Monday, August 30, 2010

Slaa akata anga Morogoro

LEO Dk. Willlibrod Slaa alikuwa mkoani Morogoro, katika wilaya za Mikumi na Mvomero. Mikutano imefana. Amesisitiza haja ya Morogoro kuwa na wabunge wa upinzani ili kuongeza uwajibikaji katika halmashauri za mkoa huu, na katika nchi nzima kupitia Bunge; na kudhibiti wizi wa fedha za umma.

Akiwa Mikumi, alimlipua mwenyekiti wa kamati ya kampeni za CCM, Abdulahman Kinana, akisema kigogo huyo ana mkono katika biashara chafu za makampuni ya meli; akamtaka ajielekeze katika masuala ya kitaifa badala ya kumwandama yeye (Slaa). Akasisitiza kwamba ana ushahidi wa kauli zake, kwani hana historia ya kukurupuka.

Kauli hiyo ya Dk. Slaa inakuja siku moja baada ya Kinana kujibu mapigo ya makada wa Chadema, hasa Mabere Marando, ambao waliwataja hadharani vigogo wanaohusika na ufisadi mkubwa, huku CCM ikilalamika kwamba chama hicho cha upinzani kinatoa matusi.

Katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za Chadema, Marando alisema vigogo waliohusika na wizi wa EPA ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Rostam Azizi na Edward Lowassa, akasema waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi ni dagaa wanaoonewa ili kuficha madhambi ya wahusika wenyewe wa ufisadi.

Juzi Kinana alijitokeza na kumbeza Dk. Slaa, kwamba anatumia lugha ya matusi kwenye kampeni kinyume cha makubaliano waliyosaini. Dk. Slaa jana alisema mtu akiiba anaitwa mwizi; na kwamba kumwita hivyo si matusi.

1 comment:

Anonymous said...

Wape vibao vyao dk Slaa. wao wanaogopa hata kutaja neno ufisadi kwa sababu wanajua kuwa mafisadi ni wao. hawawezi kujishtaki. sasa anapotokea mtu wa kuwashtaki wanakimbilia maadili ya uchaguzi ambayo waliyasuka hivyo ili wasiumbuliwe katika kampeni. wape wezi wakubwa hao k(NENO BAYA) wanatesa wananchi na kisha kwenda kuwachekea majukwaani!!!!!

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'