Haijapata kutokea. Terehe 11.Agosti.2007 iliandika historia mpya Tanzania. Wafanyakazi wameandamana na kuilaani serikali ya awamu ya nne kwa kuwadhalilisha, kuwasahau na kuwafanya watumwa katika nchi yao. Ujumbe wao ulifikishwa kwa maandamano, nyimbo, mabango na hotuba kali. Gazeti la Mwananchi Jumapili linaripoti hivi:
Wafanyakazi wampa Rais Kikwete siku 30
*Wamtaka Katibu wao kumwona na kurejesha majibu
*Wadai matumizi ya sheria kudai haki yameshindikana
*Walalamikia mishahara ya wabunge na ununuzi wa mashangingi
WAFANYAKAZI mkoani Dar es Salaam, wamempa siku 30 Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Nestory Ngulla, kufikisha malalamiko yao kwa Rais Jakaya Kikwete na kurejeshewa majibu, kuhusu nyongeza duni ya mishahara, ili kuepusha hatua nyingine watakazotumia kudai mishahara.
Tamko hilo lilitolewa na wafanyakazi hao kupitia risala yao iliyosomwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha maandamano ya amani yaliyoandaliwa na vyama 18 vya wafanyakazi nchini kupinga kima cha chini cha mshahara wa serikali, kilichopitishwa na bunge hivi karibuni.
Baadhi ya vyama hivyo, ni pamoja na cha Walimu (CWT), Sekta ya Afya (Tughe), Migodi, Nishati, Ujenzi (Tamico), Serikali za Mitaa (Talgwu), Mabaharia (Tasu), Walinzi binafsi (Tupse), Mashambani (Tpawu), Shughuli za Meli (Dowuta), Mawasiliano (Tewuta), Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (Raawu), Waandishi wa Habari (TUJ) na Chodawu.
Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wafanyakazi hao, Katibu wa Raawu, Kanda ya Mashariki, Evarist Mwalongo alisema wamefikia hatua hiyo wakiamini kwamba, matumizi ya kisheria kudai mishahara yatawafikisha katika hali mbaya.
"Hali hiyo itakuwa imelazimishwa na serikali. Wafanyakazi hatutaki kufikia hali hiyo kwani Uhuru wa nchi hii tuliutolea jasho sisi wenyewe," alisema Mwalongo na kushangiliwa na umati wa wafanyakazi waliohudhuria mkutano huo.
Mwalongo alisema, wafanyakazi mwaka huu, wanadai nyongeza ya mishahara kutokana na kukithiri kwa shida baada ya nyongeza hiyo kulimbikizwa kwa miaka zaidi ya 13 iliyopita, hali ambayo imesababisha makali ya maisha kutovumilika tena.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imekosa huruma na kuacha kutambua kuwa wafanyakazi nchini ndio waliodai Uhuru wakisaidiana na wakulima, badala yake imekuwa ikiwajali wafanyabiashara peke yake kwa kuwafanya kama ndio mhimili wake wa kusimamia sera, uchumi na siasa za nchi.
Mbali na hilo, Mwalongo alisema serikali imefikia kupuuza hata sheria zilizotungwa kusimamia na kulinda masilahi na masuala ya wafanyakazi.
Alisema inasikitisha kuona Wizara ya Utumishi chini ya Waziri wake, Hawa Ghasia, imeamua kudharau sheria namba 19 ya mwaka 2003 inayohusu majadiliano na vyama vya wafanyakazi kupanga mishahara ya watumishi wa serikali.
"Mheshimiwa Ghasia ameamua kupuuza utawala wa sheria na kuanza ukurasa mpya. Amepanga mishahara ya watumishi kadri alivyoona yeye kutoka Sh75,000 hadi Sh84,000.
Mshahara wa Sh84,000 unakatwa kodi ya Sh 600 kama kodi ya PAYE na akiba ya uzeeni Sh8,400, zinabaki Sh 75,000 ambazo ndiyo mshahara wa zamani.
"Mshahara huo ukigawa kwa Sh 30 utaona mfanyakazi ataishi kwa Sh2,500 kila siku ambazo zitumike kama matumizi mengine ya lazima kila siku. Kwa mantiki hiyo ndiyo maana vyama vya wafanyakazi vilipendekeza kima cha chini kiwe Sh315,000 sawa na Sh10,500 kwa siku," alisema Mwalongo.
Alisema inasikitisha pia kuoana Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana chini ya Waziri wake, Kapteni John Chiligati, imeamua kulala usingizi kwa kutosimamia sheria namba 6 ya mwaka 2004 inayotakiwa kuunda Baraza la kupanga kima chini cha mishahara kwa ajili ya sekta binafsi ambako kuna hali mbaya kupindukia kwa kuendelea kupata mshahara wa Sh48,000 tangu mwaka 2002.
