Wednesday, September 08, 2010

Hii ndiyo Kauli ya First Lady wa Slaa

Kwa waliokuwa wanasubiri kauli ya First Lady wa Dk. Slaa, hasemi tena. Soma hiki hapa:

Josephine Mushumbusi, amezungumza kupitia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia ni wakili wa Dk Willibrod Slaa, Tundu Lissu, akaviambia vyombo vya habari kuhusu tuhuma zinazowakabili yeye na Dk. Slaa kuwa kwa mara nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimerejesha mfumo wa uchaguzi unaobadilishwa kuwa mfumo ya kijinga (a silly season). Akasema kwamba CCM wamekuwa wakikishambulia Chadema kuwa ni chama Wachagga; kwamba baadhi ya viongozi wake ndio walimuua Chacha Wangwe; na kwamba Dk Slaa ametumwa na kanisa Katoliki kugombea urais; lakini baada ya kuona hadithi hizo zimepuuzwa, sasa wameibuka na suala jipya na “ndoa za Dk. Slaa” wakidhani zitawasaidia kugeuza macho ya umma kutoka kwenye masuala muhimu ya wakati huu.

Akasema CCM hawataki Dk. Slaa na Chadema wajadili wizi, ubadhirifu wa fedha na mali za umma; hawataki wajadili wizi wa Sh. bilioni 772 zilizoibwa katika mwaka 2008/9 tu, kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali; hawataki Chadema itaje majina ya wezi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT); hataki Chadema wajadili jinsi JK na rafiki zake, akina Edward Lowasaa, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na Rostam Azizi walivyofilisi taifa hili; hawataki Chadema ijadili madai halali ya wafanyakazi wa Tanzania na ahadi za ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’ CCM hawataki Chadema kijadili sera mbadala ambazo zinalenga kuwakomboa Watanzania kutoka lindi la umaskini.

Wanataka kulielekeza taifa zima katika kujadili masuala ya ‘chumbani’ kwa Dk. Slaa; analala na nani, ana wake wangapi, kawapata wapi na kadhalika; ili kwa kufanya hivyo mgombea wao awarubuni wananchi kwa ziara mikoani na ahadi kemkem zisizotekelezeka.

Tundu Lissu amesisitiza kuwa kila wanapoona wamebanwa, CCM huwa wanabuni njama za kukomoa washindani wao, kama walivyofanya huko nyuma. Alitoa mifano ya kilichotokea miaka ya 1995 na 2005.

Mwaka 1995: Kwa kumwogopa Mrema aliyekuwa tishio kwa CCM, walimtumia mwanamke mmoja, aitwaye Angelina, wakidai ni kimada aliyezaa na Mrema; akawa analala getini kwa Mrema, Masaki, Dar es Salaam. Wakamdhalilisha. Baada ya uchaguzi, Mrema akashindwa, na suala la Angelina halikujadiliwa tena.

Mwaka 2005 tishio la CCM ilikuwa Chama cha Wananchi (CUF), hasa Zanzibar. CCM wakamtumia Inspekta Jenerali wa Polisi, Omar Mahita, siku chache kabla ya uchaguzi, kudai kuwa amekamata lori lenye mapanga, majambia, visu na silaha nyingine zenye nembo ya CUF. Wakakipaka chama matope. Baada ya uchaguzi, hatukuelezwa lolote kuhusu visu hivyo.

Mwaka huo huo, katika uchaguzi wa ndani ya chama, baada ya kundi la JK kuona limezidiwa mno, likaamua kumzushia Dk. Salim Ahmed Salim likidai ni Mwarabu, na muuaji wa Rais Abeid Amani Karume. Wakamhujumu, Na baada ya uchaguzi hawakuzungumzia tena uarabu wa Dk. Salim.

Mwaka 2010: Tishio la CCM ni Chadema na Dk. Slaa. Baada ya kuona upepo unawaendea vibaya, CCM wameamua kufanya siasa za mtaro wa maji taka; hizi wanazotumia watu kumwandama Dk Slaa.

