Sunday, June 28, 2009

Michael Jackson: Skendo Tupu


Tumesikia na kusoma mengi mazuri ya Mfalme wa Pop, hayati Michael Jackson. Hapa kuna skendo za maisha yake ya nyumbani - yeye na pesa, watoto, ndugu, marafiki na majirani - zinazosimuliwa na mlezi wa watoto wake, Grace. Soma mwenyewe hapa.

Saturday, June 27, 2009

Serikali inataka kulikoroga jeshi letu?



Serikali imeamua kulipaka jeshi letu matope ya ufisadi, kulifanya ngao ya ufisadi wa vigogo, huku ikisisitiza kwamba ni kwa maslahi na usalama wa taifa. Je, inajua madhara yake? Ni haki kulitumia jeshi letu kulinda matumbo machafu ya wanasiasa? Huu ndio mjadala wa Maswali Magumu wiki hii.

Wednesday, June 24, 2009

Ijue Nguvu ya Sikio lako la Kulia

Ijue nguvu ya sikio lako na kulia na jinsi ya kulitumia la mwenzio katika mawasiliano. Soma hapa.

Tuesday, June 23, 2009

Uingereza wapata Spika mpinzani

Baada ya Spika wa awali kujiuzulu kwa kashfa, Bunge la Uingereza limechagua Spika mpya John Bercow (46) ambaye anatoka chama cha upinzani cha Conservative. Mtazame hapa akitambulishwa na kutambuliwa rasmi baada ya kupata baraka za Malkia; na hapa akikubali majukumu ya kazi yake mpya n akuwashukuru wabunge. Hizi hapa ni hotuba za viongozi wa vyama vikuu Bungeni: 1. Waziri Mkuu , Gordon Brown (Labour). 2. Kiongozi wa Upinzani , David Cameron (Conservative). 3. Kiongozi wa chama cha upinzani , Nick Clegg( Lib Dem). Msikilize Spika mpya akimnanga mbunge mzee aliyekataa kumuunga mkono kwa kigezo cha umri. Huu ndiyo utaratibu wa kumpata Spika wao.

Sunday, June 21, 2009

Rostam Mbunge Bubu




Imedhihirika kwamba miongoni mwa wabunge wote (319) wa Tanzania yupo mmoja, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (pichani kulia), ambaye hajawahi kuuliza swali Bungeni wala kuchangia katika mjadala wa jambo lolote katika vikao vya Bunge kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo (Desemba 2005-Juni 2009. ) Je, anatumia ubunge wake kufanya nini? Pitia orodha ya wabunge bubu wa Tanzania, utoe maoni yako.

Thursday, June 18, 2009

Hukumu muhimu kwa wanablogu: Kublogu na siri haviendani

Kama ulitaka kublogu na kutunza siri, fikiri upya. Hukumu hii inawanyanganya wanablogu haki ya kuwa na siri kwa sababu kazi yao si yao binafsi bali ya jamii. Soma hapa.

Sunday, June 14, 2009

Saturday, June 13, 2009

Yajue manono ya Ronaldo

Umeipata hii ya kipato cha Ronaldo? Atakuwa analipwa paundi 55 (karibu 110,000/=) kila dakika, hata kama yuko usingizini. Soma habari kamili hapa.

