Sunday, February 04, 2007

Miaka 30: Hukumu ya CCM


Uchambuzi huu murua, ulioandikwa na Mwandishi Wetu wa gazeti la Mwananchi, umechukuliwa kutoka gazeti la Mwananchi Jumapili, Februari 5, 2007 ukiwa na kichwa cha habari MIAKA 30 CHAMA TAWALA KIMESAHAU NGUZO ZILIZOKIJENGA. Kweli. Tukiihukumu CCM kwa miaka 30 ya umri wake, tuna kila sababu ya kukubaliana na mwandishi huyu. Endelea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), leo kinaadhimisha sherehe za kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. Mengi yamezungumzwa kuhusu historia ya chama hiki, lakini kubwa ni kuwa, sasa CCM imegeuka na kuacha nguzo zilizo katika bendera yake.Kwa namna yoyote ile, chama hicho kinaonekana hakichangamani kimatendo na nembo zinazokipambanua katika bendera yake.

Bendera ya CCM ina nembo ya jembe na nyundo, jembe likiwakilisha wakulima na nyundo wafanyakazi. Rangi ya kijani inabeba bendera ya chama hiki, ikiashiria maisha bora kwa wanachama wake, lakini pia maana hii inazua maswali zaidi sasa ambapo hali ya maisha ya wananchi hasa kundi la wakulima na wafanyakazi inazidi kuwa duni kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Wakulima wameweka rehani kazi yao kwa wafanyabiashara na serikali, hasa inapokuja suala la bei za mazao na uzalishaji wenyewe. Ukame umekuwa kero na hakuna mkakati wa kilimo cha manufaa, kilimo kinachozingatia umwagiliaji na chenye kutumia zana za kisasa na chenye muelekeo wa kuboresha uzalishaji.

Mfano, zao la korosho linakosa ununuzi na serikali, inaonyesha kushindwa kuwadhibiti wanunuzi ambao ni wafanyabiashara wa zao hilo. Mazao kama pareto, katani, karafuu, pamba na mengine ya biashara hayawanufaishi tena wakulima. Ulimaji wa mazao haya umebakia wa rasharasha na hakuna mikakati ya wazi ya kukuza uzalishaji wake. Bei za mazao hayo zimekuwa zikishuka bila kuwiana na kupanda kwake, huku gharama za uzalishaji zikionyesha wazi kupanda hali inayowafanya wakulima kutoona faida.

Huku ni kushindwa kwa CCM, chama ambacho kimeendelea kunufaika na kutawala dola tangu kuzaliwa kwake, licha ya kuwa Tanzania sasa inafuata mfumo wa vyama vingi, mfumo uliopitishwa na kuanza mwaka 1992. Hali hii ni tofauti na nchi za jirani kama; Malawi, Kenya na Zambia ambazo vyama vyao vyenye umri unaokaribiana au kuzidi ule wa CCM vilishapigwa mweleka katika chaguzi za vyama vingi.Kama kuna mafanikio katika maisha ya watanzania hakuna uwezekano wa kuyatenga na sera za CCM, na kama kuna kudorora kwa maendeleo CCM inahusika pia.

Ukweli kuna kushindwa katika muendelezo wa sera za CCM na chama sasa hakiwezi kusimama na kutangaza itikadi yake na mikakati yake ya muda mrefu kama ilivyokuwa wakati wa uanzishwaji wake mwaka 1977.Wafanyakazi wa Tanzania wako katika hatihati siku zote tangu kuingia sera za ubinafsishaji, sera zilizoambatana na upunguzaji wa wafanyakazi, kupungua kwa ajira katika sekta rasmi na pia kufa kwa viwanda mbalimbali nchini.Eneo pekee ambalo linaonekana kuwa kauli mbiu ya viongozi wa CCM ni biashara, nchi haijaweza kuzalisha soko la ndani kwa ajili ya bidhaa za humu lakini imezidi kuzungumzia suala la ujasiliamali.

Wafanyabiashara wana nguvu ya maamuzi katika chama kufuatia uwezo wao wa kukifanya chama kifanye kazi. Chama hiki licha ya kujirithisha mali zote zilizozalishwa wakati wa mfumo wa chama kimoja, bado hakijaweza kujiendesha na uhakiki wa mali zake unazua maswali.Miradi mbalimbali ya chama hiki ilikufa na baadhi ya mali zake kutumiwa na wajanja wachache.

Chama sasa hakitegemei tena ada ya wanachama wake badala yake michango ya wafanyabiashara na matajiri. Chama sasa kinazungumzia sera za ustawisho kwa matajiri maana ndio wana nafasi pia ya kuchaguliwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Mwana CCM maskini anabaki na nafasi ya kupiga kura tu na hawezi kuchaguliwa.

Chama sasa kinawatumia matajiri katika kuwania nafasi mbalimbali ili kurahisisha wao kutumia nguvu zao kiuchumi kujipigia kampeni na pia kusaidia wagombea wengine wa chama hicho. Inachikifanya sasa CCM ni kusaka viti vingi katika nafasi za uwakilishi na sio kugombania kupata viongozi bora, wenye dira na nia ya kuendeleza nchi na watu wake.Kwa hali hii nafasi ya maamuzi kutoka kwa raia wa chini, wakulima na wafanyakazi ni finyu.

Hali hii inahatarisha maisha ya kundi kubwa la watu ambao ni maskini nchini, kufuatia wawakilishi kutokuwa na mipango ya wazi ya namna ya kuendeleza vipaumbele vya maendeleo katika nchi.

No comments:

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'