Tuesday, February 21, 2006

Taaluma ya Zombe ni ipi?

ALIPOULIZWA na waandishi wa habari mapema mwaka huu juu ya habari kwamba watu wanne waliouawa na polisi jijini Dar es Salaam hawakuwa majambazi bali wafanyabiashara, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Abdallah Zombe, aliwataka wananchi wasiingilie kazi ya polisi. Alisisitiza:

"Upolisi ni taaluma kama nyingine. Unasmomewa. Sisi ndio tunaweza kusema fulani ni jambazi au la..."

Sasa wenye taaluma yao, wakiongozwa na Jaji Kipenka Musa, wametoa taarifa ya tume inayoonyesha kuwa waliouawa hawakuwa majambazi. Askari polisi 15 wamehusishwa na mauaji hayo ya kikatili na uporaji wa mamilioni ya shilingi.

Zombe ameumbuka. Wananchi wanahoji: "Taaluma yake ni ipi sasa?" Taarifa zinasema naye yuko chini ya ulinzi, anahojiwa, huku akisubiri kuvuliwa vyeo vyake ili ashitakiwe kwa makosa yake, ingawa vyanzo vya kipolisi vimesema hatashitakiwa kwa mauaji, bali kwa 'makosa mengine.'

Lililo wazi ni kwamba wananchi wanaonekana kuchukizwa na kitendo cha Zombe kutopelekwa mahakamani Jumapili 20.02.2006 pamoja na askaro polisi wanne waliokwisha kamatwa.

Nashangaa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, anatoa kauli za kupinga taarifa za vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa Zombe. Watu wanajua kwamba alikwisharudishwa mkukumkuku kutoka Rukwa alikokuwa amepelekwa kuwa RPC; wanajua kuwa amekuwa akihojiwa makao makuu ya polisi; lakini Tibaigana anasema Zombe hajatiwa mbaroni, wala hahusiki!

Anaficha nini? Sasa kama hajatiwa mbaroni, katiwa wapi? Tibaigana hajaeleza Zombe yuko wapi? Anamkingia kifua? Vyovyote itakavyokuwa, Zombe keshakuwa Zombe, na wananchi wanataka serikali imzombe, haki itendeke! Vinginevyo, tutasema bado serikali inaendekeza kulindana.

Wednesday, February 15, 2006

Nimerejea ulingoni

WAPENDWA wanablogu, nilipotokomea sikuaga, kwa sababu haikuwa nia yangu kujitenga nanyi. Sasa nimerejea. Kwa muda nilikuwa mafichoni. Baadhi ya walionikosa kwenye blogu walitumia njia nyingine za kuwasiliana nami, wakahoji kama niko uhamishoni! Hata bila kujibu nilikuwa wapi, nafurahi kuwatangazia maswahiba wote kwamba sasa nimo ulingoni. Nimefurahi kuwakuta wanablogu wapya, kina Jeff Msangi (niliyemuathiri binafsi kuingia kwenye blogu) wakiwa wanatamba. Picha za Muhidin Issa Michuzi zimekuwa kivutio kingine. Hoja tekenyo za Reginald Simon zimekuwa kiburudisho kikubwa, bila kusahau hoja nyeti za painia Ndesanjo Macha. Nakiri kwamba nilikosa mengi katika muda niliokuwa mbali na wanablogu. Yawezekana pia nimewanyima machache kadhaa niliyokuwa nayo. Tafadhari mnisamehe. Sasa nimerejea.

Thursday, February 09, 2006

Picha iliyowaponza Tanzania Daima Hii Hapa


NOVEMBA 6, 2005 Gazeti la Tanzania Daima lichapishwalo na Free Media Ltd ya Dar es Salaam, lilikuwa na habari na makala nzito juu ya kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar wiki hiyo uliomrejesha Rais Amani Karume madarakani. Mbele ya gazeti kulikuwa na picha hii. Gazeti liliuzwa hadi likaisha. Walilenga kuchekesha, wakanunisha wakubwa. Walitumaini wako huru, wakajikuta mahabusu. Soma hapa. Na dunia nzima ilitambua ubabe wa serikali ya Tanzania. Ona!

Saturday, January 14, 2006

Limekuja Lenyewe, Hili Hapa


KILE zilichoshindwa timu zetu za soka, Coca-Cola imeweza: kulileta kombe la dunia Tanzania. Walau imetuwezesha kuliona, kulishika, kulinusa na kupiga nalo picha. Walau hili tumeliweza! Sijui uwezo wetu ndo umeishia hapo, au tumehamasika!

