Sunday, September 16, 2007

Hawa ndio wala nchi?


Hili ndilo linaitwa sasa kundi la wala nchi. Gazeti la Serikali, Habari Leo Jumapili, tarehe 16. Septemba 2007, limemnukuu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibord Slaa, akiwataja 11 bora wanaodaiwa kushiriki katika ulaji na uuzaji nchi kwa namna moja au nyingine, kutokana na nyadhifa zao za kisiasa, kitaaluma au kwa sababu ya uwakala au ukaribu wao na wenye madaraka. Waliotajwa ni:
1. Rais Jakaya Kikwete

2. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

3. Waziri Mkuu Edward Lowassa

4. Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi

5. Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge

6. Waziri wa Viwanda na Biashara Basil Mramba

7. Gavana wa Benki Kuu (BoT) Daudi Balali

8. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Gray Mgonja

9. Katibu Mkuu Wizara ya Maji Patrick Rutabanzibwa

10. Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono
11. Mbunge wa Igunga Rostam Aziz (pichani juu).
. Tuhuma zao kamili hizi hapa.

14 comments:

Anonymous said...

Walijifanya wajanja, sasa mwisho wao unakaribia. Kwa hali ilivyo leo, hata wakijifanya wanamshitaki Dk. Slaa yatawalipukia kama lilivyokuwa suala la Zito, maana wananchi wamechoka. Hili ni kundi la marafiki ambalo limekuwa linakula kwa muda mrefu, tena bila kunawa. Sasa zamu ya Watanzania kujitetea imewadia.

Anonymous said...

Huko nyuma katika blog hii bwana Siriha aliwahi kuuliza kuwa kama Jakaya hawakemei wakina Karamagi tafsiri yake ni nini kwa sisi wananchi? Nadhani tafsiri sahihi ni hii inayojitokeza sasa kuwa nayeye yumo ,hawa wengine ni wakala tu!! Kama Rais, asijidanganye kuwa alichaguliwa kwa kura nyimgi kwa hiyo anaweza kuwachezea watanzania akumbuke tu kwamba Rais Estrada wa ufilipino pia alipewa urais through populism lakini mambo yakamgeuka na sasa yuko LUPANGO maisha!! Hawa mafisadi siku zao ndio zinawadia.

Anonymous said...

Naona Sasa Huko Tanzania kuna watu makini sana, Napenda ifike mahali Tanzania kuwa na Watu na bunge makini lenye uwezo wa kuwahoji watu wazembe na wanaliigiza taifa hasara kama hapa marekani. Hivyo kama ndio hivyo watu na serikali yetu ni uzao wa rushwa. kama Kuna mtu jasiri kati yao atangaze kuwa mimi sikutoa rushwa. Naona kuna Mbovu katika Katibu ya Nchi. sio accountable kwa watu hivyo ufisadi unazidi kila wakati. Sio hali nzuri kwa watu maskini wa Tanzania.
Josh Michael Colorado USA

Anonymous said...

Ni vizuri kuwa Dk Slaa ametaja. lakini wananchi wanafanya nini? Kushangilia tu? Inatosha? Angalia majina hayo, ni wazi kabisa kuwa hatutarajii TAKUKURU ifanye kazi yake kwa haki katika hili. Hii ni kesi ambayo uamuzi inabidi uchukuliwe na wananchi
Nyanje, DSM

Anonymous said...

Du! Hata Muungwana yumo? basi, tumekwisha!

Anonymous said...

Hao ndio mafisadi wenyewe...aka JK 11. Siku zao zinahesabika, si unajua mabwege nao wanazindukaga , na wakizinduka hawashikiki wala kukamatika.

Anonymous said...

TAKUKURU?UNACHEZA WEWE?TAKURU WENYEWE WANARIPOTI KWA RAIS, RAIS MWENYEWE AMEWEKWA MADARAKANI NA HAO WAFISADI, ACHILIA MBALI NA YEYE NI MMOJA WAO...TAKURU ILIKUWA INAFANYA USANII TU CHAGUZI ZA CCM, ILE NI SEHEMU YA PROPAGANDA BAADA YA KUONA HOJA ZA BOT NA BUZWAGI ZIMEWAKALIA PABAYA. FUATILIA NDUGU YANGU KESI HIZO KAMA HAUJAKUTWA ZIMETUPILIWA MBALI KWA KUKOSA USHAHIDI...