Sunday, June 07, 2009

Vijana CCM Bukoba acheni kujikomba

VIJANA wa leo wanafanyaje siasa tofauti na vijana wa zamani? Vijana waliosoma, wenye elimu (walau wenye makaratasi yanayoonyesha hivyo) wanafanyaje siasa tofauti na wale ambao hawakupata bahati ya kuelimika kama wao?
Wakilinganishwa na vijana waliowatangulia, vijana wa leo wana vipaumbele gani vilivyo bora? Na wakilinganishwa na wazee wa leo, vijana wa leo wanaonyesha matumaini gani ya kuwa na uzee mwema hapo baadaye?
Je, Tanzania yetu hii tukiikabidhi kwa vijana hawa tulionao, itakuwa salama zaidi kuliko ilivyo leo mikononi mwa wazee wanaong’ang’ania ujana? Je, wanaowabeza vijana wa Tanzania, wana haki ya kufanya hivyo? Au kuna sampuli ya vijana wanaosababisha bezo linalowaumiza vijana wote?
Je, Umoja wa Vijana wa CCM una haki tena ya kujiona wao ndio wawakilishi wa fikra, tabia na mwelekeo halisi wa vijana wa Tanzania? Je, vijana wa Tanzania, kwa ujumla wao, wanaonyesha jeuri, ujuzi, umakini, nguvu, upeo, wepesi, udadisi, moyo wa kujituma na wa harakati kuliko waliowatangulia?
Mfumo wetu wa elimu na malezi, umetulelea vijana wenye sifa hizo au umetufyatulia vibaraka na wapambe wa mfumo uliopo walio wepesi kunyanyaswa, kupuuzwa na kutumiwa kwa maslahi ya walio madarakani, hata kwa kuteketeza maslahi ya taifa la kesho?
Je, dhana ya taifa la kesho ipo kweli, au maisha yote yanakamilika na kumalizika leo tu? Kama kesho ipo, ni nani anabaki kuwa mlinzi wa hiyo kesho?
Nimejiuliza maswali haya na mengine baada ya kusikia kilichotokea Bukoba Mjini wiki hii, ambapo Umoja wa Vijana wa CCM, umetoa hundi ya shilingi milioni moja (1,000,000/-) kumlipia Rais Jakaya Kikwete kiasi anachohitaji kuchukulia fomu ya kugombea tena urais mwaka 2010.
Wamempa pia Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Sued Kagasheki, hundi ya laki moja (100,000/-) ili aweze kulipia fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM mwaka 2010.
Najua kampeni zinazoendelea ndani ya CCM. Siwaonei wivu Rais Kikwete na Balozi Kagasheki. Naelewa pia kwamba vijana hao wametoa michango hiyo kama hamasa ya kisiasa. Ni kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010.
Lakini najiuliza, hizi ndizo siasa zinazowafaa watu wanaojiita vijana katika karne ya 21? Kwa staili hii, wao wanajifanya watu wa kuiga au wa kuigwa? Hii ndiyo sampuli ya vijana wa Bukoba? Wanaleta aibu au sifa kwa vijana wenzao kimkoa na kitaifa?
Hii dhana ya kumchangia pesa rais inatokana na nini? Ni kwamba Rais Kikwete ni mhitaji wa pesa kwa kiwango hicho cha kutegemea misaada ya kuchangiwa au kupewa? Je, vijana hawa wana fedha nyingi za kugawa hata kwa Rais Kikwete?
Je, vijana hawa wamejitosheleza au wana miradi mikubwa kiasi kwamba pesa hiyo inatokana na faida kubwa waliyopata, na sasa wameamua kutoa mchango kwa ‘maskini Kikwete na Kagasheki?’
Ni kweli kwamba katika bajeti yao ya mwaka huu pesa hiyo ilitengwa kwa ajili ya kununulia fomu ya Rais Kikwete mwaka ujao? Ni kweli Rais Kikwete alihitaji kuchangiwa milioni moja na kundi kama hili? Je, hii pesa ni ya vijana hao au wamepewa ili wafanyie mbwembwe na harakati za kisiasa?
Najua kinachofanyika hapa ni kampeni; ni propaganda; ni mbwembwe; ni kujitangaza. Lakini hii ndiyo staili ambayo inawafaa vijana wetu, tena baadhi yao wasomi? Je, siasa za namna hii zitatuendeleza?
Je, CCM Bukoba imeendelea, imeridhika na ina ziada ya pesa kiasi cha kutoa misaada kwa wengine wanaohitaji, nje ya mkoa, akiwamo rais?
Vijana hawa hawa ambao wamekuwa wanakinga bakuli kwa Mbunge wao, ambao baadhi yao wamekuwa wakitumika kumsifia mchana na kumshambulia usiku, leo wamepata wapi jeuri ya pesa ya kumsaidi yeye badala ya kukarabati majengo ya ofisi zao zilizochakaa na kuweka mikakati ya kuboresha vipato vya watendaji katika ofisi zao?
Balozi Kagasheki amekuwa akitumia fedha zake nyingi kufadhili miradi mbalimbali katika jimbo lake. Vijana hawa waliwahi kumchangia katika kufadhili mradi gani kwa ajili ya maendeleo ya wakazi wa Bukoba?
