Tuesday, August 14, 2007

Nauliza Kujibiwa

Mpendwa msomaji, nakamilisha mada yangu katika mazungumzo nitakayoshiriki kwenye kongamano la Highway Africa litakalofanyika Septemba 10-12, 2007, Rhodes University, Afrika Kusini. Nimefikiri kwamba ni vema kupata na kutumia mawazo ya wanablogu wenzangu na wasomaji wa blogu hii katika maswali kadhaa ninayojiuliza. Naomba ushiriki wako kwa kujibu maswali yafuatayo kwa kadiri unavyoona inafaa. Nakuhakikishia kwamba nitakapohitaji kutumia mawazo yako mahali popote, nitakunuu bila kuongeza chumvi. Asante. ANSBERT NGURUMO.

1. Kama wewe ni mwanablogu, kwa nini unablogu? Kama si mwanablogu, kwanini unasoma blogu?

2. Je, ni vema wanablogu (na wachangiaji wa maoni) watumie majina yao halisi? Faida na hasara zake ni nini?

3. Je, matumizi makubwa ya blogu yanamaanisha enzi za vyombo vya habari vya kale (redio, magazeti na TV) vimepitwa na wakati?

4. Je, wanablogu wanawajibika kwa nani?

5 comments:

Evarist Chahali said...

1.Binafsi ninablogu kwa sababu kuu tatu.Moja,napendea kuwasiliana na jamii kwa njia hiyo (blogging).Siwezi kutuma barua yenye mawazo au mtazamo wangu kwa kila mwanajamii ulimwenguni.Blogu yangu inanisaidia sana kurahisisha azma hiyo.Pia katika njia hiyo ya mawasiliano iliyorahisishwa na teknolojia ya mtandao,nanufaika na comments ambazo nyingi ni darasa kubwa pengine zaidi ya kuhudhuria taasisi ya elimu.Pili,napendelea kuandika (iwe e-mail,shairi,barua,nk).Kwa vile blogging inahusisha kuandika (japo si kwa mkono),moja kwa moja imetokea kuwa ni miongoni mwa hobbies/interests zangu.Tatu,ninaandika makala kwenye gazeti moja la huko nyumbani,na blogu yangi inatumika kama kumbukumbu (archive) ya makala zangu zinazotoka kwenye gazeti hilo.

2.Nadhani ni vema,japo si lazima,kwa mwanablogu kutumia jina halisi.Nilisoma mahala flani ambapo jamaa mmoja alikuwa akiandika makala za "diary" ya Steve Job wa Apple,ilhali yeye sio Steve.Imechukua muda mrefu kwa jamaa huyu kubainika (hakuchukuliwa hatua) lakini kwa namna flani wapo waliomwona mtu huyo kama si mwadilifu japokuwa alichokuwa akiandika kilikuwa kikiwavutia wengi.Inapendeza kumjua mtenda kitu (hasa kikiwa cha manufaa),na inasaidia urahisi wa mawasiliano ya njia-mbili (interactivity) kati ya bloga na hadhira yake.Kwa mtoa maoni,kutumia jina halisi kunamwezesha bloga kuwasiliana nae (mtoa maoni) kirahisi.Kwa kutoweka jina lake,mtoa maoni anajinyima fursa ya kupewa majibu au feedback kuhusu maoni yake,japo bloga anaweza kufanya hivyo kwenye sehemu ya comments.Hata hivyo,kutoweka jina hakuathiri ubora wa maoni ya mtoaji alimradi kutoweka jina huko hakufanywi kwa sababu ya kutoa maoni yasiyofaa (eg matusi).
3.Kwa mtazamo wangu,blog ina nafasi ya pekee katika sekta ya mawasiliano lakini haifuti umuhimu na nafasi ya nyenzo nyingine za habari kama runinga,radio na magazeti.Nyingi ya nyezo hizo za "asili" zinaendeshwa kitaasisi zaidi tofauti na blogu nyingi zinazoendeshwa kibinafsi zaidi (kwa maana ya mtu mmoja mmoja),lakini hilo pia linaweza kuwa na faida hasa pale taasisi ya mawasiliano inapopandikiza matakwa yake watendaji wa taasisi husika.Ni kama barua pepe zisivyoweza kupoteza kabisa uuhimu na nafasi ya barua "za kawaida."Pia blogu zinaathiriwa zaidi na ukweli kwamba hadhira yake kubwa ni watu wenye kufahamu na/au wenye access ya teknolojia ya mtandao,na kwa hali hiyo inawatenga zaidi wale ambao hawana access kwenye teknolojia hiyo,mfano vijijini.Lakini radio,na runinga kwa kiasi flani,imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano hata kwa wale wasiojua kusoma.Magazeti yana hadhira ya watu wanaojua kusoma lakini ukiachilia mbali suala la bei,yanapatikana kirahisi.Hata hivyo,blogu kwa mfano ile ya mjengwa,inaweza kuwa nyenzo muhimu katika maeneo ambayo radio zinasikika,runinga zinaonekana na magazeti yanafika,lakini nyenzo hizo tatu hazina makazi/kituo mahala husika.Ironically,wakati blogu inaweza kutoa habari ambazo pengine ni vigumu kupatikana kwa nyenzo "asilia" za habari,wadau wa eneo husika wanaweza kuwa hawanufaiki (kwa maana ya kuziona habari hizo) kutokana na kukosa teknolojia ya mtandao.Kingine ni athari za subjectivity ya bloga.Ni rahisi kwa umma usiokwenda mbali zaidi kuchungiza mantiki ya habari,kuamini gazeti,radio au tv kuliko blogu kutokana na imani (inayoweza kuwa sahihi) kuwa blogu ni mawazo na utashi wa bloga.Hilo linaweza kuepukwa kwa bloga kuwa objective katika anachokiweka humo japo sote twafahamu kwamba hakuna kitu kama absolute objectivity.
4.Bloga anawajibika zaidi kwa hadhira yake,maana kama ingekuwa ni suala la kujifurahisha yeye mwenyewe basi angejiandikia yeye mwenyewe.Ieleweke kuwa kuwajibika kwa hadhira hakumaanishi kuifanya blogu iwe ya kuridhisha tu ahadhira hata pale inapopaswa kukosolewa.Pia bloga anawajibika kwake mwenyewe kwani kwa kuwa na sense of responsibility,anajiongezea heshima na kuaminika machoni kwa hadhira yake.Tukiwajumuisha watoa maoni katika swali hili,nadhani wao wanawajibika kwao binafsi (eg pale wanapotoa comments zinazohitaji ufafanuzi) lakini pia wanawajibika kwa jamii.Ni kama vile kupata fursa ya kutoa maoni mkutanoni kisha kutoitumia vizuri fursa hiyo.
Naomba kusisitiza kuwa huo ni mtazamo wangu binafsi,na yeyote yuko huru kunikosoa.