Anonymous said...

Mamaa even the pres. who is said to fight this s##T!

Ansbert Ngurumo said...

Ya Mkapa na Kikwete

7. BENJAMIN WILLIAM MKAPA

Benjamin William Mkapa alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 alipomaliza kipindi chake cha pili. Ufisadi wote ulioelezewa katika waraka huu ulitokea wakati wa utawala wa Rais Mkapa na anawajibika nao moja kwa moja ama kwa kuubariki au kwa kuunyamazia. Zaidi ya hayo, kuna ushahidi unaoonyesha kwamba wakati akiwa madarakani Rais Mkapa alishiriki moja kwa moja au kwa kutumia ndugu na/au washirika wa karibu wa familia yake katika ufisadi mkubwa na uliolipotezea taifa fedha nyingi.

Kwa mfano, wakati akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mkapa alitumia wadhifa huo kuhakikisha kwamba kampuni iitwayo Tanpower Resources Limited inamilikishwa asilimia 85 ya hisa za kampuni ya Kiwira Coal Mines Ltd. inayochimba mkaa wa mawe huko Kiwira Mkoani Mbeya. Hisa zilizobaki asilimia 15 zinamilikiwa na Serikali. Tanpower Resources Ltd. ni kampuni iliyoanzishwa kwa ajili ya kuinuifaisha familia ya Rais Mkapa na washirika wake wa karibu. Taarifa za BRELA zinazonyesha kwamba wakurugenzi wa Tanpower Resources Ltd. ni Anna Mkapa, mkewe Rais Mkapa, Nicholas Mkapa, mtoto wa Rais, Bwana Joseph Mbuna, wakili wa kujitegemea na baba mkwe wa Nicholas Mkapa, Daniel Yona, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa utawala wa Rais na bwana Joesph Mapundi. Baada ya Tanpower Resources Ltd. kutwaa umiliki wa Kiwira Coal Mines Ltd. kwa nguvu za Ikulu ya Rais Mkapa, iliingia mkataba na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini TANESCO wa kujenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia mkaa wa mawe na kuiuzia umeme TANESCO. Mkataba huo utainufaisha kampuni ya Kiwira Coal Mines Ltd., na kwa hiyo Rais Mkapa, familia na washirika wake wa karibu kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 271 kwa wakati wote wa mkataba.

8. RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Desemba 2005. Kabla ya kuwa Rais, Mheshimiwa Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo Nje na Uhusiano wa Kimataifa kuanzia 1995 hadi 2005, Waziri wa Fedha 1994 hadi 1995 na Waziri wa Maji, Nishati na Madini kuanzia mwaka 1990 hadi 1994. Kama Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Mheshimiwa Kikwete alishiriki moja kwa moja katika kusaini mikataba mibovu ya madini na makampuni ya madini ya kimataifa ambayo kwayo taifa limeendelea kupoteza utajiri mkubwa na kuinyima Serikali uwezo wa kifedha wa kuhudumia wananchi. Kwa mfano, mnamo tarehe 10 Aprili 1990, Major Jakaya Mrisho Kikwete aliingia mkataba wa madini ya kampuni ya SAMAX Limited ambapo kampuni hiyo ilipewa leseni ya kuchimba dhahabu katika eneo la Lusu, Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora. Matokeo ya mkataba huo, maelfu wa wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu waliokuwa eneo hilo waliondolewa kwa nguvu na vikosi vya FFU na bila ya kulipwa fidia yoyote. Hadi leo wananchi hao hawajalipwa fidia yoyote licha ya miaka zaidi ya kumi ya kufuatilia haki zao. Baada ya kutwaa utajiri wa dhahabu wa eneo hilo, SAMAX Limited iliuza eneo hilo kwa kampuni ya Ashanti Goldfields ya Ghana kwa dola za Marekani milioni 253. Ashanti Goldfields nao wakauza eneo kwa kampuni ya Resolute Limited ya Australia kwa kiasi kisichojulikana cha fedha za kigeni. Resolute Limited ndio waliojenga na wanamiliki Mgodi wa Dhahabu wa Golden Pride ulioko eneo la Lusu, Nzega hadi sasa na ambao ulifunguliwa mwezi Novemba 1998.