Monday, November 14, 2005

TEKNOHAMA Kazini; Sengerema Hadi Tunis


Felician Ncheye ni mkazi wa Sengerema, mkoani Mwanza. Kazi yake ni kutoa huduma ya mawasiliano kwa njia ya mtandao wa kompyuta kwa wakazi na wapita njia wa Sengerema kwa kutumia kituo chake, Sengerema Telecentre. Katika picha hii, yupo Tunis, kwenye Banda la Tanzania, katika mkutano wa dunia kuhusu Jamii ya Habari na Mawasiliano (WSIS), alikokwenda kuwaonyesha wananchi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwamba naye wamo katika mtandao. (Picha na Ansbert Ngurumo 14.11.2005)

Kazi na Tabasamu


Anaitwa Amissa Chayeb, mhudumu katika mgahawa mmojawapo katika kituo cha kumbi za mkutano, KRAMA Palexpo, Tunis, unapofanyikia mkutano wa Umoja wa Mataifa ulioikusanya dunia nzima kujadili namna ya kutumia TEKNOHAMA. Kazi ya Amissa ni kuwapatia wateja huduma- chai, kahawa, maziwa na vitafuno kidogo - lakini dakika hii, hawapo. Afanyeje? Sana sana kutabasamu, akimngoja mmoja mmoja anayeingia.

TEKNOHAMA Yapamba Moto Tunis


MACHO ya dunia nzima yapo jijini Tunis, nchini Tunisia; Afrika Kaskazini. mataifa tajiri na maskini yamewakilishwa, kujadili namna ya kuzifanya teknolojia za habari na mawasiliano yamtumikie binadamu. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Mark Mwandosya. Hapa katika picha, Prof. Mwandosya anafuatilia kikao cha maandalizi ya mkutano huo kilichohudhuriwa na mawaziri na maofisa kadhaa kutoka serikalini. Nyuma yake (aliyevaa miwani) ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Salim Msoma. (Picha na Ansbert Ngurumo)

Wednesday, September 14, 2005

Nani Anaimiliki Bendera Ya Taifa?


MVUTANO juu ya matumizi ya Bendera ya Taifa nchini Tanzania uliozuka katika kipindi cha kampeni za uchaguzi, umezua mjadala mpya katika jamii. Sasa watu wanahoji. Kwani Bendera ni nini hasa? Nani anaimiliki? Soma Hapa.

Friday, September 09, 2005

Friday, September 02, 2005

CCM imemshauri vibaya Kikwete

MWAKA 1995 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichangamkia mdahalo wa wagombea urais, wakati huo kikiwa kimemteua Benjamin Mkapa. Mwaka huu, chama hicho hicho kikiwa na mgombea mpya, Jakaya Mrisho Kikwete, kimekwepa mdahalo huo kikisingizia ratiba ngumu ya mgombea. Uamuzi huo wa CCM umezua hisia na maswali mbalimbali katika jamii. Wengine wanasema Kikwete kaogopa. Wengine wanasema CCM haikuhitaji mdahalo huo. Woga au si woga, kwa nini CCM imeingia mitini? Tafakari.

Monday, August 01, 2005

Utani Kwa Wachagga!

Mzee mmoja toka Machame (Bwana Oforo) ambaye alikuwa
mkali sana kwa binti yake aitwae Manka, anaamka
asubuhi na kutaarifiwa kwamba binti yake ana mimba!

Bwana Oforo: "Aisee we Manka, nakwenda kazini,
nikirudi leo ni lazima uniambie ni nani kafanya uchafu
huu" Anafoka na kuondoka kuelekea ofisini.

Mchana akapigiwa simu na Mama Manka na kuambiwa kwamba
yule jamaa aliyempa mimba bintiye yupo nyumbani
anamsubiri kwa mazungumzo!

Mzee akachukua panga lake na kulinoa kabisaaa kwa
ajili ya kwenda kumteketeza mwanaharamu huyo.

Kufika nyumbani mambo yanakuwa hivi:

Kijana aliyempa mimba binti: "Mmmh Mzee ni kweli mi
ndiye nimempa mimba binti yako, na kusema kweli sina
mpango wa kumuoa. Lakini akizaa mtoto wa kiume
nitakupa TShs 1 million na ghorofa Kariakoo kisha
nachukua mtoto. Akizaa mtoto wa kike nakupa TShs 1
million na duka Sinza! Lakini je mzee, ikitokea bahati
mbaya mimba hii ikaharibika itakuwaje? "
Mzee Oforo: "Aisee babaangu eeeh itabidi tu umpe mimba
nyingine, hakuna jinsi!"

Sunday, July 24, 2005

Tusipojipenda, nani atatupenda?

Je, nawe u miongoni mwa Watanzania wanaoona aibu kujitambulisha wanapokuwa nje ya nchi? Unaogopa kuzungumza Kiswahili? Unapungukiwa nini? Hebu pata mawili matatu kutoka kwa mwanaharakati Jeff Msangi aishiye Kanada, kama alivyoandika katika safu yake ya WARAKA KUTOKA KANADA kwenye gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Julai 24, 2005, uk. wa 13. Bofya hapa.

Waijua Mikoba ya Baba na Mama Mkapa Ikulu ?