Jambo moja ni wazi. Hatuwezi kuwapangia matumizi ya pesa za chama. Lakini tunaweza kuwashauri. Kwa sehemu kubwa, matumizi kama haya yanaonyesha udhalili wa wahusika; na yanawafanya waonekane wanajikomba kwa maslahi finyu ya kisiasa.
Nisingehoji sana kama pesa hizi zingetolewa na jumuiya isiyo ya vijana. Wala nisingewasema sana kama zingekwenda kwa watu wanaozihitaji, ambao wanataka kugombea ubunge au urais lakini vipato vyao haviwawezeshi kupata viwango hivyo vya pesa.
Wapo wananchi wanataka kugombea ubunge, lakini wanatengwa na mfumo unaothamini pesa kuliko utu. Baadhi yao wangeweza kuwa wawakilishi wazuri tu, lakini kwa kuwa hawana pesa ya kununua fomu na kuhonga wakati wa kampeni, wanatupwa nje ya ulingo wa siasa.
Kama vijana hawa wangewatambua watu wa aina hii, wakawapa hamasa kwa kuwachangia pesa, tungeona wamefanya jambo la maana. Lakini pia, vijana ndio wangetarajiwa kukisaidia chama chao kuondoa taratibu kongwe na za kibaguzi zinazoleta matabaka kwenye chama chao na katika taifa kwa ujumla.
Badala ya kukaa tu na kuabudu mifumo hii, vijana wangekuwa wabunifu na jasiri zaidi kwa kuwashawishi wazee kuondokana na mifumo mikongwe ndani ya chama.
Zaidi ya hayo, vijana hawa ndio wangepaswa kukikosoa chama, kukipa changamoto ndani na nje ya vikao, kukitetemesha na kukitikisa ili kirejee katika misingi ya chama cha wakulima na wafanyakazi; chama cha mlalahoi, Mtanzania mlipa kodi; chama wa waadilifu na watu wenye uchungu na nchi hii.
Sifa wanazomwaga kwa viongozi walioshindwa kazi, ni dalili tosha kwamba vijana wenyewe wamezeeka kabla ya wakati wao; wamegeuka wachafuzi na wakorogaji wa siasa za Tanzania; wamekuwa waviziaji na wazengeaji wa vyeo vya kuteuliwa; wanajikomba na kujidhalilisha; wanatanguliza maslahi yao finyu.
Duniani kote, uhai na maendeleo ya taifa hutegemea zaidi vijana; si tu kwa misuli yao bali hasa kwa akili na ubunifu, ujasiri na moyo wa kuthubutu kubadilisha mazoea.
Lakini sehemu kubwa ya vijana wa Tanzania, hasa wenye nafasi katika mfumo wa utawala wan chi hii, wanashangilia mazoea ya muda mrefu, na yaliyochoka na kuchokwa hata na baadhi ya walioyaasisi. Kuna tatizo gani?
Tunapowaza kutengeneza sera za maendeleo yetu, tunalenga mustakabali wa taifa miaka 30 na zaidi ijayo. Hapa tunazungumzia kizazi kijacho – watoto na wajukuu wetu. Tunazungumzia urithi tutakaowaachia watoto tunaowazaa leo na watoto wao.
Hatuwazi kutafuna na kuteketeza kila kilichopo leo, kana kwamba tunawakomoa wale tuliowatangulia kuzaliwa. Uchungu na ugomvi wa baadhi yetu na watawala, tunapojadili uoza na ufisadi wao, unatokana na fikra hii kwamba walio madarakani na wapambe wao, wameendekeza dhana ya kukomoa kizazi kijacho.
Laiti vijana wa leo wangejua kuwa ni jukumu lao kuwazuia watawala na kudhibiti ukomoaji huu unaoendelea kulitafuna taifa lililojaliwa raslimali nyingi mno, lakini linasifika duniani kote kwa amani na utulivu katikati ya umaskini uliokithiri.
Wanaotusifu wana sababu zao. Si zetu. Sifa za watu wa nje hazileti chakula mezani kwetu. Hazilipi kodi ya nyumba; hazitujengei shule wala hazitulipii karo ya watoto wetu. Hazitibu wagonjwa wetu.
Lakini sifa hizo zinalegeza mioyo yetu, na zinawahakikishia wanaotusifu fursa ya kutumia raslimali zetu kuendeleza mataifa yao; kuwawekea hazina vijana na watoto wa mataifa yao kwa kutumia jasho la vijana na watoto wetu. Ni wajibu wetu, hasa vijana wa leo wa Tanzania, kusema, ‘hapana!’
Si sifa ya kujivunia kwa watawala wetu kumeza ndoani za mataifa makubwa, huku wakivikwa vilemba vya ukoka na kutunukiwa tuzo na shahada za bure ili waendelee kutengeneza na kuchonga mirija mirefu, mikubwa na imara zaidi ya kuhamishia utajiri wa nchi zetu kwa wakoloni wapya, wababe wa utandawazi.
Ni jukumu la vijana kuhakikisha kuwa ujana wao na wa watoto wao haunyonywi na vijana wa wakoloni weusi au weupe au wowote wale, kwa kisingizio chochote kile.