Mnamo tarehe 5 Agosti 1994 Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete aliingia tena mkataba na kampuni ya madini Kahama Mining Corporation Ltd., kampuni tanzu ya kampuni ya Sutton Resources ya Canada. Ijapokuwa mkataba huu unaonyesha wazi kwamba ulikuwa unahusu eneo la Butobela Wilaya ya Geita Mkoani Mwanza, mwezi Agosti mwaka 1996 Kahama Mining Corporation wakisaidiwa na vikosi vya FFU walivamia eneo la Bulyanhulu, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na kuwaondosha kwa nguvu watu takriban laki nne waliokuwa wakiishi na kuchimba dhahabu katika eneo hilo. Baada ya kutwaa eneo hilo kwa nguvu za kijeshi, Sutton Resources iliiuza Kahama Mining Corporation na Bulyanhulu kwa Kampuni ya Dhahabu ya Barrick Gold Corporation ya Toronto, Canada kwa dola za Marekani milioni 280. Leo hii Bulyanhulu ni moja ya migodi tajiri kwa dhahabu katika Bara la Afrika.

- Kwa mujibu wa Dk. Slaa

Ansbert Ngurumo said...

4. GRAY S. MGONJA

Bwana Gray Mgonja ni Katibu Mkuu wa siku nyingi wa Wizara ya Fedha. Vile vile ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania na anashikilia nafasi ya ukurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold Limited ambayo maelezo yake tumeyatoa kuhusiana na ufisadi unaomhusu Gavana Balali na Andrew Chenge. Kwa kuzingatia nafasi yake kama Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Mkurugenzi katika Benki Kuu na vile vile Mkurugenzi katika Tangold Ltd. iliyolipwa mabilioni ya fedha za umma katika mazingira yenye utata mkubwa, ni wazi kwamba kumekuwepo mgongano mkubwa wa kimaslahi unaomhusu Bwana Mgonja.

5. PATRICK W.R. RUTABANZIBWA

Kwa miaka mingi Patrick Rutabanzibwa alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini wakati mikataba mibovu ya madini inasainiwa na kashfa kubwa ya IPTL inatokea. Kwa sasa Bwana Rutabanzibwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na vile vile Mkurugenzi wa kampuni ya kigeni ya Tangold Limited. Ufisadi unaomhusu umeelezewa kwa kina katika maelezo yanayomhusu Gavana Balali na Andrew Chenge. Hapa pia kuna mgongano mkubwa kati maslahi yake binafsi kama Mkurugenzi wa kampuni binafsi iliyopokea mabilioni ya fedha za umma na maslahi ya umma aliyotakiwa kuyalinda akiwa kama kiongozi wa umma.

6. NIMROD ELIREHEMA MKONO

Mheshimiwa Nimrod E. Mkono ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji na Mshiriki Mkuu wa kampuni ya mawakili ya Mkono & Company Advocates ya Dar es Salaam. Barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali inaainisha kuwa Benki Kuu imekuwa ikilipa malipo makubwa kwa Mkono & Co. Advocates hasa yale yanayohusu kesi ya Valambhia ambapo Benki Kuu inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 60. Kwa mujibu wa barua ya wakaguzi tayari Mkono & Co. Advocates wamekwishalipwa shilingi 8,128,375,237 kwa fedha taslimu kwa kesi hiyo ambayo bado iko mahakamani. Malipo haya ni sawa na asilimia 13.5 ya deni lote inalodaiwa Benki Kuu. Hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ni kuwa kesi hii haina muda maalumu wa kumalizika na hivyo inawezekana kabisa malipo ya wanasheria yakazidi kiasi cha fedha inachodaiwa Benki Kuu.

Lakini hoja nyingine ya kimsingi ni kama malipo haya kwa mawakili yanaruhusiwa chini ya Kanuni za Malipo ya Mawakili na Uamuzi ya Gharama za Kesi za mwaka 1991, Tangazo la Serikali Na. 515 la mwaka 1991 (Advocates’ Remuneration and Taxation of Costs Rules, 1991). Kanuni hizi zimeweka kiwango cha malipo ya mawakili katika kesi ambazo fedha inayodaiwa ni zaidi ya Shilingi milioni 10 kuwa ni asilimia tatu. Kwa kufuata masharti ya sheria hii ya malipo ya mawakili, kampuni ya Mkono & Co. Advocates ilipaswa kulipwa Shilingi bilioni 1.8.