Rais Benjamin Mkapa na Mkewe, Anna, wanakaribia kuondoka Ikulu baada ya miaka 10. Inavyoonekana, wapenzi hawa wawili wameamua kuandika historia na kutengeneza mafao yao ya kustaafu kwa kuanzisha mifuko. Baadhi ya Watanzania wanaiita Mikoba ya Baba na Mama Ikulu. Wanasemaje? Pata uhondo.

Thursday, July 07, 2005

Simu kwenye mizani? Pengine, si Tanzania

Na Kanku Gambire
SERIKALI ya Tanzania imepiga marufuku matumizi ya simu kwa wafanyakazi katika mizani ya barabarani. Kwa nini? Je, inawezekana? Soma Hapa.

Monday, July 04, 2005

Kwako Binafsi, Maisha Yana Maana Gani?

Na Ansbert Ngurumo

TAFAKARI pamoja nami juu ya fumbo hili; maisha. Kwangu, Maisha ni Mapambano, kama ilivyo kwa Askofu Mkuu wa Rochester, N.Y, Fulton J. Sheen.

Huyu naye aliamini hivyo na alitumia fumbo la Pasaka kueleza maana ya maisha. Alisema: “Kama maisha yetu hayana msalaba, hatutaweza kamwe kuliona kaburi tupu. Kama hakuna taji la miiba, hakutakuwa na shada la maua ya nuru. Bila ya Ijumaa Kuu hakutakuwa na Pasaka.”

Mahali pengine aliwahi kunukuliwa akilinganisha na kutofautisha uelewa wa wafuasi wa Yesu na ule wa wauaji wake. Alisema kwamba wafuasi wa Yesu hawakumtaraji afufuke, lakini waliomwua walitaraji ufufuko wake. Anatoa mfano, wale wanawake walikwenda kaburini Jumapili alfajiri kuupaka mwili wake manukato kama ilivyokuwa desturi. Hawakuwa na wazo kwamba angeweza kufufuka.

Maria Magdalena alipokutana na Yesu bustanini, alidhani amekutana na mtunza bustani. Na Maria Magdalena huyo huyo alipowaletea mitume wa Yesu habari za ufufuko, hawakumwamini. Njiani kuelekea Emmaus, wanafunzi wake wawili walikuwa na mazungumzo yaliyoonyesha kwamba wamekata tamaa.

Tazama kiwango hiki cha tofauti. Wakati watu hawa waliokuwa karibu na Yesu kwa muda mrefu wakikosa imani, wale wasiomwamini walimzika na kuweka jiwe kubwa kaburini. Kwa nini? Zaidi ya hayo waliweka walinzi! Kwa nini? Pasaka ya kwanza ya Agano Jipya haikuwa na starehe tuliyo nayo sasa. Ilikuwa siku ya mapambano ya mawazo, imani, kifo na maisha. Pata tafakuri zaidi hapa.

Iko wapi orodha ya wateule wa Nyerere kuwa marais?

Na Evelyn Kashoka

MOJA ya sababu za watawala kugeuka madikiteta duniani ni kushindwa kuwajibika. Ni kushindwa kutoa kile ambacho walitarajiwa kuleta na hata kushindwa kutoa majibu kwa maswali mengi ya wale ambao wanawatawala.
Makala iliyochapishwa na gazeti la Tanzania Daima, ukurasa wa 14 wa Toleo la Jumapili, 26 Juni 2005, yenye kichwa kisemacho “Walioshindwa kumsema Nyerere akiwa hai wakae kimya,” ilikuwa na sura zote za kidikiteta.
Inasema hivi: “Kama (watu) walishindwa kumsema Nyerere akiwa hai, sasa wakae kimya!” Amri hii ina maana ya kutunyamazisha. Kama walivyo madikiteta, mwandishi hana uvumilivu; ni mwoga wa hoja kinzani, kachoka na inavyoonekana, kaishiwa hoja.
Habari zaidi soma hapa.

Wabunge wamekacha vikao wasiifunde serikali

Na Nikita Naikata

SITAKI kuona Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania likiwa tupu. Wabunge hawamo. Waliomo ni wa kuokoteza.
“Nikae pale ili iweje? Wenzangu wananichafulia jimboni. Nikikaa hapa ina maana nimekata tamaa na sitaki kuingia katika ushindani,” amesema mbunge mmoja aliyekuwa akipanda ndege kwenda mkoani kwake. Habari kamili soma hapa.

Hofu yatawala CCM

•Wanachama waanza kuogopa kuhujumiana
•Hajapatikana kiongozi wa kumnadi Jakaya Kikwete
•Kisa? Kejeli za kuitana washindi na wajeruhiwa
•Wasema ubabe wa Mkapa unawapa hoja wapinzani


Na Ansbert Ngurumo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kuweka mkakati wa
kujipanga kukabiliana na upinzani katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu, lakini tayari kimeanza kuwa na hofu ya
kuhujumiwa na wanachama wake. Habari kamili soma hapa.
My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'