Monday, July 04, 2005

Kwako Binafsi, Maisha Yana Maana Gani?

Na Ansbert Ngurumo

TAFAKARI pamoja nami juu ya fumbo hili; maisha. Kwangu, Maisha ni Mapambano, kama ilivyo kwa Askofu Mkuu wa Rochester, N.Y, Fulton J. Sheen.

Huyu naye aliamini hivyo na alitumia fumbo la Pasaka kueleza maana ya maisha. Alisema: “Kama maisha yetu hayana msalaba, hatutaweza kamwe kuliona kaburi tupu. Kama hakuna taji la miiba, hakutakuwa na shada la maua ya nuru. Bila ya Ijumaa Kuu hakutakuwa na Pasaka.”

Mahali pengine aliwahi kunukuliwa akilinganisha na kutofautisha uelewa wa wafuasi wa Yesu na ule wa wauaji wake. Alisema kwamba wafuasi wa Yesu hawakumtaraji afufuke, lakini waliomwua walitaraji ufufuko wake. Anatoa mfano, wale wanawake walikwenda kaburini Jumapili alfajiri kuupaka mwili wake manukato kama ilivyokuwa desturi. Hawakuwa na wazo kwamba angeweza kufufuka.

Maria Magdalena alipokutana na Yesu bustanini, alidhani amekutana na mtunza bustani. Na Maria Magdalena huyo huyo alipowaletea mitume wa Yesu habari za ufufuko, hawakumwamini. Njiani kuelekea Emmaus, wanafunzi wake wawili walikuwa na mazungumzo yaliyoonyesha kwamba wamekata tamaa.

Tazama kiwango hiki cha tofauti. Wakati watu hawa waliokuwa karibu na Yesu kwa muda mrefu wakikosa imani, wale wasiomwamini walimzika na kuweka jiwe kubwa kaburini. Kwa nini? Zaidi ya hayo waliweka walinzi! Kwa nini? Pasaka ya kwanza ya Agano Jipya haikuwa na starehe tuliyo nayo sasa. Ilikuwa siku ya mapambano ya mawazo, imani, kifo na maisha. Pata tafakuri zaidi hapa.

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'