Kampuni ya mawakili ya Mkono & Co. Advocates imekuwa ikitajwa kuhusiana na kashfa kubwa za ufujaji na/au ubadhirifu wa fedha za umma kwa muda mrefu. Kwa mfano, ‘Taarifa ya Uchunguzi Kuhusu Tuhuma Dhidi ya Makampuni ya Tanfarms Ltd., Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd. Yanayomilikiwa na V.G. Chavda Kuhusiana na Matumizi Mabaya ya Fedha za Debt Conversion Programme’ iliyotolewa Bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Edward Oyombe Ayila mwezi Novemba 1994 ilisema yafuatayo kuhusu Mheshimiwa Nimrod Mkono: “Mhe. Spika si nia yangu kulichosha Bunge lako tukufu na hotuba ndefu lakini ni vizuri nikaelezea juu ya uhusiano unaotia mashaka kati ya V.G. Chavda na Mashamba yake na Subash Patel mwenye makampuni ya DECO ART, MM Motors, MM Garage, Hotel Sea Cliff, City Bureau De Change na Nimrod Mkono, Wakili wa kujitegemea ambaye pia ni Mkurugenzi katika makampuni ya AZANIA AGRICULTURAL ENTERPRISES, LIBERTY LEATHER SHOE LTD., AZANIA EXIMCO, n.k. (AIMS GROUP OF COMPANIES)

Baada ya kuelezea uhusiano huo ulivyokuwa Mheshimiwa Ayila alimalizia kwa kusema yafuatayo: “Mheshimiwa Spika, ni vigumu kabisa katika hali ya kawaida kwa mtu yeyote kuamini kwamba makubaliano haya na uhusiano uliojitokeza hapa haukuwa wa hila. Chavda kwa kupitia wakili wake Nimrod Mkono, aliomba Mahakama Kuu kuzuia kabisa shughuli za Kamati (permanent injunction). Aidha ni wakili huyo huyo ambaye ameshuhudia uuzaji wa deni la Deco Art (reassignment) kwa Chavda. Mheshimiwa Spika, hali hii ukiitazama kwa undani utaona kwamba pengine kuna kitu kinafichwa. Nimrod Mkono alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Oxford Services Ltd. na pia anamiliki Kampuni ya Marcus Ltd., makampuni ambayo kwa pamoja yamefaidika kwa kuupata jumla ya Shs. 4,477,870,279.61 chini ya utaratibu wa DCP.”

- kwa Mujibu wa Dk. Slaa

Ansbert Ngurumo said...

VIONGOZI WA UMMA WALIOKO KATIKA ORODHA HII WAMEKIUKA NA/AU KUVUNJA MASHARTI YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO NA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KAMA IFUATAVYO:

A. WALIOSHIRIKI MOJA KWA MOJA KATIKA VITENDO VYA UFISADI

1. DR. DAUDI T.S. BALALI

Dr. Daudi Balali amekuwa na bado ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania tangu mwaka 1997. Katika kipindi hicho cha miaka kumi, Gavana Balali amehujumu taifa la Tanzania kama ifuatavyo:

(i) Kufuatana na barua ya wataalamu wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, ameruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia ufujaji wa fedha za umma unaodaiwa kufikia Shilingi 522, 459, 255,000 katika ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyoko barabara ya Mirambo, Dar es Salaam na Gulioni, Zanzibar. Aidha taarifa kutoka vyanzo vingine zinaonyesha kwamba mwaka 1998 kampuni ya Skanska Jensen ya Sweden ilituhumiwa kutoa hongo ya Dola za Marekani milioni 5 kwa Gavana Balali tuhuma zilizopelekea kampuni hiyo kupigwa marufuku kushiriki tenda ya ujenzi wa majengo hayo. Hata hivyo, katika mazingira yanayoashiria ufisadi mkubwa, kampuni ya Group 5 ya Afrika ya Kusini ambayo ni kampuni tanzu ya Skanska Jensen ilipewa tenda ya kujenga majengo hayo ya Benki Kuu;

