TUTAFAKARI: Miaka miwili iliyopita sidhani kama kuna Mmarekani alidhani kwamba Marekani ingekuwa na rais mweusi sasa. Leo Barack Obama ameruka vihunzi vyote, amevunja miiko yote, amekuwa rais mpya wa Marekani, na kuanza kujenga legasi yake kwa maneno mazito. Historia imeandikwa upya. Sikiliza hotuba yake ya kwanza akiwa rais.
Kwetu Tanzania, bado kuna kasumba kwamba viongozi lazima watoke Chama Cha Mapinduzi, kwa maelezo kuwa wasio wana CCM hawaonekani kuwa na uwezo wa kuongoza - ingawa waliopo ndio wameshathibitisha kwamba wameanza kuishiwa mawazo na uwezo wa kuongoza.
Kwangu mimi, ushindi wa Obama ni ushahidi na funzo tosha kwamba lolote linawezekana katika nchi yetu wakati wowote kuanzia sasa, kama kutakuwa na bidii ya kutosha. Hata wanaobezwa au wasiojulikana, na hata wasiokubalika sasa wanaweza kuiondoa CCM madarakani iwapo watajipanga vema. Najua wahafidhina watabisha kwa kuwa wanajua jambo tu - CCM. Na wanasubiri CCM ndiyo iwaruhusu kufikiri na kuamua vinginevyo.
Wenye akili pana, upeo na fikra angavu zilizofunguka, watapata fursa ya kutafakari na kuona vinginevyo. Baada ya marais 43 weupe, Marekani sasa imepata rais wa 44 mweusi katika mazingira ambayo ubaguzi wa rangi haujatokomezwa kabisa. Watanzania wanahitaji kuwa na marais wangapi wa CCM kabla ya kufanya mabadiliko? Wewe binafsi uko upande gani? Obama amekufunza nini? Jadili.
2 comments:
Obama amenifunza kwamba kasumba za kizamani na imani potofu zilizojengwa na watawala wa muda mrefu vinaweza kushindwa. Lakini vitashindwa na wale wenye moyo, wasio wepesi wa kukatishwa tamaa.
Heshima kwako Kaka Ansbert. Ukweli ni kwamba vijana wa hapa (na hasa weusi) ungewauliza miaka miwili iliyopita juu ya SHUJAA wao wangekutajia majina kama LeBron James, Kobe Bryant, Michael Jordan, Jay Z na wengine wang'arao lakini leo ni tafsiri nyingine. Si wote lakini nimeona na kuwasikia watu wakisema ukweli. Lakini pia tujue funzo kuwa alijiandaa na pia aliandaliwa. Njia ilishatakaswa na wale waliofanya vibaya zaidi yake kama kina Jesse Jackson na waliopewa madaraka wakaonesha kujali taifa kuliko pesa hata pale ilipomaanisha kupoteza nafasi zao kama Collin Powel na wengine. Kuna maandalizi mema ambayo yanaendelea nyumbani ila ni sisi tusiojiandaa kumalizia kazi zilizoanzwa. Ukweli ni kwamba nyota njema huonekana asubuhi lakiini hutambulika jioni. Kwa hiyo tuanzapo kuonesha nyota njema tusitegemee itambulike wakati huohuo, na ikiandaliwa vema itang'aa vema na kuwa mwanga wa kuinurisha dunia.
Asante sana na HESHIMA KWAKO
Post a Comment