Tukubali, tukatae; kesho ni ya vijana. Lakini kesho hiyo hiyo inaanza leo, na inatengenezwa na leo yetu.
Bahati mbaya, sioni kama vijana wenyewe wanatambua hilo au wanahangaika kuitengeneza kesho hiyo, au kuwazuia waharibifu wa leo yetu inayoleta maangamizi ya kesho yao. Kama wapo hawatoshi.
Kwa sababu ya kasumba za muda mrefu na propaganda za kisiasa zilizodumaza uwezo wa wananchi kufikiri; kwa sababu ya mfumo wa elimu ya kunakiri na kukariri; wananchi wetu wengi, vijana wakiwamo, wamekuwa mateka wa mifumo ambayo wangepaswa kusimama kidete kuihoji, kuipinga na kuiangusha.
Sina ugomvi na utendaji wa Balozi Kagasheki katika jimbo lake. Ni mmoja wa wabunge wachache wanaotumia raslimali zao binafsi kuendeleza majimbo yao. Lakini hii siyo siasa tunayotaka kujenga. Si kazi ya mtu mmoja kuwajenga wananchi milioni mbili madaraja, madarasa, barabara, nyumba za kuishi, miradi ya maji na afya, kuwanunulia magari ya wagonjwa, na kadhalika.
Tunahitaji siasa endelevu, ambazo zinakiwezesha chama na serikali ya wakati huo kuweka mifumo ya utendaji kazi, hata kama mbunge mwenyewe hachaguliwi tena au anajiuzulu. CCM Bukoba Mjini wamekuwa wakimsaliti mna kumzunguka Kagasheki, wakijua upinzani mkuwa alio nao dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Kama kuna msaada walipaswa kumpa, si pesa; sila ki moja. Huu ni uhuni, ni matusi. Kagasheki nahitaji nguvu na umoja wa kichama, ushirikiano katika kujenga mikakati ya maendeleo na ushindani wa kistaarabu; mifumo endelevu ya kuleta maendeleo ya wana Bukoba.
Kama walitaka kusaidia, basi hiyo laki moja wangemchangia mwanachama mwingine anayetaka kuchuana na Kagasheki ndani ya chama, lakini ha uwezo wa kuipata. Tungewaita mashujaa, wanademokrasia wanaokua na vijana wa kutegemewa na taifa zima.
Kwa uapnde mwingine, tungewaona mashujaa kama miongoni mwao angejitokeza kiaja anayetaka kuchukua fomu kuchuana na Rais Kikwete katika kugombea urais mwaka kesho, kwa sababu sote tunajua kwamba katika miaka mitatu hii iliyopita, mambo yamemuwia magumu!
Tunajua ugumu wa kupambana na rais aliye madarakani. Si lazima umshinde, lakini ni vema kuandika historia kwamba vijana wa Tanzania wana uwezo kukataa kusifia kasoro na udhaifu wa wakubwa.
Wana CCM wenye akili, ambao hawaridhiki na utendaji wa serikali ya awamu ya nne, lakini hawana ujasiri wa kutosha kuwanyooshea wakubwa kidole, wananyamaza. Sawa ni waoga, lakini ni bora kuliko kujidhalilisha!
Naomba nieleweke. Vijana wote hawawezi, na hawapaswi kuwa na msimamo mmoja; au kuwa katika chama kimoja; au kuwa nje ya chama. Lakini wanaotaka kumsaidia rais au nchi yao, wanaweza kufanya hivyo ndani ya chama kwa kukipa changamoto na kukibadilisha ili kiendane na zama zao.
Wanaweza kufanya kazi nzuri tu bila kutumia kama mihuri ya maamuzi ya wakubwa. Wanaweza kuingiza nguvu mpya ya kiakili na kimwili katika chama, na kukipa mwelekeo mpya ulio imara.
Siasa za kutafuta maslahi kwa kujikomba na kumwaga sifa zisizostahili ni siasa dhalili zinazoweza kufanywa na wale tu ambao wanatambua kuwa nafsi zao hazina thamani, wala utu wao hauna nafasi, na ni kivuli tu, mbele ya nafsi za wakubwa.
Kuishi, kula na kufanikiwa kwao kunategemea fadhila, uteuzi na huruma ya wakubwa. Hizi si siasa za kufanywa na vijana. Na kwa hili, tuwaulize vijana hawa wa CCM Bukoba: ‘ipo wapi jeuri, ujuzi, umakini, nguvu, upeo, wepesi, udadisi wao kisiasa?’ Tukubaliane. Wametudhalilisha

Thursday, June 04, 2009

Obama awaahidi Waislamu 'mwanzo mpya'


Kama hukuweza kusikiliza hotuba ya Rais Barack Obama, jijini Cairo, Misri, kuhusu 'mwanzo mpya' kati ya Marekani na Waislamu duniani kote, bonyeza hapa usikilize alichosema. Hata kama ulimsikia, unaweza kurudia kuisikiliza hotuba nzima, ukajikumbusha kile alichoita changamoto sita zinazoikabili dunia kwa sasa.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'