(ii) Kufuatana na barua iliyotajwa katika aya ya (i) hapo juu, Gavana Balali aliidhinisha na/au kuruhusu na/au kunyamazia malipo ya Dola za Marekani 118,396,460.36 zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi ya Meremeta Ltd. iliyokuwa inachimba dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara. Kwa miaka mingi Serikali ilikuwa ikitoa taarifa za uongo kwamba Meremeta Ltd. ilikuwa ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Kibaha, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, nakala ya usajili iliyotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales inaonyesha kwamba kampuni hiyo iliandikishwa nchini Uingereza tarehe 19 Agosti 1997 na ilifilisiwa huko huko Uingereza tarehe 10 Januari 2006. Aidha, taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya tarehe 31 Mei 2005 inaonyesha kwamba Meremeta Ltd. ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi tarehe 3 Oktoba, 1997. Vile vile taarifa hiyo inaonyesha kwamba hisa 50 za Meremeta Ltd. zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini na hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kupitia kwa Msajili wa Hazina katika Wizara ya Fedha. Inajulikana vile vile kwamba Gavana Balali aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Meremeta Ltd. kati ya mwaka 2004 na 2005. Hata hivyo, kuna utata mkubwa juu ya nani ni mmiliki hasa wa Meremeta Ltd. kwa kuwa taarifa ya BRELA inaonyesha pia kwamba makampuni mawili ya Kiingereza – London Law Services Ltd. na London Law Secretarial Ltd. – nayo yanamiliki hisa moja moja za Meremeta Ltd. Makampuni hayo yanatumia anwani moja iliyoko 84 Temple Chambers, Temple Avenue, jijini London. Haijulikani ni kwanini Gavana Balali aliruhusu fedha za umma kutumika kulipia madeni yote ya kampuni ambayo Serikali ilikuwa inamiliki hisa 50 tu wakati makampuni mengine ya kigeni yalikuwa yanamiliki hisa 52. Na kama ilivyosema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, uhalali wa Serikali kulipa madeni ya Meremeta Ltd. kwa Nedbank Ltd. badala ya kuiacha benki hiyo kudai malipo hayo kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo sawa na wadeni wengine haujulikani;

(iii) Kufuatana na barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia malipo ya Dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd. Katika hotuba yake Bungeni ya tarehe 27 Juni 2007, Waziri wa Madini na Nishati Mheshimiwa Nazir Karamagi alidai kwamba “… mali na madeni ya MEREMETA yamehamishiwa kwenye kampuni mpya ya TANGOLD ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.” Hata hivyo, barua ya BRELA ya tarehe 4 Julai 2007 inatamka wazi kwamba “Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius, na baadae kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.” Barua hiyo inaongeza kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania mnamo tarehe 20 Februari 2006 na kwamba Katiba ya kampuni hiyo haikuonyesha “majina ya wanahisa wa kampuni na mgawanyo wa hisa.” Barua hiyo ya BRELA inaonyesha kwamba wakurugenzi wa Tangold Limited ni pamoja na Gavana Balali, Gray S. Mgonja ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Andrew J. Chenge ambaye ni Waziri wa sasa wa Miundo Mbinu, Patrick W.R. Rutabanzibwa ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Vincent F. Mrisho ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha fomu Na. 1F inayohusu usajili wa kampuni za kigeni iliyowasilishwa BRELA na mawakili wa Tangold Limited na kusainiwa na Gavana Balali tarehe 20 Mei 2005 inaonyesha kwamba kampuni hii imetokea “Jamhuri ya Mauritius” na anwani yake iko Suite 520, Barkly Wharf, Le Caudan, Waterfront, Port Louis, Mauritius. Hivyo ndivyo kinavyoonyesha cheti cha usajili kilichotolewa na Msajili wa Makampuni wa Jamhuri ya Mauritius mnamo tarehe 5 Aprili 2005 na pia leseni ya biashara iliyotolewa kwa Tangold Ltd. Port Louis nchini Mauritius tarehe 8 Aprili 2005. nyaraka hizi pia zinaonyesha kwamba Tangold Limited ni kampuni binafsi (private company limited by shares). Kuna utata zaidi kwani kifungu cha 7(e) cha Katiba ya Tangold Ltd. kinaruhusu hisa za wanaomiliki kampuni hiyo binafsi kuhamisha hisa zao kwa wanandoa, baba, mama, watoto, wajukuu au wakwe zao wa kike au wa kiume! Sasa kama ni kweli kwamba Tangold Ltd. inamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia mia moja, je nani ni mke au mume au baba au mama au motto au mjukuu au mkwe wa kike au wa kiume wa Serikali ya Tanzania ambaye anaweza kuhamishiwa hisa za kampuni hiyo? Katika barua yake ya ukaguzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alidai kwamba Ofisi yake ilishindwa kuelewa uhalali wa malipo ya dola za Marekani 13,340,168.37 yaliyofanywa na Benki Kuu kwa Tangold Limited;