"Sisi wafanyakazi hatuelewi kama serikali ipo kwa ajili ya Watanzania kwani kwa mshahara wa Sh84,000 ukigawa kwa Sh10,500 kama matumizi kwa mahitaji ya lazima ya kila siku utadumu siku nane na kama mfanyakazi atakula mlo mmoja kwa siku utadumu siku 16 tu.
"Mshahara huo wa Sh84,000 ni asilimia 50 au nusu ya posho ya mbunge anayopata katika kikao cha siku moja na mshahara wa mbunge wa mwezi mmoja ambao ni Sh1,500,000 unaweza kumlipa mfanyakazi huyo kwa miezi 17.
Uchambuzi kama huu ukiwekwa watumishi wa kima cha Sh84,000 inasikitisha kiasi cha kujenga hasira mbaya katika jamii ya Watanzania," alisema Mwalongo.
Alisema pamoja na shida za mishahara duni, serikali imetengeneza mzigo mzito unaotokana na bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2007/08, iliyokuja na kodi kubwa katika mishahara, mfumuko wa bei uliotokana na bei kubwa ya mafuta ya dizeli, petroli na vilainishi vya mitambo na kwamba, usafiri wa kwenda kazini na kurudi nyumbani umekuwa pia gharama kubwa inayowatesa wafanyakazi maradufu.
"Kukosekana kwa vyombo vya usafiri, suala hili halishughulikiwi na serikali kwa vile wakuu wote wanatumia magari ya gharama za kutisha yanayowalaza usingizi wasione kuna nini kwa wananchi. Inasikitisha kuona kiongozi anapita na VX ya Sh150 milioni bila hata ya huruma kwa mtoto au watoto wa shule kama hapendi kuwapa msaada wafanyakazi wenzie ingetosha kuwaonea huruma watoto wa shule.
"Gari aina ya VX moja ingeweza kununua gari la kubebea wafanyakazi zaidi ya 100. Mfano huu ukizidishwa kwa namba ya magari ya mawaziri na watendaji wakuu wa serikali yetu utaona serikali inao uwezo mkubwa sana wa kugawa mshahara wa kuishi wa Sh 315,000 bila kikwazo," alisema Mwalongo.
Alisema mishahara midogo wanayolipwa wafanyakazi, inaleta uhafifu katika malipo ya uzeeni kwa wastaafu ambao wametumikia serikali kwa uadilifu mkubwa.
Mwalongo alisema bila kujali kuwa mishahara ni midogo, serikali bado inaendelea kuwaonea wafanyakazi kukopa kwa nguvu jasho la wanyonge, kwa kulimbikiza madai ya nauli, likizo, malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, kama vile walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam na watumishi wengine wa manispaa na mashirika mbalimbali.
Alisema wakati hali ikiwa hivyo, soko la ajira limetekwa na wageni kwa visingizio na kejeli dhidi ya wafanyakazi wazalendo, kwamba Watanzania ni wavivu, wazembe, hawajui Kiingereza na kadhalika.
"Inasikitisha wanaotoa kauli hizo ni Watanzania wenzetu bila kutambua kuwa dawa za kutibu uzembe, uvivu na kutojua Kiingereza ni malipo mazuri, mbona Watanzania wanang'ang'aniwa nchi za nje kwa bidii ya kazi na kuzungumza Kiingereza chenye fasihi tamu?
"Tunasema waache kutukejeli kuanzia sasa, iwe mwisho kuuza nafasi zetu za kazi ovyo, waone aibu wawekezaji wao wameanza kuwekeza mpaka katika vibanda vya kukaanga viazi na maua ya plastiki, watainuaje uchumi wetu?" alihoji Mwalongo.
Kutokana na hali hiyo, alisema iwapo mishahara haitaongezwa italeta athari kubwa, ikiwamo wafanyakazi kushindwa kushiriki katika vita dhidi ya rushwa, kiwango cha umaskini kitakithiri katika jamii, kipindupindu, ujinga, kukosekana tija ya taifa na nidhamu ya kazi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhadhiri Mstaafu wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji, aliishangaa serikali kuona ikikataa kutambua kwamba, wananchi hivi sasa wanakabiliwa na kipindi kigumu kutokana na kujenga mgawanyiko na mpasuko katika jamii ya Watanzania.
"Kuna kundi la matajiri na maskini, tuna tabaka la walala heri na walala hoi. Kama tutaendelea katika mwelekeo huu kwa kasi, tutajikuta tuna mataifa mawili," alisema Profesa Shivji na kushangiliwa na umati wa wafanyakazi waliohudhuria mkutano huo.
Katibu wa Kanda ya Dar es Salaam wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi nchini (Cotwu), Buhari Semvua, akizungumza katika mkutano huo, alipinga msimamo wa serikali wa kuendelea na majadiliano Septemba, mwakani na wafanyakazi kuonya kuwa iwapo serikali itapuuza malalamiko yao nchi haitakalika.
