Na Ansbert Ngurumo
NIMEFARIJIKA kwa kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba sasa amekusudia kujitoa mhanga katika vita dhidi ya ufisadi. Hii nayo ni ahadi ya nyongeza ambayo Watanzania watafuatilia utekelezaji wake.
Ameitoa wiki hii katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Dodoma.
Kilichonigusa ni nia ya rais – kujitoa mhanga ili kushinda vita dhidi ya ufisadi. Anajua kwamba ili ashinde vita hii - ili awe mwenzetu - lazima aikane nafsi yake, akubali kubeba ‘msalaba’ wake na kutufuata! Huko ndiko kujitoa mhanga.
Lazima awateme wapambe na maswahiba wake, ambao anajua walihusika katika ufisadi mkubwa unaolisumbua taifa sasa; unaomnyima usingizi.
Lazima ajiweke tayari kwa lolote litakalotokana na hatua yake hiyo, hata kama itabidi wamfitini aukose urais mwaka 2010. Naamini huko ndiko kujitoa mhanga anakozungumzia.
Lazima ajipange na sisi, awe upande wetu, na azingatie matakwa na maslahi yetu dhidi ya wachache wenye nguvu ya pesa chafu na madaraka dhalimu. Lakini anajua matokeo yake. Nguvu hiyo inaweza kumdhuru na kutokomeza ‘utukufu’ wake uliotengenezwa na wale wale anaosema atapambana nao. Huko ndiko kujitoa mhanga.
Maswali yanakuja. Je, ataweza? Maneno yake yatageuka vitendo? Ni kweli amebadilika na kuwa kama sisi? Au hiyo nayo ni kete ya kisiasa kulainishia hisia na akili za Watanzania?
Au ni kampeni zimeanza kiujanjaujanja kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu? Kimsingi, ni yeye tu anayeweza kujibu maswali haya vizuri. Wengine wote watajipendekeza na watashindwa.
Napenda kukiri, na naona fahari, kwamba nimekuwa mmoja wa wananchi waliomwandama Rais Kikwete tangu mwanzo. Taratibu, sote tutaanza kukubaliana kwamba mashambulizi yetu yamemsaidia rais kuliko sifa alizomwagiwa - hata kama hataki kukiri.
Na kama ningepaswa kuorodhesha mambo 10 tu ambayo tumeyatimiza katika miaka mitatu ya serikali ya awamu ya nne, nisingekosa la kusema. Yeye alitaja mafanikio yake; acha na sisi tutaje jinsi tulivyomsaidia.
Kwanza, tumemtoa rais kwenye sifa za vilemba vya ukoka; tukamfanya atambue uwezo na udhaifu wake halisi katika hali halisi ya ugumu wa maisha ya Watanzania na uzito wa kazi inayomkabili. Kauli yake kwamba yuko tayari kujitoa mhanga ina maana kwamba anawajua anaopambana nao. Anajijua uwezo wake, lakini anajua pia udhaifu wake ambao wenzake wanaweza kuutumia kumuumiza. Ulevi wa sifa umeanza kumtoka.
Pili, tumekomesha shamrashamra na majigambo ya ushindi wa kishindo. Walipoanza kushindwa kazi ndipo wakajua maana ya kishindo. Kura za umma ni laana kwa watawala kama hawatimizi ahadi walizotoa kwenye majukwa ya siasa. Siku hizi hata wao wanakiri kwamba mambo yamekuwa magumu. Sasa wanakubaliana na sisi; wameshindwa.
Tatu, tumemtoa tongotongo machoni. Sasa anaona vema matatizo halisi ya wananchi. Ugumu wa maisha ya Watanzania umemfanya rais na wapambe wake wasahau kabisa kaulimbiu ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania.’ Wamekubali kwamba hicho kilikuwa kibwagizo cha uchaguzi. Walikuwa wakishangiliwa sana wakati ule, sasa wakithubutu kuyasema maneno hayo wanazomewa.