(iv) Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia mkopo usio na riba wa Dola za Marekani 5,512,398.55 kwa kampuni ya Mwananchi Gold Co. Ltd. kati ya mwaka 2004 na tarehe 30 Juni 2006. Kati ya fedha hizo, deni la dola 2,807,920 limedhaminiwa kwa dhahabu ghafi ambayo ingenunuliwa kutokana na fedha za mkopo zilizotolewa na Benki Kuu yenyewe! Kwa maana rahisi ni kwamba kampuni ya Mwananchi Gold haijatoa dhamana yoyote inayoeleweka kwa mabilioni ya shilingi ilizokopeshwa na Benki Kuu chini ya Gavana Balali. Kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia mwezi Desemba 2006 Mwananchi Gold Co. Ltd. ilikuwa imeshindwa kulipa hata riba ya mkopo huo kwa kiasi cha dola za Marekani 62,847.91. “Katika mazingira haya”, inasema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, “hatukuweza kujiridhisha kwamba deni la dola la Marekani 5512398.55 inalodaiwa (Mwananchi Gold Co. Ltd.) hadi kufikia tarehe 30 Juni 2006 linaweza kulipika.” Je, ni kampuni gani hii iliyopewa mamilioni ya fedha za umma katika fedha za kigeni bila kudaiwa riba au kupewa kipindi maalumu cha kulipa mkopo huo? Kufuatana na taarifa za BRELA, Mwananchi Gold Co. Ltd. ni kampuni binafsi ambayo wanahisa wake ni Benki Kuu ya Tanzania yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (hisa 500), Mwananchi Trust Co. Ltd. (hisa 1,123) na Chimera Co. Ltd. (hisa 500). Kampuni hii ilisajiliwa kama kampuni binafsi tarehe 12 Desemba 2002. Mawakili wake ni kampuni ya mawakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Associates ikiwashirikisha aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo marehemu Francis L. Nyalali, Waziri Mkuu wa zamani Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa R. Mahalu. Wakurugenzi wa Mwananchi Gold ni Joseph Sinde Warioba, Gavana Daudi Balali, Col. J. Simbakalia, Vulfrida Grace Mahalu, Yusuf H. Mushi na raia wawili wa Italia, Paolo Cesari na Patrizio Magrini. Vulfrida Mahalu ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni binafsi ya VMB Holdings (1996) Ltd. na pia ni mke wa Profesa Mahalu ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za kuhujumu uchumi kutokana na madai ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni tatu za Serikali wakati akiwa balozi wa Tanzania nchini Italia! Kanali Simbakalia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa na Yusuf Mushi ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni binafsi ya Business Machines Consultants (T) Ltd;

(v) Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia malipo ya shilingi 131,950,750,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini. Vile vile Gavana Balali anadaiwa kuidhinisha malipo ya shilingi bilioni 4,228,658,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini. “Katika mazingira haya”, inasema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, “hatukuridhika na uhalali wa hasara ya shillingi bilioni 131.9 zinazoonekana katika taarifa za fedha hadi kufikia tarehe 30 Juni 2006….” Kwa mantiki hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu aliiasa Benki Kuu kuanzisha uchunguzi wa malipo yaliyosababisha hasara ya shilingi 131,950,750,000 na shilingi 4,228,658,000 zilizolipwa kama malipo ya madeni ya nje. Waziri wa Fedha Zakia Meghji mwenyewe amekiri kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika akaunti za malipo ya madeni ya nje katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). IMF yenyewe katika taarifa kwa vyombo vya habari ya tarehe 27 Juni 2007 imetamka kwamba “Serikali (ya Tanzania) imekwisha kusimamisha malipo kutoka akaunti hiyo hadi uchunguzi huo utakapokamilika.” Wakati Serikali ikitoa taarifa hizi kwa IMF imekataa kata kata kutoa taarifa hizi kwa umma wa Watanzania wala wawakilishi wao Bungeni.