NEW OWNERS said...

1. Kama wewe ni mwanablogu, kwa nini unablogu? Kama si mwanablogu, kwanini unasoma blogu?

Mimi ni mwanablogu, blog yangu ni www.saidiyakubu.blogspot.com na niliianzisha mahsusi kwa ajili ya kuwasiliana, kupashana habari na kuchambua masuala mbali mbali yanayohusu Tanzania na hususan watanzania waliopo nje ambao niliona katika siku za karibuni wamekuwa na mwamko mkubwa wa kufuatilia masuala ya kisiasa,kiuchumi nk yanayotokea Tanzania.

Kama mwanahabari nimekuwa nikiwapasha kwa kuandika na hasa kutumia picha wakati mwingi juu ya matukio ya Tanzania.

Blog hii iliweka historia pale tulipoamua kulivalia njuga suala la ukaguzi wa magari uliopitishwa na mamlaka ya viwango Tanzania TBS ambapo waliipa zabuni kampuni moja kinyemela na bloh ikalivalia njuga suala hilo kwa kulaani vikali na hatimaye suala hilo likafutwa na TBS.

Pia ni msomaji mzuri wa blog nyingine kadhaa kujua 'wadau' wanavyoandika na kujifunza kutoka kwao, uzuri wa blog tofauti na magazeti/radio ni kuwa wengi tunafanya kazi kwa kushirikiana na sio ushindani.


2. Je, ni vema wanablogu (na wachangiaji wa maoni) watumie majina yao halisi? Faida na hasara zake ni nini?


Nadhani ni vizuri kwa wachangiaji kutumia majina yao au picha ili kujitambulisha kwa vile inasaidia kujenga hadhi ya blog na pia kujua habari na kutegemea mrengo fulani. Mfano blog ya habari za kitanzania za nje kama binafsi inasaidia lakini pia blog ya burudani/elimu na masuala ya nyumbani ya Issamichuzi inakuwa ni rahisi kufahamika zaidi.

FAIDA:

a. Ni kujenga sifa ya blog hata kabla haijasomwa kama mwandishi anafahamika.

b. Kumjenga hadhi mwandishi ili asianguke kutoka daraja fulani la uandishi au uhariri wa blog yake.

c. Inasaidia sana wanablogu waliowanasiasa/wanakampeni nk kujulikana na hivyo kujenga ufuasi mkubwa.#



HASARA:

a. Kudharaulika mbele ya jamii kwa vile blog ni kazi binafsi wakati mwingine hisia binafsi huingia zaidi kuliko uhalisia wa jambo, mfano mimi ni mshabiki wa Manchester United/Coastal Union na hivyo inapotokea habari kuhusu hilo huwa na ushabiki usio kifani, pengine hili linaudhi wengine lakini ndio hisia zangu kama mwandishi.

b. Kuonekana mbele ya jamii kama mtaka sifa na mtu mwenye kutaka kujipendekeza iwapo utakuwa unaelemea sehemu fulani kisiasa lakini haya ni kawaida kwa vyombo vingi.