Nne, tumemfunza kwa lazima kutofautisha kazi na urafiki. Anawajua wenzake, jasho lililowatoka; pesa waliyochanga; dili walizofanya na kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana. Lakini sasa tumemfikisha mahali anaanza kutambua kwamba ni zamu ya Watanzania kupata ushindi wa kishindo – dhidi ya njama za mafisadi; na kwamba ni zamu yake sasa kujitoa mhanga.
Mafisadi hawa, hasa walio karibu naye, ndio amekuwa akiwaogopa; na yawezekana ndio hao anaowazungumzia anaposema yuko tayari kujitoa mhanga, liwalo na liwe. Kama ataweza hilo, kwanini tumlaumu? Likimshinda kwanini tusimzomee?
Tano, tumemfanya aone kuwa kuna hatari ya CCM kumilikiwa na kununuliwa na matajiri wachache – tena kwa pesa ambayo Baba wa Taifa aliwahi kuiita ‘ya bangi.’ Ni yeye tu anayeweza kuinusuru au kuitosa CCM. Na kwa kuwa ndicho chama kinachoongoza serikali kwasasa, asipokinusuru ataliangamiza taifa.
Sita, tumemfanya alazimike kuzungumza lugha yetu, na kutumia msamiati wetu. Mwaka juzi wakati mawaziri wake na viongozi waandamizi wa CCM wanazunguka mikoani kupinga harakati za wapinzani na wanaharakati dhidi ya ufisadi wa watawala, serikali ilikuwa inapinga dhana hii ya ufisadi. Yeye aliongoza harakati hizo akiziita kelele za mlango.
Na wakati fulani Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, alianzisha ngonjera na mchezo wa maneno juu ya dhana ya ufisadi, akilenga kupuuza, kupunguza makali ya neno na dhana hiyo. Hakuweza.
Lakini sasa na rais (mwenyekiti wa Makamba) anazungumzia mafisadi, tena baadhi yao ni wale wale waliotajwa pamoja naye katika orodha ya iliyoanikwa hadharani pale Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Septemba 15, 2007. Siku hiyo ndipo ilizinduliwa rasmi vita dhidi ya mafisadi; na msamiati huo ukaanza kutumika kwa kishindo kuelezea uoza unaoendekezwa na watawala, unaolikabili taifa letu.
Ni faraja iliyoje kwamba sasa na rais anatumia lugha hiyo hiyo katika kueleza hatua na mikakati ya serikali dhidi ya watu wale wale waliokuwa wanalindwa kwa nguvu zote. Amekiri kiutu uzima kwamba hawezi kushinda nguvu ya umma. Imemshinda, na sasa anatafuta fursa ya kujiunga nayo. Kwa nini tusimpongeze kama anaanza kujisahihisha?
Lakini kujisahihisha huko kusipokuwa kwa dhati kutageuka kitanzi kwake. Maana sasa wananchi wameona na wamejua kwamba naye anajua kinachoendelea na - kama alivyowahi kusema mwaka 2006 - anawajua wanaohusika. Tatizo ni pale anaposema anasubiri ushahidi kuwachukulia hatua.
Lakini mbona ushahidi unapaswa kuwakuta mahamakani? Mbona ushahidi unapaswa kuwa sehemu ya mwenendo wa mashitaka? Atapataje ushahidi asipowafikisha kwenye vyombo vya sheria? Au anataka kutuambia kwamba wote walio mahakamani na magerezani leo ni kwa sababu kesi zao zina ushahidi wa kutosha?
Mbona kuna kesi zimedumu miaka zaidi ya 10 na zinaendelea kupigwa kalenda kwa kisingizo kuwa ushahidi haujakamilika? Kwa nini linapofika suala la kuwatia mbaroni mafisadi, rais anadai kwanza upatikane ushahidi? Kwani kuwatia mbaroni ni sawa na kuwahukumu?
