Wednesday, September 29, 2010

Dk Slaa azungumzia mambo makuu matatu

Viti Maalumu

Kwanza amezungumzia suala la Viti Maalumu kupitia CHADEMA, akaweka wazi kilichoazimiwa na Kamati Kuu ya chama. Majina 105 kati ya 147 ya walioomba kuteuliwa viti maalumu, yamepitishwa; na sasa yatapelekwa Tume ya Uchaguzi kama sheria inavyodai. Walioteuliwa hawakutajwa majina kwa waandishi. Mfumo wa uteuzi ulizingatia vigezo sita (6) vilivyoainishwa na mtaalamu aliyeteuliwa na chama hicho ili kuifanya kazi hiyo, Dk. Kitila Mkumbo. Vigezo hivyo ni 1. Kiwango cha Elimu. 2. Uzoefu wa kazi ya kisiasa. 3. Uzoefu wa uongozi nje ya siasa. 4. Kugombea Jimbo. 5. Mchango wa mgombea katika chama na kampeni zinazoendelea. 6. Umri wa mtu katika chama. Kila kipengele kilikuwa na vigezo vidogo vidogo kama vinne, vyenye alama tofauti. Na kwa mujibu wa Dk Slaa na Kitila, viti hivyo vimetawanywa nchi nzima, kwa kuzingatia vigezo hivyo hivyo. Akahitimisha kwa kusema: "Ingawa kuna usemi kwamba siasa ni mchezo mbayan, kwa Chadema, siasa ni sayansi na unachezwa kisayansi." Alitumia pia fursa hiyo kusisitiza kuwa Chadema kimeweka wagombea 185 ambao ni ziaidi ya asilimia 75 ya wagombea ubunge nchi nzima; na kwamba idadi hiyo kinatarajia kuvuna wabunge wa kutosha, na kiko tayari kuunda serikali.

Usalama wa Taifa

Dk. Slaa alitumia fursa hiyo kutamka kwamba ana taarifa za kikachero kuwa Rais Kikwete ameagiza wana usalama wa taifa wasambae nchi nzima kuhujumu uchaguzi. Akasisitiza kwamba, "kwa sura ya sasa, Kikwete ameshashindwa...na amani ya nchi ikivurugika, Kikwete ndiye atabeba lawama na laana.." Alisisitiza pia kuhusu waraka uliosambazwa nchi nzima ukiwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchi nzima kufanya kila wawezalo kulazimisha ushindi wa CCM. Akasema hujuma hii inaweza kusababisha umwagaji damu, na kwamba asingependa itokee.

Utafiti na vitisho vya Synovate

"Tunasubiri kusikia Synovate wamefungua kesi. Kama hawajaenda, waende sasa. Wasipofanya hivyo tutawaharibia credibility yao hapa nchini na kimataifa. Chadema tunapofanya kitu chetu huwa haturudi nyuma. Hatuna woga. Gazeti lililoshitakiwa nalo lisiwe na woga." Baada ya hapo alionyesha vielelezo vya utafiti uliofanywa na Synovate, ambao katika kipengele GPO 6 liliulizwa swali: "Kama ucahguzi ungefanyika leo, nani ungempigia kura ya urais?" ambalo Synovate walikanusha kwamba halikuwamo katika utafiti wao, wakidai wanataka kuufanya baadaye kabla ya uchaguzi mkuu. Ukweli ni kuwa walifanya utafiti lakini CCM iliingiza 'mkono' wake baada ya kubaini kuwa matokeo hayo yalikuwa yanaonyesha Kikwete yuko nyuma ya Dk Slaa.

Tahadhari ya Mbowe

Freeman Mbowe alitoa tahadhari kwa Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, na Msajili wa Vyama vya Siasa, akisema wamepewa mamlaka ya umma, ambayo wakiyatumia vizuri wanaweza kulipeleka taifa kwenye amani, na wakifanya makosa wanalitumbukiza kwenye ghasia. Akasema kinatokea sasa, CCM wameshindwa siasa za majukwaani, na watatu hawa wako katika mikakati michafu ya kuvuruga uchaguzi. Akasema kama wanatakua kuugeuza uchaguzi wa uchakachuaji, hapatatosha! Aliwaomba Watanzania kuwa tayari kulinda maamuzi yao, kura zao. Akasisitiza: "Tunaomba Watanzania na jumuiya ya kimataifa mtuelewe..."

2 comments:

Anonymous said...

Ndugu yangu mbona hatupati updates za kila siku bwana. Maana uko kwa JK naona wanaingia kwenye facebook za watu na kutuma message...tunaomba update za kila siku.

Geoff said...

speaking from the trueth, dr. Slaa amekuwa ni threat kubwa sana kwa CCM tofauti jinsi wao walivyotarajia. kwa situation hii 2liyonayo Tanzania ya ufisadi na mafisadi tunamhitaji mpiganaji wa kiukweli na mwenye uthubutu kama Dct. Wilbroad P Slaa. Jamani tumpe "shavu" huyu dkt ili 2we na serekali yenye uthubutu wa maamuzi yenye maslahi kwa umma na sio mafisadi.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'