3. Je, matumizi makubwa ya blogu yanamaanisha enzi za vyombo vya habari vya kale (redio, magazeti na TV) vimepitwa na wakati?

Hapana, mara nyingi habari za blog hufika mapema ingawa usahihi wake wakati mwingine unatia shaka hivyo magazeti na tv bado zinabakia kuwa ni vyanzo muhimu vya habari.

Pia blog zinapatikana mtandaoni peke yake hivyo habari zake hazifiki kwa walio wengi lakini magazeti yanauzwa bara barani na yanafika sehemu nyingi zaidi.

Hata hivyo hivi sasa tumeanza kuona mashirika makubwa ya habari yakiwa na bloggers ili kuendana na muenendo huu mpya. Hii ina maanda blog kama njia ya mawasiliano inakuwa kwa kasi.


4. Je, wanablogu wanawajibika kwa nani?

Zaidi nadhani ni kwa wasomaji kama chombo kingine cha habari, ila pia baadhi ya bloggers wapo kwa ajili ya kuridhisha nafsi zao kwa kufikiria kwa sauti.

Bado hakujawa na sheria maridhawa za kudhibiti blog hivyo kuchafuana hususan katika comments za wasomaji huwa ni kubwa mno.

Anonymous said...

Nakujibu ule waraka tujadiliane. Tutaonana basi mwezi huo ujao.

Anonymous said...

1. Ninablogu kwa sababu nina nia ya kufikisha kilichomo kichwani (mawazoni/fikrani) kwangu kwa ulimwengu wa nje ya nafsi yangu. Maoni ninayopata kutoka kwa wasomaji wangu yananisaidia kuona 'maeneo' ambayo mimi sikuyaona wakati nikiwa katika mtiririko wa mawazo (fikra) zangu. Kwa msingi huo, ninaelimika na kupanuka zaidi kimtazamo na kifikra.

2. Ni vema kila mwana blogu atumie jina lake halisi au basi awe na jina la kudumu la uandishi (pen name); kwa watoa maoni, ni vizuri kila anayetoa maoni kwanza kabisa atumie hekima zake katika kuamua umuhimu wa kutumia au kutotumia jina lake. Unaweza kutoa jina na kisha watu fulani wakachukizwa na maoni yako (labda kwa sababu yanawaumbua au yanagusa interests zao) na hivyo wakaamua kukudhuru kwa njia moja au nyingine. Hapa mtu huna budi kutumia hekima zako za kuzaliwa nazo.

3. Vyombo vya habari vya kitaasisi bado vinahitajika, tutaendelea kuvitumia ingawa vinaingiliwa sana katika uchapishaji wa habari zao. Kwa hiyo, kuingia kwa blogu si mwisho wa kuwepo kwa vyombo vya habari tulivyovizoea.

4. Kwanza kabisa wanablogu wanawajibika kwa NAFSI zao. Wao wenyewe wanabeba jukumu kwa lolote wanalochapisha katika blogu zao. Pili, wanawajibika kwa umma wa binadamu, kwani hao ndio wanaotaka kuwasiliana nao, hivyo, wanawajibika kuipatia jamii kile ambacho kitaijenga jamii (hata kama ni kwa kuibomoa kwanza ili kuijenga upya).

5. Tuendelee kublogu. Tusihiane wanablogu na watoa maoni kuacha tabia mbaya za kutukanana bloguni. Tujenge hoja na si kulazimisha hoja.

Ni hayo tu.

Anonymous said...

Nina blog. Naitumia kutoa mawazo yangu nionavyo mwenyewe bila kujali ukubwa au udogo wa habari.

Mawazo yangu nayaweka hadharani hata kama sina mtu wa kuongea nae au si mwanachama wa umoja fulani.

Wana blogu ningependa hawapendi kutaja majina halisi, basi nashauri watumie vifupi (initials) vya majina yao Mfano Ali Huseni Juma atumie 'AHJ' badala ya kubuni majina ya ajabuajabu. Huu ni utashi wa mtu binafsi maana kuna mada zingine nyeti inabidi mtu asianike jina lakini ni bora vifupi vitumiwe.

Vyombo vya habari bado vina nafasi yake hasa ktk kutoa habari rasmi. Blog zetu ni mawazo yetu binafsi na hatuna access kwa viongozi au ofisi za kiutendaji kuweza kupata taarifa rasmi. Mimi sio mwandishi wa habari.
Vile vile blog zinatuunganisha socially na wanajumuia wa nchi moja au tofauti ili kuweza kubadilishana mawazo.

Nakutakia kila la heri.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'