea Uingereza kwa ziara nyingine yenye ratiba nafuu. Kikwete huyo! Akaondoka ukumbini, kwenda katika kikao hicho cha kikazi.

Watanzania walisikitika baadaye walipogundua – baada ya muda mfupi – kuwa hakwenda kukutana na waziri huyo, bali alikua katika mechi ya soka kati ya Tottenham Hotspurs na Newcastle. Walisikitika!

Licha ya baadhi ya wapenzi wake, ubalozini na nje ya ubalozi, kutetea kitendo hicho cha rais Kikwete, wakisema asingeacha kwenda kwa kuwa alikuwa amepangiwa na wenyeji wake; wakosoaji wamekuwa wakisema – hadi leo- kwamba wenyeji wa rais hawampangii rais kwenda kwenye starehe ambazo hajaziomba au hajaziafiki.

Wanasema ana haki ya kufurahi kama binadamu wengine, hasa kwa kuwa yeye anajulikana ni mpenzi wa soka. Lakini si soka lililomleta Uingereza. Na alipewa fursa ya kuchagua kati ya kuwa na Watanzania kwa walau dakika nyingine 15 ili wamhoji maswali, yeye alichagua mpira!

Ilisikika baadaye kuwa kesho yake alipata fursa ya kujumuika kwa muda wa kutosha na wana CCM waishio London. Alijua hawa wasingekuwa na maswali muhimu bali nyimbo na tenzi. Maana kwao, yanapofika matendo, CCM kwanza, Tanzania baadaye!

Ikumbukwe kuwa wananchi hao waliokusanyika pale walitoka sehemu mbalimbali za Uingereza. Si wote wanaoishi London. Rais angekwenda uwanjani, lakini angewapa muda wa kuzungumza naye na kumuuliza maswali. Alikuwa na uwezo wa kutoa hotuba fupi. Aliirefusha kama mkakati wa kuwakimbia. Na baadhi yao bado wanahoji. Alitaka kuficha nini? Au kuna uhusiano na hili sakata la rada? Maana ni wiki hiyo hiyo limezuka akiwa London.

Alipohojiwa na vyombo vya habari vya huku, Rais wetu akaonyesha ushabiki wa ununuzi huo wa rada. Anasema ilikuwa ya lazima. Lugha ile ile ya mawaziri wetu Bungeni! Akazungumzia kukerwa na bei ya rada hiyo. Hakukerwa na ‘dili’ ya ununuzi wake. Hakukerwa na taarifa za rushwa. Walau hakuonyesha kukerwa.

Sasa, baadhi ya hao aliowakimbia London, wanahoji. Rais wetu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati rada inanunuliwa, alichangiaje katika upatikanaji wa ‘dili’ hiyo? Alipata nini?

Kwa nini asichunguzwe sambamba na rais aliyekuwapo; mwanasheria mkuu wa serikali aliyekuwapo; gavana wa benki kuu; waziri wa fedha; waziri wa mawasiliano na uchukuzi; maofisa wa juu jeshini; na wengine wanaohisiwa kuhusika, ama moja kwa moja au kwa mzunguko?

Maswali haya yanaulizwa miongoni mwa Watanzana huku Uingereza, na kituo kimojawapo cha redio ya kwenye mtandao wa kompyuta kilichopo Marekani kimerusha kipindi kirefu kuhusu sakata hilo.

Sasa kinachojadiliwa pia ni kulindana kunakojitokeza ndani ya serikali yetu. Mnyororo wa uhusiano kati ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa na hii ya nne ya Kikwete, hauwezi kuleta manufaa kwa Wanzania. Unamnyima rais ujasiri wa kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa. Anaogopa asichukue hatua ambayo ikichunguzwa, naye atahusishwa kwa kuwa alishiriki katika ngazi fulani.

Mashabiki na wapenzi wa Kikwete wanaona sakata hili la rada linamgusa Mkapa. Wanataka wananchi na dunia nzima imwangalie Mkapa na watu wake. Wanasahau kwamba wakiitwa watu wake, Kikwete atakuwamo. Bado wana imani kwamba Kikwete anaweza kuwachukuliwa hatua wakubwa walioshiriki.

Wanakumbuka, na bado wanaamini kauli zilizokuwa zinasambazwa na wanamtandao, kwamba wanataka kuwaondoa wazee hawa – tena baadhi yao waliwaita “hii mijitu” – ili kujenga Tanzania mpya. Wanaona Kikwete na washirika wake wa sasa wana nguvu za kuchukua hatua nzito na kurejesha heshima ya serikali, na kukinusuru CCM kutoka kwenye shutuma za kuwa Chama Cha Majambazi. Watanzania hawa wanawaamini viongozi wetu wa sasa.

Mimi nasema, “ndiyo tunawaamini, lakini wanaaminika? Wanajiaminisha? Wanaamini kwamba Tanzania yenye neema inawezekana. Nami naamini hivyo, lakini nauliza, “itawezekana chini ya mfumo huu na kwa utaratibu huu?” Baadhi yao wanaamini kwamba Kikwete anaweza kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Nami nayataka; nayatamani maisha hayo. Ila sioni kama yanakuja. Sioni maandalizi. Sioni tofauti, bali marudio. Wapo walioamini kauli za wanamtandao, waliojiaminisha kwa Watanzania kwa ‘kumkandia’ Mkapa; na kwamba muarobaini wa matatizo ya Watanzania ni Kikwete. Leo wana jeuri ya kusema hivyo?

Kikwete ninayemuona ni huyu. Ni Mkapa mwingine katika sura tofauti. Na Kwa kuwa alijipatia umaarufu kwa kujitofautisha na akina Mkapa jukwaani, ajue kwamba hawezi kukubalika zaidi na kuaminika kwa Watanzania hadi hapo atakapojitofautisha kwa vitendo. Kikwete wetu amevaa ngozi ya Mkapa. Si aivue tumwone shujaa?

Uchambuzi huu umechapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 28. 01. 2007. Mwandishi anapatikana kwa simu +447828696142 na barua pepe ansbertn@yahoo.com.

2 comments:

Anonymous said...
This comment has been removed by a blog administrator.
Anonymous said...
This comment has been removed by a blog administrator.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'