2. ANDREW J. CHENGE

Mheshimiwa Andrew Chenge ni Mbunge wa Bariadi Magharibi na Waziri wa Miundombinu katika Serikali ya sasa ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Kabla ya hapo, Mheshimiwa Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa miaka yote kumi ya utawala wa Rais Benjamin W. Mkapa. Kwa wadhifa huo, Mheshimiwa Chenge ndiye alikuwa “mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na … aliwajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana na sheria….” Katika kipindi hicho cha miaka kumi na mbili, Mheshimiwa Chenge amehujumu taifa la Tanzania kama ifuatavyo:
(i) Kama Mkurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold Limited alishiriki na/au kufaidika na malipo haramu ya dola za Marekani 13,736,628.73 ambazo zimeelezewa kwa kirefu katika sehemu inayomhusu Gavana Balali;
(ii) Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Chenge ameshiriki kuishauri vibaya na/au kutokuishauri vizuri Benki Kuu ya Tanzania na kusababisha ufujaji wa mabilioni ya fedha za umma ambayo yameelezewa katika sehemu inayomhusu Gavana Balali;
(iii) Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Chenge ameshiriki moja kwa moja katika kutoa ushauri kwa Serikali na/au Wizara ya Nishati na Madini kuingia mikataba mibovu na makampuni mbali mbali ya madini ya kimataifa ambayo kwayo taifa limepoteza mabilioni ya fedha za kigeni. Kwa mfano, katika hotuba yake Bungeni tarehe 6 Novemba 2006, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Bernard Membe alitoa taarifa kwamba katika kipindi cha miaka mitatu hadi kufikia 2006, makampuni ya uchimbaji dhahabu yaliyoko Tanzania yaliuza dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 2,340 wakati ambapo makampuni hayo yalilipa mrahaba na kodi nyinginezo kwa Serikali za shilingi bilioni 72. Katika kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa William Ngeleja aliliambia Bunge kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 Mgodi wa kwanza wa dhahabu wa Lusu Nzega ulipofunguliwa hadi mwaka huu, makampuni ya uchimbaji dhahabu yaliuza nje dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.614 wakati Serikali ikiambulia mrahaba wa dola milioni 78 tu! Endapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Chenge angeishauri vema Serikali ya Jamhuri ya Muungano kama alivyotakiwa na Katiba ya nchi yetu, taifa lisingekuwa linapoteza utajiri wake wa madini kwa kiasi kikubwa namna hii.

3. BASIL P. MRAMBA

Mheshimiwa Basil Mramba ni Mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Rombo na Waziri wa Viwanda na Biashara na kwa miaka kumi ya utawala wa Rais Mkapa alikuwa ndiye Waziri wa Fedha. Katika kipindi hicho cha miaka kumi, Mheshimiwa Mramba amehujumu taifa la Tanzania kama ifuatavyo:

(i) Kwa kutumia wadhifa wake kama Waziri wa Fedha, alishinikiza kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani kupewa kazi ya kukagua mahesabu ya makampuni ya uchimbaji dhahabu. Chini ya mkataba wake na Serikali ya Tanzania, Kampuni hiyo inalipwa asilimia 1.9 katika ya asilimia 3 za mrahaba inaolipwa Serikali ya Tanzania na makampuni ya madini ya dhahabu. Kufuatana na barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, katika mwaka wa fedha 2005/06, Alex Stewart (Assayers) walilipwa shilingi 14,175,753,189.46 kama malipo ya ukaguzi wa mahesabu ya makampuni ya dhahabu, ijapokuwa “hakuna ripoti za ukaguzi zilizowasilishwa na wakaguzi hawa kuhusu ukaguzi uliofanywa katika mwaka 2005/06”! Vile vile Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alisema katika barua yake kwamba “hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kwamba wakaguzi hawa wa dhahabu walipatikana kwa kufuata utaratibu wa zabuni ya ushindani.”
(ii) Vile vile kuna taarifa za kuwepo kwa rushwa na/au ufisadi mkubwa kuhusiana na mkataba kati ya Serikali na Alex Stewart Assayers. Barua pepe iliyoandikwa na Erwin Flores ambaye ni Makamu wa Rais Mtendaji wa kampuni hiyo ya Novemba 14, 2006 inamtaja mtu mmoja mwenye jina la Bwana Basil ambaye ana wadhifa wa Waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano na kuwa yeye pamoja na wenzake ambao hawakutajwa wana asilimia 12.5 za hisa kwenye kampuni hiyo na kuwa analipwa na kampuni hiyo. Kwa mujibu wa Flores, hakuwezi kukawa na ushahidi wowote kuthibitisha kwamba ‘Bwana Basil’ anapokea malipo kutoka kwa Alex Stewart kwa vile malipo yote kwake yamekuwa yakifanyika nje ya nchi. Kwa kadri tunavyofahamu, mtu pekee aliyekuwa waziri katika serikali ya Awamu ya Tatu na ambaye pia ni waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na ambaye ana jina la ‘Basil’ ni Mheshimiwa Basil Pesambili Mramba. Tumemtaka Waziri wa Fedha kutupatia nakala ya Mkataba kati ya Benki Kuu na Alex Stewart, na kuwataka Mheshimiwa Basil Mramba na Erwin Flores walete maelezo yao kwetu kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka, Haki na Kinga za Bunge ya mwaka 1988 kwa barua yetu ya tarehe 18 Julai 2007 ili waweze kujibu tuhuma hizi. Bado tunasubiri majibu hayo.
(iii) Mheshimiwa Mramba amehusishwa pia na ufujaji na/au matumizi mabaya ya fedha za umma na uuzaji holela wa rasilmali za taifa letu. Kashfa hizo ni pamoja ni ununuzi wa rada ya kijeshi, ununuzi wa ndege ya Rais, na ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na National Microfinance Bank (NMB).