"Hatukubali hiyo mwakani na wajue kuwa wananchi wakikata tamaa, hatua watakazochukua, patakuwa hapakaliki, hapatoshi. Siku 30 tusipojibiwa, hizi (maandamano) za leo ni rasharasha," alisema Semvua.
Naye Ngulla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka wafanyakazi kutobabaishwa na wabunge na kuahidi kwamba, atahakikisha anafikishia serikali malalamiko yao ndani ya muda aliopewa.
Mkutano huo ulitanguliwa na maandamano ya wafanyakazi hao yaliyoanzia katika Ofisi za Makao Makuu ya Tucta, Mnazi Mmoja saa 2:00 asubuhi na kupita katika Barabara za Bibi Titi Mohamed na Morogoro na kuishia katika Viwanja vya Jangwani, huku waandamanaji wakiwa wamebeba mabango na kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kuilaani serikali.
Baadhi ya mabango yalisomeka: "Walalahoi Sh84,000 kwa mwezi, mbunge Sh120,000 kwa siku, haki iko wapi?" "Mshahara huishia nauli ya daladala, vigogo kwenye mashangingi, kima cha chini kiongezwe, hii ni haki", "Mishahara iendane na hali halisi ya uchumi wa nchi kwa sasa", "Bila walimu Rais Kikwete ungekuwa wapi? Mbona hutukumbukwi?"
"Nauli za likizo hazitolewi kwa wakati kwa nini? Walimu tunateseka", "Haturidhiki na waraka mpya wa mshahara", "RAAWU Taasisi ya Watu Wazima. Kwa ari hii, kasi hii, nguvu hii na mishahara hii ya wafanyakazi tumekwisha!" "Kuna siri gani kati ya sekta binafsi na serikali kuhusu mishahara?"
Mbali na mabango hayo, waandamanaji hao walikuwa wakiimba kwa kusema: "Na sisi hatulali, bado mapambano, mpaka kieleweke", "Kilio, kilio, kilio, tutamlilia nani?"
3 comments:
Maandamano: Serikali nayo yajibu mapigo
2007-08-11 15:24:58
Na Jane Mkonya, Jijini.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menegimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Hawa Ghasia ameliambia shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) kuwa maandamano yao hayataifanya Serikali kuongeza kiwango chochote cha fedha katika mishahara yao.
Akiongea kwa njia ya simu, Mhe. Ghasia amesema Serikali imeshangazwa na uamuzi wao wa maandamano, kwani walishaongea na TUCTA walipopeleka malalamiko yao na wakakubaliana na kiwango kilichowekwa na Serikali.
`Nimeshangaa kusikia TUCTA wataandamana leo, kwani jambo hili tulishalimaliza tulipokutana nao na tukakubaliana kuwa Serikali haitaweza kuongeza kiwango hicho kutokana na hali halisi ya uchumi,` akasema Mhe. Ghasia.
Amesema Serikali huongeza mshahara kutokana na hali ya uchumi ya mwaka wa fedha husika.
Ametaja mwaka wa fedha uliopita, yaani 2006/07 Serikali iliongeza kiwango cha mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia hamsini lakini akasema mwaka huu wameshindwa kufanya hivyo kutokana na hali halisi ya uchumi.
Amesema TUCTA inapaswa kuelewa kuwa Serikali haiko kwa ajili ya kushughulikia wafanyakazi tuu bali pia mambo mengine yahusuyo jamii kwa ujumla ikiwemo afya, elimu, miundombinu na mahitaji mengine kama maji na umeme.
`Wafanyakazi ni sehemu ndogo katika jamii, yapo mambo mengi ambayo hajakamilika na yanayohitajika kushughulikiwa na Serikali,` akasema.
Amesema kutokana na hali ya uchumi , Serikali imeshindwa kutekeleza madai ya wafanyakazi ya kulipa kima cha chini kwa shilingi 315,000.
Mwaka huu wa fedha serikali imetangaza kima cha chini cha mshahara kuwa ni shilingi 84,000.
SOURCE: Alasiri
Serikali inaposema uchumi unakua, haijui kuwa kukua huko huletwa na wafanyakazi na wakulima? Kwanini wazalishaji hawa wasifaidi matunda ya jasho lao na badala yake serikali inatumia jasho la wafanyakazi kuwahonga[corrupt] wabunge ili wasiibane serikali bungeni kwa kuwapa maslahi zaidi. Je hali ya uchumi inaruhusu tu pale wabunge wanapoomba waongezewe malipo na huwa mbaya pale wafanyakazi wanapoomba kuboreshwa hali zao???
Nchi inapoongozwa na wezi unatarajia nini?
Post a Comment