Tundu Lissu alisema kuwa Chadema hawako tayari kufanya siasa za majitaka; na kwamba Watanzania hawako katika kujadili mambo hayo, kama hali ya afya za wagombea, ambao baadhi wanadaiwa kuwa na virusi vya ukimwi kiasi cha kubadili damu kila baada ya miezi, na kwamba kwa sababu ya unyonge huo, baadhi yao waanguka mara kadhaa jukwaani.

Akasema wao hawatazungumzia baadhi ya wagombea urais wana wake wangapi, mahawara wangapi, na wamewaweka katika ofisi gani za umma, wapi wamepewa mikataba minono ya fedha kwa upendeleo, na kadhalika. Akasisitiza kwamba Chadema haitajibu uchafu unaosambazwa na vyombo vya habari, lakini akasema, “sauti yetu itasikika iwapo wataenda mahakamani.”

Akasema Chadema itazungumzia umaskini wa Watanzania na namna ya kuupunguza au kuuondoa; jinsi Tanzania ilivyo nchi ya tatu katika Afrika lakini wanakijiji wanalazimishwa kujenga shule za kata huku serikali ikifuja mabilioni ya pesa (kama hizo bilioni 772/- zilizotafunwa ndani ya mwaka mmoja.

Akasema Chadema itajadili malipo ya anasa kwa mawaziri, maisha duni ya polisi, walimu, wauguzi na makundi mengine yanayonyonywa katika jamii. Akasema Chadema itajadili jinsi ya kuboresha afya za wananchi.


Akasema, “hatutaki siasa za chumbani, bali za hadharani.”

Kwanini wamshambulie Dk Slaa? Kwa sababu ni Dk. Slaa.

- Ana rekodi ya kuwashinda CCM mara tatu, kwa miaka 15 mfululizo
- Amekuwa sauti kuu ya wananchi Bungeni, inayotetea masilahi ya umma
- Kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kuwapo Tanzania ndani ya miaka 50, ni Dk Slaa pekee aliyetaja hadharani mafisadi 11 bla woga wowote. Walioathirika kwa ujasiri wake ndio hao wanaomsakama sasa kwa mambo ya chumbani badala ya mambo ya hadharani.

2 comments:

Stella said...

Ya Mrema na kimada wa kuchorwa Angelina, ya Dr. Salim Ahmed Salim na kifo cha kusingiziwa cha Hayati Rais Karume, ya CUF na visu na majambia vya kughushi, ya Dr. Slaa na shutuma za Ukatoliki, yalipita. Hili nalo la Dr. Slaa na Josephine litapita pia.

Watanzania, masikio yasikilize lakini akili ichuje na kuamua. Yote ya huko nyuma yalikuwa batili - uzushi, uwongo, fitina, n.k, kwa nini hili nalo lisiwe batili?

Majessah said...

Yaani...CCM wanataka kutuswaga watanzania na kutufungia chumbani kwa Dr. Slaa ili tushangaeshangae tukitahamaki.... wamepita tena kwa kinachoitwa kishindo! Hongereni CHADEMA kwa msimamo unaotuthibitishia ukomavu wenu. Ni wapumbavu tu wanaohangaika kujadili masuala ya chumbani na kuacha masuala makini yanayohatarisha usalama na mustakhabali wa taifa zima.
CCM ni wanafunzi mbumbumbu kabisa wa Mwalimu Nyerere na ushahidi ni kina Kikwete waliopalilia ubaguzi miongoni mwa watanzania tena wanachama wenzao wa CCM kwa kuwaita wahamiaji haramu. Wamesahau kabisa onyo alilolitoa Baba wa taifa muda mfupi kabla hajatutoka alipofananisha wabaguzi na wachawi waliowahi kula nyama za watu kwamba huwa na kiu isiyokwisha.
Tunayafahamu mapungufu mengi ya vyumbani ya viongozi waandamizi wa CCM kuanzia mgombea wao wa uraisi hadi wadogo wa chini kabisa; lakini hatuoni sababu za kuyajadili kwa vile tuna mjadala muhimu, makini wa mustakabali wa taifa letu.
Tunasema Aluta continua; Chadema endeleeni kuwapa presha kina Makamba na ze komedi wao.
Hatudanganyikiiiiiiii........

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'