- Kwa Mujibu wa Dk Slaa

Anonymous said...

Kingunge anataka ushahidi gani zaidi ya huu? Katibu mkuu wa fedha anasomesha watoto wake Washington na mkewe yuko huko huko kwa mshahara gani kama sio ufisadi wa kutumia ofisi yake!! Iliyobaki wapinzani wajaribu kutumia interpol kupata accounts za hawa jamaa walikoficha hela huko nje walizotuibia, hapo ndipo hawatauliza ushahidi.

Anonymous said...

Kingunge anataka ushahidi gani zaidi ya huu? Katibu mkuu wa fedha anasomesha watoto wake Washington na mkewe yuko huko huko kwa mshahara gani kama sio ufisadi wa kutumia ofisi yake!! Iliyobaki wapinzani wajaribu kutumia interpol kupata accounts za hawa jamaa walikoficha hela huko nje walizotuibia, hapo ndipo hawatauliza ushahidi.

Anonymous said...

Ndugu zangu,
Unajua fadhila hulipwa kwa fadhila lakini matokeo yake ni mabaya sana hususani suala zima kama linagusa jamii moja kwa moja. Nafikiri mtakubaliana nami ya kwamba chaguzi nyingi zinazoendeshwa nchini zinahitaji mtaji wa kutosha nikiwa na maana ya fedha za kufanya kampeni (rushwa). Na katika hali ya kawaida ya watanzania wenzangu walio wengi wakiwemo wagombea wenyewe fedha hizi kwa asilimia kubwa huwa hazitoki mikononi mwao, bali huwategemea watu mbalimbali wakiwemo rafiki zao wa karibu. Michango hii huwa haitoki bure bali kuna ahadi maalum, na ahadi hizi ndizo huzaa balaa. Ukiangalia kwa makini zaidi baraza letu la mawaziri asilimia tisini na tisa ni wale waliofadhili kampeni za mheshimiwa na ili kulipa fadhila basi uongozi uligawiwa kama karanga pasipo kujali historia ya mtu. Hapa siongelei suala la elimu maana elimu sio kigezo pekee cha kumfanya mtu apewe madaraka makubwa, kuna vitu vingine vingi ambavyo vinapaswa kuangalia. Kwa kifupi tu ni kwamba sikushangaa nilipoona hiyo list. Of course hao ni wachache katika wengi kwani walioachwa ni wengi zaidi. Watanzania wenzangu tuhesabu miaka kumi ya kufunga mikanda kwa hiari yetu sisi wenyewe. Nasema kwa hiari yetu kwa maana sisi ndo wapiga kura wenyewe na lolote linalotokea katika uongozi liwe jema ama baya ni kwamba tumechangia kwa kiasi kikubwa. sitaki kusema zaidi ni bora niishie hapa.

Imani.

My photo
Nimechongwa na mambo haya: Falsafa, Fasihi, Muziki, Habari na Harakati. Sifuati mkumbo. Napenda kuhoji na kudadisi - hulka ya kifalsafa ya kuusaka ukweli - 'UKWELI ULIO UCHI.'