Kwa maoni yangu, hili ni eneo ambao bado hatujamkomboa rais. Bado anarudia kauli alizorithi kwa mtangulizi wake Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye alitumia kauli hii hii kukwepa wajibu wa serikali kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa mbele ya vyombo vya sheria.
Je, Watanzania wataelewa na kukubali urithi huu wa Kikwete kutoka kwa Mkapa? Kama Mkapa alishindwa kuturidhisha kuhusu suala la ushahidi kabla ya kuwakamata wala rushwa, Kikwete ataweza kutulegeza? Na kuna ushirika gani kati yao unaowafanya watudai ushahidi wakati wapelelezi wa kesi ndio wana jukumu la kupekua na kukusanya ushahidi?
Na mbona baadhi ya wananchi walishatangaza kwamba wana ushahidi dhidi ya mafisadi, lakini polisi hawajawahi kuwafuata kuchukua vielelezo hivyo kwa ajili ya kuendelezea upelelezi wao? Hapo ndipo inakuja shaka juu ya umakini wa kauli za wakubwa kuhusu vita dhidi ya ufisadi.
Saba, tumemfanya apunguze safari za nje, akae ofisini. Ameanza kuzoea kwamba kazi hizo si zake tena, bali ni za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Nane, tumemlazimisha kuwagusa baadhi ya vigogo ambao hakuwa amedhamiria waguswe. Serikali ilijua makosa yao mapema sana. Ilikaa kimya hadi ilipoumbuliwa na wapinzani na wanaharakati. Na si hao tu, lakini hawa ndio wamepita kwenye chekecheo la mtandao. Wengine wamebaki juu kwa sababu ni wakubwa kuliko matundu ya chekecheo, lakini si safi kuliko wadogo waliopenya! Hata kama ni hatua ya kisiasa, ni hatua imepigwa.
Tisa, tumemfanya avunje Baraza la Mawaziri na kupunguza idadi ya wizara. Awali, alidhani kwamba ufanisi wa serikali ungetokana na wingi wa mawaziri. ‘Madongo’ yetu yalimfanya atambue kasoro hiyo na akajaribu kuirekebisha.
Kumi, tumemfanya atambue – na sasa ameanza kuonyesha hivyo – kwamba zetu si kelele za mlango. Na hata kama zingekuwa za mlango, hawezi kulala usingizi hadi zitakapokoma! Bado tutaendelea kupiga kelele maana tunajua umuhimu wake.
Tunajivuna kwamba sifa bandia zimeyeyuka mithili ya barafu kwenye jua. Sasa vumbi limeanza kutua. Tunaanza kuishi katika ukweli; katika kushindwa au kuweza. Naamini kwamba katika hili hakuna mtu atakayejitokeza kuomba tumpe ushahidi.
Kwani ni wazi kwamba waliokuwa wanatembea miaka mitatu iliyopita sasa wamekuwa viwete. Waliokuwa wanaona wamekuwa vipofu. Waliokuwa wanasikia sasa ni viziwi. Waliokuwa na shibe sasa wanalia njaa.
Huu ndiyo ukweli unaomsukuma rais aseme anataka kujitoa mhanga. Hawezi kujivunia umaskini, ujinga, njaa na maradhi yanayoongezeka miongoni mwa watu wale wale waliompigia kura za kishindo. Neema za mafisadi – wa awamu ya tatu au ya nne - ni hukumu yake.
Tunachosubiri ni kuona jinsi atakavyojitoa na kuwatoa wengine mhanga. Hapo ndipo tunapopataka.
La msingi ni kwamba taratibu anaanza kuacha kudeka; kwani aliokuwa akiwadekea ndio wamemuangusha. Na ndio hao anaopaswa kuwatumia kujitoa mhanga. Yaani tumeanza kumkomaza; na tutaendelea kumkomaza ili kulijenga taifa.
No comments:
Post a Comment