Monday, October 11, 2010

Slaa: Sitaki Urais wa Damu


Akiwa mwishoni mwa ziara yake mkoani Kigoma, Dk Slaa aliwataka wananchi kujihadhari na CCM na Kikwete kuhusu kauli za kuwamga damu zinazosambazwa na wanapropaganda wa CCM. Hii ndiyo kauli yake:

“Mimi sitaki kwenda Ikulu kwa kumwaga damu ya Mtanzania yeyote. Sijatamka hata siku moja kumwaga damu. Nataka uchaguzi wa amani na utulivu. Katika mikutano yangu zaidi ya 400 niliyofanya sasa, nimehimiza watu wangu kuzingatia amani…Nyie mkipigwa shavu hili geuza jingine, msiwe chanzo cha vurugu.

“Amani haihubiriwi, bali inajengwa kama vile Chadema inavyowajenga Watanzania katika sera zake. Tunaposema kutoa elimu bure, afya bure na kuboresha makazi ni kwa faida ya Watanzania wote, hatutaki kujenga matabaka….Lakini CCM imekuwa inapeleka vijana wake kwenye makambi kujiandaa kufanya fujo…Lakini wajue kuwa amani itakuwapo kama haki itatendeka.

2 comments:

Monsignor said...

Umenena vema mheshimiwa Slaa.

Sehemu yeyote pasipo haki, amani haitakuwepo hata kama nguvu za dola zitatumika. Kuimba nchi yetu ina amani wakati wananchi wake wana jakamoyo na fukuto la matatizo nafsini mwao ni kujidanganya wenyewe. Kwa dhuluma na shida tunazoletewa na CCM na genge lao la majambazi, kamwe haitakaa kuwe na amani ya kweli nafsini mwa wananchi wanaodhulumiwa haki zao.

Kilichopo ni utulivu tu, amani inabaki utenzi wa kale ulioanza kuchusha masikioni mwa wasikilizaji wake. Viongozi lazima wajifunue na kuziacha nguo zao za dhihaka na kujua umuhimu wa kuwapatia wananchi haki na huduma bora wanazostahili bila hivyo amani wanayoimba kuwa wanaijenga majukwaani itabaki kuwa toleo la kale la shairi lililokosa vina na mizani na lenye kuudhi masikioni mwetu.

Swali kwa watanzania wanyonge, je wanajua kuwa hicho wanachodanganywa kuwa kinalindwa kwa jina la amani na hao CCM na danguro lao la wezi, kimebaki tu kuwa santuri ya kale yenye 'mikwaruzo' iliyokosa uhalisia na isiyo na mantiki ya ukweli ndani yake? Je wanajua kuwa hao wanaojidai wanakuja kwa jina la amani ndiyo wavunja amani wenyewe? Kwamba kwa matendo yao ya kifisadi na kuhujumu haki za raia wanatengeneza makovu na vidonda vyenye maumivu makali ya maisha mioyoni mwetu? Kwamba kuimba kwao amani amani amani ni ghiliba tu za kutuaminisha kuwa wanaipigania ilhali wanaibomoa kwa kutufisidi?

Sipendi unafiki wa CCM wa kuhubiri na kuimba amani, kutenda na kucheza uvunjifu wake.

Kwamba CCM wanajifanya hawajui kuwa mtu asiyejua atakula nini ifikapo jioni ya leo ilhali hajala tangu jana yake hana amani moyoni mwake?

Kwamba CCM haijui kuwa mtu aliyefiwa na mkewe wakati wa kujifungua kwa vile hospitali ipo mbali, au kwamba barabara ambayo ingetakiwa kutumika kwa ajili ya kumsafirsha mgonjwa kwa ama ambulance au 'bajaj' ni mbovu yenye mahandaki na madimbwi ya kufugia samaki au kwamba hata hilo gari lenyewe la wagonjwa au bajaj hazipo hapo kijijini, hana amani moyoni mwake?

Kwamba CCM wanajifanya hawajui mtu anayelazimishwa kunywa maji yenye sumu ya Mercury kwa vile mito na vyanzo vyote vya maji kijijini vimeingia sumu toka mgodini, na kuwa kila alalamikapo serikali inamkebehi na kutishia kumfunga, hana amani moyoni mwake?

Kwamba CCM hawajui kuwa mtu aliyebambikiwa kesi na kuhukumiwa pasi na haki kwa vile tu polisi, mkuu wa kituo cha polisi na hakimu walikula rushwa kutoka kwa mwenye pesa mmoja kumbambikia kesi, hana amani moyoni mwake?

Kwamba CCM haijui kuwa mlalahoi anaumia pale serikali inayochezea pesa nyingi kwenye mambo ya anasa na safari za viongozi kwenda kubembea nje kwa kisingizo cha kwenda kuomba misaada ya chandarua wakati mtoto wake wa chini ya miaka mitano amekufa juzi kwa malaria, ugonjwa unaozuilika na kutibika vizuri, hana amani moyoni mwake?

Kwamba mwanafunzi aliyefaulu shule ya msingi kwenda sekondari anashindwa kwenda sekondari kwa vile tu familia yake imekosa pesa za kumpeleka shule wakati serikali ina uwezo wa kumgharamia akasoma bure ama kwa gharama nafuu lakini haitaki na huku ikitoa lugha za kejeli, hana amani moyoni mwake?

Wengi hatuna amani na mfumo wa kirafiki wa kifisadi na kifamilia wa kisultani unaotumika kuongoza nchi yetu kwa sasa, kwa hivi lugha za CCM kutudanganya eti wanalinda amani ni upuuzi mtupu. Wasijidanganye nafsi zetu zinajua kuwa kuna utulivu tu ambao nao una kikomo chake na kuwa pindi jamii itakapochoka vyote vitatoweka, ingawa naombea tusifikie huko.

Anonymous said...

erfree

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'